Tupate elimu gani, Tanzania iwe bomba | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tupate elimu gani, Tanzania iwe bomba

Discussion in 'Jukwaa la Lugha' started by Mundu, Feb 20, 2010.

 1. M

  Mundu JF-Expert Member

  #1
  Feb 20, 2010
  Joined: Sep 26, 2008
  Messages: 2,720
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 145
  Nawauliza manguli, wazoefu wa kulumba
  Nimekiona kivuli, pichaye imenifumba
  Inanikata kauli, mashairi kuyaimba
  Tupate elimu gani, Tanzania iwe bomba?

  Naanza na mlimani, vitivo vyenye kufana
  Wamesoma wa zamani, elimu wameiona
  Mbona nchi taabani, umasikini kwa sana
  Tupate elimu gani, Tanzania iwe bomba?

  Elimu ya uhandisi, wakufunzi wenye dhima
  Wanabukua nahisi, matokeo mbona kimya
  Au haina nafasi, kwa dunia hii jama?
  Tupate elimu gani, Tanzania iwe bomba?

  Kwenye kitivo uchumi, maporofesa lukuki
  Sioni faida mimi, digirii zenu feki
  Mbona nchi haihami, kule chini haitoki?
  Tupate elimu gani, Tanzania iwe bomba?

  Nchi haifaidiki, hasa kwenye mikataba
  Sheria yetu ya dhiki, isiyo jaa kibaba
  Au kuna ushabiki, kila mtu anaiba?
  Tupate elimu gani, Tanzania iwe bomba?

  Watu wenye mamlaka, kwa heshima nawaita
  Wananchi tumechoka, kwa kauli zenu tata
  Kwanini mnaridhika, wakati sisi twasota?
  Tupate elimu gani, Tanzania iwe bomba?

  Siwaachi viongozi, mlioshika ofisi
  Mbona mwatuchuna ngozi, mmegeuka mafisi
  Sisi tumewapa kazi, kwanini mmetuasi?
  Tupate elimu gani, Tanzania iwe bomba?

  Nawe jemedari wetu, mkuu wa hii kaya
  Kucha kutwa kwa wenzetu, kwako unaona haya?
  Twataka ahadi zetu, chonde chonde we Jakaya
  Tupate elimu gani, Tanzania iwe bomba?

  Nchi yenye utajiri, Tanzania yasifika
  Mbona mambo siyo shwari, kwenye uchumi hakika
  Tukae tutafakari, ninajua tutafika
  Tupate elimu gani, Tanzania iwe bomba?

  Kaditama wa tamati, nimemaliza kutunga
  Mpira naweka kati, najua mmejipanga
  Tukiweka mikakati, twaweza vuna mpunga
  Napumzika jamvini, mlumbe mimi nafunga.
   
 2. M

  Mundu JF-Expert Member

  #2
  Feb 21, 2010
  Joined: Sep 26, 2008
  Messages: 2,720
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 145
  Ukimya muoneshao
  Nyinyi mlio upeo
  Tusipoamka leo
  Nchi haitagomboka

  Nchi haitagomboka
  Tukionyesha kuchoka
  Wenzetu wameamka
  Sisi bado tunaota

  Sisi bado tunaota
  Twaishi kwenye viota
  watatupeleka puta
  Hata majirani zetu

  Hata majirani zetu
  waibeza kasi yetu
  Twatembea kama chatu
  Tena tumejilegeza

  Tena tumejilegeza
  nchi haitapendeza
  kaya zetu zina giza
  Hata hilo latushinda?

  Hata hilo latushinda
  Wakati tuna matunda
  malighafi zinavunda
  Elimu yetu ya nini?

  Elimu yetu ya nini?
  Haifai maishani
  Wananchi taabani
  Taaluma ipo wapi?
   
 3. M

  MaMkwe JF-Expert Member

  #3
  Feb 21, 2010
  Joined: Sep 5, 2007
  Messages: 284
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
  Ninavyowaona mimi
  Hawa wa kwetu wasomi
  Sijui hawana ndimi?
  Maovu kuyakemea

  Inasikitisha sana
  Na rohoni kusonona
  Wanyonge tunapoona
  Wasomi wanabung'aa

  Tumetupa nguvu zetu
  Kuwasomesha wenzetu
  Wakomboe nchi yetu
  Ona wanayotufanyia

  Katu hawana mapenzi
  Na nchi yetu azizi
  Wanaona bora kazi
  Ya kuibia raia

  Wanakumbatia uovu
  kwa mikataba mibovu
  Hawajani maumivu
  Sisi wanayotutia

  Sina jibu la kutoa
  Elimu gani inafaa
  Kwani tulishakosea
  Wezi tuliwaachia

  Labda tupate kichaa
  Nchi aje ibomoa
  Tuanze upya sawia
  Lakini, hilo si la kuombea
   
 4. M

  Mundu JF-Expert Member

  #4
  Feb 21, 2010
  Joined: Sep 26, 2008
  Messages: 2,720
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 145
  Nimependa hiyo verse ya mwisho...
   
 5. Anyisile Obheli

  Anyisile Obheli JF-Expert Member

  #5
  Feb 22, 2010
  Joined: Dec 13, 2009
  Messages: 3,378
  Likes Received: 130
  Trophy Points: 160

  Hodi naja jamvini, kutoa yangu majibu
  Naomba pewa hisani, timiza wangu wajibu
  Jamani sikilizeni, msijepata sababu
  Turejee asili yetu, taifa kuliendeleza.

  Tamaa tuweke pembeni, tujari utu zaidi
  Tafakari akirini,athali za mafisadi
  Makini sote tuweni, tusije kuwa hasidi
  Turejee asili yetu taifa kuliendeleza

  Maendeleo hakuna, bila kuwa na msingi,
  Ikiwa moja hakuna, kumi haiwi shilingi,
  Yatatufaa ya jana, kuujenga mpya msingi
  Turejee asili yetu taifa kuliendeleza.

  Elimu tumeshapata,tatizo ni matumizi
  Mmmea afya utapata, tusipokata mizizi
  Wala hakuna matata, tuuache usingizi
  Turejee asili yetu taifa kuliendeleza.

  Chai yake sukari, kuutengeneza utamu
  Huwezi ramba shubiri, ukitamani utamu
  Kuwa na nyingi habari, ni kukwepa majukumu
  Turejee asili yetu, taifa kuliendeleza.

  Tukubari rudi nyuma, kutaka maendeleo,
  Tusiwe kama wanyama, waso jana wala leo,
  Mazuri kuacha nyuma, kujifanya wa kileo,
  Turejee asili yetu, taifa kuliendeleza.

  Tuachane na umimi, wa kujiwekea hazina,
  Tukuze wetu uchumi, kutengeneza safina,
  Tuondoe huu utemi, ili tuwe wa kufana,
  Turejee asili yetu, taifa kuliendeleza.

  Kulejea wetu msingi, hiyo ni Elimu tosha,
  Tusiparamie vigingi, taa zetu kutowasha,
  Asili yetu ni msingi, twendako kutuonesha,
  Turejee asili yetu, taifa kuliendeleza.
   
 6. Anyisile Obheli

  Anyisile Obheli JF-Expert Member

  #6
  Feb 22, 2010
  Joined: Dec 13, 2009
  Messages: 3,378
  Likes Received: 130
  Trophy Points: 160

  Hodi naja jamvini, kutoa yangu majibu
  Naomba pewa hisani, timiza wangu wajibu
  Jamani sikilizeni, msijepata sababu
  Turejee asili yetu, taifa kuliendeleza.

  Tamaa tuweke pembeni, tujari utu zaidi
  Tafakari akirini,athali za mafisadi
  Makini sote tuweni, tusije kuwa hasidi
  Turejee asili yetu taifa kuliendeleza

  Maendeleo hakuna, bila kuwa na msingi,
  Ikiwa moja hakuna, kumi haiwi shilingi,
  Yatatufaa ya jana, kuujenga mpya msingi
  Turejee asili yetu taifa kuliendeleza.

  Elimu tumeshapata,tatizo ni matumizi
  Mmmea afya utapata, tusipokata mizizi
  Wala hakuna matata, tuuache usingizi
  Turejee asili yetu taifa kuliendeleza.

  Chai yake sukari, kuutengeneza utamu
  Huwezi ramba shubiri, ukitamani utamu
  Kuwa na nyingi habari, ni kukwepa majukumu
  Turejee asili yetu, taifa kuliendeleza.

  Tukubari rudi nyuma, kutaka maendeleo,
  Tusiwe kama wanyama, waso jana wala leo,
  Mazuri kuacha nyuma, kujifanya wa kileo,
  Turejee asili yetu, taifa kuliendeleza.

  Tuachane na umimi, wa kujiwekea hazina,
  Tukuze wetu uchumi, kutengeneza safina,
  Tuondoe huu utemi, ili tuwe wa kufana,
  Turejee asili yetu, taifa kuliendeleza.

  Kulejea wetu msingi, hiyo ni Elimu tosha,
  Tusiparamie vigingi, taa zetu kutowasha,
  Asili yetu ni msingi, twendako kutuonesha,
  Turejee asili yetu, taifa kuliendeleza.
   
 7. Anyisile Obheli

  Anyisile Obheli JF-Expert Member

  #7
  Feb 22, 2010
  Joined: Dec 13, 2009
  Messages: 3,378
  Likes Received: 130
  Trophy Points: 160
  hiyo ni kali, labda huyu ataweza kuongoza, lakini kwa taaluma gani (mwendawazimu kama waziri wa mambombo ya ndani miaka ya 90, yaani Mrema)
   
 8. M

  Mundu JF-Expert Member

  #8
  Feb 22, 2010
  Joined: Sep 26, 2008
  Messages: 2,720
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 145
  Asante kwa jibu lako
  Umeonesha mwamko
  Anyisile we kiboko
  Kichaa ni suluhisho

  Tukipata kiongozi
  Kichwani mwenye uchizi
  Tutaukata mzizi
  Wa wetu umasikini?

  Je nasi wananchi
  Tunaoishi kijichi
  Ili tuijenge nchi
  Yatupasa tuwe vipi?
   
 9. Anyisile Obheli

  Anyisile Obheli JF-Expert Member

  #9
  Feb 23, 2010
  Joined: Dec 13, 2009
  Messages: 3,378
  Likes Received: 130
  Trophy Points: 160
  Mundu nimekupata,
  Asante yako sijaifuta,
  Yafaa kama mafuta,
  Yatokanayo na ufuta.

  Wametuongoza timamu,
  Kutuimanisha mizimu,
  Heri mwendawazimu,
  Taifa kushika hatamu.

  Kijichi siyo tatizo,
  Atawaondolea mizozo
  Atawapeni mwongozo
  Imara kama nguzo.

  Muwe wapole kijichi,
  Kama juisi parachichi,
  Mtaipenda nchi,
  Wazimu akiishika.
   
 10. M

  Mundu JF-Expert Member

  #10
  Feb 25, 2010
  Joined: Sep 26, 2008
  Messages: 2,720
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 145
  Obheli umesifia
  kichaa anatujia
  kutuonyeshea njia
  neema tutaiona?

  sisi tuwe watulivu
  tena wenye usikivu
  mbona wanivunja mbavu
  pekee hawezi ndugu

  nchi ni kombinesheni
  ya sisi wavijiweni
  nawale wenye mpini
  ndipo itasonga mbele

  swali bado lipo pale
  lauliza vilevile
  ni elimu gani ile
  tusome tuende mbele?


   
 11. The Son of Man

  The Son of Man JF-Expert Member

  #11
  Feb 25, 2010
  Joined: Feb 9, 2010
  Messages: 12,412
  Likes Received: 2,042
  Trophy Points: 280
  Safi best ila mwenzenu hapa mchango sina manake kujibu kwa mashairi mwenzenu sijui. All in all michango yenu ni mizuri wanamalenga. I appreciate. Nawatakia usiku mwema. Mwogopeni na kumwomba Mungu daima dawama!
   
 12. K

  KunjyGroup JF-Expert Member

  #12
  Feb 26, 2010
  Joined: Dec 7, 2009
  Messages: 352
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 33
  Remove CCM from power. Hawana nia ya kuinua elimu sababu wanafaidika na ujinga wa wananchi. Hawataki kutawala wasomi bali mbumbumbu ili waburuzwe. Wangekuwa wana usongo an elimu yetu wangewafukuza waziri na wasaidizi wake wote baada ya kuona wameshindwa kazi. Angalia matokeo, wameshtuka?
   
 13. Anyisile Obheli

  Anyisile Obheli JF-Expert Member

  #13
  Feb 26, 2010
  Joined: Dec 13, 2009
  Messages: 3,378
  Likes Received: 130
  Trophy Points: 160
  Mundu nimejaribu,
  Swali lako kulijibu,
  Kukwepa sikujaribu,
  Kuutimiza wajibu.

  Tuliyonayo Elimu,
  Kweli ni ya kudumu,
  Tumeuleta ugumu,
  Sa tusione vigumu.

  Asili kuirejesha,
  Hiyo ni Elimu tosha,
  Mapito kuyanyoosha
  Taifa kutoangusha.

  Tumevamia uzungu,
  Na tumekuwa mizungu,
  Hatujawa na uchungu,
  Tunazalisha majungu.

  Tuachane na usasa,
  Taifa lisiwe tasa,
  Tukaziache anasa ,
  Tusije huko kunasa
   
 14. M

  Mundu JF-Expert Member

  #14
  Feb 27, 2010
  Joined: Sep 26, 2008
  Messages: 2,720
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 145
  nakubali anyisile
  wewe umeenda shule
  usemayo ndiyo yale
  yatakayo tunasua

  tatizo nimebaini
  nchi kuwa masikini
  tumeacha umakini
  wa kujali utaifa

  kila mtu nimchoyo
  hafanyi kazi kwa moyo
  tufanyayo haya siyo
  hayanemeshi taifa

  hata tungesoma sana
  kwa vidato vilofana
  kama hatutashikana
  bure tunajisumbua

  lamgambo nalipiga
  kwa tambo si kwa kuiga
  nchi ni kama mafiga
  ya kuivisha ubwabwa

  Figa la kwanza ni watu
  tena watu wenye utu
  watu wenye roho kwatu
  waloshikana pamoja

  la pili niwatawala
  wale wasopenda kula
  waongoze bila hila
  tutapata burudiko

  Figa la tatu elimu
  iliyo shika hatamu
  Elimu jama muhimu
  ya kutupatia TUNU

  Ninamuomba rabuka
  muumba wa kutukuka
  atupe bila kuchoka
  baraka na nema zake.
   
 15. Anyisile Obheli

  Anyisile Obheli JF-Expert Member

  #15
  Mar 17, 2010
  Joined: Dec 13, 2009
  Messages: 3,378
  Likes Received: 130
  Trophy Points: 160
  hakika tukiamka tutapiga hatua
   
 1. This site uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
  By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.
  Dismiss Notice
 1. This site uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
  By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.
  Dismiss Notice
Loading...