Tungo nzuri za fasihi ya Kiswahili

Tungo nzuri za fasihi ya Kiswahili

Jeremia Mhanuzi

New Member
Joined
Apr 11, 2026
Posts
2
Reaction score
0
MAHABA YASIYOKOMA.
Mimi binafsi huwa ni mpenzi wa tungo mbalimbali za sanaa ya kiswahili.

Tangu utotoni, nimekuwa nikipendelea sana kusoma vitabu na machapisho mbalimbali yaliyoletwa nyumbani ama na mzee wangu au kaka na dada zangu walionitangulia kufika shule. Mpaka sasa nawezasema, nimesoma vitabu vyingi sana, vya kutosha kunisahaulisha lini hasa niliinza kupendezwa na tabia hii. Kama ni mafunzo, basi nimejifunza mengi sana toka ndani ya vitabu na machapisho mbalimbali niliyoyasoma. Vitabu vya dini, vitabu vya elimu ya darasani, vitabu vya simulizi, hadithi, tenzi na ushairi ambao bila shaka ulinivutia sana. Nilishawahi kuwa na tabia ya wizi na udokozi mdogo mdogo kama ilivyokuwa kwa watoto wengi waliokulia katika mazingira ya ushawishi.

Hata hivyo sikuwahi kujutia kuwa na tabia hiyo ambayo bila shaka ndiyo imeniumba kuwa hivi nilivyo sasa. Utotoni niliiba na kuficha vitu vingi visivyo mali yangu, nikajimilikisha, nikavifanya kuwa vya kwangu na sikutaka viguswe na mtu yeyote. Kitu pekee ninachojivunia mpaka sasa, ni vile sikuwa mwizinjaa, yaani mwizi wa vitu vitamu mdomoni au vile vipendwavyo na utumbo mpana. Niliiba vitu vya kuvutia, vitu vichache vilivyouvutia ufahamu wangu. Niliiba maandishi mengi yaliyoipunguza akiba ya vitabu vya mzee wangu kwa kiasi kikubwa. Yake ikapungua, yangu ikaongezeka. Mpaka sasa namshukuru sana mzee wangu kwa kuniruhusu kila nilipodokoa maandishi yake, akanionya kila nilipoyatunza vibaya, akaniadhibu kila nilipoyapuuzia. Sasa nimekuwa mtu mzima, siibi tena kwasababu sipaswi kuiba. Ninatengeneza mwenyewe, ijae akiba ya kutosha; ili akikua aibe kama vile mimi nilivyomuibia mkubwa.

Uzoefu wa maisha ya kale, umenifunza namna ya kupenda. Nimejipata katikati ya mahaba yasiyokoma juu ya kile kilichozivutia sana fahamu zangu tangu utotoni. Kuna mahaba yasiyokoma baina yangu na kila utungo mtamu wa fasihi za kiswahili. Huwa zinanivutia sana: (I) Simulizi na hadithi tamu za fasihi, hasa zile za ujasusi na upelelezi. Mvuto wa kipekee huwa uninapata kila ninapozisoma tungo tamu za ushairi wa kiswahili. Siyo tu ushairi kwa sababu una jumbe za mahaba niyapendayo sana, hunivutia kwa namna safi zinavyofikisha ujumbe huo kwa namna ya kibabe sana. Tangu niyagundue mahaba haya yasiyokoma, nilijitahidi sana kujifunza namna bora zaidi ya kuyatunza mahaba ninayoyafurahia sana. Darasa la hiyali nililohudhuria, lilinifundisha namna ya bora zaidi ya kuumba na kuandaa hiki nikipendacho kwa namna ya kuvutia zaidi. Sasa ninayenzi vizuri mahaba yasiyokoma baina yangu na hiki nikipendacho. Nakiandaa mwenyewe kwa namna nzuri niipendayo, kikiwa tayali, nakifurahia toka ndani kwasababu nakijua nje ndani mithili ya kata na mtungi wake.

KWA WALE WAPENZI WA TUNGO NZURI ZA FASIHI YA KISWAHILI, WENYE MAHABA YASIYOKOMA JUU YA SANAA YA UANDISHI. KARIBUNI SANA NDANI YA UZI HUU, TUFURAHIE KWA PAMOJA KUSOMA TUNGO HIZI AMBAZO BILA SHAKA NI URITHI HALISI UTAKAOISHI VIZAZI NA VIZAZI.

LEO NAUZINDUA UZI HUU KWA KUWEKA WAZI UTUNGO HUU MFUPI, CHEMBE KIDOGO YA KUHUISHA MAHABA YASIYOKOMA NDANI YANGU.



​
MWANZONI MWISHONI.

Sianzi ninaanzisha, Nilichokitamatisha,
Zao nilolizalisha, Zaidi nalizidisha,
Nini siri ya maisha, Ikaipita motisha,
Sasa yanihamasisha, Hatima ilonitisha.

Sitoi sijumulishi, Nisijibu kwa utashi,
Nitaponaje uzushi, Likiharibika pishi,
Nimejifunza kuishi, Siyo kungoja mazishi,
Nyimbo hazihamasishi, Asipokuwa mwandishi.

Natumai pana mwisho, Chapa ya utambulisho,
Tamati ya maonesho, Nani tanifuta jasho,
Wapi nitakuwa kesho, Vipi nitapata posho,
Tafakhuri ya miisho, Inadai maboresho.

Ninayo mengi kichwani, Hamasa ya ushindani,
Limenitoka moyoni, Kosa kuu la mwanzoni,
Natalajia usoni, Kuiua ile soni,
Narudi upya mwanzoni, Naanza upya mwishoni.
 

Attachments

MAHABA YASIYOKOMA.
Sehemu ya pili katika mfululizo mrefu wa tungo tamu za fasihi ya kiswahili ziendazo kwa jina la Mahaba Yasiyokoma. Leo ninakuletea mkasa mdogo uliowahi kunikuta, ukawa chanzo kikuu cha wazo la uumbaji wa tungo nyingine iliyobeba hisia zangu. Nikashawishika kuandika kuweka kumbukumbu sawa, ili hata mkasa atakapokwisha, niwe na kitu cha ziada. Cha kunikumbusha mimi ni nani, wapi nilikotoka na wapi ninakoelekea.​


TONGE LA MOTO.

Licha ya kufakamia, Utamu sikusikia,
Badae nikang'amua, Tonge kumbe la bandia,
Mwanzoni nilipania, Mwishoni nikaumia,
Tonge la moto adhabu, Ndani linaniharibu.

Mazoea bila chai, Nilimeza kama yai,
Mdomo ukakinai, Likanitoa nishai,
Likaumba uadui, Kutisha wangu uhai,
Tonge la moto adhabu, Ndani linaniharibu.

Nikumbukapo tukio, Naliona lile zao,
Liloleta mshangao, Kunitosa bila ngao,
Uchu na matamanio, Vyaniletea kilio,
Tonge la moto adhabu, Ndani linaniharibu.

Nizitazamapo ngeu, Tonge naliona jau,
Lini tapata walau, Maumivu nisahau,
Nilioneshe dharau, Maisha nipande dau,
Tonge la moto adhabu, Ndani linaniharibu.

Nani anisaidie, Zawadi nimpatie,
Tumbo anifungulie, Tonge moto nilitoe,
Nani nimsimulie, Tiba akanipatie,
Tonge la moto adhabu, Ndani linaniharibu.
 

Attachments

Back
Top Bottom