Tundu Lissu aunguruma Bungeni!

Tundu lisu yuko anasoma hotuba ya kambi ya upinzani wizara ya sheria na katiba, ameshasema mahakama zetu hazina uhuru, rais ana mamlaka makubwa pengine hata juu ya mahakama. Tuendelee kujuzazana hapa.
 
Kwa kweli viongozi wazuri kwa taifa hili wako kambi ya upinzani!!!!!!!!! Mzee, tupe zaidi za huko mjengoni kwa huku kwetu umeme wameungeleja tayari.
 
Kasema kama wazanzibar tunataka muungano basi na tuchague ni aina ipi ya muungani tunaitaka.huyu jamaa ni kichwa leo mpa ndungai kamkubali ni bingwa wa kuvunja rekodi
 
Tundu lisu amekamilika na amewasilisha vizur kwa mpangilio mzur wa hoja zilizoshiba.
Cha kushangaza wakati anachangia waziri wa katiba na sheria mh Selina Kombani alikua anacheka cheka.cjui ilikua dharau au vp?
 
sa unategemea nini kaka zaidi ya hilo! yule mama hana kitu, kawekwa pale kwa vigezo na sifa fulanifulani (ndo maana anachekacheka) hayupo kwa mambo ya kisheria!
 
Tundu lisu amekamilika na amewasilisha vizur kwa mpangilio mzur wa hoja zilizoshiba.
Cha kushangaza wakati anachangia waziri wa katiba na sheria mh Selina Kombani alikua anacheka cheka.cjui ilikua dharau au vp?

Siku zote wahenga wanatuasa kufanya maandilizi na kumjua mpinzani kabla hujaingia ulingoni. Wakubwa walimpa Selinda Kombani wizara ya sheria kabla hawajasoma nani atakuwa mpinzani wake. Sasa ni kibano mtindo mmoja.
 
Siku zote wahenga wanatuasa kufanya maandilizi na kumjua mpinzani kabla hujaingia ulingoni. Wakubwa walimpa Selinda Kombani wizara ya sheria kabla hawajasoma nani atakuwa mpinzani wake. Sasa ni kibano mtindo mmoja.
<br />
<br />
tehe tehe tehe!umenichekesha sana mkuu.
 
WIZARA YA SHERIA NA KATIBA:
KAMA NI TUNDU LISSU BASI WIZARA ITAKUA IMEMPATA MTU LAKINI KAMA NI KOMBANI BASI NI MTU NDIO KAPATA WIZARA KAMA HALI ILIVYO HIVI SASA NCHINI - KAZI KWELI KWELI!!!!


Endapo Mhe Tundu Lissu anaweza akawa waziri wa SHERIA NA KATIBA leo hii basi nasema hadi hapo wizara hiyo itakua IMEMPATA KIONGOZI thabiti; nadhani hilo halina ubishi.

Lakini kwa kuwa mtu aliyeukwaa hilo
ZALI LA MENTALI ni huto tumama, basi nako hadi hapo nijisemee tu kwamba, kwa tofauti kidogo, safari hii itakua ni kwamba ni huyo mama Kombani ndiyo atayekua amebahatik kupata WIZARA DHABITI na wala si vinginevyo.

Hivyo aheri ya Tundu Lissu ndani ya nyumba kuliko kuwa na hili
lisanamu kiongozi ofisini!!!!!!!
 
tundu lissu yuko vizuri.magamba watakoma mwaka huu.mimi ni ccm lakini natamani tu nirudishe kadi sema nikimuwaza nyerere nangojea kidogo.lakini inshort mibunge ya ccm na nape ni kero na janga la taifa,
<br />
<br />
Pole sana ila nakushauri rudisha tu hiyo kadi maana Nyerere wala hakuoni na hata kama angeweza kukuona wala hatakulaumu!
 
FULL TEXT HII HAPA .

MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA KATIBA NA SHERIA, MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.)
KUHUSU
MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KWA MWAKA 2011/2012
(Kanuni ya 99(7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007)

UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Kwa vile tumeshapongezana na kupeana shukrani za kutosha; kwa kuzingatia matakwa ya kanuni ya 151 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007, inayohusu salamu za pongezi; na kwa kutambua ufinyu wa muda wa nusu saa nilio nao, naomba uniruhusu niokoe muda wa majadiliano kwa kufanya kile ninachowajibika kukifanya kwa mujibu wa kanuni ya 99(7).

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri wa Katiba na Sheria imeanzishwa kwa mujibu wa kipengele cha 12 cha Nyongeza ya Waraka wa Rais uliochapishwa kama Tangazo la Serikali Na. 494 la tarehe 17 Desemba 2010. Majukumu ya Ofisi hii yameainishwa katika Tangazo la Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 2010 (The Ministers [Assignment of Ministerial Functions] Notice, 2010) lililochapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 494A la tarehe 17 Desemba 2010. Kwa mujibu wa Nyongeza ya Pili ya Tangazo hilo, pamoja na meingine, Ofisi ya Waziri wa Katiba na Sheria imekasimiwa majukumu ya masuala ya kikatiba, uendeshaji na utoaji wa haki, uendeshaji mashtaka na haki za binadamu.

Mheshimiwa Spika, Baadhi ya majukumu haya ni ya kikatiba kwani yamewekwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977. Kwa mfano, kwa mujibu wa ibara ya 4(1) ya Katiba, shughuli zote za mamlaka ya nchi zinazohusu uendeshaji na utoaji wa haki “... zitatekelezwa na kudhibitiwa na ... vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki....” Vyombo hivyo viwili, kwa mujibu wa ibara ya 4(2) ni Mahakama ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 107A(1), “mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Mahakama.”

Mheshimiwa Spika, Majukumu mengine ya kikatiba ya Ofisi ya Waziri wa Katiba na Sheria ni pamoja na Katiba yenyewe. Vile vile, masuala yote yanayohusu uendeshaji wa mashtaka ni ya kikatiba kwa mujibu wa ibara za 59B(1) na (2) za Katiba zinazounda Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ambaye “... atakuwa na uwezo wa kufungua, kuendesha na kusimamia mashtaka yote nchini.” Aidha, haki za binadamu nayo pia ni masuala ya kikatiba kufuatana na Sehemu ya Tatu ya Sura ya Kwanza ya Katiba yenye kufafanua haki za binadamu na wajibu muhimu; na Sehemu ya Kwanza ya Sura ya Sita yenye kuunda Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na kuipa mamlaka na majukumu yake.

MGAWANYO WA MADARAKA NA UHURU WA MAHAKAMA

Mheshimiwa Spika, Mfumo wetu wa kikatiba na kiutawala umejengwa katika misingi ya mgawanyo wa madaraka na uwajibikaji iliyowekwa na Katiba. Ibara ya 4(1) na (2) ya Katiba inaweka msingi wa kikatiba wa mgawanyo wa madaraka baina ya vyombo vyenye mamlaka ya utendaji, vyombo vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki na pia vyombo vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma. Vyombo hivi vitatu vya dola havitakiwi, na wala haviwezi, kujitenga katika utekelezaji wa majukumu yao ya kikatiba. Hata hivyo, pamoja na mahusiano kati yao, vyombo vya dola vinatakiwa kuwa huru katika utekelezaji wa majukumu yao. Ndio maana ibara ya 107B ya Katiba inaelekeza kwamba: “Katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia tu masharti ya Katiba na yale ya sheria za nchi
Hii ni muhimu zaidi kwa vyombo vya utoaji haki kwani bila uhuru huo, vyombo hivyo vinaweza kujikuta vikihatarisha au kukiuka haki za watu kwa kuegemea zaidi kwa mamlaka nyingine hasa hasa Serikali. Hii ni kwa sababu, katika utekelezaji wa majukumu yake ya kikatiba na kisheria ya kila siku, Serikali hujikuta ikiingilia haki mbali mbali za wananchi. Vitendo hivyo mara nyingi huishia katika vyombo vya utoaji haki kwa ajili ya maamuzi yao. Bila kuwa huru, vyombo vya utoaji haki vinaweza kujikuta vikiiwezesha Serikali kuingilia haki za kimsingi za wananchi au kuhalalisha ukiukwaji wa haki za binadamu za wananchi.
URAIS WA KIFALME NA UHURU WA MAHAKAMA
Mheshimiwa Spika, Kwa muda wote wa uhai wetu kama taifa huru, mfumo wetu wa kikatiba na wa kisiasa umejengwa juu ya nguzo moja kuu ambayo mwanazuoni wa Kenya, Profesa H.W. Okoth-Ogendo, aliwahi kuiita Urais wa Kifalme (Imperial Presidency). Hii inatokana na ukweli kwamba katika mfumo huu, Rais ana madaraka makubwa sana sio tu ya kiutendaji bali pia ya kiutungaji sheria kwa vile, kwa mujibu wa ibara 62(1) ya Katiba, Rais ni sehemu ya Bunge. Vile vile Rais ana kivuli kirefu cha kikatiba katika utekelezaji wa masuala mbali mbali ya kimahakama kwa kutumia mamlaka makubwa aliyonayo katika uteuzi wa viongozi wote wa ngazi za juu za Mahakama. Kwa mfano, chini ya mfumo wetu, Rais anamteua Jaji Kiongozi na majaji wote wa Mahakama Kuu ya Tanzania [ibara ya 109(1) ya Katiba]; na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania [ibara ya 118(2) na (3)].

Mheshimiwa Spika, Ni kweli kwamba Rais anatekeleza wajibu wake kikatiba wa kuteua majaji kwa mashauriano na Tume ya Utumishi wa Mahakama [ibara ya 109(1) na 113(1)] na Jaji Mkuu [ibara ya 118(3) ya Katiba]. Hata hivyo, ni muhimu kutambua na kusisitiza ufinyu wa mamlaka ya ushauri kwa mujibu wa Katiba yetu. Hii ni kwa sababu chini ya ibara ya 37(1) ya Katiba, “... Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote, isipokuwa tu pale anapotakiwa na Katiba hii au na sheria nyingine yoyote kufanya jambo lolote kulingana na ushauri anaopewa na mtu au mamlaka yoyote
Vile vile, kwa mujibu wa ibara ya 112(2) ya Katiba, wajumbe wote wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ni wateuliwa wa Rais na, kwa sababu hiyo, Rais anashauriwa na watu aliowateua yeye mwenyewe na ambao halazimiki kufuata ushauri wao! Katika mazingira haya ya kikatiba, ni rahisi kwa Rais kuteua watu kuwa majaji au viongozi wa juu wa Mahakama ya Tanzania kutokana na vigezo vingine nje ya utaalamu au uzoefu wao wa kitaaluma. Aidha, katika mazingira haya, ni rahisi kwa wateuliwa wa Rais kuamini kwamba wameteuliwa kwenye nafasi kwa nasaba zao na ukaribu wao na Rais au watu wake wa karibu na kwa hiyo wanajiona wana deni la kulipa fadhila kwa Rais kwa kufanya maamuzi yatakayompendeza yeye au Serikali yake. Mfumo huu wa kikatiba unajenga mazingira ya wateuliwa wa Rais kujipendekeza kwake au kwa Serikali yake (sycophancy) ambayo matokeo yake ni uendeshaji na utoaji haki uliojaa woga au upendeleo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba mazingira haya ya kikatiba yanatishia moja kwa moja uhuru wa Mahakama ya Tanzania na hayana budi kuangaliwa upya katika mjadala wa kikatiba unaoendelea sasa hivi.

Mheshimiwa Spika,Badala ya madaraka ya Urais wa Kifalme juu ya Mahakama ya Tanzania kupunguzwa ili kuwe na uwiano bora zaidi wa mgawanyo wa madaraka kati ya Serikali na Mahakama ili kulinda uhuru wa Mahakama, Sheria ya Uendeshaji Mahakama, 2011 iliyotungwa na Bunge hili tukufu katika Mkutano wake wa Tatu, imemwongezea Rais madaraka makubwa zaidi katika uendeshaji wa Mahakama. Kwa mujibu wa kifungu cha 7(1) cha Sheria hiyo, Rais ndiye atakayemteua Mtawala Mkuu wa Mahakama; na ndiye anayeamua masharti ya ajira ya Mtawala Mkuu wa Mahakama [kifungu cha 7(6)]. Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 9, mamlaka ya nidhamu juu ya Mtawala Mkuu wa Mahakama ni Rais. Sheria hii vile vile inampa Rais hata mamlaka ya kuanzisha au kuvunja nafasi za kimahakama na zisizokuwa za kimahakama baada ya kushauriwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama [kifungu cha 21(1)].
Kama ambavyo nilipata kusema wakati natoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni juu ya Muswada wa Sheria hiyo, kifungu hiki kinakwenda kinyume na matakwa ya ibara ya 36(1) ya Katiba inayompa Rais mamlaka ya kuanzisha au kufuta ofisi za utumishi wa umma “... bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii na sheria nyingine yoyote....” Nafasi za kimahakama kama za majaji na mahakimu zimewekwa ama na Katiba yenyewe au na sheria nyinginezo na kwa hiyo Rais hana mamlaka ya kuzianzisha au kuzifuta!

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama vile vile inatishia uhuru wa mahakama kwa kuruhusu wanasiasa na watendaji wa Serikali kusimamia nidhamu za watumishi wa kimahakama. Kwa mfano, chini ya kifungu cha 50(5), Kamati za Maadili ya Watumishi wa Kimahakama za Mikoa zimepewa wajibu wa kushughulikia nidhamu za Mahakimu wa Wilaya na Mahakimu Wakazi wa mikoa husika. Kamati hizi zinaoongozwa na Wakuu wa Mikoa ambao pia wanateua wajumbe wengine wawili kati ya wajumbe sita wa Kamati [kifungu cha 50(1)]. Na kama ambavyo nimepata kusema wakati nilipowasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni juu ya Muswada wa Sheria hii, utaratibu huu unahatarisha uhuru wa mahakama kwa sababu Wakuu wa Mikoa “... wana tabia ya kuingilia utendaji wa mahakama zetu na mara nyingi ni wakiukaji wa sheria na taratibu za nchi yetu. Mara nyingi Mahakama ni vyombo pekee katika mikoa vyenye mamlaka kisheria ya kuwadhibiti pale wanapokiuka miiko ya kisheria ya kazi zao

Mheshimiwa Spika, Kivuli hiki kirefu cha Urais wa Kifalme katika uongozi na utekelezaji wa mamlaka ya utoaji haki wa Mahakama ni tishio kwa uhuru wa mahakama na utekelezaji wa majukumu yake. Licha ya viapo vyao vya kutenda haki bila hila, woga au upendeleo, wateuliwa wa nafasi mbali mbali za uongozi au utendaji wa Mahakama wana uwezekano mkubwa wa kujiona wanawajibika kwa mamlaka yao ya uteuzi, yaani Rais. Aidha, watendaji wa Mahakama ambao wanawajibika kinidhamu kwa mamlaka zinazoongozwa na watendaji wa Serikali na makada wa chama tawala kama Wakuu wa Mikoa wanakuwa na woga wa kushughulikia kesi zinazowahusu watendaji na makada hao na/au Serikali wanayoiwakilisha. Dalili za woga huu ni nyingi na zitazidi kuongezeka kwa sababu ya Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama. Tayari tumeanza kusikia taarifa za baadhi ya Wakuu wa Mikoa kuwafuata mahakimu ili kuulizia mwelekeo wa kesi zinazohusu wanachama au viongozi wa vyama vya upinzani hasa hasa CHADEMA. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kwamba huu ni muda mwafaka, sambamba na mjadala wa mfumo mpya wa kikatiba, kuyashughulikia masuala haya ili Mahakama ya Tanzania iondokane na kivuli kirefu cha Urais wa Kifalme na kuiwezesha kuwa huru kutenda haki kwa mujibu wa viapo vya watendaji wa Mahakama ya Tanzania.

AMLIPAE MPIGA ZOMARI ...?

Mheshimiwa Spika, Pengine tishio kubwa kuliko mengine yote kwa uhuru wa Mahakama za Tanzania limekuwa sio tu kuingiliwa na wanasiasa na watendaji wakuu wa Serikali. Tishio kubwa zaidi ni lile la Serikali kutumia udhibiti wake wa hazina ya taifa kuinyima Mahakama rasilmali za kuiwezesha kutimiza wajibu wake kikatiba. Kama nilivyosema katika hotuba yangu wakati nawasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu Muswada wa Sheria ya Uendeshaji Mahakama, moja ya matatizo makubwa yanayokabili mahakama zetu nchini ni pamoja na “vipaumbele vyake kutozingatiwa katika migawanyo ya bajeti za Serikali za kila mwaka.” Wasiofuatilia kauli za Serikali Bungeni wanaweza kufikiri kwamba haya ni maneno ya kila siku ya wapinzani wasioona mema mengi ambayo Serikali mbali mbali za CCM na mtangulizi wake, TANU, zinadaiwa kuyafanya katika kipindi cha miaka hamsini ya uhuru wetu.

Mheshimiwa Spika, Kwa wenye fikra hizo, naomba niwakumbushe kauli ya aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria wakati huo, Mh. Dr. Mary M. Nagu, wakati alipowasilisha hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2006/2007: “... Changamoto zilizoainishwa kimsingi zinatokana na ufinyu wa bajeti inayotengwa kila mwaka wa fedha. Mara nyingi na kwa kipindi kirefu, kiasi kinachotolewa huwa hakilingani na mahitaji halisi ya Wizara.” Naomba niwakumbushe pia kauli ya mrithi wa Mh. Dr. Nagu katika Wizara hiyo Mh. Mathias M. Chikawe wakati wa hotuba yake ya bajeti ya mwaka 2009/2010: “... Changamoto zilizoainishwa kimsingi zinatokana na ufinyu wa bajeti inayotengwa kwa ajili ya Wizara yangu kila mwaka wa fedha. Mara nyingi kiasi kinachotolewa huwa hakilingani na mahitaji halisi ya Wizara, na hata kiasi kidogo kinachotengwa hakitolewi kwa wakati na wala hakitolewi chote, jambo ambalo linaathiri sana Mpango Kazi wa Wizara yangu.” Na kama nitakavyoonyesha baadaye kidogo, hoja hizi za ‘Sungura Mdogo’ ndio zimekuwa wimbo wa Serikali kila mwaka kuhusu bajeti za Wizara ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Spika,Hali ya miundo mbinu ya mahakama zetu ni ya kusikitisha na haisameheki kwa upande wa Serikali ambayo ndio yenye udhibiti wa hazina ya umma. Kwa mfano, wakati Serikali imejenga majengo mapya ya Ofisi za Wakuu wa Mikoa yote na Wilaya zote na Wizara mbali mbali katika kipindi cha miaka hamsini ya uhuru wetu, Kanda nane kati ya kumi na tatu za Mahakama Kuu ya Tanzania zimeendelea kutumia majengo yaliyorithiwa kutoka dola ya kikoloni. Kanda nne kati ya tano zilizobaki na Divisheni tatu za Mahakama Kuu, yaani Divisheni ya Biashara, ya Kazi na ya Ardhi zinatumia majengo yaliyoazimwa au kuchukuliwa kutoka taasisi nyingine za umma! Ni Kanda moja tu za Mahakama Kuu ya Tanzania – Kanda ya Bukoba – ambayo imejengewa jengo jipya ya Mahakama katika kipindi cha miaka hamsini ya utaifa wetu. Na hata hilo moja halijakamilika hadi leo!

Mheshimiwa Spika, Kwa karibu miaka thelathini tangu kuanzishwa kwake, Mahakama ya Rufani ya Tanzania ilikuwa ikichangia jengo moja na Masjala Kuu ya Mahakama Kuu, Dar es Salaam. Mwaka 2004, ukarabati wa jengo la iliyokuwa Hoteli ya Forodhani wa kulifanya kuwa Makao Makuu ya Mahakama ya Rufani ya Tanzania ulianza. Ukarabati huo ulikamilika na jengo kuanza kutumika mwaka 2006. Hata hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa kwamba Serikali imeamua sasa kuliuza Jengo hilo kwa wawekezaji wapya wa iliyokuwa Kempinski Kilimanjaro Hotel ili libomolewe na eneo lake ligeuzwe kuwa maegesho ya magari ya wageni wa hoteli hiyo! Kwa hatua hii, Mahakama Rufani ya Tanzania itatakiwa ikapangishiwe tena mahali pengine pa kufanyia kazi zake za utoaji haki.

Mheshimiwa Spika, Wakati Serikali imeridhia jengo la mahakama ya juu kabisa katika mfumo wetu wa kimahakama na wa kikatiba libomolewe ili wageni wa Kempinski Kilimanjaro Hotel wapate maegesho ya magari yao, Serikali imetenga shilingi sifuri kwa ajili ya Fungu 40 kasma 6313 inayohusu ukarabati wa Mahakama ya Rufaa! Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi Bungeni kama taarifa za kuuzwa kwa Jengo la Mahakama ya Rufani ya Tanzania na mipango ya kulibomoa ili eneo lake ligeuzwe kuwa maegesho ya magari ni za kweli. Na kama ni za kweli, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iliambie taifa Mahakama ya Rufani ya Tanzania itahamishiwa wapi ili kupisha wageni wa Kempinski Kilimanjaro Hotel kuegesha magari yao!

Aidha, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuachana na mpango huo wa aibu mara moja kwa sababu unarudisha nyuma mafanikio yote yaliyopatikana kwa Mahakama ya Rufani ya Tanzania kuwa na jengo lake yenyewe na hivyo kupunguza mrundikano wa majaji, mawakili, watumishi wa mahakama na wadau wa kesi ambao umekuwepo kwa miaka mingi katika jengo la Masjala Kuu ya Mahakama Kuu ya Tanzania. Ni Serikali ya aina gani hii inayobomoa majengo ya mhimili mkuu wa dola kama mahakama ili kutafuta nafasi ya watu wanaoenda kujiburudisha hotelini kuegesha magari! Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ituepushie fedheha na aibu hii kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, Kama nilivyoonyesha kwenye hotuba yangu ya tarehe 15 Aprili mwaka huu, hali ya miundo mbinu ya Mahakama za chini ya Mahakama Kuu ni mbaya kama ilivyokuwa kwa mahakama za juu. Hata hivyo, licha ya hali hii mbaya, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 500 tu kwa ajili ya Fungu 40 kasma 6310 inayohusu ujenzi na ukarabati wa mahakama za wilaya. Aidha, kasma 6312 inayohusuujenzi na ukarabati wa mahakama za mwanzo imetengewa shilingi milioni 500 vile vile. Hali hii mbaya ya miundo mbinu ya Mahakama ya Tanzania na mafungu haya kidogo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wake peke yake ni ushahidi wa kutosha kwamba mfumo wa uendeshaji na utoaji haki katika nchi yetu haujawahi kupewa kipau mbele na Serikali kwa miaka yote hamsini ya uhuru wetu. Kwa bahati mbaya huu sio ushahidi pekee wa Serikali kupuuzia vipau mbele vya mfumo wetu wa uendeshaji na utoaji haki kwa miaka yote ya uhuru wetu.

Mheshimiwa Spika, Haijawahi kutokea kwa Rais wa nchi hii au mawaziri wake kushindwa kufanya safari yoyote ndani au nje ya nchi kwa sababu ya ufinyu wa fedha zilizotengwa kwa ajili hiyo. Na wote tu mashahidi kwamba kwa mwaka huu peke yake, Bunge hili tukufu limeidhinisha zaidi ya shilingi bilioni 135 kwa ajili ya safari za Rais na ‘matumizi mengineyo ya kitaifa’! Rais na Baraza la Mawaziri ndio wanaounda mhimili wa kwanza wa dola la Tanzania. Aidha, hatujawahi kuambiwa kwamba Bunge hili tukufu limeshindwa kufanya Mkutano wake hata mmoja, au mikutano ya Kamati zake za Kudumu, kwa sababu ya ufinyu wa bajeti au ‘udogo wa sungura.’ Bunge hili tukufu linaunda mhimili wa pili wa dola letu. Hata hivyo, imekuwa ni jambo la kawaida kwa Mahakama ya Tanzania – mhimili wa tatu wa dola la Tanzania - kushindwa kufanya vikao vyake kwa sababu ya ufinyu wa bajeti inayotengwa kila mwaka kwa ajili hiyo.

Mheshimiwa Spika, Takwimu za Serikali yenyewe juu ya jambo hili zinaonyesha jinsi ambavyo Urais wa Kifalme umedhoofisha uwezo wa Mahakama ya Tanzania kutekeleza wajibu wao wa kikatiba wa kuwa “mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano”, kutumia maneno ya ibara ya 107A(1) ya Katiba. Kwa mfano, kwa mwaka wa fedha 2010/2011, Mahakama ya Rufani ilipanga kufanya vikao ishirini na mbili vya kusikiliza kesi za rufaa. Hata hivyo, kutokana na kutokupatiwa fedha kulingana na mahitaji yake halisi, Mahakama hiyo iliweza kufanya vikao kumi na sita tu hadi kufikia mwezi Machi 2011. Vile vile, Mahakama Kuu katika Kanda mbali mbali kumi na tatu zilipanga kufanya jumla ya vikao 124 katika kipindi hicho. Hata hivyo, kutokana na kutokupatiwa fedha zinazolingana na mahitaji halisi ya vikao hivyo, Mahakama Kuu iliweza kufanya vikao kumi na tano tu na Kanda sita hazikufanya kikao hata kimoja!

Mheshimiwa Spika, Sio Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani tu ambazo zimekwazwa kutekeleza wajibu wao kwa sababu ya ufinyu wa bajeti. Hali ni mbaya zaidi katika mahakama za chini. Kwa mfano, wakati ambapo Mahakama za Mahakimu Wakazi na za Wilaya zilikuwa na uwezo wa kusikiliza kesi 110,000 katika mwaka wa fedha 2010/2011, kwa ukomo wa bajeti waliowekewa na Serikali, mahakama hizo zimeweza kusikiliza mashauri 27,000 au 24.6% ya uwezo wao. Aidha, Mahakama za Mwanzo zilikuwa na uwezo wa kusikiliza kesi 242,000 kama zingeweza kutumia uwezo wa watumishi waliopo kwa sasa, licha ya upungufu mkubwa wa Mahakimu unaozikabili Mahakama za Mwanzo nchini. Hata hivyo, kwa sababu wa kupewa fedha pungufu, Mahakama za Mwanzo zimeweza kusikiliza takriban mashauri 70,000 tu, au 28.9% ya uwezo wao.

Mheshimiwa Spika, Kwa ujumla wake, katika mwaka wa fedha 2010/2011, Mahakama ya Tanzania imeweza kusikiliza 29% tu ya mashauri ya madai na jinai kwa kutumia idadi ya majaji na mahakimu waliopo kwa sasa na kwa kutumia miundo mbinu hafifu iliyopo. Ukweli ni kwamba kiasi hicho ni kikubwa hasa hasa ikitiliwa maanani kwamba katika kipindi hicho hicho, ukomo wa bajeti iliowekewa Mahakama ya Tanzania ilikuwa 23.5% ya mahitaji yake halisi. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2009/2010, kiasi halisi kilichotolewa – bila kujali kilitolewa lini – kilikuwa 23% ya mahitaji halisi kwa mwaka huo!
Katika mazingira haya, Mheshimiwa Spika, magereza hayawezi kuacha kujaa mahabusu ambao wanateseka na kuozea magerezani sio kwa sababu wana hatia yoyote bali kwa sababu hakuna hakimu au jaji wa kusikiliza kesi zao; au kwa sababu waliopo hawajatengewa fedha za kuwawezesha kusikiliza kesi hizo. Katika mazingira ya namna hii, maneno ya ibara ya 107A(2)(b) ya Katiba yetu kwamba katika kutoa uamuzi wa mashauri ya madai na jinai kwa kuzingatia sheria, Mahakama zinatakiwa “... kutochelewesha haki bila sababu ya kimsingi” yanaonekana kama ni kejeli na dhihaka ya kikatili na kifedhuli kwa wale wote wanaotaabika magerezani kwa sababu ya kesi zao kutokusikilizwa kwa wakati. Katika hali hii, dira ya Wizara ya ‘haki kwa wote kwa wakati’ ingeonekana kama kichekesho kinachowafaa zaidi Ze Comedy kama isingekuwa inahusu maisha ya binadamu wanaoteseka magerezani bila kuwa na hatia yoyote!

Mheshimiwa Spika, Kama nilivyosema katika hotuba yangu kwenye Bunge hili tukufu mnamo tarehe 15 Aprili 2011, kwa sababu ya kuzinyima mahakama fedha zinazolingana na mahitaji yao halisi na hata zinazolingana na ukomo wa chini uliowekwa na Hazina, “... Mahakama ya Tanzania imekuwa ni mdeni mkubwa na sugu.” Takwimu za madeni ya Mahakama zetu yanayotokana na kushindwa kulipia vifaa, huduma na stahili mbali mbali za majaji, mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama zinapatikana katika ukurasa wa 92-93 wa Taarifa Rasmi (Hansard) ya Majadiliano ya Bunge ya Kikao cha Nane cha Mkutano wa Tatu wa Bunge la Tanzania cha tarehe hiyo.

Mheshimiwa Spika, Matokeo ya Mahakama ya Tanzania kuwa mdeni mkubwa na sugu wa wagavi wa vifaa, huduma na wa stahili za majaji, mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama kuna athari kubwa katika utendaji wake. Kwanza, kama alivyosema aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Augustino S.L. Ramadhani wakati alipotuhutubia Waheshimiwa Wabunge juu ya Nafasi ya Mahakama Katika Uongozi wa Nchi: “Ni vigumu sana kwa Jaji anayeishi katika nyumba inayodaiwa kodi kuweza kusikiliza na kutoa hukumu katika kesi za mwenye na mpangaji au kesi yoyote ya uvunjwaji mkataba. Lazima Jaji atoe boriti kwenye jicho lake ili aweze kutoa (sic!) kibanzi kwenye jicho la mwingine”! Wanasheria wanapenda kusema ‘haki sio tu lazima itendeke lakini vile vile lazima ionekane kuwa imetendeka.’ Majaji ambao ni wadeni sugu wanawezaje kuonekana wametenda haki kwa wadeni sugu wengine wanaokwenda mahakamani kudai malipo ya madeni yao!

Athari ya pili, Mheshimiwa Spika, ni kwamba kuwa mdeni sugu kunaiondolea Mahakama heshima na hadhi yake mbele ya jamii na hasa hasa mbele ya watendaji wa mihimili mingine ya dola kama Serikali na Bunge. Napenda kumnukuu Jaji Mkuu Ramadhani tena: “Kila nilipokwenda mikoani nilikwenda ofisini kwa Mkuu wa Mkoa na kwa Mkuu wa Wilaya kutoa heshima zangu na kusaini kitabu cha wageni. Wakuu wa Mikoa wachache walitoka ofisini mwao kunilaki nje. Wengine walibakia ofisini mwao na kutuma mwakilishi kuja kunipokea ili nikamkute Mkuu wa Mkoa ofisini mwake ingawa Jaji Mkuu amefunga safari kutoka Dar es Salaam kumfuatia yeye. Kuna wakati nilikwenda Wilaya moja na nikaambiwa kuwa Mkuu wa Wilaya aliondoka jana yake kuanza likizo ya mwaka! Hivi kweli Mkuu wa Wilaya asingeweza kuahirisha likizo kwa siku moja tu kukutana na Jaji Mkuu. Ikikumbukwa kwamba Jaji Mkuu ndiye anayemuapisha Rais ili aweze kushika madaraka ya juu kabisa katika Taifa naye DC ni mwakilishi wa huyo Mhe. Rais wilayani humo.” Kama Jaji Mkuu haheshimiwi kiasi hiki na Wakuu wa Mikoa na Wilaya, maamuzi ya Mahakama yake yanawezaje kuheshimiwa na watendaji hawa wa Serikali?

Mheshimiwa Spika, Kuwa mdeni sugu pia kunaiondolea Mahakama ya Tanzania imani kwa wagavi wa wa vifaa na huduma mbali mbali zinazohitajika kwa uendeshaji bora wa mahakama. Kupotea kwa imani hiyo ya wagavi kuna athari kubwa za kiutendaji na hata kifedha. Kama inavyosema Taarifa ya Kikosi Kazi cha Ofisi ya Rais – Uratibu na Utawala Bora juu ya Ukaguzi wa Ujenzi wa Mahakama za Mwanzo (20) Chini ya Ufadhili wa Programu ya Maboresho ya Sekta ya Sheria (LSRP) ya Machi, 2011: “Kumekuwepo na tabia sugu ya mahakama kuchelewesha kulipa wakandarasi wa miradi ya ujenzi kwa wakati hivyo kusababisha ujenzi wa mahakama kuchelewa. Hivi sasa wapo wakandarasi wengi ambao hawavutiwi na kazi zinazotolewa na mahakama. Na wakati mwingine wakandarasi hulazimika kupandisha gharama za ujenzi ili kufidia ucheleweshaji wa malipo unaotarajiwa kujitokeza kutokana na urasimu wa mahakama

‘SUNGURA MDOGO’ HAKUBALIKI TENA!

Mheshimiwa Spika, Imekuwa jadi kwa Serikali kutoa sababu za ufinyu wa bajeti kuhalalisha kuinyima Mahakama fedha za kutosha kutimiza dira ya Wizara ya Katiba na Sheria ya ‘Haki kwa Wote na kwa Wakati.’ Visingizio hivi vya ‘sungura mdogo’, ‘ufinyu wa bajeti’, n.k. vimerudiwa rudiwa katika bajeti za kila mwaka za Wizara hii. Kwa mfano, akitoa hotuba ya bajeti ya Wizara kwa mwaka 2004/2005, aliyekuwa Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba Mh. Harith Bakari Mwapachu alilieleza Bunge hili kwamba katika mwaka 2003/04, “... Sekta ya Sheria kwa ujumla wake imeendelea kukabiliwa na matatizo ambayo yanaathiri kasi na ufanisi wa utendaji. Matatizo hayo yametokana hasa na ufinyu wa Bajeti ya Serikali. Ufinyu huo wa Bajeti umeendelea kuathiri utoaji na usimamizi wa haki na utawala wa sheria.”

Mheshimiwa Spika, Katika hotuba yake ya Bajeti kwa mwaka 2005/2006, Mh. Mwapachu alirudia tena hoja ya ‘udogo wa sungura’: “... Wizara kwa ujumla wake imeendelea kukabiliwa na matatizo ambayo yanaathiri kasi na ufanisi wa utendaji. Matatizo hayo yanatokana hasa na Bajeti ya Serikali kutoweza kukidhi mahitaji halisi ya asasi za Wizara.” Na kama tulivyoonyesha, visingizio hivi vilirithiwa na Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete kama ushahidi wa hotuba ya bajeti ya mwaka 2006/2007 iliyotolewa na Mh. Dr. Nagu unavyothibitisha. Vile vile, katika hotuba yake ya bajeti ya mwaka 2007/2008, Mh. Dr. Nagu alirudia “... kuwepo matatizo makubwa ya ufinyu wa bajeti” kama moja ya changamoto zilizosababisha Wizara kutotekeleza kikamilifu na kwa ufanisi baadhi ya majukumu yake.

Mheshimiwa Spika, Hotuba pekee ambayo haikuzungumzia kabisa tatizo la ‘ufinyu wa bajeti’ au ‘udogo wa sungura’ ni ile iliyotolewa na Mheshimiwa Chikawe wakati alipowasilisha bajeti ya mwaka 2008/2009. Hata hivyo, mwaka uliofuata kama tulivyokwisha kuonyesha, Mh. Chikawe alirudi kundini kwa kurejea tena dhana hiyo ya ‘sungura mdogo’! Mh. Chikawe aliendeleza jadi ya ‘ufinyu wa bajeti’ na ‘sungura mdogo’ kwenye Bajeti ya Wizara ya mwaka jana pale aliposema kwamba: “... Wizara yangu bado inakabiliwa na changamoto nyingi katika vyombo vyake vya utoaji haki nchini. Aidha, changamoto nyingi zinazoikabili Wizara ni pamoja na uwezo mdogo wa Serikali kifedha na rasilimali watu katika vyombo vyake vya utoaji haki kwa wananchi wake na kusababisha kuendelea kuwepo kwa mlundikano wa mashauri ya jinai na madai kwa kiwango kikubwa....” Aidha, Mh. Chikawe alikiri kwamba licha ya idadi ya watumishi wa kada mbali mbali wa Mahakama kuongezeka, “... bado uwezo wa Serikali kifedha ni mdogo kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika utoaji wa haki hapa nchini. Pia Wizara yangu ina upungufu wa nyenzo za kufanyia kazi kama magari, ofisi, samani, na nyumba za watumishi. Changamoto hizi zinaathiri utekelezaji wa azma ya Serikali ya upatikanaji wa haki kwa wote mapema na kupunguza tija ya Taasisi mbali mbali zilizoko chini ya Wizara.”

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria hajasema katika hoja yake ya leo kwamba fedha anazoomba Bunge hili tukufu liidhinishe kwa Wizara yake kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo kwa mwaka huu wa fedha hazitoshi; wala bajeti hii ni finyu; na wala hajasema kwamba sungura huyu ni mdogo. Hii ni licha ya ukweli kwamba Serikali haijatenga fedha zozote za maendeleo kwenye Fungu 18 la Mahakama Kuu na Mahakama za Mahakimu Wakazi tangu mwaka wa fedha 2010/2011-2011/2012. Aidha, kwa kipindi hicho hicho, hakuna fedha zozote zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwenye Fungu 19 linalohusu Mahakama za Wilaya na za Mwanzo.

Mheshimiwa Spika, Ukimya wa Mheshimiwa Waziri kuhusu suala la utoshelevu wa fedha anazoomba ziidhinishwe na Bunge hili tukufu sio wa ajabu, kwani katika utafiti wangu kwa ajili ya hotuba hii, sijaona yeyote kati ya mawaziri wote waliomtangulia Mheshimiwa Waziri wa sasa wa Sheria na Katiba aliyewahi kuliambia Bunge hili tukufu kwamba bajeti walizokuwa wanaziombea idhini ya Bunge hazitoshi. Kwa sababu hiyo, pengine haitakuwa makosa kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuchukulia ukimya wa Mheshimiwa Waziri katika jambo hili kuwa ni imani yake kwamba fedha anazoomba mwaka huu zitatosheleza mahitaji yote ya Wizara yake.

Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri ameliambia Bunge hili tukufu kwamba bajeti ya mwaka jana ilikuwa finyu ndio maana majukumu ya utoaji haki hayakutekelezwa kwa ufanisi. Maneno haya ya bajeti finyu na sungura mdogo ni utetezi ambao unapaswa kupuuzwa na Bunge hili tukufu. Ni maneno yanayokuja kama after thought baada ya Serikali kushindwa kutekeleza wajibu wake. Kwa jambo hili, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli kama bajeti hii ya mwaka huu inatosheleza mahitaji yote yatakayoiwezesha Mahakama ya Tanzania kutoa haki kwa wote kwa wakati kama ilivyo dira ya Wizara.

Mheshimiwa Spika, Kama Serikali itakiri kwamba fedha zilizotengwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya Mahakama ya Tanzania hazitatosha kuiwezesha kutekeleza wajibu wake kikatiba, basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe pungufu ya fedha hizo kutoka kwenye Fungu Na. 98 la Wizara ya Ujenzi, Kasma Na. 4168 inayohusu ‘Miradi Maalum ya Ujenzi wa Barabara’ ambalo – baada ya shilingi bilioni 95 kuchotwa na kupelekwa Wizara ya Uchukuzi – sasa limebakisha shilingi bilioni 253.075. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba kama ilikuwa halali kwa Serikali kutoa shilingi bilioni 95 kutoka kwenye Fungu hilo baada ya kuwa zimekwishaidhinishwa na Bunge kwa ajili ya Wizara ya Ujenzi na kuzipeleka kwenye Fungu Na. 62 la Wizara ya Uchukuzi, haiwezi ikawa haramu kwa Serikali hiyo hiyo kutoa fedha nyingine kutoka Fungu hilo hilo na kuzipeleka kwenye mafungu yote yanayohusu Mahakama ya Tanzania.

UFISADI MAHAKAMANI?

Mheshimiwa Spika, Inaelekea kwamba Mahakama ya Tanzania nayo imekumbwa na aina ya kansa inayojukana kitaalamu kama fisadiosis, au kwa jina lililozoeleka hapa kwetu, ufisadi ambayo imesambaa kila mahali katika mfumo wetu wa kiutawala. Dalili za kuenea kwa kansa hii katika Mahakama ni pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma zinazotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo ya Mahakama ya Tanzania. Naomba kuthibitisha jambo hili kwa kutumia mradi wa ujenzi wa majengo ya mahakama chini ya Programu ya Maboresho ya Sekta ya Sheria (Legal Sector Reform Program) ambayo imekuwa ikifadhiliwa na nchi wafadhili pamoja na Benki ya Dunia kwa karibu miaka mitano sasa.

Mheshimiwa Spika,Chini ya LSRP, Mahakama ya Tanzania ilipanga kujenga majengo kumi ya mahakama na kukarabati mengine kumi yaliyochakaa kila mwaka kuanzia mwaka wa fedha 2007/2008. Fedha za utekelezaji wa miradi hiyo zimekuwa zikitolewa na wafadhili katika bajeti ya maendeleo kupitia mradi wa LSRP kila mwaka. Hata hivyo, kwa mujibu wa Taarifa ya Kikosi Kazi cha Ofisi ya Rais, “utekelezaji wa miradi hiyo umekuwa hauridhishi kiasi kwamba wafadhili wamefikia hatua ya kutishia kujitoa na kusitisha ufadhili wao.” Ukaguzi wa miradi hiyo uliofanywa na Kikosi Kazi hicho unaonyesha kwamba “hadi sasa ni mahakama tatu tu zilizoweza kujengwa na kukamilika kwa kipindi chote hicho.” Mifano michache ya dalili za kansa ya ufisadi kwenye miradi hiyo inatosheleza kuthibitisha uwepo wa tatizo hili ndani ya Mahakama.

Mheshimiwa Spika, Moja ya majengo yaliyotarajiwa kukarabatiwa chini ya LSRP ni jengo la Mahakama ya Mwanzo ya Kirua Vunjo, wilayani Moshi Vijijini katika Mkoa wa Kilimanjaro. Kwa mujibu wa Taarifa ya Kikosi Kazi cha Ofisi ya Rais, jengo la Mahakama hiyo “kwa nje limekarabatiwa vizuri na kumalizika. Hata hivyo, kwa ndani jingo hilo lina mipasuko kwenye kuta na sakafuni. Aidha, mbao za dari zimeliwa na mchwa na kusababisha ceiling board zote kuanguka chini. Kwa ujumla, kazi iliyofanyika hairidhishi na haijafikia kiwango kilichotarajiwa kulingana na thamani ya fedha iliyotumika.” Cha ajabu kabisa ni kwamba “mkandarasi alikwishakabidhi jengo toka mwaka 2009 na kulipwa fedha yake yote ikiwemo retention money

Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo ya Basotu katika Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara nao umegubikwa na utata wa ufisadi. Kwa mujibu wa Taarifa ya Kikosi Kazi cha Ofisi ya Rais, ingawa ujenzi wa Mahakama hiyo umekamilika kwa 75%, mkandarasi ameshalipwa 95% ya fedha zake “... ijapokuwa hadi sasa mkandarasi ameshindwa kumaliza kazi na kukabidhi mradi.” Timu ya ukaguzi ya Kikosi Kazi cha Ofisi ya Rais ilibaini kwamba Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) “... waliruhusu mkandarasi kulipwa kiasi kikubwa cha fedha ambacho hakilingani na kazi iliyokwishafanyika

Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo ya Bereko katika Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma nao umezua maswali juu ya uadilifu wa wahusika. Ujenzi huo ulitakiwa kuwa wa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ilitakiwa kumalizika tarehe 20 Julai, 2008. Kwa mujibu wa Taarifa ya Kikosi Kazi cha Ofisi ya Rais, “... Mahakama ilikwishamlipa mkandarasi shilingi 141,704,940 ikiwa ni pamoja na advance kwa ajili ya awamu ya pili. Hata hivyo, malipo hayo yalifanyika kabla ya mkandarasi hajamaliza na kukabidhi kazi za awamu ya kwanza, na wala bila kuwepo mkataba wowote kwa ajili ya awamu ya pili ya ujenzi huo.” Aidha, “... hakukuwepo mchanganuo ‘Approved Bill of Quantities’, zinazoainisha kazi zitakazofanywa na mkandarasi katika awamu hiyo ya pili.” Kwa sababu hizo, “hadi sasa ni vigumu kujua gharama halisi za mradi huu wa Mahakama ya Bereko kwa vile hakuna mkataba mahususi kwa ajili ya kazi hiyo ya ujenzi

Mheshimiwa Spika, Miradi mingine ya ujenzi wa mahakama ambayo imeonyesha dalili za ufisadiosis ni Mahakama ya Mwanzo ya Shelui wilayani Iramba katika Mkoa wa Singida; Mahakama ya Mwanzo ya Ilolangulu wilayani Uyui katika Mkoa wa Tabora; Mahakama ya Mwanzo ya Makuyuni katika Wilaya ya Monduli mkoani Arusha; na Mahakama ya Mwanzo ya Mwanga Mjini katika Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro. Kikosi Kazi cha Ofisi ya Rais kilichokagua miradi hiyo kilibaini kwamba jengo la Mahakama ya Mwanzo ya Shelui “... liko katika hali isiyoridhisha”; kwa Ilolangulu “... mkandarasi hakuweza kukamilisha kazi katika muda ... uliopangwa kutokana na sababu zisizokuwa na msingi pamoja na usimamizi hafifu”, lakini TBA ilimwidhinishia malipo “... wakati kazi ilikuwa haijaanza kufanyika ambapo ... alilipwa fedha zote”!

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Mahakama ya Mwanzo ya Makuyuni, ujenzi wake ‘haujaanza’ na “kiwanja kilichokuwepo mwanzoni kimechukuliwa na Halmashauri baada ya kukaa muda mrefu bila kuendelezwa.” Aidha, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Monduli “... hajawahi kujua kama Mahakama ya Mwanzo ya Makuyuni imo katika mpango wa kujengwa chini ya LSRP.” Kama ilivyokuwa kwa Makuyuni, Kikosi Kazi cha Ofisi ya Rais kiliambiwa kwamba ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo ya Mwanga Mjini nao ulikuwa ‘bado haujaanza.’

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashangazwa na kusikitishwa sana na utendaji wa aina hii wa Mahakama ya Tanzania. Kama taasisi inayosimamia sheria na iliyojaa wanasheria kama Mahakama ya Tanzania inaweza kufanya malipo ya mamilioni ya shilingi za walipa kodi bila kuwepo mkataba wa kazi inawezaje kuwaridhisha Watanzania kwamba maamuzi mbali mbali juu ya haki na wajibu wa wananchi yanafanywa na watu wanaojua kweli sheria za nchi yetu na sio na ‘vihiyo’ wa sheria! Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazitaka mamlaka husika kuwachukulia wote waliohusika hatua stahiki haraka iwezekanavyo ili kurudisha imani ya Watanzania kwa Mahakama ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, Utendaji wa aina hii sio tu unatilia shaka uadilifu wa watendaji wa kimahakama na uwezo wao wa kitaaluma, bali pia unawapa nguvu wale wote ambao wamehusika katika kuudhoofisha mfumo wetu wa utoaji haki kwa kuwapa hoja kwamba Mahakama ya Tanzania haina uwezo wa kusimamia fedha zake. Mfano mzuri wa hatari hii ni Taarifa yenyewe ya Kikosi Kazi cha Ofisi ya Rais. Baada ya madai kwamba ofisi ya Msajili wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania “... haina wataalamu wa fani nyingine zaidi ya wanasheria ambao kazi yao ya msingi ni kwenda mahakamani ...” na kwamba wanasheria hawafundishwi utawala wa fedha wawapo chuoni “... lakini hivi sasa kila mtu mahakamani anatamani awe msimamizi mkuu wa fedha ...”, Taarifa hiyo ilipendekeza kwamba “... muundo wa uongozi wa mahakama urekebishwe kiasi kwamba kuwepo na kada mbili, ya utawala na ile ya wanasheria. Kada ya sheria ishughulikie maswala ya kuendesha kesi mahakamani na kada ya uongozi wa mahakama ihusike na mambo yote ya utawala ikiwemo kusimamia miradi ya maendeleo ya mahakama.” Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba haikuwa bahati tu kwamba mwezi mmoja baada ya Kikosi Kazi cha Ofisi ya Rais kuwasilisha Taarifa yake serikalini, Muswada wa Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama uliletwa Bungeni chini ya Hati ya Dharura na kupitishwa kuwa sheria baada ya siku mbili za mjadala! Nimeshaeleza madhara ya Sheria hii kwa uhuru wa Mahakama ya Tanzania kutenda haki bila hila, woga au upendeleo. Taarifa ya Kikosi Kazi cha Ofisi ya Rais ilikuwa ni Farasi wa Troy (Trojan Horse) katika vita ya Urais wa Kifalme dhidi ya Mahakama ya Tanzania.

MCHAKATO WA KATIBA MPYA


Mheshimiwa Spika, Tarehe 11 Machi 2011, Serikali ilichapisha Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Katiba ya mwaka 2011 (The Constitutional Review Bill, 2011) katika Gazeti la Serikali la tarehe hiyo. Muswada huo uliletwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge hili tukufu kwa Hati ya Dharura. Hata hivyo, baada ya upinzani mkubwa dhidi ya Muswada huo kujitokeza karibu nchi nzima, Serikali ililazimika kuundoa katika ratiba ya shughuli za Bunge kwa maelezo kwamba itaufanyia marekebisho na kuurudisha Bungeni katika Mkutano huu wa Bunge. Hata hivyo, licha ya Muswada huo kuwepo katika ratiba ya awali ya shughuli za Bunge, baadae ratiba hiyo ilifanyiwa mabadiliko kwa kuuondoa Muswada kwenye ratiba hiyo.

Mheshimiwa Spika, Dana dana yote hii inaonyesha jinsi suala la utaratibu wa namna ya kupata Katiba mpya kwa ajili ya nchi yetu lilivyo muhimu. Tofauti na kauli za awali za Serikali, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba sheria inayoweka utaratibu wa kupatikana kwa Katiba mpya ina umuhimu mkubwa wa karibu sawa na Katiba yenyewe. Utaratibu wa kidemokrasia, shirikishi wa makundi makuu ya kijamii na ulio wazi utapelekea nchi yetu kuwa na Katiba mpya ambayo sisi wote tutaweza kujivunia. Kwa upande mwingine, utaratibu uliojaa ukiritimba wa kirasimu, unaohodhiwa na watu au taasisi chache na unaofanyika gizani na/au kwa siri utaleta Katiba mpya kwa jina tu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba katika hali ya sasa ya kisiasa ya nchi yetu, utaratibu huu hauwezi kukubalika na wananchi walio wengi na utasababisha machafuko makubwa ya kisiasa na kijamii.

Kwa bahati mbaya, Mheshimiwa Spika, Serikali inaelekea kufikiri kwamba inaweza kuwalazimisha Watanzania kukubali utaratibu wa aina hiyo. Hii ni kwa sababu Kambi Rasmi ya Upinzani imepata nakala ya Rasimu ya Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Katiba, 2011 iliyofanyiwa marekebisho ambayo inatazamiwa kuletwa Bungeni kwa tarehe ambayo haijulikani bado. Rasimu ya Muswada huu inathibitisha kwamba Serikali haina nia yoyote ya kuweka utaratibu wa kidemokrasia, ulio shirikishi wa makundi makuu ya kijamii na kisiasa katika kupata Katiba Mpya. Kwa upande mwingine, Rasimu inapendekeza utaratibu wa kupata Katiba Mpya uliojaa urasimu na unaoendeleza hodhi ya Urais wa Kifalme ambayo ndiyo imekuwa hulka kuu ya mfumo wetu wa kikatiba na kisiasa.

Mheshimiwa Spika, Rasimu ya Muswada inapendekeza kumpa mamlaka makubwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa mashauriano na/au makubaliano na Rais wa Zanzibar ya kuteua Tume ya Kupitia Katiba yenye wajumbe wasiozidi thelathini. Aidha, Rasimu ya Muswada inapendekeza kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa mashauriano na/au makubaliano na Rais wa Zanzibar ataipatia Tume hiyo hadidu za rejea na muda wa kumaliza kazi yake na kuwasilisha taarifa. Utaratibu huo huo wa mashauriano na makubaliano utatumika katika uteuzi wa Katibu wa Tume; na Sekretariati ya Tume ambayo itateuliwa na Waziri wa Katiba na Sheria kwa makubaliano na Waziri mwenzake wa Zanzibar. Katibu na wajumbe wa Sekretariati wanatakiwa kuwa watumishi wa umma ambao, hata kwa mujibu wa utaratibu wa sasa wa kikatiba, wanawajibika kwa Rais.

Mheshimiwa Spika, Rasimu ya Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Katiba inaendeleza pia mfumo wa Urais wa Kifalme kwa mapendekezo juu ya uwasilishaji wa taarifa ya Tume. Hapa inapendekezwa kwamba Tume ya Mapitio ya Katiba itawasilisha taarifa yake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar. Aidha, “baada ya mashauriano na makubaliano na Rais wa Zanzibar na baada ya kumalizika kwa taratibu za ndani zinazohusu utungaji wa sera, Rais atamwelekeza Waziri kuwasilisha Muswada wa Katiba katika Bunge la Katiba kwa ajili ya kupitishwa kwa vifungu vya Katiba.” Pendekezo hili ni la hatari kubwa. Kwanza, ‘kumalizika kwa taratibu za ndani zinazohusu utungaji wa sera’ maana yake ni kwamba mpaka Baraza la Mawaziri liridhie Muswada huo ndio utapelekwa kwenye Bunge la Katiba! Kwa mujibu wa Katiba, wajumbe wote wa Baraza la Mawaziri ni wateuliwa wa Rais.

Mheshimiwa Spika, Mfumo wa Urais wa Kifalme pia unaonekana katika mapendekezo yanayohusu Baraza la Katiba. Kwa mujibu wa kifungu cha 20 cha Rasimu ya Muswada, Rais – kwa makubaliano na Rais wa Zanzibar – na baada ya kushauriwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na yule wa Zanzibar ataunda Baraza la Katiba na kuteua wajumbe wake. Baada ya kuundwa, Baraza la Katiba litateua Spika na Naibu Spika ambao watatakiwa kutoka katika sehemu tofauti za Jamhuri ya Muungano. Spika na Naibu Spika watatakiwa kula kiapo mbele ya Makatibu wa Baraza la Katiba ambao ni Katibu wa Bunge wa sasa na Katibu wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar wa sasa. Wote hawa, kwa mujibu wa Katiba na Katiba ya Zanzibar ya 1984, ni wateuliwa wa Rais na/au wa Rais wa Zanzibar na wanatakiwa kula kiapo kwa Rais!

Mheshimiwa Spika, Rasimu ya Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Katiba inapendekeza kwamba kazi ya Baraza la Katiba iwe moja tu: kutunga Katiba Mpya na mambo yanayohusiana nayo. Baada ya kufanya kazi hiyo, Baraza litakuwa limejifuta lenyewe, ijapokuwa kujifuta huko kwa Baraza hakutamzuia Rais kuliunda upya Baraza siku za baadae likiwa na wajumbe wale wale kwa lengo la kufanya mabadiliko ya Rasimu ya Katiba Mpya kabla Rasimu hiyo haijapitishwa! Rasimu inapendekeza kwamba ili Katiba Mpya ipitishwe ni lazima ipate ridhaa ya theluthi mbili ya wajumbe wote wanaotoka Tanzania Bara na idadi hiyo hiyo ya wajumbe wanaotoka Tanzania Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, Rasimu ya Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Katiba inapendekeza pia kwamba Katiba Mpya ipatiwe nguvu na uhalali wa kisheria kwa kupitia kura ya maoni itakayoratibiwa na kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Tume hizi mbili – kwa mashauriano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar - ndizo zitakazotengeneza swali litakaloulizwa kwenye kura ya maoni. Utaratibu utakaotumika katika kura ya maoni ni ule unaotumika katika chaguzi za kawaida katika nchi yetu, yaani Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sura ya 343, Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292 na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, 1984. Ijapokuwa kura ya maoni itaamuliwa kwa wingi wa wapiga kura (simple majority), Rasimu ya Muswada inapendekeza kwamba ili kura hiyo iwe halali ni lazima angalau 65% ya wapiga kura wote waliojiandikisha Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar washiriki katika kupiga kura. Rasimu ya Muswada inapendekeza kwamba Rais ndiye atakayeamua, kwa namna atakavyoona inafaa, kuanza kutumika kwa Katiba Mpya!

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi kama Rasimu ya Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Katiba ndio inawakilisha msimamo wa Serikali juu ya mchakato wa kutungwa kwa Katiba Mpya. Kama ni hivyo, basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuweka wazi msimamo wake Muswada huu haukubaliki hata kidogo. Kwanza, Kambi Rasmi ya Upinzani haikubaliani na mamlaka makubwa yanayopendekezwa kupewa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar chini ya Muswada huu. Urais wa Kifalme kama kanuni kuu ya kikatiba na kisiasa ndiyo ambayo imetufikisha hapa tulipo leo: taifa lenye wananchi maskini, lililojaa ufisadi, lisilojali demokrasia na haki za binadamu na lenye kuongozwa na watawala wasiowajibika kwa wananchi au kwa vyombo vya uwakilishi vya wananchi. Mfumo huu hauwezi kutumika tena kulipatia taifa letu Katiba Mpya ya kidemokrasia itakayokidhi mahitaji ya karne hii na nyingine zijazo.

Pili, Mheshimiwa Spika, mapendekezo ya Rasimu ya Muswada hayakubaliki kwa sababu yanaweka mchakato wa Katiba Mpya kwenye huruma na/au fadhila ya Rais wa Zanzibar na siasa za Zanzibar kwa ujumla. Kwa mapendekezo haya, Rais wa Zanzibar asipokubaliana na jambo lolote linalohitaji ridhaa yake basi mchakato mzima utasimama au kusitishwa. Aidha, endapo katika kura ya maoni inayopendekezwa, theluthi mbili ya Wazanzibari hawatakubaliana na Katiba Mpya basi Katiba hiyo haitapitishwa hata kama inakubaliwa kwa kiasi kikubwa na wananchi wa Tanzania Bara. Mustakbala wa taifa letu hauwezi kuwekwa tena rehani kwenye siasa za Zanzibar na kwenye matakwa ya Wazanzibari kwa kiasi hicho. Kuhusiana na jambo hili, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba Rais wa Zanzibar ahusishwe tu katika masuala ya kikatiba ambayo ni ya Muungano tu. Nje ya masuala hayo, Rais wa Zanzibar hana sababu yoyote ya kuhusishwa na mchakato wa kikatiba unaohusu mambo ya Tanzania Bara.

Aidha, wajumbe wa Tume ya Mapitio ya Katiba ambao watatoka Zanzibar wahusike tu katika mchakato wa masuala ya kikatiba ambayo ni ya Muungano tu. Vile vile, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza wananchi wa Zanzibar washiriki katika kura ya maoni inayohusu mfumo mpya wa Muungano tu. Hii ndio kusema kwamba, kama vile ambavyo viongozi, wawakilishi na wananchi wa Tanzania Bara hawajashirikishwa katika mchakato wa kikatiba wa Zanzibar kwa sababu ulihusu mambo yasiyokuwa ya Muungano, vivyo hivyo viongozi, wawakilishi na wananchi wa Zanzibar wasishiriki katika mchakato wa kikatiba wa mambo yasiyokuwa ya kikatiba kwa upande wa Tanzania Bara.

Mheshimiwa Spika, Kwa kuzingatia historia halisi ya Muungano wetu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba wakati umefika kwa wananchi wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kuamua - kwa mara ya kwanza katika historia yetu na kwa uhuru kabisa - kama wanataka kuendelea kuwa na Muungano na wa aina gani. Hili halijawahi kufanyika na ndio maana Muungano umeendelea kuwa kero kwa wananchi wengi wa nchi hizi mbili. Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kwamba suala la ridhaa ya wananchi ni la umuhimu mkubwa na ni lazima lishughulikiwe kwanza kabla ya mchakato unaopendekezwa na Rasimu ya Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Katiba kuanza na/au kupitishwa.

Aidha, kwa kuzingatia historia yetu halisi ya kikatiba na kisiasa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza mfumo mpya wa kutunga Katiba Mpya ambao hautatawaliwa na kivuli kirefu cha Urais wa Kifalme. Kikubwa hapa ni kwamba, badala ya wajumbe wa Tume ya Katiba kuteuliwa na Rais kama inavyopendekezwa na Rasimu ya Muswada, wajumbe hao wateuliwe kutokana na mapendekezo ya vyama vya siasa, hasa hasa vile ambavyo vina uwakilishi Bungeni, taasisi zisizokuwa za kiserikali na za kitaaluma, makundi maalum ya kijamii pamoja na Serikali yenyewe. Aidha, badala ya Sekretariati ya Tume kujazwa warasimu wa Serikali ambao ni wateuliwa wa Rais kama inavyopendekezwa, Sekretariati hiyo itokane na wajumbe watakaoteuliwa na Tume yenyewe na ambao watawajibika moja kwa moja kwa Tume yenyewe badala ya kuwajibika kwa Rais kama ilivyo sasa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina imani, sio tu na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, bali pia na mfumo mzima wa kisheria na kitaasisi unaoendesha chaguzi za nchi yetu. Mfumo huu na watendaji wake wameonyesha wazi kutokuwa huru na kutumiwa na Chama cha Mapinduzi kuchakachua matokeo ya chaguzi mbali mbali hapa nchini. Kwa maana hiyo, Tume ya Uchaguzi ya Taifa, na ile ya Zanzibar, haiwezi kuachiwa jukumu kubwa la kuendesha kura ya maoni kwa ajili ya kupata Katiba Mpya. Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba Serikali ilete bungeni muswada wa mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba na ya sheria husika za uchaguzi kwa lengo la kuiunda upya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa lengo la kuhakikisha inasimamia zoezi la kura ya maoni kwa uhuru na bila upendeleo kwa chama tawala. Muswada huu vile vile utatoa fursa kwa Bunge hili tukufu kutunga vifungu vinavyowezesha Katiba Mpya kutungwa ambavyo havipo kwa Katiba ya sasa. Kutofanya marekebisho haya kutafanya sheria yoyote ya kuweka utaratibu wa kupata Katiba Mpya kuwa batili kwa kwenda kinyume na matakwa ya Katiba ya sasa ambayo hairuhusu Katiba Mpya kutungwa ila inaruhusu tu marekebisho ya Katiba yenyewe.

UENDESHAJI WA MASHTAKA YA JINAI

Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya uendeshaji wa mashtaka ya jinai imekasimiwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa mujibu wa ibara ya 59B(2) ya Katiba. Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 59B(4), katika kutekeleza mamlaka yake, “Mkurugenzi wa Mashtaka atakuwa huru, hataingiliwa na mtu yeyote au na mamlaka yeyote na atazingatia ... nia ya kutenda haki, kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za utoaji haki na maslahi ya umma.” Kanuni hii kuu imetamkwa pia na kifungu cha 8 cha Sheria ya Utumishi wa Mashtaka ya Taifa, Na. 27 ya 2008 (National Prosecutions Service Act, 2008) ambayo pia imefafanua na kutilia nguvu mamlaka haya ya kikatiba. Kwa mujibu wa Sheria hii, Mkurugenzi wa Mashtaka ana mamlaka sio tu ya kudhibiti mashtaka yote ya jinai bali pia kuratibu shughuli za upelelezi wa makosa ya jinai [kifungu cha 16(1)]. Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 17(1) na (3), Mkurugenzi ana uwezo wa kutoa maelekezo ya maandishi kwa ofisa yeyote wa umma ili apatiwe taarifa yoyote inayohusu upelelezi au uendeshaji wa mashtaka ya jinai na ofisa huyo anatakiwa kutii maelekezo hayo.

Mheshimiwa Spika, Ili kumwezesha Mkurugenzi wa Mashtaka kutekeleza wajibu wake wa kikatiba kwa uhuru kamili na bila woga au upendeleo, Mkurugenzi wa Mashtaka amewekewa kinga ya ajira yake. Kwa mujibu wa kifungu cha 19(1) na (2) cha Sheria ya Utumishi wa Mashtaka ya Taifa, sifa, masharti na mafao ya ajira ya Mkurugenzi wa Mashtaka yatakuwa sawa na yale ya ajira ya Jaji wa Mahakama Kuu. Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 19(3), Mkurugenzi wa Mashtaka hawezi kuondolewa kwenye madaraka yake isipokuwa kwa kushindwa kutimiza wajibu wake kwa sababu ya ugonjwa au kwa kukiuka Kanuni za Maadili ya Kitaaluma ya Maafisa wa Sheria, Mawakili wa Serikali na Wanasheria Walioko kwenye Utumishi wa Umma chini ya Sheria ya Utekelezaji wa Mamlaka ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura ya 268 ya Sheria za Tanzania. Hii ndio kusema kwamba, kwa mujibu wa Sheria Na. 27 ya 2008, utaratibu wa kumwondoa Mkurugenzi wa Mashtaka kwenye ajira yake hauna tofauti na utaratibu wa kumwondoa Jaji wa Mahakama Kuu kwenye ajira yake.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba utaratibu huu wa kikatiba na kisheria umempa Mkurugenzi wa Mashtaka nyenzo za kutosha kisheria za kupambana na uhalifu mkubwa hapa nchini na vile vile kuzuia matumizi mabaya ya mfumo wa uendeshaji na utoaji haki na hasa hasa ya mfumo wa mashtaka ya jinai. Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashangazwa na kusikitishwa na kushindwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kufungua na/au kuendesha mashtaka yanayohusu matukio makubwa ya ufisadi ambayo yametikisa taifa letu Serikali ya Awamu ya Nne ilipoingia madarakani miaka sita iliyopita.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua uwepo mahakamani wa kesi kadhaa za ufisadi zinazowahusu aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara wa zamani Basil Mramba na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Gray Mgonja na maafisa kadhaa wa ngazi za kati wa Benki Kuu ya Tanzania. Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haiamini kwamba hawa ndio wahusika pekee wa matukio yote ya ufisadi ambao umelitia taifa letu hasara kubwa. Hii ni kwa sababu tangu mwaka 2007, ushahidi wa kutosha unaowaunganisha viongozi na maafisa waandamizi wa Serikali ya Awamu ya Tatu na wa Awamu ya Nne na maswahiba wao wa kibiashara umetolewa hadharani mara baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) – akisaidiwa na mimi mwenyewe – kusoma Orodha ya Mafisadi (The List of Shame) katika Mkutano wa Hadhara wa Mwembe Yanga, Temeke, Dar es Salaam tarehe 18 Septemba 2007.

Mheshimiwa Spika, Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ushahidi wa maandishi uliotajwa katika Orodha ya Ufisadi na nyaraka nyingine zinazohusiana na Orodha hiyo zinaonyesha kuhusika kwa viongozi wa ngazi za juu kabisa serikali katika kashfa`kubwa za Meremeta Ltd., Tangold Ltd., Deep Green Finance Ltd., Kagoda Agricultural Co. Ltd., Kiwira Coal Mine, Radar ya BAE Systems, Richmond, Dowans na nyinginezo nyingi. Kushindwa kuwachukulia hatua stahiki wahusika hawa, pamoja na kutupiana mpira kati ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kunathibitisha sio mapungufu ya kisheria bali mapungufu ya uwezo wa kiutendaji kama sio wa kimaadili.

Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2010 /2011 Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ilishughulikia kesi kubwa za rushwa zipatazo ishirini na tisa ambazo zilihusisha thamani ya fedha ya shilingi bilioni 288. Kati ya kesi hizo, kesi za wizi wa fedha za Benki Kuu ya Tanzania (EPA) zilikuwa na thamani ya shilingi bilioni 37, uhujumu uchumi shilingi bilioni 12, kuisababishia serikali hasara shilingi bilioni 225, kusafisha fedha haramu shilingi bilioni 10 na wizi wa kutumia silaha shilingi bilioni 4.1. Kwa kuzingatia hata Rais Kikwete mwenyewe alishawahi kukiri kwamba fedha za EPA zilizoibiwa zilikuwa jumla ya shilingi bilioni 133, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutamka Bungeni ni kwa nini Mkurugenzi wa Mashtaka hajaona busara ya kuwashtaki wezi wa mabilioni yaliyobaki ya EPA hadi sasa.

Mheshimiwa Spika, Kwa sababu ya mapungufu hayo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa tamko rasmi kwa Bunge hili tukufu kama huu sio muda muafaka kwa Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kumshauri Rais kuunda Mahakama Maalum -kwa mujibu wa kifungu cha 19(4) cha Sheria ya Utumishi wa Mashtaka ya Taifa - kwa lengo la kuchunguza suala la kumwondoa madarakani Mkurugenzi wa Mashtaka kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kikatiba na kisheria. Aidha, kwa vile ajira ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU haina kinga za kisheria ilizo nazo ajira ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa tasmi kwa nini hadi sasa Rais hajaona busara ya kutumia mamlaka yake chini ya ibara ya 36(1) na (2) ya Katiba kufuta uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake kisheria.

UBAMBIKIZAJI RAIA KESI ZA UONGO

Mheshimiwa Spika, Kama nilivyoonyesha mwanzoni, Mkurugenzi wa Mashtaka ana jukumu kikatiba na kisheria kuzuia matumizi mabaya ya utaratibu wa utoaji haki. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasikitishwa na kushindwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kuzuia matumizi mabaya ya utaratibu wa utoaji haki ambayo yamekithiri ndani ya Jeshi la Polisi kwa askari polisi kukamata na kufungulia wananchi kesi za uongo zinazohusu tuhuma za makosa makubwa ya jinai ambayo hayana dhamana kisheria. Kwa mujibu wa Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa mwaka 2002/03 iliyochapishwa mwezi Mei 2005, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) iligundua kwamba malalamiko mengi iliyoyapokea kuhusu Jeshi la Polisi “... yaligusia polisi kubambikizia raia kesi....” Taarifa hiyo inathibitisha kwamba msongamano wa mahabusu katika magereza yetu kulingana na idadi ya wafungwa ni ishara ya “... kushindwa kwa mfumo wa dhamana chini ya Sheria ya Mwenendo wa Jinai, Sura ya 20 ya Sheria

Mheshimiwa Spika,Naomba kutumia mfano wa kesi kubwa alizofunguliwa Diwani wa Kata ya Bumera katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kwa mwaka 2005-2010, Mheshimiwa Tengera Marwa. Mwaka 2008 Mheshimiwa Marwa alizushiwa tuhuma ya mauaji na kufunguliwa kesi ya mauaji PI Na. 11 ya 2008 katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime. Sambamba na kesi hiyo ya mauaji, Mheshimiwa Marwa pia alizushiwa kesi ya ujambazi wa kutumia silaha na kufunguliwa Kesi ya Jinai Na. 469 ya 2008 katika Mahakama hiyo hiyo. Baada ya kuteseka gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja kwa sababu kesi zote mbili hazina dhamana kisheria, Mkurugenzi wa Mashtaka - kwa kutumia mamlaka yake ya nolle prosequi - alimfutia Mheshimiwa Marwa mashtaka yote mawili na hivyo akaachiliwa huru.

Mheshimiwa Spika,Baada ya Mheshimiwa Tengera Marwa kuchukua fomu za uchaguzi ili aweze kutetea kiti chake cha Diwani wa Kata ya Bumera wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2010, tarehe 5 Agosti 2010 alikamatwa tena na kufunguliwa kesi ya jinai ujambazi wa kutumia silaha Na. 255 ya 2010 katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime. Mwezi Septemba 2010, kesi hiyo nayo ilifutwa kwa nolle prosequi ya Mkurugenzi wa Mashtaka. Hata hivyo, Mheshimiwa Marwa hakuachiwa nafasi ya kuwa huru kwa muda mrefu kwani muda mfupi kabla ya Uchaguzi Mkuu, alikamatwa tena na kufunguliwa kesi nyingine ya mauaji yenye PI Na. 39 ya 2010. Sambamba na kesi hiyo ya mauaji, pia alifunguliwa kesi tena ya ujambazi ya kutumia silaha Na. 465 ya 2010. Kesi ya mauaji PI Na. 39/2010 ilifutwa kwa mara nyingine tena kwa nolle prosequi ya Mkurugenzi wa Mashtaka iliyotolewa mapema mwaka huu.

Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, matumizi mabaya ya mfumo wa utoaji haki dhidi ya Mheshimiwa Tengera Marwa hayakwisha kwani tarehe 5 Mei 2011 alifunguliwa kesi nyingine ya mauaji yenye PI Na. 21 ya 2011 na kwa hiyo ameendelea kuteseka kwenye Gereza la Rumande la Wilaya ya Tarime. Katika kipindi hicho, Mheshimiwa Marwa amefunguliwa kesi tatu za mauaji na tatu ujambazi wa kutumia silaha. Katika kipindi hicho hicho, Mheshimiwa Marwa amefutiwa kesi za mauaji mara mbili na kesi za ujambazi wa kutumia silaha mara mbili. Kesi mbili zilizobaki zinaonyesha Mkurugenzi wa Mashtaka ameishiwa nguvu kwa sababu ya nolle prosequi zake zote kupuuzwa na uongozi wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime na Rorya.

Mheshimiwa Spika, Matumizi mabaya ya mfumo wa uendeshaji na utoaji haki ya namna hii ni makosa ya jinai kwa mujibu wa kifungu cha 102 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania; na adhabu yake ni kifungo cha miaka saba kwa mujibu wa kifungu cha 104 cha Sheria hiyo. Pamoja na ukweli huo, Mkurugenzi wa Mashtaka hajachukua hatua zozote za kisheria dhidi ya maafisa husika wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime na Rorya. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi Bungeni kama ni sera ya Serikali kwa Jeshi la Polisi kupuuza mamlaka ya kikatiba na kisheria ya Mkurugenzi wa Mashtaka pale mamlaka hayo yanapokuwa tofauti na maslahi au matakwa ya Jeshi la Polisi au watendaji wake.

Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe tamko ni kwa nini hadi sasa Mkurugenzi wa Mashtaka hajachukua hatua zozote za kisheria kuwafungulia mashtaka ya jinai ya matumizi mabaya ya utaratibu wa uendeshaji na utoaji haki watendaji wote wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime na Rorya kwa kuendelea kumtesa gerezani Mheshimiwa Diwani Tengera Marwa licha ya nolle prosequi kadhaa za Mkurugenzi wa Mashtaka. Vile vile Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe kauli kama, kutokana na matukio kama haya ya matumizi mabaya ya utaratibu wa uendeshaji na utoaji haki, huu sio wakati muafaka kwa Serikali kuleta muswada wa mabadiliko ya sheria mbali mbali za jinai ili kufuta vifungu vinavyozuia watuhumiwa wa makosa makubwa ya jinai kupatiwa dhamana na hivyo kuondoa kabisa uwezekano wa Jeshi la Polisi la kukiuka haki za binadamu kwa kutumia sheria.

HAKI ZA BINADAMU

Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Tatu ya Sura ya Kwanza ya Katiba inahusu haki za binadamu na wajibu muhimu. Kwa mujibu wa ibara ya 30(3) ya Katiba, jukumu la kuhifadhi na kulinda haki na wajibu muhimu zilizotolewa na Katiba ni wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Ili Mahakama Kuu itimize wajibu wake huo, mwaka 1994 Bunge hili tukufu lilitunga – kwa mujibu wa ibara ya 30(4) – Sheria ya Utekelezaji wa Haki na Wajibu wa Binadamu, Sura ya 3 ya Sheria za Tanzania. Kifungu cha 15 cha Sheria hiyo kinamtaka Jaji Mkuu – baada ya mashauriano na Waziri - kutunga kanuni zitakazoweka utaratibu wa namna ya kufungua na kuendesha kesi zinazohusu ukiukwaji wa haki na wajibu wa binadamu. Hadi leo hii hakuna Jaji Mkuu hata mmoja ambaye ametunga kanuni hizo, miaka 17 baada ya kutungwa kwa Sheria yenyewe. Matokeo yake ni kwamba watu wengi wameshindwa kufungua mashauri yanayohusu haki na wajibu wa binadamu kwa kukosekana utaratibu wa kikanuni uliofikiriwa na kifungu cha 15 cha Sheria hiyo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli bungeni ni kitu gani kimekwamisha utungwaji wa kanuni husika cha kifungu hicho.

Mheshimiwa Spika, Pengine kizingiti kikubwa zaidi kwa utekelezaji wa haki na wajibu muhimu wa binadamu zilizotolewa na Katiba imekuwa ni masharti ya kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki na Wajibu wa Binadamu kinacholazimu Mahakama Kuu kuwa na majaji watatu wakati wa kusikiliza kesi hizo. Katika mazingira halisi ya Mahakama Kuu ya nchi yetu yenye uhaba mkubwa wa majaji, imekuwa na vigumu kwa majaji watatu kupatikana kwa wakati mmoja ili kusikiliza na kuamua kesi zinazohusu haki za binadamu. Matokeo yake ni kwamba kesi nyingi zinakaa muda mrefu mahakamani hadi wadaawa wanakata tama na kuziachia. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri Serikali iandae muswada wa marekebisho ya Sheria hiyo ili kurudisha utaratibu wa zamani wa kesi za haki za binadamu kusikilizwa na Jaji mmoja. Hii itarahisisha wadaawa kwenda mahakamani kudai haki zao za msingi na Mahakama Kuu kuyafanyia maamuzi maombi ya wadaawa hao kwa wakati muafaka.

Mheshimiwa Spika, Matatizo mengine yanayohusu utekelezaji wa haki za binadamu yanasababishwa na Mahakama ya Tanzania yenyewe na hasa hasa majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani ya Tanzania. Tofauti na ilivyokuwa miaka ya mwanzo ya utekelezaji wa haki za binadamu ambayo ilishuhudia kesi nyingi zikiamuliwa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani, kuanzia miaka ya katikati ya tisini na kuendelea mahakama zetu za juu zimeingiwa na hofu ya kufanya maamuzi yanayohusu haki na wajibu wa msingi kama zilivyoainishwa na Katiba. Badala yake, mahakama zetu za juu zimekuwa mabingwa wa kujificha katika vichaka cha masharti ya kiufundi na mara nyingi kesi zenye masuala ya msingi na muhimu kisheria zimetupiliwa mbali kwa sababu tu ya kuwepo makosa ya kiufundi ya kisheria wakati zinafunguliwa.

Mheshimiwa Spika, Hofu hii ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani inashangaza na kusikitisha sana kwa sababu inakwenda kinyume moja kwa moja na matakwa ya ibara ya 107A(2)(e) ya Katiba inayoitaka Mahakama “... kutenda haki bila kufungwa kupita kiasi na masharti ya kiufundi yanayoweza kukwamisha haki kutendeka.” Aidha, kama nilivyoonyesha mwanzoni, ibara ya 107B ya Katiba inazipa uhuru mahakama zote katika utekelezaji wao wa mamlaka ya utoaji haki. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba moja ya sababu zinazofanya Mahakama ya Tanzania kudharaulika na kupuuzwa na wananchi na watendaji wa Serikali ni pamoja na kuabudu huku kwa masharti ya kiufundi hasa hasa yanapoonekana kwamba yatakwamisha haki kutendeka!

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA


Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya haki za binadamu na wajibu kwa jamii zilizoainishwa na Katiba vile vile zimewekewa utaratibu mwingine wa kikatiba na kisheria. Sehemu ya Kwanza ya Sura ya Sita ya Katiba inaunda Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) na kuipa majukumu na mamlaka ya kuyatekeleza majukumu hayo. Kwa mujibu wa ibara ya 130(1) ya Katiba majukumu ya CHRAGG ni pamoja na kuhamasisha hifadhi ya haki za binadamu na wajibu kwa jamii; kupokea malalamiko ya uvunjaji wa haki za binadamu na kuyachunguza; na, kama itabidi, kufungua mashauri mahakamani ili kuzuia uvunjaji wa haki za binadamu.

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa ibara ya 129(2) na (3) ya Katiba, CHRAGG inaundwa na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Makamishna wengine wasiozidi watano na Makamishna Wasaidizi, ambao wote wanateuliwa na Rais baada ya mashauriano na Kamati ya Uteuzi. Na kwa mujibu wa ibara ya 129(5), ukomo wa kushikilia nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Makamishna wote ni vipindi viwili vya miaka mitatu mitatu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina taarifa kwamba, kwa sababu ya ukomo huo wa kikatiba, CHRAGG kwa sasa haina Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wala Makamishna kwa sababu waliokuwepo walishafikisha ukomo wa ofisi zao na Rais hajateua wengine wapya. Kama taarifa hizi ni za kweli basi inatoa ujumbe mbaya sana kwa wananchi kwamba masuala ya haki za binadamu na wajibu muhimu kwa jamii sio kipaumbele cha Serikali. Dhana hii inatiliwa nguvu na ukweli kwamba katika mwaka huu wa fedha, jumla ya shilingi 824,918,000 ambazo ni fedha zote za maendeleo zilizotengwa kwa CHRAGG ni fedha za kutoka nje. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuthibitisha ukweli wa taarifa hizi na kulieleza taifa ni kwa nini hali hii imeruhusiwa itokee.

MWISHO
Mheshimiwa Spika, Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wajumbe wote wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni chini ya uongozi wa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Mheshimiwa Freeman A. Mbowe kwa ushauri na ushirikiano uliowezesha maandalizi ya maoni haya. Aidha, niwashukuru familia yangu – mke wangu mpenzi Alicia Bosensera na mapacha wetu Agostino Lissu na Edward Bulali – kwa kuendelea kuvumilia upweke unaotokana na ‘Daddy’ kuwa mbali muda mwingi kwa sababu ya majukumu mazito ya kibunge. Aidha, niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Singida Mashariki kwa imani na nguvu wanayonipa kila siku kwa kuendeleza msimamo wetu thabiti wa kukataa kunyanyaswa, kunyonywa na kupuuzwa na ‘Ndaa ya Njou’! Mwisho naomba nichukue fursa hii kuwashukuru viongozi, wanachama na wapenzi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wananchi wote wa Tanzania ambao wameendelea kutuunga mkono na kututia nguvu katika kipindi hiki muhimu katika historia ya nchi yetu. Ninawaomba waendelee kutuunga mkono na kututia nguvu katika siku ngumu na za majaribu makubwa zinazokuja!

Mheshimiwa Spika, Baada ya maelezo haya marefu, naomba kukushukuru na wewe binafsi na naomba kuwasilisha.
---------------------------------------------------------------
Tundu Antiphas Mughwai Lissu
MSEMAJI & WAZIRI KIVULI, SHERIA, KATIBA NA UTAWALA
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
Agosti 24, 2011
 
Its a disgrace to have a historic structure like the Court of Appeals building be demolished to make way for a parking lot for a luxury hotel, what kind of a gvt. would even consider an idea like that? & What does it say about the intention of this gvt. when they are ready to destroy RULE of LAW for a parking lot for a lux hotel. Where are their priorities? Actually, this intent symbolizes this gvt. mindset, to them RULE of LAW, JUSTICE simply needs to be destroyed for the sake of a parking lot for a lux hotel.
This thought explains why the most expensive case in Dar's history is still languishing in the DAR HC today, after the Corut of Appeals years ago determined the case, but it still in the courts today, why? Because its a special project of few TZ officials &their friends. Again, RULE of LAW subverted so that billing & invoicing can go on at the BOT. Money flows ouT! & NO one cares to stop this daylite robbery! Just like NO one cares to stop the destruction of JUSTICE to make way for lux hotel parking lot!!
 
Hivi kwanini mtu kama Tundu Lissu asiwe waziri wa katiba na sheria hata kama yupo upinzani???? Hapa tunachoangalia ni maslahi ya taifa na si maslahi ya mafisadi, maana atawafunga wengi sana sio kama yule mama kombani aliesema eti serikali haina pesa kwa ajili ya mchakato wa katiba mpya..
<br />
<br />
kaka kasungura ni kadogo.
 
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikalikutoa kauli rasmi kama Rasimu ya Muswada waSheria ya Mapitio ya Katiba ndio inawakilisha msimamo wa Serikali juu yamchakato wa kutungwa kwa Katiba Mpya. Kama nihivyo, basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuweka wazi msimamo wakeMuswada huu haukubaliki hata kidogo. Kwanza, Kambi Rasmi ya Upinzani haikubalianina mamlaka makubwa yanayopendekezwa kupewa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Raiswa Zanzibarchini ya Muswada huu. Urais wa Kifalme kamakanuni kuu ya kikatiba na kisiasa ndiyo ambayo imetufikisha hapa tulipo leo:taifa lenye wananchi maskini, lililojaa ufisadi, lisilojali demokrasia na hakiza binadamu na lenye kuongozwa na watawala wasiowajibika kwa wananchi au kwavyombo vya uwakilishi vya wananchi. Mfumo huu hauwezi kutumika tena kulipatiataifa letu Katiba Mpya ya kidemokrasia itakayokidhi mahitaji ya karne hii nanyingine zijazo.

Pili, mapendekezo ya Rasimu ya Muswada hayakubalikikwa sababu yanaweka mchakato wa Katiba Mpya kwenye huruma na/au fadhila ya Raiswa
Zanzibar na siasa za Zanzibar kwa ujumla. Kwa mapendekezo haya,Rais wa Zanzibarasipokubaliana na jambo lolote linalohitaji ridhaa yake basi mchakato mzimautasimama au kusitishwa. Aidha, endapo katika kura ya maoni inayopendekezwa,theluthi mbili ya Wazanzibari hawatakubaliana na Katiba Mpya basi Katiba hiyohaitapitishwa hata kama inakubaliwa kwa kiasikikubwa na wananchi wa Tanzania Bara. Mustakbala wa taifa letu hauwezi kuwekwa tenarehani kwenye siasa za Zanzibarna kwenye matakwa ya Wazanzibari kwa kiasi hicho. Kuhusiana na jambo hili,Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba Rais wa Zanzibar ahusishwe tu katika masuala yakikatiba ambayo ni ya Muungano tu. Nje ya masuala hayo, Rais wa Zanzibar hana sababuyoyote ya kuhusishwa na mchakato wa kikatiba unaohusu mambo ya Tanzania Bara.Aidha, wajumbe wa Tume ya Mapitio ya Katiba ambaowatatoka Zanzibarwahusike tu katika mchakato wa masuala ya kikatiba ambayo ni ya Muungano tu.Vile vile, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza wananchi wa Zanzibar washiriki katikakura ya maoni inayohusu mfumo mpya wa Muungano tu. Hii ndio kusema kwamba, kamavile ambavyo viongozi, wawakilishi na wananchi wa Tanzania Barahawajashirikishwa katika mchakato wa kikatiba wa Zanzibar kwa sababu ulihusumambo yasiyokuwa ya Muungano, vivyo hivyo viongozi, wawakilishi na wananchi waZanzibar wasishiriki katika mchakato wa kikatiba wa mambo yasiyokuwa yakikatiba kwa upande wa Tanzania Bara.

Huu ndio ukweli tunaotaka badala ya kuzoeleka na lugha ya kwamba tupo kwenye mchakacho wa kutafuta ufumbuzi miaka nenda rudi.
 
[h=2]
icon1.png
"Seven Blunders of the World CHADEMA"[/h]



1.
Wealth without work = Lema

2. Pleasure without conscience = Sugu

3. Knowledge without character = Lisu

4.
Commerce without morality= Mbowe

5.
Science without humanity = Mdee
 
Back
Top Bottom