Tundu Lissu aunguruma Bungeni! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tundu Lissu aunguruma Bungeni!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mpaka Kieleweke, Aug 24, 2011.

 1. Mpaka Kieleweke

  Mpaka Kieleweke JF-Expert Member

  #1
  Aug 24, 2011
  Joined: Feb 27, 2007
  Messages: 4,137
  Likes Received: 67
  Trophy Points: 145
  Hapa nawapa baadhi ya dondoo za hotuba yake ambayo itawekwa hapa jamvini baadae kidogo.

  URAIS WA KIFALME NA UHURU WA MAHAKAMA
  Mheshimiwa Spika,

  Kwa muda wote wa uhai wetu kama taifa huru, mfumo wetu wa kikatiba na wa kisiasa umejengwa juu ya nguzo moja kuu ambayo mwanazuoni wa Kenya, Profesa H.W. Okoth-Ogendo, aliwahi kuiita Urais wa Kifalme (Imperial Presidency). Hii inatokana na ukweli kwamba katika mfumo huu, Rais ana madaraka makubwa sana sio tu ya kiutendaji bali pia ya kiutungaji sheria kwa vile, kwa mujibu wa ibara 62(1) ya Katiba, Rais ni sehemu ya Bunge. Vile vile Rais ana kivuli kirefu cha kikatiba katika utekelezaji wa masuala mbali mbali ya kimahakama kwa kutumia mamlaka makubwa aliyonayo katika uteuzi wa viongozi wote wa ngazi za juu za Mahakama. Kwa mfano, chini ya mfumo wetu, Rais anamteua Jaji Kiongozi na majaji wote wa Mahakama Kuu ya Tanzania [ibara ya 109(1) ya Katiba]; na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania [ibara ya 118(2) na (3)].

  Mheshimiwa Spika,
  Ni kweli kwamba Rais anatekeleza wajibu wake kikatiba wa kuteua majaji kwa mashauriano na Tume ya Utumishi wa Mahakama [ibara ya 109(1) na 113(1)] na Jaji Mkuu [ibara ya 118(3) ya Katiba]. Hata hivyo, ni muhimu kutambua na kusisitiza ufinyu wa mamlaka ya ushauri kwa mujibu wa Katiba yetu. Hii ni kwa sababu chini ya ibara ya 37(1) ya Katiba, "... Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote, isipokuwa tu pale anapotakiwa na Katiba hii au na sheria nyingine yoyote kufanya jambo lolote kulingana na ushauri anaopewa na mtu au mamlaka yoyote."

  Vile vile, kwa mujibu wa ibara ya 112(2) ya Katiba, wajumbe wote wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ni wateuliwa wa Rais na, kwa sababu hiyo, Rais anashauriwa na watu aliowateua yeye mwenyewe na ambao halazimiki kufuata ushauri wao! Katika mazingira haya ya kikatiba, ni rahisi kwa Rais kuteua watu kuwa majaji au viongozi wa juu wa Mahakama ya Tanzania kutokana na vigezo vingine nje ya utaalamu au uzoefu wao wa kitaaluma. Aidha, katika mazingira haya, ni rahisi kwa wateuliwa wa Rais kuamini kwamba wameteuliwa kwenye nafasi kwa nasaba zao na ukaribu wao na Rais au watu wake wa karibu na kwa hiyo wanajiona wana deni la kulipa fadhila kwa Rais kwa kufanya maamuzi yatakayompendeza yeye au Serikali yake. Mfumo huu wa kikatiba unajenga mazingira ya wateuliwa wa Rais kujipendekeza kwake au kwa Serikali yake (sycophancy) ambayo matokeo yake ni uendeshaji na utoaji haki uliojaa woga au upendeleo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba mazingira haya ya kikatiba yanatishia moja kwa moja uhuru wa Mahakama ya Tanzania na hayana budi kuangaliwa upya katika mjadala wa kikatiba unaoendelea sasa hivi.

  Mheshimiwa Spika,
  Badala ya madaraka ya Urais wa Kifalme juu ya Mahakama ya Tanzania kupunguzwa ili kuwe na uwiano bora zaidi wa mgawanyo wa madaraka kati ya Serikali na Mahakama ili kulinda uhuru wa Mahakama, Sheria ya Uendeshaji Mahakama, 2011 iliyotungwa na Bunge hili tukufu katika Mkutano wake wa Tatu, imemwongezea Rais madaraka makubwa zaidi katika uendeshaji wa Mahakama. Kwa mujibu wa kifungu cha 7(1) cha Sheria hiyo, Rais ndiye atakayemteua Mtawala Mkuu wa Mahakama; na ndiye anayeamua masharti ya ajira ya Mtawala Mkuu wa Mahakama [kifungu cha 7(6)].

  Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 9, mamlaka ya nidhamu juu ya Mtawala Mkuu wa Mahakama ni Rais. Sheria hii vile vile inampa Rais hata mamlaka ya kuanzisha au kuvunja nafasi za kimahakama na zisizokuwa za kimahakama baada ya kushauriwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama [kifungu cha 21(1)].

  Kama ambavyo nilipata kusema wakati natoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni juu ya Muswada wa Sheria hiyo, kifungu hiki kinakwenda kinyume na matakwa ya ibara ya 36(1) ya Katiba inayompa Rais mamlaka ya kuanzisha au kufuta ofisi za utumishi wa umma "... bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii na sheria nyingine yoyote...." Nafasi za kimahakama kama za majaji na mahakimu zimewekwa ama na Katiba yenyewe au na sheria nyinginezo na kwa hiyo Rais hana mamlaka ya kuzianzisha au kuzifuta!

  Mheshimiwa Spika,
  Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama vile vile inatishia uhuru wa mahakama kwa kuruhusu wanasiasa na watendaji wa Serikali kusimamia nidhamu za watumishi wa kimahakama. Kwa mfano, chini ya kifungu cha 50(5), Kamati za Maadili ya Watumishi wa Kimahakama za Mikoa zimepewa wajibu wa kushughulikia nidhamu za Mahakimu wa Wilaya na Mahakimu Wakazi wa mikoa husika. Kamati hizi zinaoongozwa na Wakuu wa Mikoa ambao pia wanateua wajumbe wengine wawili kati ya wajumbe sita wa Kamati [kifungu cha 50(1)]. Na kama ambavyo nimepata kusema wakati nilipowasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni juu ya Muswada wa Sheria hii, utaratibu huu unahatarisha uhuru wa mahakama kwa sababu Wakuu wa Mikoa "... wana tabia ya kuingilia utendaji wa mahakama zetu na mara nyingi ni wakiukaji wa sheria na taratibu za nchi yetu. Mara nyingi Mahakama ni vyombo pekee katika mikoa vyenye mamlaka kisheria ya kuwadhibiti pale wanapokiuka miiko ya kisheria ya kazi zao."

  Mheshimiwa Spika
  ,
  Kivuli hiki kirefu cha Urais wa Kifalme katika uongozi na utekelezaji wa mamlaka ya utoaji haki wa Mahakama ni tishio kwa uhuru wa mahakama na utekelezaji wa majukumu yake. Licha ya viapo vyao vya kutenda haki bila hila, woga au upendeleo, wateuliwa wa nafasi mbali mbali za uongozi au utendaji wa Mahakama wana uwezekano mkubwa wa kujiona wanawajibika kwa mamlaka yao ya uteuzi, yaani Rais. Aidha, watendaji wa Mahakama ambao wanawajibika kinidhamu kwa mamlaka zinazoongozwa na watendaji wa Serikali na makada wa chama tawala kama Wakuu wa Mikoa wanakuwa na woga wa kushughulikia kesi zinazowahusu watendaji na makada hao na/au Serikali wanayoiwakilisha. Dalili za woga huu ni nyingi na zitazidi kuongezeka kwa sababu ya Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama. Tayari tumeanza kusikia taarifa za baadhi ya Wakuu wa Mikoa kuwafuata mahakimu ili kuulizia mwelekeo wa kesi zinazohusu wanachama au viongozi wa vyama vya upinzani hasa hasa CHADEMA. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kwamba huu ni muda mwafaka, sambamba na mjadala wa mfumo mpya wa kikatiba, kuyashughulikia masuala haya ili Mahakama ya Tanzania iondokane na kivuli kirefu cha Urais wa Kifalme na kuiwezesha kuwa huru kutenda haki kwa mujibu wa viapo vya watendaji wa Mahakama ya Tanzania.

  Mheshimiwa Spika,
  Wakati Serikali imeridhia jengo la mahakama ya juu kabisa katika mfumo wetu wa kimahakama na wa kikatiba libomolewe ili wageni wa Kempinski Kilimanjaro Hotel wapate maegesho ya magari yao, Serikali imetenga shilingi sifuri kwa ajili ya Fungu 40 kasma 6313 inayohusu ukarabati wa Mahakama ya Rufaa! Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi Bungeni kama taarifa za kuuzwa kwa Jengo la Mahakama ya Rufani ya Tanzania na mipango ya kulibomoa ili eneo lake ligeuzwe kuwa maegesho ya magari ni za kweli. Na kama ni za kweli, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iliambie taifa Mahakama ya Rufani ya Tanzania itahamishiwa wapi ili kupisha wageni wa Kempinski Kilimanjaro Hotel kuegesha magari yao!

  Aidha, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuachana na mpango huo wa aibu mara moja kwa sababu unarudisha nyuma mafanikio yote yaliyopatikana kwa Mahakama ya Rufani ya Tanzania kuwa na jengo lake yenyewe na hivyo kupunguza mrundikano wa majaji, mawakili, watumishi wa mahakama na wadau wa kesi ambao umekuwepo kwa miaka mingi katika jengo la Masjala Kuu ya Mahakama Kuu ya Tanzania. Ni Serikali ya aina gani hii inayobomoa majengo ya mhimili mkuu wa dola kama mahakama ili kutafuta nafasi ya watu wanaoenda kujiburudisha hotelini kuegesha magari! Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ituepushie fedheha na aibu hii kwa nchi yetu.

  UBAMBIKIZAJI RAIA KESI ZA UONGO
  Mheshimiwa Spika,
  Kama nilivyoonyesha mwanzoni, Mkurugenzi wa Mashtaka ana jukumu kikatiba na kisheria kuzuia matumizi mabaya ya utaratibu wa utoaji haki. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasikitishwa na kushindwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kuzuia matumizi mabaya ya utaratibu wa utoaji haki ambayo yamekithiri ndani ya Jeshi la Polisi kwa askari polisi kukamata na kufungulia wananchi kesi za uongo zinazohusu tuhuma za makosa makubwa ya jinai ambayo hayana dhamana kisheria. Kwa mujibu wa Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa mwaka 2002/03 iliyochapishwa mwezi Mei 2005, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) iligundua kwamba malalamiko mengi iliyoyapokea kuhusu Jeshi la Polisi "... yaligusia polisi kubambikizia raia kesi...." Taarifa hiyo inathibitisha kwamba msongamano wa mahabusu katika magereza yetu kulingana na idadi ya wafungwa ni ishara ya "... kushindwa kwa mfumo wa dhamana chini ya Sheria ya Mwenendo wa Jinai, Sura ya 20 ya Sheria."

  Mheshimiwa Spika,
  Naomba kutumia mfano wa kesi kubwa alizofunguliwa Diwani wa Kata ya Bumera katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kwa mwaka 2005-2010, Mheshimiwa Tengera Marwa. Mwaka 2008 Mheshimiwa Marwa alizushiwa tuhuma ya mauaji na kufunguliwa kesi ya mauaji PI Na. 11 ya 2008 katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime. Sambamba na kesi hiyo ya mauaji, Mheshimiwa Marwa pia alizushiwa kesi ya ujambazi wa kutumia silaha na kufunguliwa Kesi ya Jinai Na. 469 ya 2008 katika Mahakama hiyo hiyo. Baada ya kuteseka gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja kwa sababu kesi zote mbili hazina dhamana kisheria, Mkurugenzi wa Mashtaka - kwa kutumia mamlaka yake ya nolle prosequi - alimfutia Mheshimiwa Marwa mashtaka yote mawili na hivyo akaachiliwa huru.

  Mheshimiwa Spika,
  Baada ya Mheshimiwa Tengera Marwa kuchukua fomu za uchaguzi ili aweze kutetea kiti chake cha Diwani wa Kata ya Bumera wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2010, tarehe 5 Agosti 2010 alikamatwa tena na kufunguliwa kesi ya jinai ujambazi wa kutumia silaha Na. 255 ya 2010 katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime. Mwezi Septemba 2010, kesi hiyo nayo ilifutwa kwa nolle prosequi ya Mkurugenzi wa Mashtaka. Hata hivyo, Mheshimiwa Marwa hakuachiwa nafasi ya kuwa huru kwa muda mrefu kwani muda mfupi kabla ya Uchaguzi Mkuu, alikamatwa tena na kufunguliwa kesi nyingine ya mauaji yenye PI Na. 39 ya 2010. Sambamba na kesi hiyo ya mauaji, pia alifunguliwa kesi tena ya ujambazi ya kutumia silaha Na. 465 ya 2010. Kesi ya mauaji PI Na. 39/2010 ilifutwa kwa mara nyingine tena kwa nolle prosequi ya Mkurugenzi wa Mashtaka iliyotolewa mapema mwaka huu.

  Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, matumizi mabaya ya mfumo wa utoaji haki dhidi ya Mheshimiwa Tengera Marwa hayakwisha kwani tarehe 5 Mei 2011 alifunguliwa kesi nyingine ya mauaji yenye PI Na. 21 ya 2011 na kwa hiyo ameendelea kuteseka kwenye Gereza la Rumande la Wilaya ya Tarime. Katika kipindi hicho, Mheshimiwa Marwa amefunguliwa kesi tatu za mauaji na tatu ujambazi wa kutumia silaha. Katika kipindi hicho hicho, Mheshimiwa Marwa amefutiwa kesi za mauaji mara mbili na kesi za ujambazi wa kutumia silaha mara mbili. Kesi mbili zilizobaki zinaonyesha Mkurugenzi wa Mashtaka ameishiwa nguvu kwa sababu ya nolle prosequi zake zote kupuuzwa na uongozi wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime na Rorya.

  Mheshimiwa Spika
  ,
  Matumizi mabaya ya mfumo wa uendeshaji na utoaji haki ya namna hii ni makosa ya jinai kwa mujibu wa kifungu cha 102 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania; na adhabu yake ni kifungo cha miaka saba kwa mujibu wa kifungu cha 104 cha Sheria hiyo. Pamoja na ukweli huo, Mkurugenzi wa Mashtaka hajachukua hatua zozote za kisheria dhidi ya maafisa husika wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime na Rorya. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi Bungeni kama ni sera ya Serikali kwa Jeshi la Polisi kupuuza mamlaka ya kikatiba na kisheria ya Mkurugenzi wa Mashtaka pale mamlaka hayo yanapokuwa tofauti na maslahi au matakwa ya Jeshi la Polisi au watendaji wake.

  Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe tamko ni kwa nini hadi sasa Mkurugenzi wa Mashtaka hajachukua hatua zozote za kisheria kuwafungulia mashtaka ya jinai ya matumizi mabaya ya utaratibu wa uendeshaji na utoaji haki watendaji wote wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime na Rorya kwa kuendelea kumtesa gerezani Mheshimiwa Diwani Tengera Marwa licha ya nolle prosequi kadhaa za Mkurugenzi wa Mashtaka. Vile vile Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe kauli kama, kutokana na matukio kama haya ya matumizi mabaya ya utaratibu wa uendeshaji na utoaji haki, huu sio wakati muafaka kwa Serikali kuleta muswada wa mabadiliko ya sheria mbali mbali za jinai ili kufuta vifungu vinavyozuia watuhumiwa wa makosa makubwa ya jinai kupatiwa dhamana na hivyo kuondoa kabisa uwezekano wa Jeshi la Polisi la kukiuka haki za binadamu kwa kutumia sheria.


   
 2. M

  Malunde-Malundi JF-Expert Member

  #2
  Aug 24, 2011
  Joined: Jan 10, 2008
  Messages: 1,287
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Ni ktk kipindi kipi mkuu naomba kuelewa
   
 3. Saint Ivuga

  Saint Ivuga JF-Expert Member

  #3
  Aug 24, 2011
  Joined: Aug 21, 2008
  Messages: 39,471
  Likes Received: 19,861
  Trophy Points: 280
  stay tuned guys
   
 4. U

  Uwezo Tunao JF-Expert Member

  #4
  Aug 24, 2011
  Joined: Nov 14, 2010
  Messages: 6,947
  Likes Received: 12
  Trophy Points: 0
  Eee jaama tukakahabarishane kwa wakati juu ya kinachojiri Mjengoni jamani maana mpaka hapa mmefanya kututia tu hamasa kuu!!!!!!!!!!!!

   
 5. The Emils

  The Emils JF-Expert Member

  #5
  Aug 24, 2011
  Joined: Apr 16, 2011
  Messages: 570
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Hivi kwanini mtu kama Tundu Lissu asiwe waziri wa katiba na sheria hata kama yupo upinzani???? Hapa tunachoangalia ni maslahi ya taifa na si maslahi ya mafisadi, maana atawafunga wengi sana sio kama yule mama kombani aliesema eti serikali haina pesa kwa ajili ya mchakato wa katiba mpya..
   
 6. Dr wa ukweli

  Dr wa ukweli JF-Expert Member

  #6
  Aug 24, 2011
  Joined: Feb 28, 2011
  Messages: 892
  Likes Received: 27
  Trophy Points: 45
  Points, lakini watapuuza kama kawaida yao!
   
 7. Barubaru

  Barubaru JF-Expert Member

  #7
  Aug 24, 2011
  Joined: Apr 6, 2009
  Messages: 7,162
  Likes Received: 29
  Trophy Points: 0
  Mambo mazito hayo. Alafu mnasema Tanzania inafuata Rules of Law.

  Poleni sana
   
 8. Mpaka Kieleweke

  Mpaka Kieleweke JF-Expert Member

  #8
  Aug 24, 2011
  Joined: Feb 27, 2007
  Messages: 4,137
  Likes Received: 67
  Trophy Points: 145
  Hotuba yake itasomwa leo jioni majira ya saa kumi na moja , yapo mengi makubwa zaidi , hii nchi ni kama vile inaendeshwa na sysytem ya autopilot
   
 9. Dr wa ukweli

  Dr wa ukweli JF-Expert Member

  #9
  Aug 24, 2011
  Joined: Feb 28, 2011
  Messages: 892
  Likes Received: 27
  Trophy Points: 45
  Mgao kwetu ni 36hrs kalaptop kangu ndio kanazima, jairo karudi kazini, ndio twafa kijumla
   
 10. AMARIDONG

  AMARIDONG JF-Expert Member

  #10
  Aug 24, 2011
  Joined: Jun 24, 2010
  Messages: 2,506
  Likes Received: 48
  Trophy Points: 0
  kazi ni kwao
   
 11. REBEL

  REBEL Senior Member

  #11
  Aug 24, 2011
  Joined: Dec 15, 2010
  Messages: 164
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 35
  tundu lissu yuko vizuri.magamba watakoma mwaka huu.mimi ni ccm lakini natamani tu nirudishe kadi sema nikimuwaza nyerere nangojea kidogo.lakini inshort mibunge ya ccm na nape ni kero na janga la taifa,
   
 12. ERIC JOSEPH

  ERIC JOSEPH JF-Expert Member

  #12
  Aug 24, 2011
  Joined: Aug 10, 2011
  Messages: 570
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Jamaa hawa hawasikii mana mana masikio yao yamewekewa pamba ila tutapaza sauti kwa nguvu mpaka watasikia
   
 13. S

  SEAL Team 6 JF-Expert Member

  #13
  Aug 24, 2011
  Joined: Jun 10, 2011
  Messages: 655
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Ole wao wakileta porojo za kuzuia maandamano, tunaandamana.
   
 14. Felixonfellix

  Felixonfellix JF-Expert Member

  #14
  Aug 24, 2011
  Joined: Feb 16, 2010
  Messages: 1,680
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 135
  mhh haya ngoja tusubiri
   
 15. Jituoriginal

  Jituoriginal JF-Expert Member

  #15
  Aug 24, 2011
  Joined: Feb 8, 2010
  Messages: 362
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 35
  Tindu lisu alitakiwa kuwa attorney general,badala ya ule mwizi wa n'gombe .
   
 16. Mlachake

  Mlachake JF-Expert Member

  #16
  Aug 24, 2011
  Joined: Oct 13, 2009
  Messages: 2,923
  Likes Received: 631
  Trophy Points: 280
  Kuna jamaa alisema kuliko Tindu Lisu aingie Bungeni Bora yeye aukose Urais. Nimeanza kuamini maneno yake. huyu jamaa kweli ni changa moto.
   
 17. kikahe

  kikahe JF-Expert Member

  #17
  Aug 24, 2011
  Joined: May 23, 2009
  Messages: 1,273
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  Nchi ina udhalimu sana. Mungu aisaidie sana tanzania maana bila haki taifa litaangamia
   
 18. Mpaka Kieleweke

  Mpaka Kieleweke JF-Expert Member

  #18
  Aug 24, 2011
  Joined: Feb 27, 2007
  Messages: 4,137
  Likes Received: 67
  Trophy Points: 145
  Mheshimiwa Spika,Hali ya miundo mbinu ya mahakama zetu ni ya kusikitisha na haisameheki kwa upande wa Serikali ambayo ndio yenye udhibiti wa hazina ya umma. Kwa mfano, wakati Serikali imejenga majengo mapya ya Ofisi za Wakuu wa Mikoa yote na Wilaya zote na Wizara mbali mbali katika kipindi cha miaka hamsini ya uhuru wetu, Kanda nane kati ya kumi na tatu za Mahakama Kuu ya Tanzania zimeendelea kutumia majengo yaliyorithiwa kutoka dola ya kikoloni. Kanda nne kati ya tano zilizobaki na Divisheni tatu za Mahakama Kuu, yaani Divisheni ya Biashara, ya Kazi na ya Ardhi zinatumia majengo yaliyoazimwa au kuchukuliwa kutoka taasisi nyingine za umma! Ni Kanda moja tu za Mahakama Kuu ya Tanzania – Kanda ya Bukoba – ambayo imejengewa jengo jipya ya Mahakama katika kipindi cha miaka hamsini ya utaifa wetu. Na hata hilo moja halijakamilika hadi leo!
  Mheshimiwa Spika, Kwa karibu miaka thelathini tangu kuanzishwa kwake, Mahakama ya Rufani ya Tanzania ilikuwa ikichangia jengo moja na Masjala Kuu ya Mahakama Kuu, Dar es Salaam. Mwaka 2004, ukarabati wa jengo la iliyokuwa Hoteli ya Forodhani wa kulifanya kuwa Makao Makuu ya Mahakama ya Rufani ya Tanzania ulianza. Ukarabati huo ulikamilika na jengo kuanza kutumika mwaka 2006. Hata hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa kwamba Serikali imeamua sasa kuliuza Jengo hilo kwa wawekezaji wapya wa iliyokuwa Kempinski Kilimanjaro Hotel ili libomolewe na eneo lake ligeuzwe kuwa maegesho ya magari ya wageni wa hoteli hiyo! Kwa hatua hii, Mahakama Rufani ya Tanzania itatakiwa ikapangishiwe tena mahali pengine pa kufanyia kazi zake za utoaji haki.
  Mheshimiwa Spika, Wakati Serikali imeridhia jengo la mahakama ya juu kabisa katika mfumo wetu wa kimahakama na wa kikatiba libomolewe ili wageni wa Kempinski Kilimanjaro Hotel wapate maegesho ya magari yao, Serikali imetenga shilingi sifuri kwa ajili ya Fungu 40 kasma 6313 inayohusu ukarabati wa Mahakama ya Rufaa! Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi Bungeni kama taarifa za kuuzwa kwa Jengo la Mahakama ya Rufani ya Tanzania na mipango ya kulibomoa ili eneo lake ligeuzwe kuwa maegesho ya magari ni za kweli. Na kama ni za kweli, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iliambie taifa Mahakama ya Rufani ya Tanzania itahamishiwa wapi ili kupisha wageni wa Kempinski Kilimanjaro Hotel kuegesha magari yao!
  Aidha, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuachana na mpango huo wa aibu mara moja kwa sababu unarudisha nyuma mafanikio yote yaliyopatikana kwa Mahakama ya Rufani ya Tanzania kuwa na jengo lake yenyewe na hivyo kupunguza mrundikano wa majaji, mawakili, watumishi wa mahakama na wadau wa kesi ambao umekuwepo kwa miaka mingi katika jengo la Masjala Kuu ya Mahakama Kuu ya Tanzania. Ni Serikali ya aina gani hii inayobomoa majengo ya mhimili mkuu wa dola kama mahakama ili kutafuta nafasi ya watu wanaoenda kujiburudisha hotelini kuegesha magari! Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ituepushie fedheha na aibu hii kwa nchi yetu.
   
 19. Elli

  Elli JF-Expert Member

  #19
  Aug 24, 2011
  Joined: Mar 17, 2008
  Messages: 26,828
  Likes Received: 10,140
  Trophy Points: 280
  mmmmh makubwa tena haya, naomba achomeke na lile la mheshimiwa jaji Mkuu Mstaafu Augustine kuondlewa walinzi nyumbani kwake siku moja baada ya kustaafu kama ailivyolisema yeye mwenyewe dodoma juzi...
   
 20. G

  Giddy Mangi JF-Expert Member

  #20
  Aug 24, 2011
  Joined: Feb 14, 2011
  Messages: 833
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 0
  Lissu Tindu MB Mh naomba speed yenu iwe kubwa zaidi kwani tutakapokata Tamaa hakuna wa kuturudisha nyuma kamwe.Watanzania tumechoka sana.
   
Loading...