Tundu Lissu asimulia alikofichwa baada ya kukamatwa

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ametegua kitendawili cha nini kilimpata baada ya kukamatwa Septemba 10, 2023 huku Polisi wakimtaka kuripoti baada ya mwezi mmoja.

Lissu, walinzi wake na baadhi ya viongozi wa chama hicho walikamatwa Septemba 11, 2023 katika mji wa Karatu kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko isivyo halali na kuzuia polisi kufanya kazi yao.

Kufutia kukamatwa huko, viongozi na wapenzi wa chama hicho walikumbwa na sintofahamu baada ya kufuatilia kituo cha kikuu Jijini Arusha walikoelezwa kuwa kapelekwa lakini hawakumkuta.

Lakini saa mbili usiku, aliachiwa kwa dhamana kutoka kituo cha Polisi.

Akisimulia mkasa mzima jana, Lissu alidai kuwa Polisi walikwenda kumhifadhi kituo cha Polisi Monduli, kabla ya kumhamishia kituo cha kikuu.

Wakati huo akiwa kituo cha Polisi Monduli, viongozi, wanachama na wafuasi wa chama hicho, wakihusisha kitengo cha Intelijensia walianza kumsaka Lissu na wakati huo huo wakitumia mitandao ya kijamii kueleza kila hatua wanayopitia.

Moja ya ujumbe uliosambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii hususan Whatsapp ni ule uliotumwa saa 11:40 alasiri na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Elisa Mungure, ukieleza kuwa gari la Lissu lilionekana eneo la Magereza.

“Taarifa za kuonekana magari ya Lissu eneo la Magereza uwanja mdogo wa ndege wa Arusha jioni. Wana Arusha twendeni hapo sasa,” ulisomeka ujumbe huo ambao ulifanya kitengo cha inteligensia cha Chadema kwenda katika eneo hilo.

Wanaintelijensia hao walifanikiwa kuliona gari la Lissu aina ya Toyota Prado nyeupe likielekea mjini na kulifuatilia huku wakirekodi video zake hadi lilipoingia kituo cha kikuu cha Polisi na baadaye Lissu na wenzake kuachiwa kwa dhamana.

Katika mkutano wake wa jana, mwanasiasa huyo aliwatambulisha washirika waliokamatwa naye kuwa ni David Jumbe (msaidizi wake), John Kanonyele (dereva), Frank Kagoma na Esau Bwire, ambao wote ni wa safu ya ulinzi.



Lissu alivyopelekwa Monduli





Akizungumza na waandishi wa habari usiku juzi nyumbani kwa kaka yake, wakili Aluthe Mughway baada ya kuachiwa, Lissu alisema awali polisi walimweleza wanampeleka kituo kikuu Arusha, lakini akashangaa anapelekwa Monduli.

“Mimi na wenzangu watano tulikamatwa mapema leo (juzi) hotelini Karatu kwenye hoteli ya Ngorongoro Coffee Lounge. Sasa wakati tunapata chai ya asubuhi tukawa tumevamiwa na kundi kubwa la maaskari wakiongozwa na OCD. Walituvamia wakatukamata tukaingizwa kwenye magari na mimi niliwekwa kwenye gari la peke yangu na tukasafrishwa kutoka Karatu mimi nikalipelekwa Monduli. Mwanzoni tukiwa njiani walisema wanatupeleka Arusha.

“Tulipofika njiapanda ya Monduli wakakata kushoto kuelekea Monduli. Nikawauliza nyie maafande si mliniambia tunakwenda Arusha hii ya Monduli ni ya nini wakasema aah!! mheshimiwa ni maagizo yamebadilika tukiwa njiani. Tukaenda Monduli. Kwa hiyo nimekaa katika kituo cha Polisi Monduli mchana wote mpaka jioni ya saa 12 waliponichukua na kunileta Arusha mjini kwa ajili ya kunipatia dhamana na huko niliwakuta wenzangu wameshaletwa,” alisema Lissu.

Katika mkutano huo, Lissu alisema makosa ya kuwepo kwenye mkusanyiko bila kibali anayoshitakiwa nayo ni ya kisiasa, akidai ni makosa yanayotengenezwa na watu waliokosa hoja na kwamba alitakiwa kuripoti polisi hiyo jana.

Lissu alisema kitendo cha Jeshi la Polisi kuwasakama na kesi za aina hiyo ni kinyume kabisa na matarajio yao kwa kuwa badala ya kuwapunguzia nguvu ndio imewaongezea nguvu na imewaongezea umaarufu mara dufu.

“Nyerere (Julius-baba wa taifa) bila kesi ya uchochezi mwaka 1958 asingekuwa Nyerere. Jomo Kenyatta (wa Kenya) bila kukaa gerezani miaka saba asingekuwa Jomo Kenyatta ninayemfahamu na wengineo wengi,” alisema Lissu.



Kiini cha kukamatwa

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Justine Masejo juzi ilisema inamshikilia Lissu na viongozi wenzake watatu kwa ajili ya mahojiano kwa kufanya mkusanyiko isivyo halali na kuzuia polisi kufanya kazi yao.

“Baada ya mahojiano hayo na ukamilishwaji wa taratibu nyingine, hatua nyingine za kisheria zitafuata,” alisema Kamanda Masejo, lakini taarifa kutoka kwa viongozi mbalimbali wa Chadema Karatu na Arusha zilisema wanaoshikiliwa ni zaidi ya 15. Tafrani kati ya Lissu na Polisi ilianza Jumamosi iliyopita, baada ya polisi mjini Karatu kuuzuia msafara wake uliokuwa unakwenda ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro na wao kuamua kupinga hatua hivyo kufunga barabara.

Mmoja wa maofisa wa Polisi waliokuwa wamevalia kiraia alimsihi Lissu akubali waende pembeni kuzungumza, lakini inaelezwa baadaye Polisi walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya waliokuwa wamefuatana naye.

Kutokana na tafrani hiyo, waliamua kurudi katika hoteli na nyumba za kufikia wageni katika mji wa Karatu, lakini juzi asubuhi Lissu na walinzi wake walizingirwa na kukamatwa na Polisi, kashkash iliyowakuta pia viongozi wengine wa Chadema.

Wengine waliokamatwa ni Katibu mkuu taifa wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) Catherine Ruge, Suzan Kiwanga ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema na Twaha Mwaipaya, Katibu mwenezi wa Bavicha Taifa.

Polisi hawakuishia hapo, kwani inadaiwa waliwakamata viongozi na wanachama wengine waliokuwepo ofisi za Chadema Jimbo la Karatu juzi akiwemo Samwel Welwel ambaye ni mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Karatu.

Wengine waliokamatwa ni Joseph Mtui, John Malle, Fabiola Niima, Daniel Mnyampanda, Eliya Kibola ambaye ni Katibu wa Chadema Karatu na Valerian Qurama na Mzee Hashim, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema Taifa, Hashim Issa Juma.



Lissu, wenzake wahojiwa saa 4

Lissu na viongozi wengine wa Chadema waliokuwa wamekamatwa Karatu wamepewa dhamana jana huku yeye na walinzi wake wakihojiwa kwa saa nne jana katika Ofisi ya Mkuu wa upelelezi mkoa Arusha(RCO) na kupewa dhamana. Pia, ametakiwa kurejea Polisi Oktoba 10, 2023 huku viongozi wengine wa Chadema nao waliachiwa kwa dhamana na kutakiwa kurudi polisi Septemba 15, 2023.

Akizungumza na waandishi wa habari jana nje ya kituo cha kati Arusha baada ya kumaliza kuandika maelezo, Lissu alisema tuhuma alizokuwa akihojiwa ni kufanya mkusanyiko usio halali na kufunga barabara.

“Nimewaeleza sijafanya mkusanyiko na sikufunga barabara kwani waliofunga ni polisi wakati wanatuzuia kuendelea na safari ya Ngorongoro,” alidai Lissu.

Alidai kuwa baada ya Polisi kufunga barabara na kuona wanataka kupiga watu ndipo waliamua kukaa barabarani huku akikanusha kufunga barabara.

"Sisi kabla ya kwenda tulikuwa tayari na vibali 10 na tukaelezwa vibali vingine 17 vingetolewa Geti la kuingia Ngorongoro, lakini tukiwa njiani nje kidogo ya mji wa Karatu tulizuiwa na polisi," alisema Lissu.

Hata hivyo, alisema safari hii Jeshi la Polisi tangu lilipowakamata juzi jioni hawakuwafanyia kitu kibaya badala yake wamewahoji kistaarabu na hakulala mahabusi.

Alisema kukamatwa kwake na viongozi wengine hakutawazuia kurejea kufanya mikutano Ngorongoro na Karatu na kwamba, wanakwenda kujipanga kwa mikutano ya Kanda ya Kaskazini huku akisisitiza kuwa Ngorongoro sio gereza.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom