Burj Khalifa, ni alama na kivutio cha Dubai ambapo ni jengo refu zaidi duniani. Imebadilisha kabisa mandhari ya anga ya Dubai na linawakilisha maajabu ya uhandisi wa kisasa na ubunifu wa hali ya juu wa usanifu majengo.
Marekani na Israel
zilianzisha mashambulizi dhidi ya Iran, huku shambulio la kwanza likiripotiwa kutokea karibu na ofisi za Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei. Vyombo vya habari vya Iran viliripoti mashambulizi katika maeneo mbalimbali nchini humo, huku moshi ukionekana ukifuka kutoka katika mji mkuu, Tehran.
Vita hiyo imekuwa na athari katika maeneo mbalimbali mathalani Machi 16, 2026 tukio la moto ulizuka karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai
liliripotiwa, ukidaiwa kusababishwa na shambulio la drone lililoshukiwa kutoka Iran. Dubai ilithibitisha kwamba tanki la mafuta lililokuwa karibu na uwanja wa ndege lilishika moto, huku timu za Ulinzi wa Raia zikikimbilia eneo hilo kudhibiti moto huo.
Madai
Kumekuwapo na video inayosmbazwa mtandaoni ikionesha ndege mbili za kivita zinazokatiza pembezoni mwa jengo la Burj Khalifa lililopo Dubai zikidaiwa kurushwa na Iran kuelekea Israel.
Je, ni upi uhalisia wa video hiyo?
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck kwa kutumia nyenzo za kidigitali umejiridhisha kuwa video hiyo si halisi bali imetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya Akili Unde.
Kadhalika yapo mapungufu kadhaa ambayo yanaonesha utofauti wa video hiyo na eneo halisi. Mathalani kupitia picha za
Google Earth zinaonesha uhalisia wa eneo la Burj Khalifa ambalo halifanani na video hiyo, mfano majengo mengine yaliyo karibu na eneo hilo.
Sanjari na hilo nyenzo za kubaini maudhui yaliyotengenezwa kwa Akili Unde zinabainisha kuwa upo uwezekano wa zaidi ya asilimia 90 za video hiyo kutengenezwa kwa teknolojia hiyo.