Tuambiane ukweli, ofisi ya Mwendesha Mashitaka si huru | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tuambiane ukweli, ofisi ya Mwendesha Mashitaka si huru

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Nov 19, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Nov 19, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,688
  Likes Received: 82,540
  Trophy Points: 280
  Tuambiane ukweli, ofisi ya Mwendesha Mashitaka si huru

  Lula wa Ndali-Mwananzela Novemba 19, 2008
  Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

  KINYUME na madai ambayo tumeyasikia mara kwa mara siku za hivi karibuni, si kweli kuwa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka (DPP) iko huru. Mtu yeyote katika Tanzania anayeamini kuwa ofisi hiyo iko huru, mtu huyo anaweza kuamini pia kuwa mwezi umetengenezwa kwa siagi na ya kuwa juu yake kuna mwanamama aliyebeba mzigo wa kuni kama adhabu ya kufanya kazi Jumapili!

  Ofisi hii yawezekana ni huru kwenye vitabu vya sheria, lakini hadi leo hii haijajidhihirisha kuwa ni huru kiutendaji na katika uhalisia wake. Ninaposikia Rais anazungumza na kusema kuwa ofisi hii ni huru na ameielekeza ichukue hatua zote za kisheria dhidi ya watuhumiwa wa EPA, ninachokisikia ni kuwa ofisi hii si huru!

  Ninapomsikia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi akiwaeleza watu kuwa wasiwe na wasiwasi; kwani ofisi yake ni huru na imekuwa huru tangu kuundwa kwake, ninachokisikia ni kuwa ofisi hii siyo huru!

  Vinginevyo kama ingekuwa huru kusingekuwa na ulazima wa mtu yeyote kuwaambia wananchi kuwa "ofisi ni huru" isipokuwa kwa sababu si huru ndiyo sababu tunaambiwa hivyo!

  Kama mvua inanyesha huwezi kwenda kumshawishi mtu kuwa mvua inanyesha isipokuwa kama mtu huyo hayuko mahali ambapo anaweza kuiona na kuisikia mvua hiyo, au kwa sababu fulani hawezi kujua tofauti ya mvua na jua! Vinginevyo kuna vitu ambavyo mtu haitaji kuambiwa kuthibitisha kuwa kitu fulani kipo au hakipo.

  Kama ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ingekuwa huru, kusingekuwa na sababu ya wao kurudia rudia wimbo huu wa kutaka wananchi waamini kuwa wao ni huru. Lakini hilo peke yake halitoshi isipokuwa tukiangalia mambo yafuatayo tunaweza kuona kuwa kwa hakika ofisi hii si huru katika utendaji wake licha ya nguvu kubwa iliyo nayo.

  Kesi ya Rada: Kama ofisi yetu ya Mkurugenzi wa Mashtaka ingekuwa huru, tusingekaa kusubiri uchunguzi wa SFO (shirika la Uingereza la Uchunguzi wa Makosa ya Kifisadi) ufanyike ili na sisi tudandie.

  Mkurugenzi wetu wa Mashtaka angeanzisha uchunguzi wake yeye mwenyewe badala ya sisi kusubiri kusikia Waingereza wamegundua nini kuhusu suala la Rada. Kwa nini Watanzania tusikie kuwa Chenge ana tujisenti twake Uingereza kupitia shirika la Uingereza?

  Kwa nini Watanzania tusikie kuwa tumeingizwa mjini zaidi ya Shilingi bilioni 21 kutokana na ununuzi wa rada hii na hilo tulisikie toka nje na siyo vyombo vyetu vya ndani vya uchunguzi?

  Jibu ni kwamba, ni kwa sababu vyombo vyetu haviko huru; kwa sababu Mkurugenzi wa Mashtaka hayuko huru!

  Sakata la EPA: Hivi ni nani aliyechunguza EPA na kugundua wizi mkubwa ambao leo watu wanafikishwa mahakamani? Ni Mwendesha Mashtaka? Ni Mkurugenzi wa Upelelezi? La hasha! Ni makampuni mawili - kwanza ni Deloitte & Touche na baadae Ernst and Young.

  Hata uchunguzi wa kina Mwanyika haukuja na jambo lolote jipya ambalo wananchi walikuwa hawalijuia kabla. Sasa leo wanakuja na kutuambia kuwa wao ni "taasisi huru"! Wanatarajia na sisi tukubali tu kwa vile wamesema? Kama wangekuwa huru kwa nini wasichunguze zaidi ya mwaka 2005/2006 wa EPA?

  Leo hii huyu Mkurugenzi wa Mashitaka anapopeleka hawa jamaa mahakamani kutokana na mwaka huo, anajuaje kama kuna wengine waliiba kipindi cha 2004/2005 au 2003/2004? Hajachunguza vipindi hivyo, na hawezi kuchunguza kwa sababu hayuko huru!

  Kama kweli angekuwa huru angeingilia kati pale uchunguzi huu ulipoanza tu na kutaka kufanya uchunguzi wa kina badala ya kutegemea ripoti ya wakaguzi hawa; tena kwa mwaka mmoja tu.


  Asingeweza kufanya hivyo kwa sababu kufanya hivyo ni dalili ya kuwa huru, lakini kwa vile yeye si huru basi anafanya kile anachoruhusiwa kufanya.

  Zaidi ya yote kitendo cha Rais kuunda timu ya kuchunguza kitendo cha uhalifu ni ushahidi wa wazi kuwa wale walioapa kufanya kazi hiyo hawakuwa huru kuanzisha wao wenyewe na badala yake walihitaji msukumo kutoka Ikulu kuweza kufanya kitu ambacho kiko ndani ya nguvu zao.

  Hivi si ingekuwa mfano mzuri wa uhuru wa asasi hizo kama Bw. Mwanyika (Mwanasheria Mkuu) ndiye angeitisha wenzake na kuanza kazi mara moja ya kuchunguza EPA? Lakini asingeweza kufanya hivyo bila kuwasiliana na Ikulu kupata baraka zao!

  Kesi nyingine za BOT: Kama kweli Mkurugenzi wa Mashtaka ni taasisi huru mbona hadi leo hii hajaanzisha uchunguzi huru kuhusu Deep Green Finance, Mwananchi Gold, Buzwagi, Meremeta, Minara Miwili, Fedha Zilizokataliwa n.k?

  Katika nchi ambayo Mkurugenzi wake yuko huru kweli kweli, harufu ya ufisadi ulioko Benki Kuu yetu ingetosha kabisa kumfanya aunde timu maalum ya uchunguzi badala ya kusubiri Rais aiunde.

  Hebu fikiria suala la vijana waliokwama Ukraine ambapo walitelekezwa na Serikali ya Tanzania na vijana wale walidai kuwa kuna uvunjwaji wa haki zao. Mkurugenzi huru asingeweza kukaa pembeni na kuwaacha watoto wa Kitanzania wakiteseka kwenye baridi huko bila kufuatilia nini kimetokea ili kuweza kuona kama kuna mtu anastahili kufunguliwa mashtaka. Hakufanya hivyo kwa sababu hayuko huru!

  Hata leo hii japo wao wenyewe hawataki kulizungumzia ni wazi kuwa kuna njama ya ukimya ya kuficha na kutozungumzia vifo vya watoto 19 Tabora ambao walikufa katika mazingira ya kihalifu, uzembe na kutokuwajibika. Ripoti iliyotolewa imeonyesha wazi kuwa kosa la kihalifu lililosababisha vifo vya watoto wale siyo wale wachezesha disko tu bali watu wengi zaidi.

  Sasa kwenye nchi ambayo Mwendesha Mashtaka wake ni huru kweli kweli asingekaa pembeni bali yeye mwenyewe kuanzisha uchunguzi na kuingia ndani kufuatilia kila kitu ikiwemo kuwahoji Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Polisi (ndiyo anazo nguvu hizo kisheria).

  Lakini Mkugurenzi wetu sisi hajafikiria kuchunguza suala la vifo vya watoto hao, kwa sababu linagusa watu engi kweli na wengine wana urafiki wa karibu na wenye kuketi kwenye viti vya enzi! Ila nina uhakika akipigiwa simu mara moja toka kwenye ufalme wao mara moja angeanza kazi ya kufanyia uchunguzi tukio hilo.

  Lakini hadi sasa vifo vya watoto hao vimesahauliwa kwa makusudi na hakuna uchunguzi wowote huru utakaofanyika, na Mwendesha Mashtaka hana ubavu wa kuingilia kati hiyo kesi (ingawa anazo nguvu za kisheri).


  Nitoe mifano gani mingine ya kuonyesha kuwa taasisi hii siyo huru? Naweza kujaza vitabu.

  Hata hivyo, huko tunakokwenda Mwanasheria Mkuu na Mkurugenzi wa Mashtaka watalazimika kuonyesha (siyo kutuambia) kuwa wao ni taasisi huru kweli. Ni pale ambapo wao wenyewe wataanzisha uchunguzi wa mambo muhimu ya Taifa bila kusubiri baraka na kuwekewa mikono ya heri na Ikulu!

  Hadi siku hiyo itakapofika, mimi sasa hivi ninaangalia kile kinachoendelea kama mazingaombwe yaliyokithiri na kuchezea akili za Watanzania; kwani mwisho wake ni rahisi kuujua.

  Hawa ambao leo wamefikishwa mahakamani na hata wakija kukutwa na hatia ni kwa sababu moja tu nayo ni kuwa Ikulu wametoa baraka zao.

  Siku ambapo watu maarufu na wazito watafikishwa mahakamani au kuchukuliwa hatua za kisheria bila Mkuu wa Polisi kupigiwa simu, Mkuu wa Mkoa kuulizwa au kuuliza Ikulu wanasemaje, hiyo ndiyo siku vyombo vyetu kweli vitakuwa na uhuru wa kweli.

  Hadi hivi sasa ni chombo kimoja tu ambacho naamini kweli bado kimeendeleza rekodi yake ya uhuru. Nacho ni Mahakama ya Rufaa ya Tanzania. Ni wao wamekaa kati ya ubabe (tyranny) na demokrasia. Na tuombee na kujitahidi kuwaamsha ili waendelee kuwa hivyo.

  Niandikie: lulawanzela@yahoo.co.uk
   
 2. M

  Moelex23 JF-Expert Member

  #2
  Nov 19, 2008
  Joined: Oct 8, 2006
  Messages: 497
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 35
  Hapa mbona kama vile kuna kuchanganya mambo??

  Ofisi ya mwendesha mashtaka haihusiki kuchunguza wizi bali hiyo ni kazi ya Polisi na Takukuru (sp). Ofisi ya Feleshi kazi yake ni kupokea report za uchunguzi na kuangalia kama kuna sheria inaweza kutumika kupeleka charges mahakamani.

  I agree kuwa ofisi hii si Huru, but mwandishi katumia mifano ambayo inaweka analysis yake yote kuwa haina maana.
   
 3. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #3
  Nov 19, 2008
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  Inabidi usome sheria ya DPP uone nguvu zake; anaweza kuiagiza Polisi kufanya uchunguzi wowote ule..
   
 4. H

  Hofstede JF-Expert Member

  #4
  Nov 19, 2008
  Joined: Jul 15, 2007
  Messages: 3,584
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 0
  Hii si makala ya Mwanakijiji kwenye Raiamwema, Mzee Mkjj hebu tufafanulie maana nimesha connect dots
   
 5. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #5
  Nov 19, 2008
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  Hiyo ni makala ya "Lula" kwenye Rais Mwema...
   
 6. Mwawado

  Mwawado JF-Expert Member

  #6
  Nov 19, 2008
  Joined: Nov 2, 2006
  Messages: 998
  Likes Received: 28
  Trophy Points: 35
  Tusipoangalia tutarudi kulekule kwenye kuwabatiza majina watu...Huyu Mwandishi wa Raia Mwema anaitwa "Lula" na huyu wetu hapa anaitwa "Mwanakijiji".Ni watu wawili tofauti lakini wana mawazo yaliyofanana.
   
Loading...