Tohara kwa Kabila la Wamasai

Tohara kwa Kabila la Wamasai

Page 94

JF-Expert Member
Joined
Oct 22, 2015
Posts
5,202
Reaction score
15,232
Kabila hili ni la pili kwa umaarufu zaidi barani Africa, ni moja kati ya Makabila yanayojivunia sana Utamaduni wao.

Moja kati ya Tamaduni ambayo imekuwa ngumu kuzisahau ni Jando na Unyago.

Leo ningependa tuifahamu kuhusu Tohara ya Kimasai kwa watoto wa Kiume.
Kimasai, tohara ni njia kuu ya kumthibitisha mvulana kuwa sasa amekomaa kuwa Mwanaume halisi.

Kuna baadhi ya taratibu ambazo lazima zifatwe ili tohara iweze kufanyika.

Kwanza,kuna sherehe maalum ya kumtangaza Mvulana kwa jamii nzima kuwa anaandaliwa kwa ajili ya Tohara. Sherehe hii huitwa "Irmong' Loondomono". Sherehe hii huambatana na uchinjwaji wa ng'ombe au kondoo (hutegemea na uwezo wa familia husika) kwa kila kijana. Yaani kama vijana wapo sita wanaoandaliwa kwa ajili ya Tohara basi ng'ombe/kondoo sita huchinjwa.
Ng'ombe huyu huchinjwa nje kidogo, pembeni kabisa ya nyumba ya mama yake kijana. Ng'ombe huyu huchinjwa na Wanawake wakishirikiana na Wazee. Nyama hizo huliwa na wazee,wanawake na watoto. Morani hawaruhusiwi kula. Hii ni kwa sababu sheria za Kimasai haziwaruhusu Morani kula nyama yoyote iliyotiwa jicho na mwanamke awaye yeyote. Badala yake, Morani hupewa chochote cha kuchinja porini, mahali ambapo wanawake hawawezi kupafikia. Mambo mengine mengi huendelea kwenye shereje hiyo lakini sitazielezea humu.

Kesho yake, ngozi zile huanikwa juani ili zikauke vema.

Baada ya ngozi kukauka,huchorwa michoro maalum juu yake. Hii huitwa "Esirineta o Loondo". Michoro hii ina maana zake.

Kisha wakishachora michoro hiyo,wale vijana hunyolewa hutolewa nje. Hii maana yake ni kwamba tangu wanavyotangazwa kuwa wanaandaliwa kwa tohara hutakiwa kukaa ndani. Haimaanishi kwamba wanakaa ndani tu,huruhusiwa kuzurura na kufanya mambo mengine. Siku hii huitwa "Engitupukunoto" Huambatana na mambo mengine ya kimila ambayo hazina maana sana kubandikwa humu. Siku hii huambatana pia na kukamata panzi kisha kuwachomeka kwenye vijiti mchongoko ikiashiria kwamba kijana kaua simba hivyo anastahili kuwa Morani.

Hii imeanzishwa baada ya kuona kuwa Simba ni wakali na ngumu kupatikana.

Siku moja kabla ya Tohara, vijana hunyolewa kipara kutoka kichwani mpaka kwenye nyusi za macho mpaka sehemu za siri. Kijana pia hutakiwa kuleta mti maalum (hutofautiana kutoka familia moja mpaka nyingine). Mti huu unatakiwa uwe umenyooka haswa. Kijana anatakiwa aisake aina hiyo ya mti mpaka aipate. Kwa hiyo kijana kabla hajaifika siku anatakiwa awe amejua ataupata wapi huo mti ili siku ikifika ananyooka tu mpaka kuufikia. Kwenda kuuchukua unasindikizwa na Morani.

Mti huu kuna taratibu zake za kuukata. Kwanza wewe na wale waliokusindikiza mnatakiwa mvae nguo za blue,pia hutakiwa kukatwa na shoka. Kabla ya kufanya yote hayo,unatakiwa uubarikia kwa kuumwagia maziwa maalum huku unatamka maneno ya baraka kwake. Mkishaukata,mnaanza kuelekea nyumbani. Lazima muimbe nyimbo maalum mpaka mfike. Haitakiwi mfikishe nyumbani kabisa bali mtauficha mahali ambapo siyo mbali sana na Nyumbani.
Mti huu ni maalum kwa ajili ya kuimbiwa na wanawake siku ya Tohara.

Kijana akishafika hutengenezewa viatu maalum. Viatu hivi ni maalum kwa ajili ya Siku hiyo. Hutengenezwa na ngozi tupu ya ng'ombe na anayetengeneza ni mjomba wa kijana. Mtu asiye na uhusiano wowote wa kijana haruhusiwi mahala hapo. Pia kipisi chochote cha ngozi hiyo haitakiwi kupotea,hii ni mbaya kwa sababu watu wengine wanaweza kutumia kumfanyia mbaya kijana. Hivyo wanaochonga viatu hivyo huwa makini sana. Wakishachongewa viatu kijana huvalishwa hirizi maalum moja mguu wa kulia na nyingine shingoni. Hii humlinda kijana dhidi ya macho ya walimwengu. Kisha huvalishwa nguo nyeusi tii na tayari kuelekea kuimbiwa.

Mara nyingi vijana hawa huimbiwa na wenzao waliotoka jando siku si nyingi. Hawa huitwa "Isikolyo". Hawa nao huvaa nguo nyeusi na hujipaka rangi nyeupe inayoitwa Enduroto. Shughuli hii ya vijana kuimbiwa mara nyingi huanza saa 11 au 12. Mara tu baada ya ng'ombe kufika zizini.Vijana hawa huimbiwa wakiwa wamesimama uchi wa mnyama. Bila chembe yoyote ya nguo.
Vijana hawa huimbiwa huku wakichapwa chapwa kidogo,kwa fimbo vidogo vilivyounganishwa kwa pamoja. Pia manyonya ya mbuni hutumiwa kuchapia hao vijana wanaoandaliwa kwa tohara.

Kuna wengine wahuni,hupachika vitu vyenye ncha kali kama viembe kwenye hayo manyoya hivyo huwasababishia wenzao maumivu makali sana. Wengine pia huwatemea mate na kuwashika shika makalio.

Hii yote humfanya kijana kukasirika kwa kudhalilishwa hivyo kuweza kuhimili maumivu yatokanayo na kisu cha Daktari.Vijana hawa huimbiwa kuanzia saa 11 jioni mpaka muda tayari kwa ajili ya kushikwa na mtaalamu. Ukumbuke kuwa hatakiwi kuketi muda wowote wala kuvaa nguo yeyote mpaka muda wa tohara. Vijana hawa huimbiwa usiku mzima mpaka asubuhi. Skolyo wakichoka hupokezana na wenzao,hivyo usitegemee kwamba watapata muda wa kupumua kidogo. Kijana mwenye jeuri huchapwa mno na kufanyiwa visa vingi sana.

Muda wa kijana kutahiriwa ukikaribia,maziwa hukamuliwa moja kwa moja na kijana hupewa yakiwa na lile joto. Wakishapewa maziwa hayo,huimbiwa tena dakika kadhaa kisha hupitishwa mlango mwa zizi kwenda kuogeshwa.Maji anayoogeshwa nayo ni maalum. Kwanza huwekwa juu ya nyumba kwa usiku mzima huku ikiwa imehifadhiwa ndani ya sufuria. Ndani ya sufuria huwekwa maji,kichuma maalum na sindano. Maji haya huwa ya baridi sana. Sijui ni mechanism gani hufanyika.

Kijana hutakiwa kwenda kuoga karibu na sanzu ambayo hutumiwa kufungia Boma la ngombe! Kijana huoga huku akiminiwa maji na kijana mdogo ambaye bado hajapitia tohara.Maji haya pia ni ya utakaso. Kwamba kama una tabia zisizopendeza uzioshee mbali,au kama kuna laana inayokufata uioshee mbali. Sio kuoga maalum bali tu kumwagiwa maji.Maji yakishaisha kijana hupewa sufuria ili kuipiga teke ikiwa ishara ya kukasirika na sasa kukimbilia kwenye kisu.Kila kijana huwa na ngozi yake maalum ya kulalia kwa ajili ya kutahiriwa. Ngozi hupangwa kutokana na umri wa vijana wanaofanyiwa tohara. Yaani kutoka mkubwa kuelekea mdogo. Age descending order.

Kijana hujilaza kwenye ngozi huku akiwa ameinuliwa kichwa kidogo na mtu ambaye ameandaliwa kumshika.Zamani kulikuwa na kisu kimoja tu kwa kila daktari. Kisu hiki kilikuwa na mikanda mekundu na hutumiwa kwa vijana wote wanaofanyiwa tohara. Yaani akimaliza kwa mmoja anaosha na maziwa kisha hutumia kwa mwingine. Mpaka amalize. Endapo kitakosa makali katikati ya shughuli,hulazimika kunoa kisha kuendelea nayo. Siku hizi angalau wamejitahidi. Hawaruhusu kutumiwa kwa kisu kimoja. Kuepuka gharama,madaktari hununua vile visu vidogo kutoka hospitalini.

Watu wengi sana hujikusanya kushuhudia shughuli. Hata wale waliolala huamka na kuja kuona mambo yanavyofanyika. Kijana anatakiwa aonyeshe dhahiri kuwa sasa anafaa kuwa Askari wa jamii na Mwanaume kamili. Hatakiwi kuonyesha kwamba anahisi maumivu ya aina yoyote. Hatakiwi kutingishika sehemu yoyote ya mwili. Huruhusiwi hata kupepesa macho,vidole wala makunyanzi ya usoni. Mbaya zaidi hutakiwi kuonyesha kuhema kwa nguvu. Hemea ndani kwa ndani.

Kufanya moja ya hayo niliyoyataja wakati unatahiriwa huonyesha kwamba u muoga pamoja kuwa umekua lakini hustahili kuwa morani. Watu wanachunguza kila sehemu ya mwili wako na endapo utatingishika Maskolyo hukimbia na kuingia zizini kupiga ng'ombe kwenye pembe zao. Hii huashiria dharau sana kwa boma husika. Kijana anatakiwa kuvumilia mpaka pale atakapomalizwa.

Daktari anapofika kwanza humpaka kijana rangi fulani nyeupe pee,nilishasema awali inaitwa "Enduroto" kwenye dushelele lake na kumpiga nayo kwenye mapaja. Hii humsaidia kuona vema na hata endapo damu itatoka isimtatize daktari. Pia kuna msaidizi ambaye either anajifunza au anamsaidia tu bila nia yoyote ya kujifunza.

Muendelezo:

Mtaalamu huyu baada ya kumpaka hiyo nduroto huanza kuchonga kwa utaalamu kabisa kwa kurudisha govi huko nyuma mpaka mahali atakapoona panafaa. Kisha huvuta kwa nguvu sana huelekea upande wa magotini. Kisha hupimia kwa kidole na kutoboa kishimo kidogo kwa juu kisha kupitisha dushelele juu yake hivyo kukifanya ile govi kuning'inia kwa chini. Ikishaning'inia kigovi kile hukatwa kwa mbele kidogo. Baada ya hapo hummwagia maziwa pale alipotahiriwa kisha huamshwa.


Baada ya hapo kijana huinuliwa na kuambia ateme mate kama ishara ya kuuaga uvulana na kuukaribisha uanaume. Hapo ndipo mvulana huzichanga karata zake na kuhimiza kutotema mate mpaka apewe ng'ombe.

Kwa mfano,kaka yake atamuambia tema mate nikupe ng'ombe jike,mwingine tema mate nikupe mbuzi,mjomba wake tema nikupe mbuzi jike,mwingine tema nikupe beberu. Baada ya hapo kijana hunyanyuka na kupelekwa ndani kwa mama yake.

Malipo ya Daktari mara nyingi huwa mbuzi au kama vijana wapo wengi hupewa ndama. Kwa siku hizi kwa sababu wamekuwa wa maeneo ya mbali huhitaji pesa taslimu na baada ya hapo huondoka zao. Gharama hutofautiana kutoka mmoja mpaka mwingine.

Daktari hawa huwa hawaishi maisha marefu sana. Hii ni kutokana kuwa wanaamini wanagusa damu nyingi za watu hivyo damu zile huwafatilia. Lakini endapo sehemu kubwa anaowafanyia tohara watashindwa kuhimili maumivu basi anaendelea kupata baraka. Pia malipo ya kijana aliyeshindwa kuhimili maumivu huwa na malipo ya ziada kuliko yule aliyehimili.
 
Naupdate Uzi usisite kurefresh mara nyingi kwani kuna sehemu zimejirudia katika kuudumbukiza huku ndani. Pia bado sijaumalizia.
 
Uzi mzuri Kuna haja ya kuyaweka haya kwenye maandishi yaani vitabu ili kizazi kijacho kifaidike nayo. Kuyaacha hiyo ni kupoteza maarifa
 
Uzi mzuri Kuna haja ya kuyaweka haya kwenye maandishi yaani vitabu ili kizazi kijacho kifaidike nayo. Kuyaacha hiyo ni kupoteza maarifa
JF itaishi milele. Watayakuta huku.
 
Kumbe ndo mambo yalivyo. Huku kwetu nimealikwa kwenye sherehe ya watoto wa kimasai, sherehe hiyo imeanza leo jion itamalizika keshokutwa. Mtoa uzi hebu nambie huwa wanatahiri mida gani ili kesho mapema niwahi kushuhudia maana sitaki kusimuliwa.
 
Kumbe ndo mambo yalivyo. Huku kwetu nimealikwa kwenye sherehe ya watoto wa kimasai, sherehe hiyo imeanza leo jion itamalizika keshokutwa. Mtoa uzi hebu nambie huwa wanatahiri mida gani ili kesho mapema niwahi kushuhudia maana sitaki kusimuliwa.
Zamani ilikua saa 12 lakini siku hizi hutegemea na ratiba Dr. Cha kufanya wewe ulizia wanakatwa saa ngapi ili ukaone mambo!
 
Zamani ilikua saa 12 lakini siku hizi hutegemea na ratiba Dr. Cha kufanya wewe ulizia wanakatwa saa ngapi ili ukaone mambo!
Duh, tatizo huku wanaficha sana mambo haya. Kuna mwnfz wangu mmoja nilimuuliza jana hiyo sherehe yahusiana na nn, akasema kuwa ni ya watoto waliobalehe ila na wasichana wapo kundini. Je yawezekana na wasichana pia wakafanyiwa tohara?(kukeketwa)
 
Uzi mzuri Kuna haja ya kuyaweka haya kwenye maandishi yaani vitabu ili kizazi kijacho kifaidike nayo. Kuyaacha hiyo ni kupoteza maarifa
Haya maarifa hayapotei ndugu ,wanarithishana kizazi hadi kizazi
 
Duh, tatizo huku wanaficha sana mambo haya. Kuna mwnfz wangu mmoja nilimuuliza jana hiyo sherehe yahusiana na nn, akasema kuwa ni ya watoto waliobalehe ila na wasichana wapo kundini. Je yawezekana na wasichana pia wakafanyiwa tohara?(kukeketwa)
kutokana na katazo la Serikali sasa hivi wasichana hukeketwa wakiwa wadogo sana. Ukiweza kunambia maeneo uliyopo nitakuambia kama bado inafanyika hata ukubwani. Umasaini msichana huolewi bila kukekerwa na watoto wa kike wenyewe hung'ang'anizia wakeketwe ili wawe syangikiki.
 
kutokana na katazo la Serikali sasa hivi wasichana hukeketwa wakiwa wadogo sana. Ukiweza kunambia maeneo uliyopo nitakuambia kama bado inafanyika hata ukubwani. Umasaini msichana huolewi bila kukekerwa na watoto wa kike wenyewe hung'ang'anizia wakeketwe ili wawe syangikiki.
Nipo mkoa wa pwani. Huku kuna wamasai wakutosha kabisa.
 
Nadhan n muhim yawekwe kwenye maandish IL wasio masai wawe na fursa ya kusoma vizaz na vizaz
Shida ni kwamba wasio masai hawatakiwi kuyajua haya ,japo alichoeleza mleta mada ni sehemu ndogo sana ya tohara
 
Shida ni kwamba wasio masai hawatakiwi kuyajua haya ,japo alichoeleza mleta mada ni sehemu ndogo sana ya tohara
Sio lazima tujue kw undan sana hata kwa historia kama hii itakua poa
 
Back
Top Bottom