Kuna baadhi ya watu wanaamini kuwa wanaume waliyofayiwa tohara hupata tatizo la upungufu wa nguvu za kiume pindi wanapokua, na ni kundi ambalo lipo katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU kwa urahisi ukilinganisha na wale ambao hawajafanyiwa tohara.
Ukweli upoje?
Ukweli upoje?
- Tunachokijua
- Tohara ni upasuaji mdogo unaofanyika ili kuondoa ngozi ya mbele inayofunika sehemu za siri za mwanamme.
Asili ya utamaduni huu ni imani za kidini, ambazo baadae zilithibitishwa kuwa na faida kiafya. Leo, watu hutahiri kwa sababu za kiafya, au za kidini.
Mwanamme huzaliwa na ngozi inayofunika kichwa cha sehemu zake za siri hivyo kupitia tohara, ngozi hii huondolewa kwa kufanya upasuaji mdogo usiotumia muda mrefu sana, kati ya dakika 15-30. Kwa sababu za kiusalama, pamoja na kuhakikisha kuwa tendo hili linafanyika kwa ufanisi mkubwa, ni vizuri kama likifanywa hospitalini.
Watoto wadogo wanaofanyiwa tohara huwa na faida kubwa ya kutokupata maumivu makubwa kama watu wazima, kutumia muda mchache zaidi kwenye upasuaji pia uponaji wa kidonda huchukua muda mfupi sana kati ya siku 7-10 pekee.
Kwa mujibu wa WHO na Kituo cha Udhibiti na Kinga ya Magonjwa cha Marekani, CDC, tohara huwa na faida kubwa kwa mwanamme ikiwemo kupunguza nafasi ya kuugua Saratani ya uume pamoja na magonjwa mengine ya zinaa hasa VVU/UKIMWI.
Hii inatoa maana kuwa tohara haiongezi nafasi ya kupata maambukizi ya VVU/UKIMWI bali hupunguza nafasi hiyo. Ikumbukwe kuwa ngozi inayofunika umme huwa ni laini na nyepesi sana kuchanika panapotokea msuguano wakati wa tendo la ndoa, hii ni hatari kwa afya na inaweza kuongeza maambukizi ya magonjwa ya zinaa, VVU ikiwemo.
Kuhusu kupunguza nguvu za kiume, ni muhimu kwanza kufahamu kuwa kinachoondolewa wakati wa tohara ni ngozi tu isiyo na athari yoyote kwa ukuaji wa via vya uzazi wa mwanamme, pamoja na ufanisi wake katika kushiriki tendo la ndoa.
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za kisayansi, upungufu wa nguvu za kiume huchangiwa na mambo mengi sana, lakini tunaweza kuyagawa kwenye makundi makubwa mawili ambayo ni-
- Sababu za kisaikolojia na kihisia
- Sababu za kibaiolojia, ambazo huhusisha uwepo wa magonjwa mengine pamoja na baadhi ya changamoto kwenye mfumo wa homoni, au neva za fahamu.