Tofauti kati ya baba mzazi na 'baba sperm donor'

IsangulaKG

JF-Expert Member
Oct 14, 2010
706
385
Kama ilivyo kawaida yangu nipatapo muda kidogo nakuja kujisemea (talking to myself) hapa kwenye ukuta wangu.

Hivi karibuni nimeona video ya mchungaji mmoja akielezea umuhimu wa vijana waishio mjini kuwakumbuka 'wazazi' wao ambao wengi huishi vijijini. Wakati nakubaliana na hoja kuu kwa ujumla, pia napata nafasi ya kutafakari kuhusu tofauti ya mzazi 'baba mzazi' na mtu yule ambaye alitoa msaada wa mbegu za kiume kwa mama (sperm donor). Hapa sitamuongelea mama kwa sababu mara nyingi anahusika katika malezi kwa asilimia 100 pale ambapo sperm donor anapomaliza kutimiza wajibu wake.

Suala la kumpa mwanamke mimba hasa kwa watu wenye uchumi wa chini mara nyingi hutokea kama ajali kwenye safari ya starehe. Mara nyingi hakuna kivuli wahusika hukaa na kupanga kuwa sasa tuzae huku wakiakisi mchakato mzima wa malezi ya mimba, maandalizi ya kujifungua, gharama za elimu kwa mtoto atakayezaliwa na afya kwa ujumla. Kwa sababu kama wangepata fursa ya kutafakari haya na yakawa kichocheo cha maamuzi yao ya kupeana mimba naamini 'population' hasa mitaa yetu ya uswahilini isingekuwa kama ilivyo sasa. Ni kwa sababu haya hayazingatiwi ndiyo maana 'baba sperm donor' hujikuta anaingia mitini baada ya kutimiza wajibu wake na akaambiwa 'tayari'. Huona kama ni kosa la mwanamke kupata mimba na wengine huenda mbali kusema 'wametegeshewa'. Mzazi mama ambaye amepewa mbegu pengine kwa hiari ya matarajio kuwa mtowaji atadunwa na moyo wake kwa fahari ya kuwa Baba Mzazi, huanza kuchakarika kwa kujipakaza shida mpaka kiumbe kile kitoke tumboni mwake. Anaweza akafanya vibarua, akapika ama kuuza pombe za kienyeji ili mradi mtoto apate lishe na elimu. Wakati huo baba sperm donor tayari amehamishia majeshi mahali pengine akitafuta kutimiza wajibu wake wa ku'donate' sperm. Wababa wa aina hii huzijua raha, hujisifu kwa idadi ya vimwana walionao na si afya na elimu ya watoto wao.

Mungu si Athumani, mtoto akajitutumua kwa msaada wa mama yake na pengine wasamalia wema akafika chuo kikuu mara akapata kazi yake nzuri. Wakati huohuo baba sperm donor anakuwa amechoka viungo kutokana na kutikisa kiuno kwenye starehe zake...kachoka kiuchumi na kimwili. Ni kawaida watu wa aina hii kuanza kuwanyapianyapia watoto waliofanikiwa pasipo kujua walipitia mapito gani. Ataanza kulalamika kwa jamii kuwa 'mtoto hamjali' na jamii pia hufumbia macho 'uovu wake wa kutokumjali mwanae akiwa mdogo na huanza kumlaumu mtoto' Utasikia misemo kama vile 'wazazi ni Mungu wa duniani' pasipo kujua kuwa hata Mungu anapendwa kwa wema anaowatendea watoto wake. Wengine watasema 'samehe saba mara sabini' wakisahau kuwa hata Mungu msamaha ulimshinda akamwaga mvua ya Gharika wakafa wanadamu wengi tu. Hapa ndipo unapoona tatizo lililojificha kwamba wanajamii wengi hupenda 'kufurahia mafanikio ambayo hawajashiriki kuyatafuta'. Na, kwamba pengine wanajamii wengi ni wazazi wa aina ya hii ya baba sperm donor.

Kabla hatujawahimiza watoto kuwajali wazazi wao, kwanza tuwahimize wazazi kutimiza wajibu wao kimalezi. Hata mti unaweza kuupanda lakini mpaka uumwagilie utiye na mbole ndo uje ukupe matunda mazuri. Binadamu si kuku ambao kazi ya jogoo ni kutiya mbegu na kumwachia mama kukomaa vidole kwa kufukuafukua na kuwapatiwa watoto lishe hadi wanapoweza kujitegemea wakati ambao jogoo kaenda kupandilia kwingine. Kila mzazi lazima alipwe kiasi kile kile anachompimia mwanaye. Haiwezekani uwe baba sperm donor, mwanao ahangaike kwa mihangaiko ambayo hata inapunguza life expectancy yake halafu akishafanikiwa unakuja kukenua magego na kutoa utomvu wa tamaa mdomoni.

Kabla ya Mchungaji kuhimiza vijana wawakumbuke wazazi wao, ni lazima kwanza awahimize wababa wawe wazazi na si sperm donor. Imani yangu ni kuwa mtoto ambaye hana vidonda vya maumivu ya kutengwa na mzazi wake wakati wote wa utoto wake hawezi kuwasahau wakati yeye akila starehe mjini. Baba ambaye anawajibika kwa kila mbegu anayoipanda, haijalishi ana uwezo wa kupanda ngapi lakini akiweza kuzihudumia mbegu zake na akaja kusahaulika baadae hapo wanajamii tuna haki ya kulalama. Lakini hatuwezi kupanda basi la walalamikaji huku vichwani tumejitwika ndoo za maarifa ya shida alizopitia huyo anayelalamikiwa kumtenga mzazi wake kutokana na kutengwa na mzazi huyo huyo.

Kama nilivyosema, hapa najiongelesha tu na sitarajii niakisi mawazo ya wengi kwa sababu sote twatofautiana.

Isangula KG

Facebook:
 
Back
Top Bottom