Hatuhitaji kununua mitambo ya Dowans kumaliza tatizo la umeme
TATIZO la ukosekanaji wa umeme wa uhakika wa kuendesha gurudumu la maendeleo na uchumi wa nchi yetu, ambalo lilianza kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 1994, hivi sasa limekuwa la kudumu pasi na taasisi yoyote ile ama ya kiserikali au ya kibinafsi kupata ufumbuzi wa kudumu. Kimsingi, tatizo hili ni la kisera zaidi kuliko kiutendaji, kwani, bila sera thabiti, ufumbuzi hautapatikana.
Ni jambo la kushangaza na kusikitisha, licha ya jitihada nyingi za asasi za kiraia zinazofanya utafiti na kuvumbua mbinu nyingi endelevu za nyenzo bora na za gharama nafuu za nishati, Serikali na vyombo vyake imeshindwa kutumia matokeo ya tafiti hizo. Mshangao zaidi unatokana na ukweli kwamba Serikali imepuuzia jitihada hizo, kana kwamba hazina manufaa yoyote yale kwa Taifa kwa ujumla. Kwa mfano, hivi majuzi, asasi inayoitwa Appropriate Rural Technology (ART) ilizindua kinu kidogo cga kuzalishia umeme kinachotumia gesi ya kibaologia (biogas), ikiwa ni uvumbuzi uliofanyika baada ya kufanya marekebisho katika mfumo wa kuchoma mafuta wa injini ya kinu cha kawaida kinachotumia mafuta ya petrol. Ubunifu huo umewezesha kinu hicho, ambacho kinapatikana kwenye maduka yanayouza vinu hivyo, kuweza kutumia gesi hiyo ya kibaolojia ambayo inazalishwa kwa gharama nafuu, na baada ya kuzalishwa inapatikana bila ya gharama yoyote nyingine ya nyongeza. Kinu hicho kinazalisha umeme katika kiwango cha KVA 650 hadi 800, kutokana na mahitaji ya mtumiaji.
Shamba la mkonge mkoani Tanga nalo limezindua kinu cha kuzalisha umeme kinachotumia gesi hiyo ya kibaolojia inayotokana na mabaki ya zao la mkonge, katika kiwango cha Mega Watt 1, jambo ambalo linatoa matumaini kwamba jitihada zaidi zinaweza kufanyika ili kuiwezesha Tanzania kuwa na vyanzo vingi mbadala vya umeme.
Lakini kinachoshangaza zaidi ni kwamba licha ya kwamba TANESCO ilitambua wazi kuwapo kwa tatizo la upatikanaji wa umeme wa uhakika, hakuna mbinu zozote mbadala zilizowekwa bayana. Kinachoonekana wazi wazi ni kwamba, hakuna ubunifu wowote au mawazo yoyote mbadala yaliyojadiliwa kwenye himaya ya uongozi mzima wa TANESCO, badala yake, TANESCO na watendaji wake wamekuwa wakitegemea vyanzo vya kawaida vya uzalishaji wa umeme, kama vile generator (turbines) za Dowans, Songas, IPTL na vinu vya mabwawa ya maji ya Kidatu, Kihansi na Mtera!
Tumekuwa tukipata taarifa mbali mbali kwenye vyombo vya habari vya kidunia, kama vile CNN, kupitia vipindi vyake kama vile Eco Solutions kwamba vyanzo vya nishati ya mafuta ya petrol vinaelekea kukauka, jambo ambalo linasababisha gharama ya mafuta kwenye masoko duniani kuongezeka mwaka hadi mwaka. Taarifa hizi, angalau, zingetuzindua kutoka kwenye usingizi mkubwa tulionao, na tukaanza kuendeleza jitihada za tafiti zilizofanyika, pia pamoja na kuanza kutumia vyanzo mbadala vya upatikanaji wa upepo, jua, na kadhalika.
Kupungua kwa upatikanaji wa mafuta yatokanayo na petroli ni jambo ambalo lilitabiriwa miaka mingi iliyopita, kwani, mafuta hayo yanayochimbwa kutoka ardhini hupatikana kwa viwango tofauti na hatimaye kila kisima kinachochimbwa hufikia wakati kikakauka kabisa. Jambo hili lingetuzindua kutoka kwenye usingizi tulionao, kama walivyofanya wenzetu wa Marekani, ambao tayari wamekamilisha tafiti mbali mbali na kuweza kubuni teknolojia madhubuti za uzalishaji wa umeme kutokana na nishati itokanayo na joto la jua, kwa jina lingine, Stirling Energy Systems, utafiti uliodhaminiwa na Wizara ya Nishati ya Marekani na kuendeshwa na Chuo Kikuu cha California, cha mjini Berkeley, jimboni California.
Marekani kwa sasa ni nchi inayoongoza katika teknolojia hii ya Stirling, na kwenye kada mbali mbali, ikizingatiwa kwamba nchi nyingi barani Afrika zinapata jua kwa muda mrefu zaidi kwa kuwa wakati wa msimu wa baridi kwenye nchi za Ulaya/Marekani, muda wa jua kuwaka unapunga teknolojia hiyo imeonekana kuwa hatari kwa nchi zinazozalisha mafuta ya petroli, kwani, ikipatikana kabla ya muda muafaka (ambapo itapatikana kwa bei ya juu zaidi kuliko sasa), nchi nyingi barani Afrika zitaacha kabisa kutumia mafuta ya petroli kwa kuzalishia umeme, na zitakuwa zinajitegemea katika uzalishaji wa umeme, kutokana na urahisi na ubora wa teknolojia hii ya Stirling.
Wadau wengi wa nishati nchini Tanzania wanaona kwamba kuanza kuzungumzia teknolojia ya Stirling ni sawa na ndoto za Alinacha, kwani, kama kawaida ya Watanzania wengi, wanaonesha udhaifu wa kifikra kwa kusema kwamba
hayo ni mambo ya wakubwa
walioendelea. Lakini cha ajabu ni kwamba, hata siku moja hawajiulizi ni nani aliyewateua hao wakubwa kuwa na ukiritimba wa fikra na telnolojia, na kutuacha sisi wadogo kuwa mafukara wa teknolojia na fikra?
Hata kama hatutaanza kuzungumzia teknolojia ya Stirling, basi, tuanze kuweka mikakati ya matumizi ya nishati ya upepo unaopatikana kwa wingi sana hapa nchini kwa madhumuni ya kuzalisha umeme. Hata kama tutaanzia kwenye mitambo midogo midogo, yenye uwezo wa kuzalisha Kilo Watt 1 hadi 10, mitambo hiyo ikiwa mingi itaondoa kabisa tatizo hilo la upatikanaji wa umeme. Si lazima Tanzania yote iwe kwenye umeme wa gridi, kwani hapo ndipo tunapokosea, kwa kudhani kwamba ni lazima umeme unaopatikana nchini uzalishwe na TANESCO peke yake.
Wakala wa Umeme Vijijini (REA) tayari wameweka mazingira mazuri ya Watanzania kuwekeza kwenye sekta ya umeme, kuanzia kwenye viunga vya miji mikubwa hadi vijijini. Lakini fursa hizi hazijatumiwa ipasavyo kwa kuwa Watanzania walio wengi wanaona kwamba wao hawana nguvu ya kujishughulisha na uzalishaji wa umeme, badala yaka fursa hizo zinatumiwa na watu wachache hususan wageni ambao wanajiamini kwamba wanaweza.
REA ina nafasi kubwa ya kuwaelimisha wananchi kuhusu wajibu wao na haki zao katika uzalishaji wa nishati ya umeme, jambo ambalo watalifanya katika siku za usoni. Lakini Watanzania wakiamka, umeme utapatikana.
Hatuhitaji kununua mitambo ya Dowans kumaliza tatizo la umeme. Ufumbuzi wa tatizo hili uko mikononi mwetu.
Kwa maoni, maswali, mapendekezo:
Tuma email kwa
info@strategos.co.tz
P.S. Nilikuwa mmoja wa wajumbe walioshiriki kwenye kongamano la Siku ya Viwanda ya Afrika, lililofanyika kwenye Ukumbi wa Karimjee, takriban wiki mbili zilizopita. Kamishna wa Nishati kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Bashir Mrindoko, alizungumzia nafazi za uwekezaji zilizopangwa (kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Nishati) ambazo ziko kwenye hatua mbali mbali za utekelezaji. Ni nafasi moja tu ya uwekezaji kwenye nishati mbadala, ambayo imewekwa, nayo ni ya uzalishaji wa MegaWatt 100, kwa kutumia teknolojia ya umeme unaotokana na nguvu za upepo (Wind Power). Je, Serikali inatambua upepo peke yake kama teknolojia kuu ya nishati mbadala, au kuna nyinginezo? Jambo lingine ni kwamba, kwa Sasa, kwa mujibu wa Mrindoko, Serikali yetu inaona kwamba Watanzania hawana uwezo (au hawataki?) wa kuwekeza kwenye sekta hii nyeti ya nishati! Je, hii ni kweli? Kama si kweli, kwa nini Serikali haiwapigii kelele wawekezaji wazawa kujikita kwenye uwekezaji wa uzalishaji wa umeme, kuanzia MegaWatt 100 na kuendelea? Penye nia PANA NJIA!