The Other Half (Simulizi)

The Other Half (Simulizi)

*THE OTHER HALF*



*SEASON 1 - THE LEGEND OF ANABELLE*



EPISODE 47


Si lazima kuwa Nabii ili kuweza kuona nyakati zijazo na wala si lazima kuwa mtume ili kuwa wakala wa habari njema. Kuna jambo au kitu au kiumbe kilicho juu ya sisi wote, si Mungu kwa kuwa Mungu ni mkuu zaidi. Lakini kiko kiumbe ambacho kilipata kuwepo kabla hata ya mito, maziwa, bahari na hata jua kupata kuwepo. Mwenye werevu wa kujua siri zote kuu juu ya ardhi. Mwenye uhai usiokoma kwa maelfu na maelfu ya miaka. Mwenye kujidhihirisha katikati yetu kama binadamu mara kadhaa katika umbo la uanadamu. Mwanzilishi wa starehe, anasa tangu mwanzo wa ustaarabu wa dunia.

Pengine ndiye ambaye alijidhihirisha akiwa katika hali ya ubinadamu kupitia mashujaa wa historia kama Mfalme Alexander, au shujaa wa vita kama Archilles. Pengine alijidhihirisha tena katila sura ya wanataaluma kama Leonardo Da Vinci au mwanamapinduzi wa kimuziki kama Morzart.

Hakuna anayejua, lakini kiko kiumbe cha hali ya juu zaidi yetu. Kiumbe ambacho kina uhai usio koma. Kiumbe ambacho kimewahi kukutana ana kwa ana na Zeus, Mungu wa Kigiriki. Kiumbe ambacho kimewahi kufanya jaribio la kumuoa Hera, Mungu mkuu wa miungu yote ya kike ya kale. Kiumbe ambacho kimewahi kukabiliana na kutunishiana misuli na Hades, mungu wa vita na mungu wa ulimwengu wa giza.

Hakuna kitabu cha imani ambacho kimethubutu kumzungumzia kiumbe huyu na vitabu vya kihistoria ni vile vitabu vya siri pekee ambavyo vimethubutu kutia mkono kumdhihirisha.

Mara ya mwisho alijidhihirisha katika karne ya 16 akiishi katikati yetu. Kwa zaidi ya karne tano hakuna mwanahistoria ya giza ambaye amefanikiwa kunasa walau dalili ya uwepo wake katikati yetu. Lakini ni tukio moja tu, tukio ambalo limetokea mwaka 2038 ndilo ambalo liliamsha uwepo wake kutoka chini kabisa ya vilindi vya bahari na hatimaye kwa mara ya kwanza kuonekana dalili ya uwepo wake katikati yetu. Tukio la kufunguliwa kwa chupa kutoka katika sanduku la Pandora.

Kalamu hii ikawe ushuhuda wa yale ambayo yametokea, yanatokea na yatakuja kutokea siku chache za usoni.


******


Mawimbi ya bahari yalikuwa yanapiga kwa nguvu kiasi na kuwasukuma akina Mzee Caleb na wenzake ambao walikuwa wamelala pembezoni mwa bahari mchangani bila kujitambua.

Kadiri ambavyo mawimbi yalivyokuwa yanapiga na kuwasukuma ndivyo ambavyo yalikuwa kama yanawatikisa ili kuwaamsha warudi katika ufahamu.

"Koh koh koh koh..!!"

Walker ndiye alikuwa wa kwanza kuamka kabla ya wenzake wote. Alijitahidi kusimama japo bado alikuwa anatapika na kichwani ana kizungu zungu.
Pale mchangani walikuwa wamelala wenzake wengine makomando sita pamoja na Mzee Caleb.

"Mzee mzee mzee! Mzee Caleb.!"

Walker alimkimbilia kwanza mzee Caleb ambaye alikuwa amelala pembeni yake huku akiwa hajitambui.
Alitumia karibia dakika nzima kumtikisa mpaka Mzee Caleb alipoamka na kupata ufahamu.

"Koh koh… tuko wapi.!?" Mzee Caleb alimka huku anahema kwa nguvu na kukohoa mfululizo.

Kabla Walker hajajibu, makomando wenzake nao walikuwa wameamka tayari. Silaha ambazo walikuwa nazo awali walipokuwa wanaingia msitu wa Ox kule Maryland hawakuwa nazo tena. Wala yale mabegi ya mgongoni ya kijeshi hawakuwa nayo tena.

"Nini kimetokea?" Mmoja wa wale vijana makomando akauliza.

Walisimama pale kwenye pwani wakiangaza macho huku na huko. Mara ya mwisho walipokuwa na fahamu zao walikuwa ndani ya msitu wa Ox na wakikuwa wanakaribia kushambuliwa na kuraruriwa vipande vipande na binadamu wa ajabu ambaye alikuwa anawafuatilia.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Mbele yao kulikuwa na bahari ambayo ilienda mbali kuzidi hata upeo wa macho yao. Nyuma yao pale pwani kama mita ishirini hivi kutoka pale ambako walikuwa wamesimama kulikuwa na msitu mnene.

"Mzee unafahamu tuko mahali gani hapa?" Walker alimuuliza mzee Caleb ambaye naye alikuwa anageuka geuka kupepesa macho kupatazama vyema pale walipo.

"Sifahamu tuko mahala gani.!" Mzee Caleb alijibu huku anaemdele kugeuka geuka kutazama yale mandhari yanayowazunguka.

"Kuna kitu hapa!" Mmoja wa makomando aliwaita akiwa amesimama kama mita kumu kutoka wenzake walipo.

Kwa haraka wote wakatembea kwenda pale ambapo mwenzao alikuwepo.

"Kuna nyayo za binadamu hapa!" Yule komando akawaonyesha wenzake walipofika pale alipo.

Pale ambapo alikuwa amesimama mchangani kulikuwa na nyayo kadhaa za binadamu ambazo zilionekana zilikuwa za watu ambao walikuwa wametembea kutoka hapo pwani kuelekea kwenye ule msitu ambao ulikuwa mbele yao.

"Ni akina nani hawa?" Mmoja wa makomando akauliza.

"Unauliza swali ambalo sio sahihi… hatuwezi kujua ni akina nani… lakini tunapaswa kujiuliza walichokuwa wanakifanya… tazama hapa!" Walker alijibu huku akiwaonyesha kitu fulani kwenye zile nyayo pale mchangani.
"Hizi ni seti za nyayo za watu zaidi ya nane au kumi kabisa… tazama hapa… hizi ni seti za watu wanne ambao wanaonekana walikuwa wamebeba kitu chenye pande nne"

"Kabisa… tazama hapa mbele inaonekana kuna mtu mmoja alitangulia na nyuma mtu mwingine.…" komando mwingine naye akaongeza.

"Walibeba kitu kama jeneza… lakini tazama hapa!" Walker akawaonyesha tena kitu fulanipale mchangani. "Kuna seti nyingine za nyayo ambazo zinaongozana na hizi lakini zimejitenga kidogo! Inaonekana walikuwa kama wasindikizaji.!"

"Au walikuwa wanafuatilia nyayo hizo nyingine kama sisi tunavyofanya!" Mzee Caleb alichangia kwakutoa wazo mbadala.

"Umewaza vyeama kabisa mzee… labda walikuwa nao wanafuatilia nyayo hizi zingine kama sisi.." Walker akaunga mkono wazo la Mzee Caleb.

Wakazitazama zile nyayo pale mchangani kwa umakini kwa dakika kadhaa na hatimaye wakakata shauri kuzifuatilia.

Walizifuatilia zile nyayo mpaka kuingia ndani kabisa ya msitu. Kama dakika ishirini hivi baadae, mbele yao umbali kama wa mita thelathini hivi kulikuwa na Kasri kuu kuu sana. Kama kasri la kifalme la miaka ya zamani mno. Kutokana na hali ya giza giza ambayo ilikuwepo pale walipo ilifanya wajihisi kama vile wako kwenye ulimwengu mwingine kabisa, ulimwengu wa kale wa kama karne kadhaa nyuma japo ilikuwa ni karne ya ishirini na moja mwaka 2038. Kasri hilo ambalo halikuwa na umeme au hali yoyote ya usasa, kwenye kuta zake zilikuwa zimening'inizwa chemli za mafuta ya taa kwa ajili ya kutoa mwangaza wa kasri hilo.

"Ni nini hiki?" Mmoja wa makomando aliuliza.

"Kuna njia moja tu ya kufahamu… tuingine ndani yake!" Walker akajibu huku akiwa amekaza macho yake kuelekea Kasri lilipo.

"Kama kuna ulinzi?" Mmoja wa wale makomando akauliza.

Swali lake hasa lilikuwa halimaanishi hasa wasi wasi wao kama kulikuwa na ulinzi wa kuzuia kuingia bali swali hilo lilikuwa linaakisi hofu waliyonayo kwamba labda walikuwa wanakabiliana na kitu cha tofauti kabisa ambacho hawawezi hata kupambana nacho kwa ujuzi na umahiri wao wa kijeshi.

"Tazameni.!" Mzee Caleb aliwagutusha kutoka kwenye mjadala wao na kuwaonyesga kidole kuelekea kule lilipo Kasri.

Kwenye geti lake kuu kuu, kulikuwa na watu wanatoka nje. Mzee Caleb, Walker na wenzake wakarudi nyuma kidogo na kujibanza nyuma ya mti huku wakichungulia kutazama wale ambao walikuwa wanatoka nje ya lile Kasri.
Walikuwa ni watu wanne, wanaume wawili na wanawake wawili. Kati yao, watu wawili, mwanamke na mwanaume walikuwa ni watu weusi na wawili wengine mwanamke na mwanaume walikuwa ni wazungu.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
"Hivi mnaona kile ambacho mimi nakiona?" Walker aliwauliza wenzake kwa kunong'ona lakini sauti yake ikionyesha kabisa taharuki ambayo alikuwa nayo.

Wote wakakodoa macho kutazama pale kwenye geti ili kung'amua kile ambacho Walker alikuwa anakiona.

"Mungu wangu, simani macho yangu.!!" Mzee Caleb akajishika mkono kifuani kwenye moyo kutokana na taharuki.

"Ndio Mzee… yule ni Vice President David Logan!!"

Walker aliongea huku wote wakiwa wamemkazia macho mwanaume wa kizungu ambaye alikuwa ameongozana na wale watu wengije watatu wakitoka ndani ya geti la lile Kasri.

"Tunafanyaje?" Moja ya makomando wale aliuliza.

"Yule ni Makamu wa Rais wa nchi yetu… ni lazima tuhakikishe kama yuko salama!" Walker aliongea huku bado akiwatazama wale watu ambao walikuwa wanatoka kwenye geti na David Logan.

"Lakini haonekani kama yuko kwenye hatari… anaonekana yuko hapa kwa hiari yake kabisa.!" Mzee Caleb akaongea.

"Ni jukumu langu kama afisa wa Ulinzi wa nchi yangu kuhakikisha yuko salama… lets go!" Walker ambaye ndiye alikuwa kamanda wa wenzake kwa sasa hakutaka kujadili zaidi… aliamuru wote wamfuate.

Walitembea kwa tahadhali kubwa kuwafuata wale watu pale getini.

"Kuweni tayari kwa lolote!" Walker aliwataahadhalisha wenzake kuwa macho ikitokea wakishambuliwa kwa ghafla.

Kadiri ambavyo walikuwa wanawasogelea kutoka msituni ndivyo ambavyo pia wale watu waliongozana na Logan na pamoja na Logan mwenyewe walisimama na kuanza kutazama msituni.
Yule mwanaume mmoja mweusi aliye pamoja na kina Logan alionekana kuwaonyeke ishara ya kidole mdomoni kwamba wanyamaze wasiongee kwa kuwa kuna kitu anakisikia msituni.

Ghafla… kufumba na kufumbua. Walker na wenzake waliruka kutoka msituni na kuwazunguka Logan na wenzake.

"Muweke salama Vice President!!" Walker aliamuru.

Mmoja ya mwanajeshi mwenzake alimnyakua David Logan kwa kasi na kumtenganisha na wale watu watatu ambao alikuwa nao.
Yule jamaa mweusi ambaye alikuwa na Logan aliruka kiustadi na kuanza kupambana na akina Walker. Alionekana dhahiri kuwa alikuwa ana uwezo mkubwa wa mapambano ya ngumi lakini kutokana na kuzidiwa wingi alidhibitiwa mara moja na wanajeshi wa Walker.

"Niko salama, niko salama… hawa ni watu wema waacheni… niko salama!" David Logan alisisitiza.

Aligundua kuwa hao walikuwa ni vijana kutoka kwenye moja ya vyombo vya Ulinzi nchini Marekani.

"Una hakika uko salama Mr. Vice President?" Walker aliuliza kwa msisitizo huku wanakukuruka kumdhibiti yule jamaa mweusi.

"Nimesema waacheni!" David Logan aliongea kwa mamlaka safari hii kwa kutoa amri.

Wakamuachia yule jamaa mweusi ambaye walimdhibiti kwa kumgandamiza chini kwenye mchanga.
Jamaa mweusi aliyeachiwa na akina Walker walikuwa bado wanaangaliana kwa hasira wote wakisubiri Logan aseme kitu kuweka mambo sawa.

"Uko salama Mr. Vice President?" Walker aliuliza tena kwa mara nyingine.

"Niko salama kabisa… mmefikaje hapa?" Logan akauliza kwa mshangao.

"Ni hadithi ndefu sana… labda utueleze wewe umefikaje hapa?" Walker alijibu swali kwa swali.

Wakiwa wanasuburi maelezo, macho ya Logan na Mzee Caleb yakagongana na Logan akamtambua.

"Mzee Caleb…! Ulisikia kiiichotokea Whitehouse?" Logan akauliza akikumbusha tukio lilitokea ambapo alivamiwa na mtu mwenye kufanana kabisa na Caleb.

"Nilisikia Muheshimiwa na nimewapa hawa maelezo ni nini kinaendelea… nitakueleza na wewe pia!" Mzee Caleb akaeleza kwa kifupi tu.

"Vipi mlifanikiwa kupata kile kitabu aaahh Book of… Book of…"

"BOOK OF CODES!" Mzee Caleb akamsadia David Logan kukumbuka.

Mara ya mwisho Logan na Mzee Caleb kukutana, ilikuwa ni pale ambapo Mzee Caleb alipelekwa Whitehouse na Mkurugenzi wa CIA Bw. James Rupert ili kueleza siri iliyomo ndani ya mchoro wa George Washington unaokaa Estern Room ya hapo Whitehouse. Kisha wakaondoka kwa pamoja mpaka Chuko Kikuu cha Stanford ambako walienda kutazama chupa ambayo iliokotwa huko Maldives na kufunguliwa na kuanzisha kizaa zaa cha miji kutwaliwa duniani. Japo waliikosa chupa hiyo kwa maelezo kwanba imeibiwa na mmoja wa wataalaku wa Idara ya Akiolojia ya chuo hicho ambaye amesafiri kwenda nchini Tanzania.

Kisha wakaondoka kutoka chuoni hapo kwa msafara wa pamoja ambao ulishambuliwa na watu wa ajabu ambao baadae walikuja kugundulika ni wapiganaji wa kikundi cha siri cha Sancta Cedes.
Ndipo hapa ambapo Mzee Caleb alitoa pendekezo la kwenda Maryland kwenye msitu wa Ox kwenye kaburi la babu yake ambako walifukia kitabu cha siri kinachoitwa BOOK OF CODES ili waweze kupambana na kikundi hicho cha siri cha Sancta Cedes.
Makamu wa Rais akatoa ruhusu mkurugenzi Mkuu wa CIA Bw. James Rupert ampatie Caleb na Naomi kikosi cha siri cha kijeshi cha CIA kinachoongozwa na Ethan kiongozana na Caleb na Naomi kwenye msitu wa Ox huko Marylanda.

"Ethan na Naomi wako wapi?" Logan akamuuliza Mzee Caleb baada ya kuunganisha nukta kwamba wanajeshi hao walio pamoja na Caleb watakuwa ni vijana wa Ethan.

"Walirudi Washington baada ya kupata taarifa kuwa umevamiwa Whitehouse!" Walker akajibu.

"Kwa hiyo mnamaanisha kwamba walienda Whitehouse?" Logan aliuliza kwa taharuki kiasi.

"Ndio Mr. Vice President." Walker akajibu.

"Damnt it! Lazima yule mwanamke atakuwa amewatia nguvuni!" David Logan aliongea kwa hasira huku amejishika kichwa.

"Mwanamke gani?" Wakajikuta wote wote wameuliza kwa pamoja.

"Madam President Laura Keith.!" Logan akajibu.

Wote wakashikwa na mshangao ghafla. Hawakuwa wanajua kile ambacho kilikuwa kinaendelea nyumbani Marekani.

"Nitawaeleza.!" David Logan akajibu tena kwa kifupi tu.

"Sawa Mr. Vice President… lakini hatujui tuko mahala gani hapa na ni muhimu tukijua nini kimetokea mpaka umefika hapa..!" Walker akauliza tena.

"Tupo Rabat, Morocco!" Cindy akajibu

"Samahani sikuwatambulisha… huyu ni Dr. Cindy Wheaton… Mzee Caleb yule mtaalamu wa Akiolojia ambaye tukiambiwa pale Stanford ameondoka na chupa ya Maldives na kwenda nayo Tanzania ndiye huyu… huyu hapa anaitwa Magdalena ni mtaalamu wa Biolojia kutoka Kenyatta University na huyu hapa ni Salim, Afisa ya Idara ya Usalama nchini Tanzania.!" Logan alifanya utambulisho wa haraka haraka.

Mzee Caleb, Walker na wenzake walibakia wametumbua macho tu kama wamechanganyikiwa. Walikuwa wanajiuliza ni namna gani Makamu wa Rais David Logan siku kama moja au mbili nyuma alikuwa Whitehouse amevamiwa na watu wasiojulikana kwa mujibu wa taarifa waliyoipata na sasa hivi yuko hapa na watu kutoka Tanzania na Kenya. Ulikuwa ni mkanganyiko mkubwa vichwani mwao.

"Mr. Vice President nadhani unaweza kuhisi ni namna gani tumechanganyikiwa vichwani mwetu!" Walker akaongea tena.

"Nafahamu… lakini hatuna muda wa kupoteza! Tunapaswa kufika sehemu haraka sana!"

"Sehemu gani?"

"Tunapswa kutafuta Hekalu la Mungu Zeus lilipo hapa Rabat!" Logan aliongea huku anaanza kutembea.

Sio Mzee Caleb, Walker na wanajeshi wenzake pekee ambao walishtuka bali pia hata Cindy, Magdalena na Salim. Walipotoka ndani ambako walimkuta kama amechanganyikiwa na baadae akili zake kukaa sawa baada ya kipigo kutoka kwa Salim, hakuwaeleza wanaenda wapi bali aliwaambia tu wamfuate. Sasa hivi ndio walijua kuwa wanatakiwa kwenda kwenye hekalu la Mungu Zeus. Kwa mtaalamu wa akiolojia kama Cindy alishituka zaidi kwa maana alifahamu fika ni namna gani suala hilo haliwezekani. Kwa sababu moja Hekalu la Zeus lilikuwepo yapata miaka elfu thalathini iliyopita na pili kwa mujibu wa historia hakuna binadamu ambaye amewahi kukanyaga mguu ndani ya hekalu hilo zaidi ya miungi kumi na mbili ya Kigiriki.

"Hekalu la Zeus!" Cindy alirudia kichwani huku akiongozana na wenzake kumfuata David Logan.


Itaendelea…


*The Bold*
To Infinity and Beyond

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Mkuu nikiingia kwny group nitawezaje kuwa sambamba na wenzangu kwa episod zilizopitA yani zilizo tangulia nikiwa sipo grupuni Habibu B. Anga
 
Habibu B. Anga samahani ila group ki kawaida, kwa mwezi stor kama ngapi unaweka mwanzo mwisho yani full package ngapi?? ayo tu,,
 
IMG_3684.jpg

Kitabu changu cha kwanza NYUMA YA ULIMWENGU WA SIRI & UJASUSI kiko tayari na kitakuwa mkononi mwako mwezi huu september... kaa tayari
 
1b9a9f4142386cb81f0be1d549b2d08e.jpg



EPISODE 21 IKO HEWANI TAYARI.... TAFADHALI TEMBELEA TOVUTI ILI KUISOMA...

kuisoma kwa urahisi, nenda chini kabisa kwenye Categories kisha chagua "SHORT STORIES"...

AU

Tazama juu kabisa upande wa kuna kitufe cha (search) andika chaguo lako, mfano " The other half Episode 21"... Kisha search..

AU

Upande wa juu kushoto kuna vimistari vinne, bofya hapo utapata Mennu na kisha chagua "short stories".
Utaratibu wako kwakweli unakera,unaanzisha hadithi humu mara zinaamia kwenye tovuti,mara kwenye whasap mara kwenye kitabu.nadhan ni vizur zilizomo humu ziendelee humu,za kwenye tovuti ziwe kule,za whasap ziwe kule na za kwenye kitabu ziwe ni nyingine zinazojitegemea
 
Episode 15 kule kwenye website haipo sijui imefutwa?baada ya 14 inafuatia 17
 
Back
Top Bottom