SoC01 Thamani isiyoonekana

Stories of Change - 2021 Competition

Ditrik Deogratias

New Member
Jul 15, 2021
1
1
Mambo mengi na vitu vingi malimbali ambavyo tumekua tukivifanya binadamu na kutaka kuvifanikisha , mara nyingi huwa na mwanzo mgumu na wa kitofauti. Hii ni kutokana na matarajio makubwa sana ambayo huwa tunayawaza na kuyatengenezea picha kwenye ufahamu wetu, na kutamani kuona yakitokea mara tu tuanzapo kuyafanya yale tunayotaka yatokee hata kabla ya kuanza kuyafanya rasmi.

Ufanikishaji huonekana kua mgumu na wa kitofauti kwasababu mara nyingi picha ambayo huwa tunaijenga kwenye ufahamu wetu kabla ya utendaji huwa haipitii hatua zote za utokeaji wa yale tuliyoyapanga. Lakini pia haioneshi changamoto zote tutakazopitia, hivyo kuufanya utendaji na ufanikishaji wa yale tuliyopanga kwenda tofauti. Mara nyingi baada ya kuonekana kwa utofauti na ugumu huo hupelekea mtu husika kughairi ama kubadilisha lengo ambalo alikua amelikusudia kulifanya.

Mti mkubwa ambao tunauona kwenye uso wa dunia umependeza, unavutia kwa matawi yake na shina imara ambalo mti unao, ni kutokana na mchakato ama hatua ambazo zilichukuliwa na mbegu yake chini ya ardhi hapo mwanzo kabisa wakati wa ukuaji. Hizo hatua zote ambazo mbegu hupitia ili mti huo mkubwa kuja kuonekana na kufika katika hatua ya kupendwa kutokana na kupendeza kwake hua hazionekani. Hizo hatua ambazo hazionekani ndio thamani isiyoonekana ambayo imesababisha mti mkubwa tunaouona kupendwa.

Nyumba nzuri na ya kifahari ambayo hua inapendeza kwa muonekano wake huwa ni kutokana na aina ya msingi ambao ulijengwa mwanzoni kabisa wa ujengaji wa nyumba kabla ya chochote. Na msingi huo baada ya nyumba kukamilika huwa hauonekani wala kuzingatiwa sana. Urefu wa mlima tunaouona kupitia macho yetu, kijiografia inasemekana kwamba mlima huo una urefu kama huohuo kwenda chini ya ardhi yaani chini ya uso wa dunia. Lakini pia mchango wa watu tusiowafahamu ni mkubwa kupita wa wale tunaowafahamu.

Hii ni kutokana na asilimia kubwa ya vitu tunavyovitumia katika maisha yetu ya kila siku vimesababishwa na hao tusiowafahamu, kila siku tunakula chakula lakini hatuwafahamu waliolima au kufuga, tunatumia vyombo vya usafiri kwenda sehemu mbalimbali lakini hatujui waliovitengeneza, tuna samani mbalimbali majumbani mwetu lakini hatujui malighafi zake ziliandaliwa na kina nani.Hii ni thamani isiyoonekana.

Kupitia mifano hiyo kadhaa tumeona thamani isiyoonekana kama ni kitu chenye umuhimu mkubwa kwenye ufanyaji wa jambo. Utekelezaji na uanzishaji wa jambo lolote huanzia mbali, mahali ambapo hata faida ya jambo hilo inaweza isionekane. Kiwanda kinapoanzishwa kinaweza kufanya kazi nyingi za bure ama za faida ndogo sana ili tu kujitengenezea nafasi ya kazi zake kuonekana. Kutokea hapo thamani ya zile kazi zilizofanyika wakati kiwanda kinaanzishwa inaweza isionekane lakini kiukweli ndizo kazi halisi zilizochangia kutengeneza msingi na maendeleo ya kiwanda.

Ni kama tu mbegu ya ule mti mkubwa ilivyokua ardhini, kila kilichokuwemo ndani ya mbegu kilitumika mpaka kikaisha, mbegu ikaoza na ndipo taratibu mmea ukaanza kutengenezwa na kutokea juu ya ardhi. Mmea ukakua na ukawa mti mkubwa ambao mandhari yake ikapendeza, yote ni kutokea kule kwenye hatua ambazo hazikuonekana ambazo zilichukuliwa na mbegu. Thamani isiyoonekana ni ya muhimu. Mwanzo mdogo nao ni thamani isiyoonekana.

Thamani isiyoonekana, hatua zisizoonekana

Ditrik Deogratias.
 
Back
Top Bottom