UZUSHI Tembe za Paracetamol (P-500) huwa na Virusi vya Machupo ambaVyo ni hatari kwa Afya

Baada ya tathmini, tumebaini kuwa taarifa hii ni ya uzushi
Kuna taarifa zinasambaa Mtandaoni zikidai kuwa tembe za Paracetamol zenye jina la P-500 siyo salama kwa afya.

PARACETAMOL UZUSHI.jpg

Taarifa hii inawataka watu kutukutumia dawa hii kutokana na uwepo wa virusi vya Machupo ambavyo ni hatari kwa afya, vinaua.

Ukweli wa taarifa hii upoje?
 
Tunachokijua
Paracetamol (Acetaminophen, N-acetyl-p-aminophenol), ni dawa ya kushusha homa na kutuliza maumivu iliyoguduliwa mwaka 1893. Kwa mujibu wa takwimu za Statista, Paracetamol ni dawa ya maumivu inayotumika zaidi duniani, ambapo kwa mwaka 2022 ilishika namba 1 kama dawa iliyotumika zaidi nchini Uingereza.

Dawa hii hufahamika pia kwa majina ya kibiashara kama Panadol, Calpol, Alvedon na Tylenol.

Madai ya dawa hi kubeba Virusi aina ya Machupo
Utafutaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck umebaini kuwa madai ya tembe za Paracetamol (P-500) zenye virusi hatari vya machupo yamekuwepo kwa miaka mingi.

Mathalani, mwaka 2017 na 2019, taarifa zenye madai haya tayari zilikuwepo Mtandaoni.

68425858.jpg

Picha yenye ujumbe wa Madai hayo (Times of India, 2019)

Huu ni ushahidi kuwa madai haya siyo mapya pamoja na kuonekana yakisambaa tena mtandaoni mwaka huu (2024).

Mamlaka za Tanzania zinasemaje?
Agosti 21, 2019, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), chombo cha udhibiti kilicho chini ya Wizara ya Afya, chenye jukumu la kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na uchunguzi nchini ilitolea ufafanuzi suala hili kupitia taarifa yao kwa Umma.

Pamoja na mambo mengine, taarifa hiyo ilisema:

"Mamlaka hivi karibuni ilibaini kupitia mitandao ya kijamii uvumi ulioenea sana ukipendekeza kuwa bidhaa ambayo ni P-500® (Paracetamol) inayotengenezwa na Apex Laboratories Private Limited, Tamil Nadu, India ina virusi vya 'Machupo' ambayo inadaiwa kwa uwongo kusababisha Bolivian Hemorrhagic Fever (BHF).

Umma unafahamishwa kuwa hakuna virusi hivyo vinavyojulikana kama Machupo na hakuna virusi vinavyoweza kuishi kwenye tembe za dawa."


Aidha, TMDA ilibainisha kuwa bidhaa ya P-500® (Paracetamol) inayotengenezwa na Apex Laboratories Private Limited, India haijasajiliwa Tanzania na Mamlaka haijawahi kutoa kibali chochote cha uingizaji wa bidhaa hiyo.

Uthibitisho wa taasisi zingine Duniani
JamiiCheck imetafuta taarifa hizi mtandaoni na kubaini kuwa hazipo Tanzania pekee, pia taasisi kadhaa zimewahi kutolea ufafanuzi wake.

Agosti 2, 2017, Serikali ya Singapore iliwaasa wananchi wake kupuuza uzushi huo na kuwataka wasiisambaze zaidi pindi wanapotumiwa.

The Hindu (2017), Indian Times (2023), The Cable (2023), Africa Check (2023), AFP (2022) na Namibia Fact Check (2022) ziliwahi kukanusha pia madai haya.

Virusi vya Machupo (Machupo Virus) husababisha homa na kuvuja damu. Pia, kumekuwepo na idadi ya milipuko ya virusi vya Machupo katika baadhi ya maeneo ya Bolivia tangu mwanzoni mwa miaka ya 1950 ambapo asili ya ugonjwa huu hutajwa, lakini milipuko hii kwa kiasi kikubwa imekuwa katika maeneo maalum katika nchi hiyo, kulingana na maandiko kuhusu virusi hivyo.

Maambukizi ya ugonjwa huu huambatana na dalili za homa kali, maumivu ya misuli ya mwili, kuvuja kwa damu kwenye fizi pamoja na kifafa. Pia, huambukizwa kwa kukutana na mate, kinyesi au mikojo yenye vurusi vya Machupo kutoka kwenye panya wenye ugonjwa.

Kwa sasa, visa vya ugonjwa huu vimebainika kuwepo kwenye bara la Amerika Kusini pekee.

Ushauri
JamiiCheck inaiasa jamii kuacha kusambaza taarifa za upotoshaji, zisizo na mashiko, zisizothibitishwa au zisizo sahihi zinazohusu dawa, vifaa tiba na uchunguzi kabla ya kuwasiliana rasmi na Mamlaka ili kuepusha hofu na taharuki kwenye jamii.
3 Reactions
Reply
Back
Top Bottom