TCU KUSITISHA MASOMO NA KUHAMISHA WANAFUNZI WANAOENDELEA NA MASOMO KATIKA BAADHI YA VYUO VIKUU NCHINI

Sep 30, 2018
15
5
Updates From:
MPELLA EDUCATION BLOG



1.0 Utangulizi

Itakumbukwa kwamba mwaka 2016 Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania ilifanya ukaguzi maalum wa kuhakiki ubora katika vyuo vya elimu ya juu nchini. Aidha Tume iliendelea kufanya ukaguzi wa kawaida na wa kushtukiza katika baadhi ya Vyuo Vikuu kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo. Kutokana na matokeo ya ukaguzi huo, Tume imebaini kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazoathiri utoaji wa elimu bora katika baadhi ya vyuo.




2.0 Maamuzi ya Tume

Kutokana na changamoto za ubora zilizobainishwa katika ukaguzi uliofanywa na Tume, na kwa kuzingatia umuhimu wa kuwa na wahitimu wenye kukidhi viwango bora vya elimu kitaifa na kimataifa kwa manufaa yao binafsi, jamii zao na Taifa kwa ujumla, Tume imefanya maamuzi yafuatayo:


2.1. Kufuta Vituo Viwili vya Vyuo Vikuu na kuamuru Wanafunzi wote wanaoendelea na masomo wahamishwe Tume imefuta vibali vilivyoanzisha Vituo vya Vyuo Vikuu vifuatavyo na kuamuru wanafunzi wote wanaoendelea na masomo kuhamishwa mara moja kabla ya kuanza kwa muhula wa kwanza wa mwaka wa masomo 2018/19. 1. Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji – Kituo cha Tabora (TEKU – Tabora Centre); na 2. Chuo Kikuu cha Mt. Yohana cha Tanzania – Kituo cha Msalato (SJUT – Msalato Centre).


2.2. Kusitisha utoaji wa mafunzo na kuamuru Wanafunzi wote wanaoendelea na masomo wahamishwe Tume imesitisha utoaji wa mafunzo kwa ngazi zote kwenye vyuo vifuatavyo na kuamuru wanafunzi wote wanaoendelea na masomo wahamishiwe katika Vyuo Vikuu vingine:


1. Chuo Kikuu cha Mlima Meru (MMU);

2. Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UoB);

3. Chuo Kikuu cha Eckernforde Tanga (ETU);

4. Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta – Kituo cha Arusha (JKUAT – Arusha Centre); na

5. Chuo Kikuu Kishiriki cha Josiah Kibira (JOKUCo)


Vyuo hivi viko chini ya uangalizi maalumu na hivyo hawaruhusiwi kudahili wanafunzi wapya kwa ngazi zote za masomo (kuanzia astashahada, stashahada, shahada, shahada ya uzamili, hadi Shahada ya Uzamivu) kwenye programu zote za masomo.



2.3. Kuzuia udahili wa wanafunzi wapya Tume imezuia udahili wa wanafunzi wapya kwa ngazi zote za masomo na katika programu zote kwenye Vyuo Vikuu vifuatavyo:


1.Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala nchini Tanzania (KIUT);

2.Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU);

3.Chuo Kikuu Kishiriki cha Marian (MARUCo);

4.Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Kadinali Rugambwa (CARUMUCo);

5.Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastina Kolowa (SEKOMU);

6.Chuo Kikuu cha Mt. Yohana cha Tanzania – Kituo cha Mt. Marko (SJUT – St. Mark’s Centre); na 7.Chuo Kikuu cha Umoja wa Afrika Tanzania (UAUT).


Vyuo hivi pia viko chini ya uangalizi wa Tume, vitaendelea kutoa mafunzo kwa wanafunzi wanaoedelea na masomo na hawaruhusiwi kudahili wanafunzi wapya kwa ngazi zote za masomo (kuanzia astashahada, stashahada, shahada, shahada ya uzamili, hadi Shahada ya Uzamivu) kwenye programu zote za masomo mpaka hapo itakapoamriwa vinginevyo.


3.0 Hitimisho

Tume inavitaka Vyuo Vikuu Vyote vilivyotajwa katika taarifa hii kuzingatia na kutekeleza maelekezo haya. Aidha, Tume inawaarifu wanafunzi wote wanaotakiwa kuhama kuwasiliana na Vyuo vyao kwa ajili ya maelekezo kuhusu taratibu za kuhama na vyuo wanavyotakiwa kuhamia.


Taarifa hii pia inapatikana kwenye Tovuti ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).


Imetolewa na KATIBU MTENDAJI 25/09/2018
 
Back
Top Bottom