esther mashiker
JF-Expert Member
- May 29, 2018
- 616
- 552
TANZANIA imeweka rekodi yake ya kuwa na akiba ya fedha za kigeni, sasa ikiwa na Dola za Marekani milioni 5,079.0, sawa na zaidi ya Sh trilioni 11, kiasi ambacho ni kikubwa zaidi tangu taifa hili lijipatie uhuru. Aidha, kwa kiwango hicho, Tanzania imevuka lengo la nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) la kujiwekea akiba ya fedha za kigeni inayokidhi uagizaji wa bidhaa kwa miezi 4.5. Akizungumza juzi jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya hali ya uchumi wa taifa na utekelezaji wa Bajeti ya Serikali katika kipindi cha nusu mwaka kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema kwa akiba ya Tanzania, kiasi hicho kinaweza kukidhi kuagiza bidhaa na huduma kwa miezi mitano.
Hii ina maana kwamba, kiwango hicho cha akiba ya fedha za kigeni ni zaidi ya lengo la Serikali la kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayokidhi uagizaji wa bidhaa na huduma kwa miezi 4. Uchumi wa taifa Alisema Uchumi wa Taifa umeendelea kuwa imara, ukikua kwa asilimia 7.1 katika mwaka 2017, ikilinganishwa na wastani wa ukuaji wa 7.0 kwa miaka miwili iliyopita, yaani 2015 na 2016. Na kwa nchi za EAC, uchumi wa Tanzania ulikuwa kwa kasi zaidi 7.1% mwaka 2017 ukilinganisha na Rwanda (6.1%), Uganda (5.1%), Kenya (4.9%) na Burundi (0.0%). Pia Tanzania iliongoza katika ukuaji wa Uchumi kwa nchi za SADC. Aidha, kwa mujibu wa Dk Mpango, nchi imeendelea kuwa miongoni mwa nchi 5 bora kwa kasi ya ukuaji wa uchumi katika bara la Afrika katika nusu ya kwanza ya 2018, ikijumuisha Ethiopia (8.5%), Ivory Coast (7.4%), Rwanda (7.2%), Tanzania (7.0%), na Senegal (7.0%).
Akizungumzia mfumuko wa bei, alisema kati ya Julai na Novemba 2018, Tanzania ilikuwa na kiwango kidogo zaidi cha mfumuko wa bei ikilinganishwa na Uganda (3.3%) na Kenya (4.8%). “Mfumuko wa bei umeendelea kupungua kutoka wastani wa asilimia 4.3 mwaka 2017/18 hadi kukia kiwango cha chini kabisa kuwahi kutokea katika miaka ya karibuni cha asilimia 3.0 mwezi Novemba 2018,” alisema msomi huyo aliyebobea katika masuala ya uchumi na mipango. Mapato ya ndani Alisema katika kipindi cha miezi mitano ya kwanza ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19, Serikali imeweza kukusanya mapato ya ndani ya Sh trilioni 7.37 sawa na asilimia 88.9 ya makadirio ya kukusanya Sh trilioni 8.30 katika kipindi hicho.
Alifafanua kuwa, makusanyo hayo yanayojumuisha mapato ya halmashauri yamekusanywa kuanzia Julai hadi Novemba mwaka huu. Alisema katika makusanyo hayo, mapato ya kodi yalikia Sh trilioni 6.23 ikiwa ni asilimia 88 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 7.04 kwa kipindi hicho.
Aliongeza kuwa, ongezeko la mapato yasiyo ya kodi limetokana na kuimarishwa kwa ufuatiliaji kwenye Taasisi, Mashirika na Kampuni kulikoiwezesha serikali kupata michango na gawio stahiki kutoka kwenye uwekezaji wake. Matarajio mwaka 2019 Akizungumzia matarajio hadi Juni 2019, Dk Mpango alisema uchumi unatarajiwa kuendelea kukua kutokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea kwenye miundombinu wezeshi ya uzalishaji mali kama vile barabara, madaraja, bomba la mafuta, ujenzi wa reli kwa kiwango cha kimataifa na viwanja vya ndege; Ujenzi wa kituo cha kufua umeme utokanao na nguvu za maji katika Mto Ruji chenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,100 kwa ajili ya matumizi ya majumbani na viwandani.