Tanzania imejiondoa rasmi kwenye kipengele cha Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) kinachoruhusu watu binafsi kuishtaki Serikali

Arusha. Tanzania imejiondoa rasmi kwenye kipengele cha Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) kinachoruhusu watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali kuishtaki Serikali baada ya kupita mwaka mmoja tangu ilipoandika kusudio la kujiondoa.

Tanzania iliandika kusudio la kujitoa Novemba 21, 2020, katika ibara ya 34 (6) ya mahakama ya Afrika ya Haki za binadamu na watu, ambayo inaruhusu watu binafsi na asasi zisizo za kiserikali kuishtaki Serikali.

Kanuni zinazoongoza mahakama hiyo zinaelekeza pale kusudio la kujiondoa linapodumu kwa mwaka mmoja, nchi inakuwa imejitoa moja kwa moja.

Desemba 4, mwaka jana, akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya Tanzania kuripotiwa kuandika barua ya kuomba kujiondoa katika itifaki hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema Serikali iliandika barua ya kuomba kujitoa kwa muda katika itifaki hiyo, baada ya kutoridhishwa na baadhi ya mambo yaliyokuwa yakiendelea.

Hata hivyo, Tanzania itabakia kuwa mwanachama wa mahakama hiyo kutokana na kuendelea kuheshimu kipengele cha mwongozo uanzishwaji wa mahakama hiyo.
Uamuzi huo wa Tanzania umepokelewa kwa maoni tofauti na uongozi wa mahakama hiyo na pia wanasheria .

Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu imetoa mwito kwa Tanzania kufikiria upya uamuzi wake wa kuondoa tamko linalowazuia watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali nchini kufungua kesi dhidi ya yake kwenye ya mahakama hiyo yenye makao yake makuu jijini Arusha.

Msajili wa Mahakama hiyo, Dk Robert Eno akizungumza katika mahojiano na televisheni ya UTV juzi, alisema ingawa ni haki ya kila nchi iliyoridhia itifaki ya kuanzishwa kwa mahakama hiyo kukubali au kukataa watu wake ama asasi za kiraia kupeleka mashauri yake, lakini Tanzania ikiwa kama nchi mwenyeji inapaswa kutafakari upya uamuzi iliouchukua.

Kati ya nchi 55, wanachama wa Umoja wa Afrika(AU) ni nchi 33 pekee zilizoridhia uanzishwaji wa mahakama hiyo na kati ya hizo ni nchi tisa ndizo zilizoridhia watu wake na mashirika binafsi kupeleka mashauri yake mbele ya mahakama hiyo.

Nao wanasheria wametoa maoni tofauti kufuatia uamuzi wa Tanzania kujiondoa, Mhadhiri Mwandamizi wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Tumaini kilichopo Makumira mkoani hapa, Dk Elifuraha Laltaika alisema licha ya kuwa mtu binafsi na asasi zisizo za kiserikali hazitaweza kufungua kesi moja kwa moja katika mahakama hiyo jijini Arusha, pia zinaweza kufungua kupitia Kamisheni ya Haki za Binadamu yenye makao yake katika mji wa Banjul nchini Gambia.

Laltaka alitahadharisha jambo hilo linapaswa kutokuzwa kuonyesha kwamba ndio mwisho wa watu na mashirika yasiyo ya kiserikali kufungua kesi katika mahakama hiyo.

“Mlango mmoja ukifungwa mwingine unakuwa wazi na jambo lililofanyika si kwamba Tanzania imejiondoa kwenye itifaki ya mkataba ulioanzisha mahakama ya Afrika, bali imejiondoa kwenye tamko la kuridhia watu binafsi na asasi za kiraia kufungua kesi moja kwa moja,” alieleza Laltaka.

Dk Laltaika alisema kuwa hatua hiyo bado inaifanya Tanzania kuendelea kuwa mwanachama halali wa mahakama hiyo na inaweza kushtakiwa kupitia Kamisheni ya Haki za Binadamu.

Naye Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wanasheria Afrika (Palu), Donald Deya alisema uamuzi wa Tanzania kujitoa katika kipengele hicho cha kutoshtakiwa na watu binafsi na taasisi si jambo zuri kwani bado kulikuwa na fursa ya kufanya majadiliano na kumaliza tofauti ambazo zilijitokeza.

Deya alisema kwa sasa Watanzania walio wengi watakosa fursa hiyo, kwa itabidi wapeleke mashtaka yao kamisheni ya haki za binadamu ya Afrika ambayo ina wanachama nchi 54 ambayo nayo itakaa na kuyapitia na ikijiridhisha ndio italeta katika mahakama hiyo ya Afrika jijini Arusha.

“Mahakama hii ilikuwa ni fursa nzuri kwa Watanzania kufungua mashtaka lakini wanaweza kufungua kesi kwa mtandao na kupeleka Gambia,” alisema.

Mwananchi

Huko kipindi cha nyuma kila kitu tulikiendea kichwa kichwa kwa hofu ya kunyimwa misaada. Mahakama ya Afrika iliyobeba maslahi ya mabeberu.

Serikali isishie hapo tujitoe na hii ya EAC inayotumiwa na mabeberu na vibaraka wao kuhujumu bomba la mafuta la Hoima- Tanga.
 
Wanaanza kujiondoa taratibu, leo wameanza na kipengele hicho kesho watahamia kingine, mwisho wa siku watajitoa kabisa.

Hii nchi imeshapoteza mwelekeo, sasa tunajiendea tu.
duuuuuuh . . . . . . sijaiona mantiki ya jumla jumla ya kujiondoa hiyo mahakama ya haki za binadamu barani Afrika. Huu ndio mwanzo wa kuwa na mazonge zonge sehemu kibao
 
Back
Top Bottom