Lipumba atajwa Baraza jipya la Mawaziri• RAIS KIKWETE ASHANGILIA WABUNGE KUWASULUBU MAWAZIRI
na Bertha Mwambela, Tanga
WAKATI macho na masikio ya Watanzania yakielekezwa kwa Rais Jakaya Kikwete aliyeahidi kufanya mabadiliko makubwa kwenye baraza lake la mawaziri, jina la Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ni miongoni mwa majina yanayotajwa kuwapo kwenye baraza hilo, Tanzania Daima Jumatano limebaini.Profesa Lipumba ambaye si miongoni mwa wabunge, anatajwa kuwa mmoja wa mawaziri watakaoteuliwa kutoka nje ya wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Duru za kisiasa kutoka ndani ya CCM na CUF, zinaeleza kuwa Rais Kikwete anatarajia kumwingiza Profesa Lipumba kwenye baraza lake na kwamba anaweza kumpa wizara ya Fedha na Uchumi."Kuna taarifa kwamba Profesa Lipumba anaweza kuwa miongoni mwa sura mpya za mawaziri. Anachoweza kufanya Rais ni kumteua kuwa mbunge, kisha kumpa uwaziri."Na kwa vile Bunge linatarajiwa kukutana Juni 12 mjini Dodoma, kama kuna watu kutoka nje ya Bunge ambao Rais anataka wawemo kwenye baraza lake, anaweza kuwateua kuwa wabunge na mawaziri wateule hadi hapo watakapoapishwa bungeni, ndipo ataweza sasa kuwaapisha kuwa mawaziri," kilisema chanzo chetu cha habari.Alipoulizwa na gazeti hili kwa njia ya simu, Profesa Lipumba alisema kuwa hawezi kuzungumzia uvumi huo kwani hata yeye ameusikia kutoka kwa watu mbalimbali."Siwezi kuzungumzia nafasi yangu kuhusu taarifa hiyo, lakini ukweli ni kwamba hadi sasa sijaitwa na Rais kwa ajili ya mashauriano yoyote kuhusu jambo hilo na kimsingi najua kama ana mpango huo, angeniita, lakini sijaitwa na sina taarifa," alisema Profesa Lipumba.
SOURCE: TANZANIA DAIMA, 2 Mei 2012