TANROADS imesaini mikataba ya ujenzi wa barabara ya Mnivata – Newala – Masasi (km 160) kwa kiwango cha lami na ujenzi wa daraja la Mwiti

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania kupitia TANROADS imesaini mikataba ya ujenzi wa barabara ya Mnivata – Newala – Masasi (km 160) kwa kiwango cha lami pamoja na ujenzi wa daraja la Mwiti lengo likiwa ni kuwaondolea wananchi kero ya usafiri wa barabarani na kuboresha mtandao wa barabara na madaraja ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji, hivyo kukuza uchumi wa nchi.

Akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini mikataba hiyo iliyofanyika leo tarehe 21 Juni, 2023 katika uwanja wa Sabasaba wilayani Newala mkoani Mtwara, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, amesema pia Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara ya kutoka Mtwara hadi Mnivata yenye urefu wa km 50 kwa kiwango cha lami.

Amesema barabara hiyo ni kiungo muhimu kwa barabara kuu ya kutoka Mtwara mpaka Mbamba Bay inayojulikana kama Ushoroba wa Mtwara (Mtwara corridor) ambayo inaunganisha na nchi jirani ya Msumbiji, ambapo pamoja na manufaa hayo makubwa pia inatarajiwa kwamba shughuli za kiuchumi za wananchi waishio maeneo mradi huo zitaimarika kwani mradi utasaidia kutengeneza ajira kwa wananchi wakati wa ujenzi.

Waziri Mbarawa amesema Ujenzi wa barabara hiyo utakapokamilika utasaidia kuondoa adha ya usafirishaji wa mizigo na abiria, kuongeza usalama kwa wote, itatoa mchango mkubwa katika shughuli za utalii, kuunganisha na kuboresha hali ya usafiri na usafirishaji wa malighafi za viwandani kama vile makaa ya mawe na cement, mazao ya chakula na kilimo, mifugo, uvuvi, bidhaa za kibiashara na mazao ya misitu kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mtwara pamoja na mikoa jirani ya Lindi, Ruvuma na Pwani kwenda maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Mohamed Besta amesema mradi umegawanywa sehemu mbili ili kurahisisha utekelezaji wake ili kukamilisha mradi ndani ya muda mfupi. Sehemu ya kwanza ni kutoka Mnivata hadi Mitesa yenye urefu wa km 100, Mkandarasi ni Kampuni ya China Wu Yi Co. Ltd kutoka China kwa gharama ya Shilingi bilioni 141.964 na ujenzi umepangwa kukamilika katika muda wa miezi 36.

Sehemu ya pili ya barabara ya Mnivata - Newala - Masasi (km 160) imesainiwa mkataba leo kutoka Mitesa hadi Masasi yenye urefu wa km 60 pamoja na ujenzi wa daraja la Mwiti, Mkandarasi ni Kampuni ya China Communications Construction Co. Ltd kutoka China kwa gharama ya shilingi bilioni 92.548, na ujenzi umepangwa kukamilika katika muda wa miezi 30.

Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mha. Mohamed Besta ametoa maagizo kwa Wakandarasi wa mradi huo kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu ili kazi zikamilike ndani ya muda uliopangwa kwa viwango na gharama zinazokubalika huku akiwahakikisha Wananchi kuwa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) utasimamia utekelezaji wa mradi huo kikamilifu na kuhakikisha kuwa unazingatia viwango vya kiufundi (Technical Standards) na unakamilika kwa wakati.
1527819685.jpg
-151102350.jpg

Muonekano ya sehemu ya kwanza kutoka Mnivata hadi Mitesa yenye urefu wa km 100, Mkandarasi ni Kampuni ya China Wu Yi Co. Ltd kutoka China kwa gharama ya Shilingi bilioni 141.964 na ujenzi umepangwa kukamilika katika muda wa miezi 36.
-92046848.jpg
-1298376532.jpg

Sehemu ya pili ya barabara ya Mnivata - Newala - Masasi yenye km 160 iliosainiwa mkataba leo ni kutoka Mitesa hadi Masasi yenye urefu wa km 60 pamoja na ujenzi wa daraja la Mwiti, Mkandarasi ni Kampuni ya China Communications Construction Co. Ltd kutoka China kwa gharama ya shilingi bilioni 92.548, na ujenzi umepangwa kukamilika katika muda wa miezi 30.
 
....na ujenzi wa daraja la Mwiti
===
Mleta mada una visa kumbe. Umenishtua ujue
 
Kuna kipande cha zaidi ya km 25 kutoka Mpeta hadi masasi mjini tayari kina lami,je itaondolewa iwekwe mpya? maana naona imejumuishwa kwenye idadi ya kilometer za ujenzi.
 
Acha niwahi kupongeza kabla wale majuha hawajaja kuidai bandari yao hapa.

Kongole sana TANROADS mnaupiga mwingi.
Unaita mwenzako juha kisa tu mmetofautiana kimtizamo..inabidi ujitafari wewe kwanza.
 
Amesema barabara hiyo ni kiungo muhimu kwa barabara kuu ya kutoka Mtwara mpaka Mbamba Bay inayojulikana kama Ushoroba wa Mtwara (Mtwara corridor) ambayo inaunganisha na nchi jirani ya Msumbiji, ambapo pamoja na manufaa hayo makubwa pia inatarajiwa kwamba shughuli za kiuchumi za wananchi waishio maeneo mradi huo zitaimarika kwani mradi utasaidia kutengeneza ajira kwa wananchi wakati wa ujenzi.
Mngekuwa mnaweka hata ramani kwa hisani ya Google map au earth mbona ni bure tu hailipiwi sisi wengine hatujui hiyo mitaa
 
Mngekuwa mnaweka hata ramani kwa hisani ya Google map au earth mbona ni bure tu hailipiwi sisi wengine hatujui hiyo mitaa
Wewe naye. Si umetajiwa majina na sehemu? Unashindwa nini kutafuta kwenye Google? Kila kitu utafuniwe?
 
Back
Top Bottom