UTPC
Journalists' Union
- Apr 17, 2026
- 31
- 22
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe umebaini kuwa katika maeneo mengi ya kata hizo taka zimejaa kando ya barabara, katika mitaro, kwenye maeneo ya wazi na hata karibu na nyumba za watu, hali inayozua hofu ya kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko.
Licha ya kuwapo sheria na kanuni zinazosimamia usafi wa mazingira, utekelezaji wake unaonekana kulegalega huku mamlaka husika zikionekana kushindwa kudhibiti tatizo hilo.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, pamoja na Kanuni za Usimamizi wa taka Ngumu za mwaka 2009, taka zinapaswa kukusanywa, kuhifadhiwa na kutupwa katika maeneo rasmi yaliyoidhinishwa ili kulinda afya za wananchi na mazingira.
Hata hivyo, katika kata hizo tatu, hali halisi inaonesha kuwa sheria hizo zimebaki kwenye karatasi huku wananchi wakiendelea kuishi katika mazingira hatarishi.
Takwimu kutoka Manispaa ya Morogoro zinaonesha kuwa jiji hilo huzalisha takriban tani 377 za taka ngumu kila siku.
Lakini uwezo wa manispaa kukusanya taka hizo ni takriban asilimia 73 pekee, jambo linalomaanisha kuwa karibu asilimia 27 ya taka, sawa na tani 101.79, hubaki mitaani kila siku bila kukusanywa.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Taka na Usafirishaji Manispaa ya Morogoro, Hezron Ligala, anakiri kuwa jukumu la kitengo hicho ni kuhakikisha mji unakuwa safi kwa kuondoa taka zinazozalishwa.
Lakini takwimu hizo zinaonesha wazi kuwa mfumo wa usimamizi wa taka bado hauwezi kumudu kiasi cha taka kinachozalishwa.
Vilevile, Ibara ya 27(1) inaelekeza kuwa kila mtu ana wajibu wa kulinda maliasili za nchi, yakiwamo mazingira.
Kwa mantiki hiyo, kushindwa kudhibiti taka kunahatarisha haki ya msingi ya wananchi ya kuishi katika mazingira salama.
Hali Ilivyo
Katika Kata ya Magadu, hali ya uchafu imekuwa mbaya zaidi katika Mtaa wa Falkland, ambako uchunguzi umebaini kuwa kituo cha muda cha kukusanyia taka kimejaa kiasi cha taka kusambaa hadi maeneo mengine yasiyo rasmi.
Eneo maarufu kama “Njia ya kwa Bibi” limegeuka kuwa dampo bubu lisilo na udhibiti wowote.
Mkazi wa eneo hilo, Fatuma Agida, anasema maisha yao yamegeuka kuwa ya hatari.
"Tunazalisha taka kila siku lakini hakuna anayekuja kuziondoa. Tunachimba mashimo na kuzifukia wenyewe, lakini hata hilo mamlaka zinasema si sahihi. Sasa tuzipeleke wapi?" anauliza.
Anasema wakati wa mvua hali huwa mbaya zaidi kwani maji yanayotiririka kwenye taka huingia majumbani na kusababisha hatari ya magonjwa ya mlipuko.
Watoto wadogo, ambao mara nyingi hucheza katika maeneo ya wazi, ndio walio katika hatari kubwa zaidi.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Paschal Mesiaki, anasema taka zimekuwa zikizagaa kwa muda mrefu huku mbwa wazururaji wakizivuruga kila siku.
"Taka zimejaa kwenye dampo na mbwa wanazivuruga mchana na usiku. Harufu ni kali sana na hakuna kiongozi anayekuja kutuambia nini kifanyike," anasema.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti hili, huduma ya ukusanyaji taka katika mtaa huo ilisimama tangu Juni 2025, licha ya wananchi kulipia ada ya Sh. 3,000 kwa mwezi kwa kila kaya.
Tangu gari la taka lisimame kupita, hakuna mfumo mbadala uliowekwa.
Uchunguzi pia umebaini kuwapo mgongano wa kiutendaji kati ya viongozi wa kata na mz-
Tani 100 za taka zinavyobaki mitaani kila siku Morogoro abuni wa taka. Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira ya Mtaa wa Falkland, Hosea
Maina, anasema sababu za mlundikano wa taka ni pamoja na kkosekana kwa mzabuni wa kudumu, ufuatiliaji hafifu wa sheria na baadhi ya wananchi kushindwa kulipa ada ya taka.
Kwa upande wake, mzabuni wa taka Wajanga Sabi, anasema alilazimika kusitisha kazi kutokana na kukosa mkataba rasmi na changa-moto za malipo kutoka kwa wananchi.
"Nimefanya kazi kwa miezi minne bila mkataba rasmi. Niliona napata hasara nikaamua kuacha," anasema.
Mtendaji wa Kata ya Magadu, Ibrahim Nguya, anasema tayari wapo katika mchakato wa kuanza kazi na mzabuni mpya.
Hata hivyo, mzabuni huyo anakanusha kutia saini mkataba huo.
Wataalamu Waonya
Wataalamu wa afya wanaonya kuwa taka zisipodhibitiwa zinaweza kusababisha magonjwa hatari.
Kaimu Ofisa Afya wa Manispaa ya Morogoro, Philipo Gervas, anasema taka zisizodhibitiwa zinaweza kusababisha uchafuzi wa vyanzo vya maji, mlipuko wa kipindupindu, homa ya matumbo na magonjwa ya ngozi.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mazingira, machafu yanachangia kwa kiasi kikubwa kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza hasa kwa watoto.
Vilevile, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (CRC) ambao Tanzania imeridhia, unaelekeza katika Kifungu cha 24 kuwa watoto wana haki ya kupata mazingira safi na huduma bora za afya.
Hivyo, mazingira yenye taka nyingi yanakiuka moja kwa moja haki hiyo.
Maeneo ya miradi yageuzwa dampo
Wakazi wa Kata ya Mafisa katika Manispaa ya Morogoro wanaishi katika hofu ya kukumbwa na magonjwa ya mlipuko ikiwamo kipindupindu na magonjwa ya tumbo kutokana na kuwapo dampo la taka lisilokidhi viwango vya usalama wa afya ya jamii na mazingira.
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa dampo hilo, ambalo linatumika kupokea taka nyingi zinazo- zalishwa katika manispaa hiyo, lina upungufu mkubwa wa kimuundo na kiutendaji.
Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na kuwapo katikati ya makazi ya watu, kukosa uzio wa kuzuia watu kuingia ovyo pamoja na kutokuwa na miundombinu ya kisasa ya usimamizi wa taka.
Wataalamu wa afya ya jamii wanasema hali hiyo inaweza kuwa chanzo kikubwa cha hatari kwa wakazi wa maeneo ya jirani kutokana na uwezekano wa kuenea kwa wadudu waharibifu kama nzi, mbu na panya wanaobeba vimelea vya magonjwa.
Mbali na hilo, harufu kali inayotokana na taka zinazooza moshi wa uchomaji holela wa takana maji machafu yanayotiririka kutoka dampo hilo yanaweza kuchafua hewa, ardhi na hata vyanzo vya maji vinavyotumiwa na wakazi wa karibu.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, hususan Kifungu cha 118(2), kabla ya serikali za mitaa kutenga eneo la kutupa taka ngumu zinapaswa kufanya tathmini ya athari kwa afya ya jamii na mazingira, kuhakikisha eneo hil lipo mbali na makazi ya watu na kuweka miundombinu ya usalama ukiwamo uzio na ulinzi. Hata hivyo, masharti hayo hayajatekelezwa kikamilifu katika dampo la Mafisa.
Manispaa Yakiri
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Taka Ngumu na Usafirishaji Manispaa ya Morogoro, Hezron Ligala, anakiri kuwapo changamoto katika dampo hilo.
"Kimsingi dampo hili ni la zamani na bado halina miundombinu yote inayohitajika. Dampo linalokidhi viwango vya sheria linapaswa kuwa na mfumo maalumu wa kuhifadhi taka ili zisivuke mipaka ya eneo lake," Ligala anasema.
Anafafanua kuwa manispaa imeanza mchakato wa kutafuta suluhisho la kudumu kwa kutenga eneo jipya la kujenga dampo la kisasa katika eneo la Kiegea B.
Kwa mujibu wa Ligala, eneo la takribani ekari 100 tayari limetambuliwa kwa ajili ya mradi huo, ingawa utekelezaji wake unategemea upatikanaji fedha na kukamilika kwa taratibu za fidia kwa wananchi wa eneo hilo.
"Ujenzi wa dampo la kisasa ni ghali, hivyo tunatafuta pia uwezekano wa kupata ufadhili kutoka kwa wadau wa maendeleo," anasema.
Tahadhari Kiafya
Kaimu Ofisa Afya wa Manispaa ya Morogoro, Philipo Gervas, anasema dampo lisilodhibitiwa linaweza kuwa chanzo cha magonjwa hatarikwa jamii.
Anasema kwa mujibu wa miongozo ya afya ya jamii, eneo la kuhifadhi taka linapaswa kuwa mbali na makazi ya watu angalau mita 500 kutoka mipaka ya makazi ili kupunguza athari za kiafya.
"Dampo lisipodhibitiwa vizuri linaweza kusababisha uchafuzi wa mazingira na magonjwa kama kipindupindu, homa ya matumbo na magonjwa ya ngozi," anasema.
Mbali na changamoto ya dampo, baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Kayenzi wamelalamikia kutokuwapo utaratibu thabiti wa ukusanyaji taka katika maeneo yao.
Mkazi mmoja wa eneo hilo anasema hali hiyo imewalazimu baadhi ya wananchi kupeleka taka zao moja kwa moja katika dampo hilo, jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu uliowekwa na manispaa.
"Kwetu hakuna mfumo maalumu wa kukusanya taka. Watu wengi wanaishia kupeleka wenyewe kwenyedampo au kuzitupa karibu na eneo hilo," anasema mkazi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kayenzi, Mohamed Mwanja, anakiri kuwapo changamoto hiyo na kusema kuwa wakazi wengi wanalazimika kutafuta njia mbadala za kuondoa taka zao.
"Tangu manispaa ianze kuchukua taka kupeleka dampo, katika mtaa wetu hazijawahi kukusanywa moja kwa moja. Kila mtu anajitafutia njia ya kuondoa taka zake," anasema.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mafisasina, Pendo Senyina, anasema wananchi wengi wanalalamikia kiwango cha ada kinachotozwa kwa kaya.
Kwa mujibu wa malalamiko hayo, baadhi ya wananchi wanatakiwa kulipa Sh. 3,000 kwa kila chumba au Sh. 6,000 kwa nyumba kwa mwezi, kiwango ambacho baadhi yao wanasema ni kikubwa.
Hata hivyo, Mtendaji wa Kata ya Mafisa, Marry Simbeye, anasema mfumo wa ukusanyaji taka unaendelea vizuri kwa kuwa tayari kuna mzabuni aliyetia saini mkataba na manispaa kwa ajili ya kutoa huduma hiyo.
Anasema malalamiko mengi ya wananchi yanahusu zaidi ada ya taka kuliko huduma yenyewe.
Chamwino Walia
Wakazi wa Kata ya Chamwino katika Manispaa ya Morogoro nao wanaendelea kuishi katika mazingira yanayohatarisha afya, usalama na ustawi wao kutokana na kutofanyiwa usafi mara kwa mara kwa maeneo yaliyopitiwa na miradi mikubwa ya serikali likiwamo Bomba la Mafuta la TAZAMA na njia kuu ya umeme ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Uchunguzi umebaini kuwa maeneo hayo yamegeuka vichaka vinene na sehemu zisizo rasmi za kutupa taka. Matokeo yake ni kuenea kwa harufu kali ya mizoga, uchafuzi wa hewa na mazingira, hali inayochochea hofu ya kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu, homa ya matumbo na magonjwa ya mfumo wa hewa.
Baadhi ya wakazi wanasema hali hiyo imeathiri maisha yao ya kila siku pamoja na shughuli ndogo za kiuchumi wanazozitegemea.
Mkazi wa Mtaa wa Mwembeni, Metruda, anasema harufu kali ya mizoga inayotupwa kwenye vichaka imekuwa kero kubwa kwa wananchi wa eneo hilo.
"Tunateseka sana na harufu ya mizoga inayotupwa kwenye vichka. Afya zetu ziko hatarini na hata kufanya biashara ndogo kama kuumaandazi inakuwa vigum u kutok a n a n a harufu mbaya," anasema.
Mbali na athari za kiafya, vichaka hivyo pia vimekuwa chanzo cha hofu ya kiusalama kwa wakazi.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwembeni, Hadija Madegwa, anasema maeneo ya miradi ya TAZAMA na TANESCO yamekuwa yakiachwa na majani marefu ambayo yanatofursa kwa nyoka na wahalifu kujificha.
"Ndani ya mitaa yetu hali ya usafi iko sawa, lakini maeneo ya TAZAMAna TANESCO majani yanakuwa makubwa sana. Nyoka wanatokea na vibaka wanajificha, hivyo wananchi wanaishi kwa hofu," anasema.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Malipula, Shaban Kikova, anasema changamoto hiyo imekuwa ikiripotiwa mara kwa mara kwa mamlaka husika kupitia taarifa za viongozi wa mitaa.
Anaeleza kuwa maeneo yaliyopitiwa na bomba la mafuta yana ulinzi maalumu kwa kuwa wananchi hawaruhusiwi kufanya shughuli za kilimo au biashara ili kulinda miundombinu hiyo muhimu ya taifa.
Mtendaji wa Kata ya Chamwino, Rajabu Wanyamale, anakiri kuwapo
Mazingira
Maeneo ya miradi yageuzwa dampo changamoto ya usafi katika baadhi ya maeneo hasa yale yanayosimami- wa na TANESCO.
"TANESCO wamekuwa kikwazo mkikubwa kwa sababu wakati mwingine hawasafishi maeneo yao kwa wakati. Taka hupeperushwa na upepo na kunasa kwenye maeneo hayo, huku baadhi ya watu wakitumia vichaka hivyo kutupa taka," anasema.
TAZAMA, TANESCO
Akizungumzia suala hilo, Msimamizi wa Kituo cha TAZAMA Mkoa wa Morogoro, Pius Mikongoti, anasema wamekuwa wakipokea malalamiko ya wananchi kuhusu usafi wa maeneo yaliyopitiwa na bomba hilo.
Anafafanua kuwa awaliwananchi waliruhusiwa kulima katika maeneo hayo, jambo lililosaidia kudumisha usafi, lakini baadaye uta r a t i b u huo ulisitishwa ili kulind a miundomb i n u y a bomba la mafuta.
"Sasa tunafanya usafi kwa kufyeka majani ili kuepusha mmomonyoko wa udongo unaoweza kuathiri bomba. Tunafanya zoezi hilo takribani mara tatu kwa mwaka," anasema.
Pia soma ~ Changamoto ya Mazingira kwenye miradi mikubwa, maeneo yanageuzwa dampo
Mhandisi wa kusafirisha umeme wa TANESCO Mkoa wa Morogoro, Amani Mbamba, anasema taasisi hiyo ina ratiba ya kusafisha maeneo ya njia za umeme mara kwa mara kulingana na bajeti iliyopo.
Anasema maeneo ya karibu na makazi ya watu husafishwa kila baada ya miezi miwili, huku maeneo yaliyo mbali zaidi yakifanyiwa usafi angalau mara moja kwa mwaka.
"Hatuwezi kufyeka kila siku kwa sababu tunahudumia kilomita nyingi za miundombinu ya umeme. Hata hivyo, viongozi wa mitaa wanaweza kutupigia simu wanapoona eneo limekuwa hatarishi," anasema.
KAULI YA NEMC
Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, hususan Kifungu cha 81(1), mmiliki wa mradi au mradi wa maendeleo anapaswa kuhakikisha maeneo ya nayopitiwa na mradi yanahifadhiwa vizuri ili kuzuia uharibifu wa ardhi, maji na hewa na kulinda afya ya wananchi wanaoishi jirani.
Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Morogoro–Rufiji, Arnold Mapinduzi, anasema miradi yote mikubwa lazima ifanyiwe tathmini ya athari za mazingira kabla ya kuanza kutekelezwa.
Anasema ikiwa taasisi inayosimamia mradi itashindwa kutekeleza masharti ya usimamizi wa mazingira, mamlaka zinaweza kutoa onyo au hata kuchukua hatua za kisheria ikiwamo kutoza faini.
ANDIKO LA: Elizabeth Mwailunga
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.