Sheria ya Umeme ya mwaka 2007 (tuliipitisha bungeni 2008) inaruhusu makampuni ya binafsi kuzalisha umeme na kusambaza umeme (upande wa kuzalisha tayari IPTL na Songas wanashiriki).
Tatizo la umeme wa Tanzania ni Transmission. Uwezo wetu wa kusambaza umeme ni mdogo sana na tuna gridi moja tu. Uwekezaji katika gridi hauwezi kuwa kwa sekta binafsi (serikali ilitika kuliberalise transmission pia, nakumbuka mimi na mzee cheyo tulikataa kata kata na tukafanikiwa). Serikali ilipaswa kuwa imejenga gridi mpya ya North-West gridi ili kusafirisha umeme kwenda kanda ya Ziwa mikoa ya Kigoma, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Kagera na Mara. Mahitaji ya umeme wa mikoa hii kwa sasa kama migodi yote ikipata umeme wa gridi ni 240MW. Kwa sasa ni mgodi mmoja tu wa Bulyanhulu ndio unapata umeme wa gridi na usio na uhakika. Hii inapelekea serikali kupaata hasara mbili.
- TANESCO wanakosa soko la uhakika la zaidi ya 120 MW ambapo wangeweza kuingiza zaidi ya 120bn usd kwa mwaka na hivyo kupata fedha za kusambaza umeme vijijini na mijini. Pia hii inakosesha uchumi faida ya backward linkages kati ya sekta ya nishati na sekta ya madini (backward linkage is such that a sector that gets a lot of inputs from within the country will have strong backward linkages relative to sectors that import most of their inputs from oversees). Madhara haya tunayaona hapa chini kwenye hasara ya pili;
- Serikali inatoa misamaha ya kodi ya mafuta kwa kampuni za madini ili zizalishe umeme wake wenyewe (importing inputs). Kwa mujibu wa ripoti ya Bomani Tanzania ilisamehe jumla ya 191bn Tshs katika kipindi cha 2005/06 - 2007/08. Hii pia ina madhara katika urari wa biashara na hata thamani ya shilingi ya Tanzania pale uzalishaji unapokuwa unaongezeka katika sekta ya madini.
Uwekezaji wa transmission line ni uwekezaji mkubwa sana lakini unawezekana. Zinahitajika kama 700m usd kujenga grid hii mpya. Hapa serikali ndipo inapotakiwa kufanya kazi sawasawa.
Lakini kuna hatua za dharura zilizotakiwa kufanywa. Mojawapo ni kuwa na mtambo wa 60MW Mwanza ambao utapunguza mzigo kwenye gridi. Zabuni zilitangazwa na TANESCO toka mwezi Aprili na wazabuni kujitokeza lakini mtambo huu utaweza kufungwa na kuanza kazi mwaka 2011. Hii inatokana na taratibu za ujenzi wa mitambo kwenye viwanda. Baada ya kupata mzabuni, itabidi kuanza sasa ujenzi wa mitambo nk.
Kwa mwono wangu, matatizo ya sasa ya mgawo hayatachukua muda mrefu sana kwani mvua zitanyesha na mitambo kurekebishwa. Hata hivyo bado tutakuwa na tatizo kubwa la kanda ya Ziwa maana hata mabwawa yazalishe at 100%, kama gridi imezidiwa haitaweza kusafirisha umeme kwenda huko. Mtambo wa 60MW Mwanza ndipo unapopata umuhimu wake kwa sasa.
Kuwalaumu TANESCO sidhani kama ni sawa. Hili ni Shirika ambalo limeharibiwa sana na mikataba mibovu ambayo sio TANESCO wenyewe waliingia. Hili ni Shirika ambalo NetGroup Solution waliliingiza kaburini na ndio kwanza limetoka.
TANESCO wamejitahidi sana kwa kadiri ya uwezo wao kushugulikia suala hili kwani wao wenyewe wanajua kuwa wanapaswa kufanya kazi kwa bidii kwani wanatakiwa kubreak even mwaka 2010 ili waweze kuanza kulipa mkopo waliochukua katika taasisi za fedha. Hivyo migawo hii inawaumiza na ninajua wanaumia.
Tatizo ni commitment ya serikali katika suala hili. TANESCO waliomba 312bn kwenye bajeti ili kushughulikia masuala haya ya umeme hawakupewa kitu. Tuzingatie kuwa tuna nakisi ya 155MW za umeme kutokana na IPTL kusimama kuzalisha mpaka kesi iishe na kesi bado haijaisha.
Suala la umeme lapaswa kuangaliwa katika mapana sana. Ni kweli kuwa asilimia 12 tu ya nyumba ndio zina umeme, lakini umeme sio kwa jili ya kuwasha nyumbani tu. Umeme kwenye uzalishaji wa uchumi ni muhimu sana ili walaji wa kawaida waweze kufidiwa kwa kupata umeme wa gharama nafuu.
Ninaamini kabisa kuwa kama tukiamua kuisaidia TANESCO tunaweza kulifanya Shirika hili 'champion' wa nchi yetu. Potential zote zipo. Dhamira hakuna.