Tanesco yapingwa
2007-11-16 09:00:12
Na Joseph Mwendapole
Baadhi ya wananchi wamepinga mapendekezo ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco), kutaka kupandisha gharama za kuunganisha umeme kwa zaidi ya asilimia 200.
Endapo mapendekezo hayo yatakubaliwa, gharama hizo zitafikia Sh. 563,271, wakati awali ilikuwa Sh. 200,000.
Wakizungumza na Nipashe jana, wananchi hao walisema endapo shirika hilo litapandisha gharama hizo, wengi watashindwa kuzimudu.
Bw. Bakari Kiembe, mkazi wa Mwananyamala alisema kama mapendekezo hayo yatakubalika, nishati hiyo itakuwa kama anasa.
Alisema watu wa kipato cha chini hawatamudu gharama za kuunganishiwa umeme kwa kiasi kilichopendekezwa na shirika hilo.
Alisema uharibifu wa mazingira ambao umekuwa ukipigwa vita na serikali utaibuka kwa kasi kwa kuwa wananchi hawatakuwa na nishati mbadala.
`Mtu anajibana anajenga kajumba kake miaka kumi ndipo anamaliza na akitaka umeme unamwambia atoe Sh. 500,000 atazitoa wapi,` alihoji.
Mkazi mwingine wa Sinza, Bw. Ayubu Mtemi, alisema kupanda kwa gharama hizo ni matokeo ya shirika hilo kutokuwa na mshindani.
Alipendekeza litafutwe shirika lingine litakalokuwa likitoa huduma kama ya Tanesco ili kuondoa ukiritimba.
Bw. Mtemi alisema shirika hilo ni la umma na linapaswa kutoa huduma ambayo haiwaumizi wananchi wake lakini halifanyi hivyo.
Alisema lazima serikali iingilie kati na kutupilia mbali mapendekezo hayo kwa kuwa huduma ya umeme ni ya lazima tofauti na zingine.
`Angalau huduma ya simu unaweza kupandisha gharama kwa kuwa kupiga simu mtu anaweza kujibana, lakini suala la umeme ni lalazima,` alisema.
Aliongeza kuwa endapo mapendekezo hayo yatakubaliwa, mpango wa serikali kuwapatia nishati hiyo watanzania wengi ifikapo mwaka 2010 utakuwa ni ndoto.
Bw. Juma Mulla, wa Manzese alisema ni wakati muafaka kwa serikali kufikiria kuliuza shirika hilo kama ilivyofanya kwa mengine.
Hata hivyo, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), imekataa mapendekezo ya Tanesco mpaka itakapofanya mijadala na wananchi watoe maoni yao.
Kutokana na kukataliwa kwa ongezeko hilo, Tanesco imeamua kusitisha shughuli za kuwaunganishia umeme wateja wapya, mpaka mazungumzo yake na EWURA yatakapokamilika.
Katika ofisi mbalimbali za shirika hilo jijini Dar es Salaam, matangazo yamebandikwa yakielezea kuwa, huduma hizo zitaanza kutolewa itakapoamuliwa baadaye.
`Malipo mapya na yale ya zamani, yamesitishwa mpaka itakapotangazwa upya baadaye,` lilisema sehemu ya tangazo moja katika ofisi za Mkoa wa Ilala.
Tangazo hilo pia lilisema kuwa, hata fomu za maombi ya mwanzo, hazitatolewa kwa sasa.
Kutokana na hali hiyo, shirika hilo limesema wananchi wanaotaka kuunganishiwa umeme watatakiwa kununua vifaa wao wenyewe.
Meneja Uhusiano wa shirika hilo, Bw. Daniel Mshana, alinukuliwa akisema juzi kuwa wakati wakiendelea kujadiliana na EWURA, wateja watakaotaka kuunganishiwa umeme watalazimika kununua vifaa wao wenyewe.
source Nipashe