Tafadhali Rais Mkapa endeleza Ukimya! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tafadhali Rais Mkapa endeleza Ukimya!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mzee Mwanakijiji, Nov 25, 2009.

 1. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #1
  Nov 25, 2009
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,364
  Likes Received: 6,394
  Trophy Points: 280
  Na. M. M. Mwanakijiji

  Kuna msemo wa kiafrika unaosema, huwezi kuzuia masikio yako kusikia bali kuuzuia mdomo wako kuzungumza. Ndiyo siwezi kuzuia masikio yenu kusikia, lakini naweza kuziba mdomo wangu nisizungumze – Rais Mstaafu Benjamin W. Mkapa

  Kama kuna mtu katika Taifa letu ambaye anaamini kuwa Rais mstaafu na Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Mapinduzi Bw. Benjamin W. Mkapa alikuwa nikiongozi bora basi mtu huyo itampasa afungiwe jiwe la kusagia shingoni na “kwenda kutupwa Baharini”. Kama kuna yeyote ambaye anaamini kuwa mambo yanayosemwa juu ya uongozi wa Rais wetu huyo wa awamu iliyopita ni “wivu, chuki, masimango” binafsi dhidi yake basi na huyo naye tutamuongezea na jiwe la kukobolea! Na iwapo kuna kundi la watu ambao wanaamini kabisa kuwa Tanzania ilifanya vizuri wakati wa Rais Mkapa na hivyo tujipange kwa kupiga magoti na kutoa shukrani zetu kwake basi kundi hilo na watetezi wa uongozi wa awamu ya tatu ningelikuwa na uwezo ningehakikisha wanafutwa wote kwenye kitabu cha historia yetu.
   

  Attached Files:

 2. nguvumali

  nguvumali JF Bronze Member

  #2
  Nov 25, 2009
  Joined: Sep 3, 2009
  Messages: 4,864
  Likes Received: 143
  Trophy Points: 160
  Mkapa ana hasira na kiburi, najua atasema yote siku moja, anachosubiri ni JK, amwage ugali yeye amwage mboga.
   
 3. M

  MC JF-Expert Member

  #3
  Nov 25, 2009
  Joined: Oct 5, 2007
  Messages: 751
  Likes Received: 28
  Trophy Points: 45
  ... Nimefurahishwa na point ya Jiwe la kusagia na kukobolea..., Kama ndugu yako akikosa muonye, akitubu msamehe, akikataa kutubu wakati ameonywa mfunge jiwe la kusagia kisha mtupe baharini...
   
 4. B

  Boramaisha JF-Expert Member

  #4
  Nov 25, 2009
  Joined: Apr 29, 2009
  Messages: 820
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  MMJ, heshima zako Mzee na nakuvulia kofia kwa article yako. Kila Jumatano miye hukimbilia kununua Mwanahalisi na Raia Mwema nikusome wewe la Lula wa Ndali. Hiyo statement ya Mkapa imejaa arrogance na dharau aliyokuwanayo huyu Mzee. Nadhani ni vya kuzaliwa pia! Nasikitika Mwalimu hakuliona hilo akabeba mbuzi kwenye gunia aliyekuja kumkana hata aliyembeba. Aibu!

  Mzee wa Kijiji, kama uko nje lini utarudi nyumbani uanzishe Chama tujiunge tuzunguke nchi nzima kukusanya wanachama na hatimaye ushike usukani wa nchi yetu? Kama uko hapa nyumbani jitokeze tukuunge mkono, Unastahili kabisa kuwa kiongozi wa nchi hii!
   
 5. Ndahani

  Ndahani JF-Expert Member

  #5
  Nov 25, 2009
  Joined: Jun 3, 2008
  Messages: 14,343
  Likes Received: 1,810
  Trophy Points: 280
  BWM ni mtu wa aina yake...badala ya kuvuta pumzi na kutafuta suluhu, yeye ndo kwanza anaendelea kuyapandisha mabega yake juu akitamba bila aibu. Huyu bwana kweli anakosea. Kila kitu kina kiasi. Ni kujidanganya kufikiri kwamba mtu unaweza kufanya lolote pasipo kupata madhara yoyote. Kweli kama tumaini lake ni kwa hao watu maalumu anaowaongelea basi kazi kwake!!
   
 6. E

  Ex-Fisadi Member

  #6
  Nov 25, 2009
  Joined: Aug 19, 2009
  Messages: 79
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Simtetei Mkapa, wala siwezi kumtetea Mkapa kwa madudu yaliyofanyika katika kipindi chake!! Lakini ni vyema kusema kuwa Mkapa alikuwa shupavu, ni bahati mbaya tu kuwa alirithi nchi iliyokuwa imechoka isiyokusanya madeni, isiyokuwa na hadhi mbele ya mataifa mengine na iliyokuwa haina hata hifadhi ya fedha za kigeni. Alirithi nchi iliyokuwa imenajisiwa kwa uongozi mbayana kuchoka kabisa. Ilikuwa ni nchi ambayo haikusanyi kodi na iliyokuwa inashindwa kutawalika kiasi kwamba Baba wa taifa akalazimika kutoka kwenye kustaafu kwake na kurudi katika siasa za kuirudisha nchi katika mstari wa kutawalika!!! kwa kweli Mzee Mwinyi alikuwa ameshindwa kuitawala nchi hii ina kuigeuza kuwa kichwa cha Mwendawazimu, kiasi cha kufikirika kuwa mtu kama Augostine Mrema angeweza kutuongoza!!!

  Watawala wa sasa wameturudisha alikoitoa nchi hii na mapungufu yao ya sasa tunayapeleka kwa Mzee Mkapa. Mbona Watanzania tu wepesi wa kusahau?????

  Nawaambia tukidodosa aliyofanya Mzee Mwinyi wakati wa kipindi chake, tutagundua kuwa Mkapa alikuwa nafuu sana ila bahati mbaya watanzania tu wepesi wa kusahau.

  Ikulu ya Mwinyi si kuwa kulianzishwa kampuni binafsi kama ANBEM bali kulikuwepo na biashara hata za dhahabu na watu walikuwa wanajua hata bei ya rais wetu!!!! Je wana JF nani anaweza kujitokeza na kusema anajua bei ya Mkapa???? hakika hakuna ila tumesahau nani alifuta Azimio la Arusha na kuanzisha Azimio la Zanzibar!! Jamani tusiwe wepesi wa kusahau wapi tulipo jikwaa na kuwa tunakumbuka tulipo angukia!!!
   
 7. nguvumali

  nguvumali JF Bronze Member

  #7
  Nov 25, 2009
  Joined: Sep 3, 2009
  Messages: 4,864
  Likes Received: 143
  Trophy Points: 160
  lazima atambe, maana watawala wanamuogopa, hakuna anaeweza kusimama mbele yake kati ya hawa waliopo madarakani, akiwatizama tu wananywea.
   
 8. KILITIME

  KILITIME JF-Expert Member

  #8
  Nov 25, 2009
  Joined: Nov 17, 2009
  Messages: 267
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35


  Sasa mbona sikuelewi wewe maelezo yako na heading havina uhusiano???? swala la kufunga watu mawe yanahusiana nini na "TAFADHALI RAIS MKAPA ENDELEZA UKIMYA??????" Kwa mtazamo wangu hawamu zote za uongozi zina mazuri yake na mabaya pia!
   
 9. Scientist

  Scientist JF-Expert Member

  #9
  Nov 25, 2009
  Joined: Feb 7, 2009
  Messages: 392
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0

  (..Jambo moja ambalo nina uhakika hakuna mtetezi yeyote wa Rais Mkapa anaweza kusimama na kupinga ni ukweli kuwa mfumo wa utawala wa kifisadi (MUK) ulipandwa wakati wa utawala wa Rais Mwinyi, lakini ulimwagiliwa, kupaliliwa, na kutiwa mbolea wakati wa utawala wa Rais Mkapa. Leo hii katika utawala wa Rais Kikwete tunaanza kuvuna mavuno yake ya awali! Na bado hatujafikia hata nusu ya mbegu zilizopandwa! ...Source: Attached file MKJJ thread)

  Mkuu Ex Fisadi Hapa ishu si kusahau tuliko toka bali ni kuuweka wazi ukweli kwamba MKAPA ni mmoja wa sababu zilizotufikisha hapa tulipo kwa kiasi kikubwa!! Yeye ndiye engineer haswaa na wala si mwingine. Yes kuna mazuri kayafanya na hayo ndiyo anatamba nayo,huku ukweli wakiuficha kwamba ndiye mwanzilishi wa MUK!!
   
 10. Scientist

  Scientist JF-Expert Member

  #10
  Nov 25, 2009
  Joined: Feb 7, 2009
  Messages: 392
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Mkuu Kilitime, si usome hiyo attached file umuelewe MKJJ????
   
 11. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #11
  Nov 25, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,878
  Likes Received: 83,359
  Trophy Points: 280
  Ahsante sana MKJJ. Mimi ni mmoja wa wale ambao naamini kabisa hakuna mazuri yoyote yaliyofanywa na Mkapa na huwa nawashangaa sana wanaosema kwamba Mkapa alifanya mazuri. Naamini kabisa mazuri yanayofanywa na kiongozi wa nchi huonekana miongoni mwa wananchi walio wengi katika nchi husika. Hili halikutokea kabisa wakati wa Mkapa. Watanzania wengi waliona hali ya maisha ikiendelea kuwa ngumu mno ukiondoa wachache ambao hawafiki hata 1% ya Watanzania ambao hali zao zilineemeka.
   
 12. PakaJimmy

  PakaJimmy JF-Expert Member

  #12
  Nov 25, 2009
  Joined: Apr 29, 2009
  Messages: 16,236
  Likes Received: 309
  Trophy Points: 180
  ndo nini hiyo tena?
  Soma attachment wewe, dont jump to the conclusion!
   
 13. Companero

  Companero Platinum Member

  #13
  Nov 25, 2009
  Joined: Jul 12, 2008
  Messages: 5,475
  Likes Received: 168
  Trophy Points: 160
  Mzee Mwanakijiji kwa hisani yako naomba niweke barua hii inayoisonda kidole makala yako:

  Barua ya Wazi kwa Mheshimiwa Mkapa

  [​IMG]

  Barua ya wazi kwa Mhe. Benjamin William Mkapa, Rais mstaafu


  Mheshimiwa Mkapa,
  Assalam Alaykum.
  Nakuamkia kwa heshima na taadhima. Natumai u mzima wa afya, wewe na familia yako. Nakuombea kila la heri na mapumziko mema, pamoja na majukumu yako mengi na mazito ya kimataifa.

  Mheshimiwa, nimeshawishika kuandika barua hii baada ya kusoma kwenye tovuti (http://businessmirror.com.ph/home/opinion/14843-the-sudden-demise-of-neoliberal-economics.html) maoni yako ambayo yamenukuliwa na mwandishi wa habari Roberto Savio akiandika juu ya kifo cha uliberali mamboleo katika gazeti la Business Mirror la 19 Agosti 2009. Umenukuliwa ukisema:

  "We privatized everything the state had. Everything was bought by foreign capital because we had no national capital to compete. The foreign companies almost always closed local businesses, which were not competitive, transforming them into distributors of foreign products and driving up unemployment. The experts of the World Bank and the IMF predicted that this would happen, but they told us: Now the influx of foreign investment will lead to the creation of new, competitive and technologically current businesses that will provide the foundations for a lasting, modern development. None of this happened for us."

  "Tulibinafsisha kila kitu kilichokuwa mikononi mwa dola. Kila kitu kilinunuliwa na wawekezaji kutoka nje kwa sababu hatukuwa na mtaji wa ndani wenye uwezo wa kushindana. Makampuni ya nje yakafunga mashirika ya ndani kwa sababu hayakuwa na tija na yakayageuza mashirika haya kuwa wachuuzi wa bidhaa kutoka nje na kwa hivyo kuongeza watu wasio na ajira. Wataalam wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa walitabiri kwamba hivyo ndivyo ingekuwa, lakini wakatuambia: Uwekezaji kutoka nje utazaa taasisi za kibiashara za kisasa, zenye uwezo wa kushindana, na teknologia ya kisasa, na kwa hivyo kujenga misingi ya kudumu ya maendeleo ya kisasa. Hakuna lolote kati ya hiyo lililotokea nchini mwetu".

  Mzee, unasononeka; kwa kiasi fulani, katika lugha yako ya kidiplomasia, unalalamika. Lakini hata baada ya maanguko ya mfumo wa uliberali mamboleo na utandawazi, ambao uliushabikia sana wakati wa utawala wako, hukuwa na ujasiri wa kuomba msamaha wa watu wako. Sikulaumu. Huwezi kulaumiwa. Ni hulka ya binadamu kutokuona au kukiri kosa lake. ‘Nyani haioni ngokoye.' Katika hili huko peke yako. Katika mkutano wa kundi la nchi 20 (G20) zenye nguvu za kiuchumi ulioitishwa mjini London kuzungumzia hali mbaya ya uchumi mnamo Aprili mwaka huu, Waziri Mkuu wa Uingereza, Bwana Gordon Brown, alikiri kwamba ‘Muafaka wa Washington umekufa', alisema hivyo bila kuwaomba radhi watu wa ulimwengu, hasa wa nchi maskini, ambao waliathirika sana na "muafaka" huo wa nchi za kibeberu ambao nchi zetu zililazimishwa kuufuata.

  Mheshimiwa Rais mstaafu: Ukweli ni kwamba haya yaliyotokea sasa si matokeo yaliyokuja kwa bahati mbaya au kwa miujiza tu. Wako viongozi na hasa wasomi (angalau wachache) walisema, tena kwa uchambuzi wa kina na yakinifu, kwamba mfumo huo hautufai, hautatuletea maendeleo, bali utauongeza tu unyonywaji wa watu wetu na uporwaji wa mali zetu. Mwalimu Nyerere alijitahidi sana kupinga masharti ya nchi za kibeberu, lakini hakufanikiwa. Mzee Mwinyi alifungua milango na wewe ukakumbatia, bila kuhoji mfumo huo, hasa masharti yale ya kubinafsisha mashirika ya umma. Ni kweli mashirika mengine hayakuwa na tija, ni kweli pia mengine yalikuwa na menejimenti mbovu. Lakini je, tulijaribu kutafuta njia mbadala, licha ya hiyo ya kubinafsisha ‘kila kitu'? Wasomi wako wachache waliokosoa sera zako za kiuchumi uliwaita majina na kuwafananisha na ‘wavivu wa akili'. Ulipigia sana debe utandawazi kiasi kwamba jina lako litaingia katika historia kama mvumbuzi wa neno ‘utandawazi' katika msamiati wa Kiswahili. Uliwafumbia macho viongozi wako wakati wakitumia vyeo vyao kujilimbikizia mali na utajiri wa kupindukia – au hili pia ilikuwa ni sera ya kujenga mabepari wa ndani?

  Mbaya zaidi, mheshimiwa, chini ya uongozi wako tukakubali kutoa uhuru kwa taasisi za kifedha, na kukubali soko huria katika biashara ya fedha, (na kutokudhibiti akaunti ya mtaji (capital account)) bila udhibiti na usimamazi wowote wa dola. Hili ndilo hasa lilikuwa chanzo cha chumi zetu kuathirika kupita kiasi pale anguko la mfumo wa fedha wa kimataifa lilipotokea.

  Nchi ambazo zilikataa soko huria katika mambo ya fedha, kama China na Malaysia, hazikuathirika kama nchi zingine. Naomba nisiendelee. Wananchi wetu, pamoja na kutokuwa na usomi au ustaarabu wako au wangu, wanahisi moyoni mwao udhaifu wa mfumo wa utandawazi na binamu yake uliberali mamboleo. Ndio maana wakati wa kuadhimisha miaka kumi tangu kifo cha Mwalimu, wakalilia sana Azimio la Arusha.

  Mwalimu hakuwa malaika, alikuwa kiongozi wa kisiasa. Alikuwa na mapungufu yake lakini alijali watu wa chini, watu ambao walisahaulika kabisa katika awamu ya tatu na wanaendelea kupuuzwa katika awamu ya nne. Kila mlalahoi aliyetoa maoni yake alikuwa na maneno haya tu: Mwalimu alitujali; Azimio la Arusha lilitujali sisi wanyonge. Azimio lilitoa matumaini. Uliberali mamboleo na utandawazi ulitoa matumaini yapi kwa matabaka ya chini, zaidi ya kuwa njia ya viongozi kujilimbikizia mali bila aibu!

  Mheshemiwa Rais mstaafu, sio nia yangu kurudia yale yaliyotokea. Lakini, utakubaliana nami kwamba historia ni muhimu. Kujifunza kutokana na historia yetu na ya wengine ni hatua ya kwanza katika safari ndefu ya kujikomboa na kujiletea maendeleo halisi. Kama kweli umejifunza na umeyaona madhara ya sera ulizozikumbatia wakati ukiwa madarakani, je, huoni kwamba una wajibu wa kumsaidia mrithi wako, na hasa kutusaidia sisi wananchi, ili tujifunze kutokana na makosa ya serikali yako? Je, kweli, bado unanadi na kutunasihi kwamba utandawazi hauepukiki? Je, bado unatushauri kwamba msukumo wa maendeleo ni uwekezaji kutoka nje, uwekezaji ambao umejidhihirisha wazi ni uporaji wa maliasili yetu? Je, huoni kwamba unao wajibu, kwa upande wako, wa kufanya kila iwezekanayo – na wewe sio mtu mdogo katika nchi hii – kutusaidia kuzindua mjadala wa kitaifa juu ya hatma ya nchi yetu na bara letu?

  Wasalaam,

  Issa Shivji
  Profesa wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere
  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
  Okotoba 24, 2009
   
 14. Waberoya

  Waberoya Platinum Member

  #14
  Nov 25, 2009
  Joined: Aug 3, 2008
  Messages: 11,609
  Likes Received: 3,910
  Trophy Points: 280
  Alishangiliwa ukumbini! kwa nguvu hata wengine kutoa machozi!

  Ninachoamini ni kuwa watu wana mawazo kulingana na ufahamu walionao!

  Pili, ni wakati mzuri wa kuzuia lililotokea kwa Mkapa lisijitokeze, system mbovu na yeye aliongozwa na tamaa na dunia hii!, ambazo mtu mwingine yeyote angeweza kufanya kama system inaruhusu! note that, watu wa caliber ya JK Nyerere hawapatikani kirahisi!

  Tukibadili katiba, rais akaondolewa kinga, is the best goal for now.

  Huyu tutamlaumu, wakati is best case study that our const. is poor!

  Hivi leo umaarufu wa JK na mkapa wengi wanaona Mkapa afadhali

  MKJJ ukitaka hao wote wafe, I doubt watanzania asilimia 80 wanaweza wakafa! LOL!

  Kosa limeshafanywa tangu enzi hizo za 'yadumu mawazo sahihi ya mwenyekiti'

  urais si ufalme ni ajira! mwajiri mwananchi.

  JK can do the same, naye akipita akiodnoka tutaanza kusema na kuandika wee!

  Ndio maana nasema hatuna vyama vya upinzani kilio cha katiba ni kikubwa mno kwa msingi wa Tanzania mpya.
   
 15. M

  Mwafrika JF-Expert Member

  #15
  Nov 25, 2009
  Joined: Nov 20, 2006
  Messages: 5,490
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 0
  Hivi mwanakijiji, kwa nini unapenda sana kuandama waislam?

  Ulianza na Lowasa, ukaja kwa Masha, Chenge, Pinda, na sasa unaendeleza vita yako dhidi ya Mkapa...... (snack).
   
 16. MawazoMatatu

  MawazoMatatu JF-Expert Member

  #16
  Nov 25, 2009
  Joined: Sep 6, 2008
  Messages: 505
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 35
  Kinachoitwa "Ufisadi" leo hii ni hulka tuliyokua nayo waafrika toka enzi na enzi yaani mchanganyiko wa rushwa,ubinafsi na kutokujali maslahi ya uma.
  Tutaaandika ripoti za kulaumu, tutamaliza bandwith za jamii forum lakini ugonjwa huu una suluhisho dogo tu nalo ni "SOCIAL ENGINEERING". Yanahitajika mabadiliko ya kifikra kwa nchi nzima..!
  Soma hapa
   
 17. KILITIME

  KILITIME JF-Expert Member

  #17
  Nov 25, 2009
  Joined: Nov 17, 2009
  Messages: 267
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Mzee Mwanakijiji umeweka article yako kama attachment lakini naomba niiweke yote, si unajua BMW alisema kuwa "Watz ni wavivu wa kufikiri?" Mada ni hii hapa chini:

  TAFADHALI RAIS MKAPA ENDELEZA UKIMYA WAKO!

  Na. M. M. Mwanakijiji

  Kuna msemo wa kiafrika unaosema, huwezi kuzuia masikio yako kusikia bali kuuzuia mdomo wako kuzungumza. Ndiyo siwezi kuzuia masikio yenu kusikia, lakini naweza kuziba mdomo wangu nisizungumze – Rais Mstaafu Benjamin W. Mkapa

  Kama kuna mtu katika Taifa letu ambaye anaamini kuwa Rais mstaafu na Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Mapinduzi Bw. Benjamin W. Mkapa alikuwa nikiongozi bora basi mtu huyo itampasa afungiwe jiwe la kusagia shingoni na "kwenda kutupwa Baharini". Kama kuna yeyote ambaye anaamini kuwa mambo yanayosemwa juu ya uongozi wa Rais wetu huyo wa awamu iliyopita ni "wivu, chuki, masimango" binafsi dhidi yake basi na huyo naye tutamuongezea na jiwe la kukobolea! Na iwapo kuna kundi la watu ambao wanaamini kabisa kuwa Tanzania ilifanya vizuri wakati wa Rais Mkapa na hivyo tujipange kwa kupiga magoti na kutoa shukrani zetu kwake basi kundi hilo na watetezi wa uongozi wa awamu ya tatu ningelikuwa na uwezo ningehakikisha wanafutwa wote kwenye kitabu cha historia yetu.

  Kwa karibu miaka miwili sasa nimekuwa nikiandaa ripoti yangu ya tatu ambayo itaangalia kwa undani ushahidi wa ubovu, uzembe, kutokuwajibika na mfano mbaya kabisa wa uongozi wa taifa wakati wa utawala wa Rais Mkapa. Nitaangalia yale "mazuri" ambayo yanatajwa na kuonesha kuwa ni uzuri wa mapambo tu ambao unaweza kusifiwa. Hata hivyo nikiwa nasubiri wakati muafaka wa kuitoa ripoti hiyo ikiwa ni baada ya zile mbili za kwanza (ile ya Matumizi ya Tanzania katika usafirishaji wa silaha haramu na ile ya Meremeta) nimeona niandike kwa namna ya makala tu kupinga utukuzaji wowote ule ambao umeanza wa utawala wa Mkapa na zaidi kupinga jitihada zake za hivi karibuni kujaribu kutufanya wakosoaji wake tujisikie hatia kwani tunamuonea!

  Ukweli na usemwe
  Lengo langu siyo kudai kama baadhi ya wengine kuwa utawala wa awamu ya tatu haukufanya "lolote". Kama nilivyoandika wakati wa suala la kupaa kwa ndege ya Lowassa ni kutokuwa mkweli kwa historia na dhamira kama kuna mtu atadai kuwa serikali haijafanya "lolote". Mimi si mmoja wa wale waliofumba macho ambao hawaoni madaraja, barabara, mashule, zahanati, hospitali n.k ambazo zilijengwa chini ya utawala wa Mkapa. Yeyote anayetaka kufuatilia mafanikio hayo anaweza kutembelea tovuti ya CCM ya ccmtz.org ambako anaweza kujisomea andiko la "mafanikio ya utawala wa awamu ya tatu -1995-2005".

  Nitakuwa mjinga endapo nitaanza kubishana kama barabara ilijengwa au haikujengwa, daraja lilijengwa au halikujengwa, uwanja wa kimataifa wa mpira wa hadhi ya Kimataifa ulijengwa au la; Kama wahenga walivyosema "mwenye macho haaimbiwi tazama". Hivyo, mgongano wangu na utawala wa Rais Mkapa siyo wa kitu gani kilifanyika au hakikufanyika hasa bali ni namna ya utawala wake ulivyotengeneza mazingira ya kifisadi ambayo leo sisi kama taifa tunayalipia gharama kubwa sana.

  Mfumo wa Utawala wa kifisadi ulisimikwa chini yake
  Jambo moja ambalo nina uhakika hakuna mtetezi yeyote wa Rais Mkapa anaweza kusimama na kupinga ni ukweli kuwa mfumo wa utawala wa kifisadi (MUK) ulipandwa wakati wa utawala wa Rais Mwinyi, lakini ulimwagiliwa, kupaliliwa, na kutiwa mbolea wakati wa utawala wa Rais Mkapa. Leo hii katika utawala wa Rais Kikwete tunaanza kuvuna mavuno yake ya awali! Na bado hatujafikia hata nusu ya mbegu zilizopandwa!

  Kutokana na maamuzi mbalimbali yaliyochukuliwa chini ya utawala wake (Mkapa) mazingira yalijetengenezwa ambayo yamefanya ufisadi kuwa ni mgumu kuushinda, yametoa kinga kwa mafisadi, na zaidi sana yamefungua mlango wa watawala kututawala wapendevyo.

  Kuna mtu anabisha?

  1996 – Sheria iliyounda idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi (TISS) na hivyo kwa mara ya kwanza kurasimisha shughuli za watu wa Usalama wa Taifa katika taasisi inayotambulika na kuongozwa na sheria na muundo wa kiutendaji. Kati ya Sheria za Usalama wa Taifa duniani ya kwetu ni miongoni mwa sheria mbovu zaidi kabisa. Ni sheria iliyoweka mipaka ya ajabu kwenye idara hii na kuigeuza siyo idara ya usalama tena kama ilivyokuwa enzi za kina Mzena, Gama, Kombe na wengine waliolitumikia taifa hili. Kutumika kwa sheria hii kama nilivyoonesha mara kadhaa huko nyuma kumechangia kwa kiasi kikubwa sana kwa ufisadi uliokubuhu kwenye taasisi zetu mbalimbali kiasi kwamba wapo wanaojenga hoja kuwa idara hii hutumika kama silaha ya kisiasa.

  Mojawapo ya mambo ya ajabu kabisa katika sheria hii ni kuwakataza watu wa Usalama wa Taifa kutekeleza wao wenyewe jukumu la usalama na badala yake kuwa wakusanyaji, wachambuzi na habari za kiusalama na kijasusi na kutoa taarifa hizo kwa vyombo vingine (ibara ya 2a) Yaani, wanaona mtu anaiba EPA, Richmond wanaingia, Dowans wanadanganya BRELA badala ya kuchukua hatua za kiusalama wao wenyewe wanabakia kwenda kuwaita Polisi! – Rais Mkapa aliipitisha sheria hiyo Januari 20, 1997.

  1997- Mwaka huu uliingiwa mkataba wa hatari sana kwa usalama wa taifa letu na ambao mrindimo wake tumeusikia miezi michache iliyopita ambapo Waziri Mkuu wetu katika hali ya woga aliapa Bungeni kuwa hata kama wabunge wako tayari "kumsulubisha" na wamsulubishe lakini suala la Meremeta hatoligusa kwani ni kwa ajili ya "usalama wa taifa". Nimeonesha katika ile ripoti yangu ni kitu gani hasa kilifanyika. Mkataba wa Meremeta uliingiwa chini ya Rais Mkapa! Mengine ambayo sikuyagusa kwenye ripoti ile yanasubiri wakati wake muafaka. Lakini leo wanataka tumshangilie!

  1998 – Mwaka huo sheria mbili za ajabu kabisa ziliwahi kupitishwa na utawala wa Mkapa na wabunge wa CCM. Sheria hizi mbili ni kichocheo cha mfumo wa ufisadi katika sekta ya madini na vile vile ilitengeneza mwanya mkubwa wa maadili ya kiuongozi.

  - Kuanza kutumika kwa sheria ya Madini ya mwaka 1998 kulifungulia chini ya utawala wa Rais Mkapa uporaji mkubwa wa raslimali na utajiri wa nchi yetu. Kwa mara ya kwanza watawala wetu walitengeneza mfumo wa kufungua urithi wa watoto wetu kwa wageni kwa mtindo wa kuchota maji kisimani kama vile kisima ni chao. Utawala wa Rais Mkapa unaotaka kusifiwa leo kwa "uongozi bora" ulifungulia mlango wa "wawekezaji" kwa kile walichokiita "kuvutia uwekezaji" katika sekta ya madini. Ndipo hapo tukaona yaliyotokea kwenye sekta hiyo hadi kufikia suala la Buzwagi katika miezi ya mwanzo ya utawala wa Rais Mkapa. Migogoro mingi katika sekta ya madini na kile tunachokiita "mikataba mibovu" msingi wake ni sheria hii mbovu. Rais Mkapa aliipitisha kuwa sheria Julai 1, 1998.
  - Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilipitishwa nayo mwaka huo huo na ilikuwa na lengo la kuweka maadili katika uongozi wa umma. Sheria hiyo ilikuwa inamhusu kuanzia Rais hadi wabunge. Lengo la sheria hiyo ilikuwa ni hatimaye kujaribu kuziba pengo la kile kilichofanywa kule Zanzibar walipoliua Azimio la Arusha na kuisigida miiko ya uongozi iliyoanishwa ndani ya Azimio lile. Cha kuudhi katika sheria hiyo ni kuwa yeye mwenyewe Rais Mkapa na aliyekuwa Mwanasheria wake Mkuu Andrew Chenge ninaamini walikuwa ni wa kwanza kuivunja sheria hiyo bila kujali matokeo yake (with impunity). Leo hii wanaendelea kunesanesa na hakuna mtu mwenye uthubutu wa kuwachukulia hatua.

  Mkapa kwa kutumia nafasi yake na kuanza biashara akiwa Ikulu na uthubutu wake wa kutumia taarifa za ndani (inside information) kuhusu Kiwira na hatimaye kujiuzua mgodi huo yeye na Waziri wake wa Nishati. Kikatiba alitakiwa aondolewa madarakani wakati ule ule kwani Katiba inasema Rais anaweza kuondolewa endapo itathibitika amevunja sheria ya maadili. Lakini nani ana ubavu huo!?

  Niseme nini tena; niendelee kuchambua jinsi utawala wa Mkapa ulitengeneza mfumo wa mafanikio ya utawala wa kifisadi? Nijadili sheria ya fedha ya 2001 na 2004? Niandike juu ya sheria ya mafao ya viongozi wa kisiasa ya 1999? Nizungumzie mfumo wao wa ubinafsishaji wa makampuni yetu? Nielezee kama marudio yaliyotokea NBC, Tanesco, Posta na Simu, na kwingine?

  Nije nizungumzie yale tunayoyajua ya ufisadi katika Benki Kuu? Nirudi na kuchambua ajira ya Gavana Ballali? Nizungumzie uanzishwaji wa makampuni feki? Nielelezee kama kichaa mmoja jinsi utawala wake ulijitahidi kuua kila kizuri cha "kwetu" kwa kukimbilia cha "wageni" kwa vile wanataka kuja kutuokoa?

  Mnataka nirudi kugusia yale yaliyotokea kwenye sekta yetu ya utalii, uwindaji na elimu? Kweli tunatakia kusahau haya yote na kushangilia uwanja wa mpira, daraja la Mkapa, na barabara tu?

  Mnataka niseme kuhusu yale mabadiliko ya Katiba ya 2005 ambayo yalimtengenezea nafasi Lowassa ya kukaimu kiti cha Urais na kumuondoa Spika wa Bunge la Muungano!? Mnafikiri hatukuyaona wakati ule? Mnataka tugusie ya Mwembechai na mauaji ya Pemba? Au mnafikiri nayo tumeyasahau?

  Basi na wasimame watetezi wa Mkapa leo! Wasimame au asimame yeye mwenyewe kujitetea juu ya ya ufisadi uliokubuhu uliofanyika mbele za macho yake ambao ninadai ulitengenezwa kitaalamu na kuundiwa sheria mbalimbali ambazo zimeufanikisha!

  Ndugu zangu, wanaotaka kumsifia wamsifie kwa madhara yao wenyewe; wanaotaka kucheza chioda na lizombe kumshangilia basi na wafanye hivyo! Wale wana CCM wanaotaka kumshangilia kuwa alikuwa ni kiongozi bora basi wafanye hivyo.

  Lakini wakumbuke kuwa siyo wana CCM wote wamezugwa, siyo wananchi wote wamefumba macho na siyo vizazi vyote vitaaamini uongo hata upambwe kwa bendera, maneno ya ukali na vitisho vya madhara.

  Ushauri wangu ni kuwa Mkapa aendelee kukaa kimya tu. Natoa hoja na watetezi wake wasimame sasa waseme au wanyamaze milele! Siku moja watasimama watawala kati yetu ambao watayafunua haya yote kwa wote kuona na ndipo tutakapojua kuwa uongo hata upambwe kwa saluti haugeuki kuwa ukweli!

  Haya, niache kuandika kabla sijaambiwa "anapandikiza mbegu za chuki, dharau, na analeta mgawanyiko katika jamii"!

  Barua Pepe: mwanakijiji@mwanakijiji.com
   
 18. K

  Kapwani JF-Expert Member

  #18
  Nov 25, 2009
  Joined: Nov 17, 2009
  Messages: 668
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Siwezi kusahau kauli zake za kabehi wakati ule alipokuwapo magogoni kwa watu waliokuwa anatofautiana nao kimtazamo, kauli kama hizi " wavivu wa kufikiri" watanzania wa siku hizi wanahusisha mtu mnene aliyevaa suti na rushwa" "wivu wa kijinga"
  Sitegemei kama kuna siku mtu mwenye kauli kama hizi anaweza kujisahihisha kirahisi kwani yoote tunayozungumza yeye anatuona kama wavivu wa kufikiri....wivu wa kijinga! tunalinganisha suti na haiba yake na rushwa ......kaaaazi kweli kweli


  NANYI MTAIFAHAMU HIYO KWELI NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU
   
 19. N

  Nurujamii JF-Expert Member

  #19
  Nov 26, 2009
  Joined: Jun 14, 2007
  Messages: 414
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 35
  Mkapa ana tatizo moja kubwa: Kwake yeye "being humble is equal to humiliation". ndio maana tangu kujikuta kwenye hii aibu, either anashindwa kujibu tuhuma au akijaribu kujibu anatanguliza kiburi.

  Mkapa ushauri wangu wa bure huu hapa: Simama mbele ya umma sema i am sorry for what i did to you my fellow Tanzanians. Naombeni msamaha, tasahau yaliyopita tugange yajayo....Mimi ni binadamu na wala sio malaika. Naahidi kutumia muda wangu uliobaki hapa duniani kutoa ushauri na kumsaidia Rais aliyepo madarakani kuongoza kwa busara ili asije kuingia kwenye mtego nilionaswa....
   
 20. Ulimbo

  Ulimbo JF-Expert Member

  #20
  Nov 26, 2009
  Joined: Aug 14, 2009
  Messages: 678
  Likes Received: 41
  Trophy Points: 45
  Tatizo na viongozi wa Tanzania ni kulindana. Mkapa anaujasiri mkubwa kwamba haukuna kiongozi aliyeko madarakani anaweza kumnyooshea kidole, ndiyo sababu ananyamaza kimya. Sehemu kubwa ya viongozi wa juu walioko madarakani ni zao la Mkapa, na baadhi ya maovu mengi aliyo tenda Mkapa ndo yaliyowaweka hao viongozi madarakani. anajua wazi kuwa iwapo watambana, basi na wao pia wataumbuka.

  Laiti angetokea kiongozi ambaye hayouko kwenye blood stream ya Mkapa, na kuweka sheria ya kuwaondolea kinga hawa viongozi fisadi, basi mambo yangekuwa matamu kwani kuna mengine ambayo yatafichuliwa amboyo tusingengetegemea kuwa yapo.
   
Loading...