SoC02 Tabasamu na Mwalimu

Stories of Change - 2022 Competition
Jul 27, 2022
94
134
Mwalimu ni mwanajamii mwenye thamani kubwa sana katika ujenzi wowote wa jamii yenye mtazamo wa maendeleo endelevu. Kuna walimu rasmi yaaani walimu waliopitia katika mfumo maalumu wa mafunzo fulani ili wapate ujuzi wa kuhaulisha maarifa kwa kizazi fulani. Pia kuna waalimu wasio rasmi, hawa ni wale ambao huwa na talanta ya kuelimisha jamii kwa masuala mbalimbali yahusuyo jamii na maendeleo endelevu kwa kufundishana namna ya kujikwamua katika fikra hasi na kuuishi uchanya wenye tija.

Kwa mtazamo wa mazingira ya nchi zetu zinazoendelea bado mwalimu hajapewa thamani sawa na majukumu yake anayoyafanya kwenye jamii. Ila wasiwasi wangu pia unaletwa na maswali kadhaa ambayo inawezekana ni mitazamo yetu wenyewe sisi tuliomo kwenye kada hii ya ualimu. Najiuliza tu;

1. Je, mwalimu alisoma ualimu baada ya kukosa nafasi kwenye kada nyingine?
2. Je, mwalimu wa wito bado yupo kwenye jamii zetu?
3. Je, mwalimu anaipenda kazi yake kwa dhati ama anafanya tu ili mradi mwisho wa mwezi acheke?
4. Je, kuna mazingira rafiki ya kumfanya mwalimu atabasamu na kurithisha tabasamu kwa mwanafunzi wake?
5. Je, sisi tuliopita kwa walimu kadhaa tumewahi kuwafanya wale walimu waliotufundisha kuwa marafiki zetu au tuna mifano mibaya tu ya adhabu na kejeli?

Pamoja na maswali hayo baada ya kukaa kwenye kada hii zaidi ya miaka 15 sasa nimegundua kwamba ili mwalimu awe rafiki katika mazingira yake ya kazi, awe rafiki kwa wanafunzi wake na jamii kwa ujumla tunatakiwa kuzingatia baadhi yafuatayo;

1. MTAZAMO_CHANYA Hili ni jambo muhimu sana katika kila kada. Kuitazama kazi yako na majukumu yako katika Mtazamo chanya kwa kuziona changamoto zinazotuzunguka na kuzigeuza kuwa fursa. Tuondoe funza wa fikra duni juu ya kazi ya ualimu. Kuna wanaosema hawajawahi kuona mwalimu tajiri ila niseme tu hakuna utajiri mkubwa kama utajiri wa fikra maana ubunifu wote huanzia kwenye fikra zetu.

Nikupe mfano mdogo tu wa fursa walizozipsta waalimu kipindi cha Uviko 19 mwaka 2020 baada ya shule kufungwa. Kuna mwalimu na Kiongozi mkongwe Mama Gertrude Mongella nilipata wasaa wa kubadilishana nae mawazo anasema, "Niliona namna napata maswali mengi na namna watu walihitaji ushauri kuhusu masuala mbalimbali ya uongozi, niliamua kujifunza namna ya kufundisha kwa kutumia darasa la mtandao "Zoom" na nilipofanikiwa nikaanda darasa la uongozi na nilipata wanafunzi wengi mno kiasi kwamba kwa siku nilikuwa na saa kadhaa za kufundisha na hakika nilitengeneza pesa haswa". Huu tu ni utajiri mkubwa kabisa.

2. UPENDO Natamani kufundisha huu upendo kwa mapana na marefu ila ukipata wasaa wa kupitia machapisho kadhaa kwenye kurasa zangu za kijamii nimeuzungumzia sana huu UPENDO haswa ule usio na sababu. Ukijipenda mwenyewe utapenda unachokifanya, utaipenda kazi yako, utawapenda wanaokuzunguka haswa wateja wakuu ambao ni wanafunzi. Tunaweza kuwa marafiki wakubwa kwa wanafunzi wetu tukitengeneza mazingira rafiki baina yetu na wanafunzi. Hii itatufanya tunapoandaa mazingira ya kujifunza na kufundisha tutaangalia namna ya kuleta furaha kwetu sote na kutengeneza UPENDO ambao utadumu miongoni mwetu na kumfanya mwanafunzi apende shule, apende somo, ampende mwalimu na awapende wenzie pia.

3. TABASAMU RAFIKI Kuna namna tunapitia changamoto nyingi kwenye harakati za maisha haya ila kuna namna inabidi tufahamu tabasamu linaweza kuokoa vizazi vingi katika jamii yetu. Mwalimu hutazamwa kama kioo kwa mwanafunzi, kuna vijana/watoto wanakutana na mengi katika ukuaji wao ila anapokutana na tabasamu kwa mwalimu wake hakika anauwezo wa kuyasema yote yanayomtatiza na kutafuta suluhu kwa pamoja nakwambia kijana/mtoto huyu hawezi kumsahau kamwe mwalimu huyu.

4. MOTISHA CHANYA Ni kweli kabisa hakuna rushwa wala michango yoyote shuleni. Mwalimu huyu ili awe na UPENDO na aweze kutengeneza mazingira rafiki katika majukumu yake huihitaji motisha chanya kutoka kwenye jamii na serikali yake kwa ujumla. Uzuri wa mioyo ya walimu wengi ni mioyo yenye shukrani na kuridhika.

Tujiulize tu; ni lini tumempelekea kitenge yule mwalimu wa awali aliyetufundisha kushika kalamu na kutuwezesha leo tunaandika na kuweza kusoma andiko hili? Ni lini serikali imetambua umuhimu wa yule mwalimu anayefundisha silabi mwambatano kwa wanafunzi wa jamii inayotumia Kiswahili kama lugha ya pili? Ni lini tumeandaa sherehe za kutambua thamani ya mwalimu kwenye mitaa yetu, kata, kitongoji, kijiji ama Wilaya? Tuna harakati nyingi nyingi zinazotumia pesa kutafuta matokeo mazuri kwa wanafunzi bila kumuonesha thamani huyu mwalimu anayetokomeza matokeo mabaya.

Motisha hizi ziende sambamba pia kwa Wanafunzi maana kuna wanafunzi wanaoonesha bidii kubwa katika kujifunza, hakuna jambo zuri na linalotia moyo kama kutambuliwa kwa juhudi na mchango wako katika harakati za kufuta ujinga.

Naamini pamoja na changamoto mbalimbali zinazotukuta katika kulisogeza mbele gurudumu letu la Elimu bado tuna nafasi ya kumfanya Mwalimu awe rafiki katika mazingira yote ya ualimu. Tutarejesha tabasamu kwa mwalimu na mwanafunzi kwa kuuangalia tena mtaala wa Elimu uliotumika miaka ya 1980 hadi 1998, tuangalie namna wanafunzi walivyopenda shule pamoja na kutumwa vidumu vya maji, mifagio, majembe, fyekeo, mbolea, maua n.k.

Tuangalie namna mwalimu alivyothaminiwa miaka ile pamoja na kuchapa wanafunzi kupitiliza. Tuangalie namna mwanafunzi alifundishwa elimu ya kujitegemea kama vile kulima mbogamboga, kuandaa matuta ya viazi, alifundishwa kazi nyingi za mikono kama vile kufuma vitambaa, mikeka kwa kutumia ukili, kufinyanga vyungu na mapambo mbalimbali ya nyumbani, ushonaji, ususi, upishi na hata usafi binafsi. Hii imenikumbusha wakati wa likizo nilikuwa nilirejea nyumbani wananiita Bibi afya maana nilirejesha yote niliyofundishwa darasani kwenye vitendo haswa kufanya ule usafi wa juma na usafi wa mwezi.

Mwisho kabisa ila si kwa umuhimu, Mabadiliko yote haya ili mwalimu awe rafiki huanza na mimi, hufuata wewe na hatimaye fikra za jamii nzima ambayo ndiyo serikali yenyewe.

Mimi mwalimu mwenye kurejesha tabasamu kwa wanafunzi na jamii,
Mwalimu Demitria Thomas Gibure.
 
Nauona wito na ualimu wako na utayari wenye msukumo wa Mungu katika kuwatumikia wengine (wanafunzi) hilo ni patano lako na Mungu na nia yako ya dhati, Utende hayo ya kurithisha ufahamu na kuelekeza akili za vijana wetu kwa mtazamo chanya, utayari, furaha na kwa tabasamu ambalo Mungu amekujalia.

Upe Wito wa Ualimu hamasa chanya. Nakumbuka Vitabu vya "Someni kwa Furaha". Mada uliyoiandika kwa umakini mkubwa ndani yake ipo dhana ya wanafunzi wasome kwa furaha kutoka kwa mwalimu mwenye furaha na aliyejawa tabasamu. Penye furaha na upendo hamasa na ari ya kujifunza huongezeka.

Hii ni kweli iwe darasani na hata kwenye nyumba za ibada, iwe kwenye semina, warsha nk. Mada yako imekidhi vigezo vyote. Hongera sana.
 
Nauona wito na ualimu wako na utayari wenye msukumo wa Mungu katika kuwatumikia wengine (wanafunzi) hilo ni patano lako na Mungu na nia yako ya dhati, Utende hayo ya kurithisha ufahamu na kuelekeza akili za vijana wetu kwa mtazamo chanya, utayari, furaha na kwa tabasamu ambalo Mungu amekujalia...
Asante sana kwa nyongeza ya mawazo mazuri kabisa yenye kutia moyo wa Wito.
 
Back
Top Bottom