Taazia: Ninavyomkumbuka Dada Yangu Haki Hanya (Haki Kilomoni)

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,920
30,261
TAAZIA: NINAVYOMKUMBUKA DADA YANGU HAKI HANYA (MRS. HAKI KILOMONI)
Haki mimi ni dada yangu.

Napata akili namuona Haki na marehemu dada yangu Mengi mashoga, wote wanasoma chuo cha Shariff Abdulrahman Mtaa wa Sukuma na Mafia. Hii ni katikati 1950s tunaishi Mtaa wa Kiungani na Sikukuu.

Siku nyingine wananichukua kwa kuwalilia tunakuja sote chuoni, Mtaa wa Sukuma jirani ya club ya Young Africans. Mimi wananiacha nje wao wanaingia ndani kusoma.

Mkabala wa chuo hiki ni nyumbani kwao marehemu Jaffari na Tatu Hamza na wadogo zao, Hamidu, Mwashamba na Ghalib maarufu Gae.

Kulikuwa na kaka yao mkubwa kabisa jina limenitoka. Alikuwa na kampuni ya Security Guards na wakati naishi Masaki alikuwa akituletea askari kulinda nyumba zetu usiku.

Mimi na Mwashamba Hamza umri wetu sawa na akawa dada yangu hadi alipotangulia mbele ya haki na nilihudhuria maziko yake Kisutu.

Mwashamba aliolewa na MwanaKariakoo mwenzake Abdallah Faraji. Mwashamba alikuwa shoga mkubwa wa mke wangu na alifurahi aliposikia kuwa mwanangu wa kwanza ni somo wa mumewe yaani majina yao yamefanana.

Mwashamba tulifanyakazi sote Bandarini. Nakumbuka sana jinsi Da Tatu alivyoshughulika kwenye harusi yangu ambayo ilifanyika nyumbani kwa dada yangu Mengi Morogoro Store, Oyster Bay.

Da Tatu na dada yangu Mengi ni umri mmoja na mchezo wao mmoja.
Mimi ni mdogo wao sana.

Nakumbuka siku kabla ya harusi kulikuwa na "gathering," nyumbani kwa dada yangu basi wakaniingiza chumbani dada zangu hawa wameniweka kati kunifunda niwe mume mwema kwa mke wangu nitakaekabidhiwa kesho.

Mzungumzaji mkuu alikuwa Mariam Donna Summer. Dada Haki yeye alikuwa tayari keshaondoka anaishi Uholanzi na laiti angekuwapo tungekuwanae.

Naamini ndugu zangu wa Kariakoo wakisoma haya majina nitakuwa nimewapeleka mbali sana.

Namkumbuka Da Haki katika miaka ya 1960 mwishoni mimi nasoma St. Joseph's Convent School na yeye anafanya kazi East African Posts and Telecommunication Services (EAP&T), Idara ya Stamp Bureau.

Jengo la EAP&T lilikuwa jirani sana na shule yetu. Nilikuwa wakati mwingine mchana napita ofisininkwake kumwamkia.

Kila nikenda kumwakia wakati wa kuagana atafungua mkoba wake atatoa shilingi moja atanipa.

Hizi zilikuwa fedha nyingi sana kwa nyakati zile.

Haya ndiyo yalikuwa mapenzi na udugu tuliorithi kutoka kwa wazee wetu.

Dada Haki kila mwaka Mfungo Sita Maulidi ya Bagamoyo alikuwa akimletea fedha Shariff Abdulrahman mchango wake wa Maulid.

Da Haki kanieleza kuwa Maulid ya Bagamoyo yanamkumbusha utoto wake.
Katika vijana waliosoma chuo hiki ambao walisoma na hawa dada zangu ni Ishaka Marande na dada yake mdogo Bi. Mgeni.

Mwanae Da Haki Ali Kilomoni alikuwa kila akija likizo Dar-es-Salaam lazima atanitafuta kunipa salamu kutoka kwa mama yake.

Nilipohamia Tanga Ali alikuja kwa mama yake mdogo Bi. Hawa na alikaa muda mrefu Tanga na tukawa pamoja.

Hawa ni umri wangu na ndugu yake Kulthum sote tumesoma sekondari wakati mmoja.

Nikiwatania waume zao kuwa wameoa dada zangu bila ya idhini yangu mimi kaka yao.

Nilipostaafu na kurudi Dar es Salaam nikawa nakaa Magomeni Mapipa.

Mdogo wao marehemu Hamisi mara nyingi akija nyumbani kunikagua na tutazungumza mengi.

Turudi nyuma.
Miaka mingi ikapita sijamuona Da Haki.

Mwaka wa 2011 nikapata safari ya kwenda Berlin.
Nilikuwa Berlin kwa mwezi mzima.

Kaka yangu Prof. Charles Mgone alikuwa Hague nikaenda kumtembelea.
Yeye kama Da Haki miaka mingi walikwenda Ulaya.

Nikamwambia Prof. kuwa Dada Haki yuko Amsterdam kwa miaka mingi hatujamuona twende tukamjulie hali.

Alifurahi sana kutuona.
Kwetu sote yeye ni mkubwa na ile furaha yake siku ile ilikuwa kubwa.

Tulimkumbusha dada yetu Mengi.
Anaishi nje kidogo ya Amsterdam.

Da Haki alikuja na gari yake kutuchukua train station kutupeleka nyumbani kwake.

Siku nzima stori zilikuwa ni za Kariakoo ile tuliyokulia.

Tulipokuwa tunaagana nikamwona dada yangu amekwenda kwenye shubaka lake la vitabu akawa anachomoa kitabu pale kitabu hapa anaweka chini akavitia kwenye mfuko mzuri akanipa.

Nimeshangaa dada yangu miaka mingapi hatujaonana kajuaje mapenzi yangu kwa vitabu?

Vitabu hivi viko Maktaba na nilikuwa kila ninapoviona namkumbuka dada yangu kipenzi.

Vitabu hivi sasa vitaendelea kunikumbusha safari ya kwenda kumsalimia dada yetu mimi na kaka yangu Prof. Mgone miaka 13 iliyopita safari ambayo ilikuwa kama vile tunaagana mapema kwani hatukuonana tena baada ya siku ile.

Usiku huu ndiyo nimepokea taarifa ya msiba.

Niliingia Maktaba kutafuta picha nilizompiga dada yangu nyumbani kwake Amsterdam.

Allah amfanyie wepesi safari yake dada yetu.
Amin.

Picha za kwanza mbili ni dada yetu na sisi nyumbani kwake Amsterdam.

Picha ya tatu ni Mwandishi na kulia na wa mwanzo ni Ali Kilomoni mtoto wa kwanza wa marehemu Dada Haki na huyo mwingine ni mwanangu Faraj tukiwa Tanga.

1705289017963.png

1705289070243.png

1705289099602.png
 
Apumzike kwa amani dada yako huyu... Poleni sana nguli wetu wa historia ya Tanganyika na Zanzibar
 
Sh Mohamed
MashaAllah, Mwenyeezi Mungu amekujaaliya kipaji cha uandishi, nami nimo katika kudondoa mawili matatu,
Yalaiti wengi wetu tungelikuwa tunakusoma kwa ajili ya kuelimika basi hakika tungelifaidika mengi
Ahsante
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom