I'm curious. Nini hasa kilichofanya Kikwete aamue kuvunja mtandao "uliojengwa na Lowassa" ambao ndio uliomuingiza yeye madarakani? Tuseme alikwishapiga hesabu zake mapema akiwa na lengo la "kummaliza Lowassa" mara tu baada ya kufanikiwa kuwa rais kwa msaada wa mtu huyohuyo aliyemuaminisha kuwa na urafiki naye? Kwamba baada ya hapo Lowassa hatakuwa na manufaa tena kwake? Inawezekana kuwa JK ni muumini wa falsafa za Niccolo Machiavelli za kutumia watu kufanikisha malengo/maslahi binafsi kisha kuwatupilia mbali - hata kuwaangamiza? Kwamba kwake suala la urafiki, uswahiba na hisia za aina hiyo hazina nafasi katika utu wake? Ndio maana anaweza kudumisha tabasamu na bashasha mbele ya umma hata kama behind the scenes anaagiza watu wanaotishia maslahi yake, ya familia yake na ya utawala wake kufanyiwa maovu?
Mleta mada umefurahia Kikwete "kuuvunja" mtandao wa Lowassa. Ingekuwa vyema basi pia ungetoa ufafanuzi ni kwa malengo gani na kwa maslahi ya nani? Ni sisi Watanzania ndio wanufaika au ni mchezo wa kuzidiana kete (battle of wits) kati ya wanamtandao - tena mmoja akiwa ndiye mjuzi (JK) na mwingine akitumika kama zoba (EL)? Majuzi mzee Butiku alilalamika kuwa CCM na serikali yake vimeharibiwa na hao "wanamtandao". Naona ukweli unadhihirika kwenye mada kama hii. Sawa. Inawezekana, katika mchezo wa wanamtandao, Lowassa keshamalizwa nguvu na JK na hivyo CHADEMA imeingia mkenge na kupoteza. Hii ina mana gani kwetu wananchi? Tukubali kuendelea kuwekwa poni na magwiji wa mtandao?
Ninachokiona ni mchezo uleule ukiendelezwa na JK kupitia Magufuli. Naye anatumiwa kama kete tu ya kukirudisha madarakani chama ambacho sasa kinadhibitiwa kikamilifu na upande wa JK kwa falsafa ileile ya Machiavelli. Inawezekana hata teuzi nyingi zilizofanywa muda mrefu na karibuni ni sehemu (game plan) ya mchezo huo. Na si Magufuli tu. Marehemu Mtikila, Dk Slaa, mama Maria, mzee Mwinyi, n.k. nao wameshawekezwa kwenye mkakati huo. Hivyo, kati yao wote hakuna aliyekuwa na au mwenye ubavu wa kuleta mabadiliko ya maana katika mfumo na uendeshaji wa chama na serikali.
Kwangu mimi, hii ni sababu tosha ya kuiondoa CCM madarakani ili kuinusuru nchi kuwekwa rehani na watu wenye maslahi binafsi pekee, wasio na chembe ya uzalendo wala utu. Ni bora kuanza kwa kuvunja "spell" ya "CCM mtandao" - hata kwa kumtumia aliyekuwa mmoja wao ambaye wamemzidi kete na kumfanya zoba na ambaye, naamini, anaweza kudhibitiwa kirahisi zaidi ndani ya mabadiliko. Hii itafanya, kwanza, CCM yenyewe ijisafishe kwa dhati na, pili, watakaokuwa madarakani watambue kuwa umma umeshachukua mamlaka yake ya kudhibiti watawala bila hofu kwa kutumia mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Hatuwezi kuacha taifa liendelee kuendeshwa kwa falsafa za Machiavelli.