Sumaye amgwaya Lowassa!

Hana lolote mnafiki huyo mbona alipokuwa PM aliwahi kusema "ukitaka maisha yako yakunyookee jiunge na CCM"

Leo hii anakula matapishi yake mwenyewe! wanasiasa wa CCM wengi ni vigeugeu.

Hapana aliwaambia wafanya biashara wa Moshi wakitaka mambo yao ''yanyooke'' wajiunge na CCM
 
Angesema hayo walipokuwa wakibishana kuwa rushwa iitwe takrima na Takrima halisi ifutwe.
 
Mtu wangu we unachewa sana kuleta updates,uwe unazipitia threads maana sishakwepo sana humu
 
Huyu hakuwa Waziri Mkuu wa Mr. Clean ? ina Maana hakupata kiwanda au Madini yoyote ?Ina Maana Mr. Clean hakushauriana nae kwa MIAKA 8 ? Lowassa alikuwa Waziri Mkuu kwa Miaka 2 angalia Anavyotuteteresha na Mapesa ya Ma Dowans, Mara Tanesco Mara Serengeti... Mara nyumba za wabunge na National Housing kuuzwa
Na wewe Unagushi hata lile shamba la heka 100 Morogoro sio chochote ?
 
Huyu Sumaye Mi namwona kama BOYA tu kwani huu ufisadi uliomo ndani ya chama chake analiona na hata hakuna siku ametoa kauli zaidi ya kupalilia uovu tu!
Sasa leo anakumbuka shuka ingali kumekucha,huyu hana nyimbo,VUA GAMBA VAA GWANDA ndio ingekuwa safi na ajisafishe ndani ya mafisadi na matrilion ya shilingi aliyojiwekezea aweke wazi kwa faida ya wanainchi!

Huyu sijaona jipya kwake!
 
Hana jipya. WanaJF naomba kuuliza ivi ukiwa waziri mkuu mstaafu ina maana ukihama chama unakosa haki zako za uwaziri mkuu mstaafu au katika serikali hii ya Tanganyika inakuwaje. Mi nafikiri waziri mkuu unakuwa kiongozi wa wote bila kujali chama. Na stahiki zako unawezapata hata ukihama chama kama wewe ni waziri mkuu mstaafu. Naomba nielezeni

Unaendelea kupata haki zako zote... hata Maalimu Seif... alikuwa anapata hata alivyokuwa CUF.
 
Sumaye hana ubavu wa kupambana na Lowasa hata kwa dakika moja tu,ila ni kweli chaguzi za ccm zimetekwa na wanamtandao,kumbuka uchaguzi 2010 Selelii,mh sitta (uspika) na wengine wengi.

Lowasa has nothing to do with kuanguka Sumaye Hanang' watu msipende kuishi kwa hisia kuliko uhalisia.....Both Lowasa and Sumaye are the target katika huu mchujo ila tu wanapunguzwa nguvu kwa hatua na uangalifu mkubwa from the worst devil to the better devil kama unavyokata miti mikubwa huku ukiogopa isije ikakuanguakia kabla hujatengeneza njia ya kukimbia ikikaribia kudondoka....

Uzuri ni kuwa this time adui ni mtu wa nyumbani mwako mwenyewe ambaye anaweza fungua mlango wakati mume lala mashujaa waingie bila kubomoa milango ya miji na kuchukua vilivyo vyao....Lets create more confusion kwenye ushirika wa uchawi....Let us break down their Babel tower tuone kama wataweza kuujenga tena wakiwa kila mtu anaongea luga yake....Please clap hands for we are almost there!
 
Wakuu,

Nipo kwenye ukumbi tayari na nitawajuza kila kinachoendelea ikiwa ni pamoja na picha. Mods mtanisadia kuziweka sawa kwakuwa nitakuwa naandika kadiri matukio yanavyojiri.

Ni hapa Courtyard Hotel - Dar

attachment.php
Hivi kweli aliyesema JK dhaifu alitumia kalamu kuitafuta ikulu na sasa anatumia mtutu!! eh!!!
 
Mimi nilikuwa na maoni tofauti kidogo - kama Watanzania na Viongozi wetu tungekuwa ni watu wa kuheshimiana bila kughubikwa na ubinafsi na roho ya kuchafuana - nafikili suala hili la Mh.Sumaye kudhalilishwa nadhani kusingekuwepo.

Ninacho taka kusema hapa ni kwamba kuna haja gani ya kuwadhalilisha Mawaziri wakuu walio pita? Kwa mawazo yangu naona wangeruhusiwa tu kuwa members wa NEC bila ya kuangahika kupigiwa kura majiboni mwao au kitaifa; hawa ni viongozi ambao waliwahi kuwa Watendaji wakuu Serikalini, wanajuwa siri nyingi za TAIFA - Sasa wakibakizwa kama washauri wakuu ndani ya NEC kuna ubaya gani? Mambo ya kukomoana hayafahi hata kidogo, nchi hii ikivurugika hakuna ambaye atabaki salama tusije tukajidanganya.

Kuna haja gani ya kufitinisha watu wasielewane hata wakiwa wanatoka kijiji au mkoa mmoja, au kushinikiza watu wachukuwe form za kuomba uwakirishi ndani ya NEC hata kama hawana interest ili mradi wamuwekee kahuzibe mtu wanaye muona TISHIO kwao. Ni mara chache kumuona/kumsikia Mh.Sumaye akitoa shutuma ambazo hazina mshiko, yaani nilivyo muona jana alikuwa visibly dejected - kwa kuwa aliwahi kuwa kiongozi mkuu katika TAIFA letu na ana uwezo mkubwa wa kujuwa mambo yanayo endelea ndani ya Serikali yetu na TAIFA letu ana uwezo kutumia sources chungu nzima zilizo wahi kuwa chini yake at one time - Watanzania wenzangu kauli zake tunapaswa kuzitafakali kwa umakini sana na Serikali yetu kuzifanyia kazi bila ya kuwa na ushabeki wa VIKUNDI ndani ya chama tawala, nanavyo hisi mimi tusipuuzie kauli zake hata kama kwa wengine zinaonekana si chochote si lolote - kwa mawazo yangu naona hali sio nzuri kusema UKWELI. Sasa hivi nilikuwa na angalia luninga kuhusu uchaguzi wa UVCCM huko MARA watu wanapigana ngumi wanatupiana viti kisa ? Wasimamizi walikuwa wameonga watu ili wachaguliwe - hii nini lakini!!!!!
 


Waandishi Wetu

Toleo la 261
3 Oct 2012




  • Asema mafisadi wamemwangusha
  • Wakiingia 2015 atakula nao sahani moja
  • Hiyo ni iwe kwa tiketi ya CCM au kwingine


BAADA ya kushindwa kwenye uchaguzi wa ndani ya chama chake, waziri mkuu wa zamani, Frederick Sumaye sasa anasema ni kazi ngumu kushinda CCM kama huna fedha.

Amekuwa akiwaambia watu wa karibu naye kwamba kuangushwa kwake na rafiki yake wa zamani, Dk. Mary Nagu, katika kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC) wilayani kwao Hanang, wiki iliyopita, kulichangiwa na matumizi makubwa ya fedha na tishio kwa wapinzani wake wanaomuona kuwa anaweza kuharibu ndoto zao za kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka 2015.


Tayari mwanasiasa huyo amesema atazungumza na waandishi wa habari wiki hii kuelezea ya mayoni mwake, lakini habari ambazo Raia Mwema inazo zinasema pamoja na kulalamikia rushwa kwenye uchaguzi huo, Sumaye anaweza kuzungumzia pia uwezekano wa yeye kuwania urais mwaka 2015, hata ikibidi, kupitia chama kingine cha siasa au kama mgombea binafsi kama Katiba itaruhusu.


Wachambuzi wanasema kwamba maana ya maneno haya ya Sumaye ni kwamba wapinzani wake wasiamini kwamba kwa kumshinda Hanang, basi kazi imekwisha. Kwamba kwake ni aluta continua. "Alikua anasita kuwania urais baada ya makundi mbalimbali ya kijamii kumuomba ajitose kuwania nafasi hiyo, lakini sasa matokeo ya juzi yamemfanya aone Taifa linakwenda kubaya kwa siasa kutawaliwa na mbinu chafu na rushwa. "Kwa sasa lazima atapambana, na hasa kama wanaotuhumiwa kwa rushwa wakijitosa kuwania urais, na yeye atajitosa kupambana nao hata ikibidi nje ya CCM," anasema mmoja wa watu walio karibu sana na Sumaye.


Mwandishi Wetu wa mkoani Manyara anaripoti kwamba kwa matukio yalivyokuwa kuelekea uchaguzi, isingekuwa rahisi kwake kuvuka kutokana na msimamo wake wa kupinga matumizi ya fedha katika chaguzi na hiyo ni kati ya sababu zilizomwangusha mwanasiasa huyo, ingawa watu wake wanasema matokeo hayo yamempa nguvu zaidi.


Sumaye aliyehudumu kwa miaka 10 kama waziri mkuu na ambaye alikuwa mbunge wa Jimbo la Hanang tangu mwaka 1985 hadi mwaka 2005 alishindwa na mbunge wa sasa wa Hanang Dk. Nagu ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na Uwekezaji) mtu ambaye huko nyuma alikuwa rafiki yake mkubwa.


Taarifa za Sumaye kushindwa zilianza kuvuja mapema hata kabla ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi huo saa 10:00 alfajiri juzi, huku baadhi ya wapambe wake wakilazimika kuondoka ukumbini wakimwacha msimamizi wa uchaguzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Elaston Mbwilo, kutangaza matokeo ambayo tayari yalikwishakufahamika.


Mbwilo alitangaza kwamba Sumaye alipata kura 481 huku Dk. Nagu akiibuka na kura 648. Mgombea mwingine, aliyekuwa anawania nafasi hiyo, Leonce Marmo Bura, alitangaza kujitoa mapema ili apate fursa ya kugombea nafasi ya Ujumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ambao alishinda.


Ushindi huo wa Nagu ambao unadaiwa kuwa umetokana na nguvu za kisiasa kutoka nje ya Jimbo la Hanang na matumizi makubwa ya fedha, umelalamikiwa sana watu wa kambi ya Sumaye. Mmoja wa makada walioongoza kampeni ya Sumaye ameliambia Raia Mwema kuwa mmoja wa wanasiasa wakongwe ambaye anadaiwa kupanga mkakati wa kuwania nafasi ya urais (jina tunalihifadhi kwa sasa) ndiye aliyesuka mkakati wa Sumaye kuangushwa.


"Jambo hilo liko wazi, tangu mwanzo wa uchaguzi huu ambao awali wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya waliondoa jina la Nagu kwa maelezo kuwa ana nafasi nyingi za uongozi, lakini Kamati ya Siasa ya Mkoa ilirudisha jina lake kwa nguvu," alieleza kada huyo na kuongeza:


"Kwa muda mrefu Sumaye amekuwa mwathirika wa siasa za makundi ndani ya CCM kwa kushughulikiwa na mkono usioonekana. Tunaamini kuwa hiyo ndiyo sababu za msingi za kushindwa kwake lakini ukweli utabaki kuwa wananchi wa Hanang walikuwa na imani naye."


Aidha, inadaiwa pia kwamba hata taratibu za uchaguzi kwa kiasi kikubwa zilikiukwa na taarifa zinaeleza kuwa wajumbe wengi waliopiga kura hawakuwa wajumbe halali wa mkutano huo wa uchaguzi.


"Kati ya mbinu chafu zilizotumika ni ile ya wajumbe kuuza vitambulisho vyao vya mkutano kwa kiasi cha shilingi 100,000 kwa wajumbe wengine ambao ni mamluki waliolipwa fedha na kuingia katika ukumbi wa mkutano kupiga kura," alidai kada mwingine.


"Maafisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa pamoja na wale wa Usalama wa Taifa walikuwapo eneo la mkutano lakini uwepo wao haukusaidia kitu, wajumbe waliendelea kugawiwa fedha na kampeni ziliendelea hata ndani ya ukumbi kinyume na sheria za uchaguzi,"alieleza.


Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara, Ndekubali Ndeng'aso, hakupatikana juzi kutolea ufafanuzi madai ya makada hao wa CCM.


Ukiacha yaliyomsibu Sumaye, karibu majina yote ya wana CCM ambao wamekuwa wakitajwa katika orodha ya wagombea urais kupitia CCM imekuwa ikijitengeneza.


Hao ni pamoja na Edward Lowassa ambaye amepita katika Wilaya ya Monduli, katika uchaguzi uliovuta hisia za wengi kutokana na kuwa huko nako waziri mkuu wa zamani mwingine, Lowassa, alikuwa anapambana na hasimu wake wa kisiasa kwa muda mrefu Dk. Salash Toure.


Katika uchaguzi huo, kama ilivyotarajiwa, Lowassa alimshinda vibaya Toure kwa kupata kura 709 huku daktari huyo mstaafu akiambulia kura saba tu kumuacha Lowassa akipaa, na pamoja naye, wakiingia wapambe na maswahiba wake waliotapakaa nchi nzima.


Wengine ambao tayari wamepita ni Profesa Mark Mwandosya, Samuel Sitta (kupitia Bunge), Emmanuel Nchimbi na majina kadhaa ambayo yanasubiri kura za Mkutano Mkuu, ya kina Bernard Membe, Stephen Wassira, William Lukuvi, Makame Mbarawa na Shamsi Vuai Nahodha.


Taarifa kutoka mkoani Arusha zinasema wilayani Simanjiro, Mbunge wa Jimbo hilo, Christopher Ole Sendeka alishinda ujumbe wa NEC kwa kupata kura 471 na kumshinda mpinzani wake ambaye ni mfanyabiashara maarufu Justin Nyari aliyepata kura 130 wakimuacha mgombea mwingine, Lenganasa Soipe kupata kura 5.


Katika nafasi ya uenyekiti, Brown ole Suya alitetea nafasi kwa kupata kura 423 na kumshinda mpinzani wake Lengay Mako Lazier aliyepata kura 168.


Kutoka mkoani Mwanza, Mwandishi Wetu anaripoti kwamba uchaguzi wa viongozi mbali mbali katika ngazi ya Wilaya kwa Chama Cha Mapinduzi Mkoani Mwanza uliofanyika mwishoni wa juma lililopita umekiweka cha hicho katika mtihani mkubwa kutokana na baadhi ya washindi waliopatikana kusemekana ni wa makundi hasimu katika siasa za Mkoa wa Mwanza.


Wachambuzi mbalimbali wa mambo ya siasa wanasema kuwa kwa matokeo hayo yanaweza kukiweka chama katika wakati mgumu zaidi na kufanya juhudi zake za kutaka kurejesha haiba yake katika siasa za Mwanza zipambane na vikwanzo vingi ikiwamo misuguano ya ndani ya chama kwa baadhi ya viongozi wanaotokana na makundi hasimu kisiasa.


Katika wilaya ya Nyamagana inaelezwa na wachambuzi wa mambo kuwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo na waziri wa mambo ya ndani wa zamani, Lawrence Masha, ambaye ameshinda nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kuwakilisha wilaya hiyo atatakiwa kufanya kazi kwa karibu sana ili kukihuisha chama hicho na Raphael Shilatu ambaye amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama wa Wilaya hiyo.


Shilatu, ambaye ni mfanyakazi wa Kampuni ya Sahara Media Group, inayomilikiwa na aliyekuwa mjumbe wa NEC wa Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo, anaeelezwa kuwa yuko katika kambi ya mwajiri wake ambaye amekuwa hayuko katika mahusiano mazuri kisiasa na Masha tangu wakiwa wabunge wa Ilemela na Nyamagana kabla ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 uliowamwaga wote, tena nafasi zao zikichukuliwa na wagombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).


Akizungumza na gazeti hili kuhusu ushindi huo mmoja wa wajumbe wa kamati ya siasa ya Mkoa wa Mwanza aliyetaka asitajwe jina lake gazetini alisema ya kuwa Wilaya hiyo itakuwa na chanagmoto kubwa sana kwa kuwa viongozi wake wanatoka katika kambi mbili zinazohasimiana kisiasa na kwamba ili waweze kukitumikia chama watalazimika kuzika tofauti zao kwa maslahi ya chama.


"Ninachoweza kusema ni ukweli kwamba wana changamoto kubwa, Masha mpaka sasa hawako vizuri (katika mahusiano ya kisiasa) na mmoja wa wagombea uenyekiti wa nafasi ya Mkoa ambako mwenyekiti wake ndiyo kambi yake, wanaweza wakaamua kuweka tofauti kando kwa maslahi ya chama lakini itakuwa kazi ngumu kutokana na shinikizo la kila kundi," alieleza mtoa habari huyo.


Akizungumzia hali hiyo kapteni mstaafu Anasser Mkiwa, mmoja wagombea waliogombea nafasi ya uenyekiti wa Nyamagana ambaye hata hivyo jina lake halikupishwa na NEC, alisema ya kuwa kuelekea uchaguzi huu chama kilijenga imani kwa wananchi kuwa kinakwenda kujisafisha lakini kimeshindwa kutumia nafasi hiyo na badala yake kimeonyesha jinsi kilivyozidiwa nguvu na makundi ambayo ndiyo yamekuwa chanzo cha chama hicho kupoteza mvuto kwa wananchi.


Alisema ya kuwa hali iliyotokea Nyamagana ni kielelezo cha chama kushidnwa kusimamia taratibu na kanuni zake kwa kuwa kilipaswa kuwaepuka watu wenye makundi na kuteuwa watu ambao hawafungamani na upande wowote ili kukinusuru chama na minyukano ya makundi.


"Chama kinajitengenezea matatizo chenyewe, sisi watu tusiokuwa na makundi na tunaosema ukweli hawataki kutusikiliza, tunaonekana wabaya, wamelemewa na nguvu za makundi, wako watu wamevunja kanuni lakini wanatazamwa tu, busara ya kawaida ilikuwa inataka kuwaacha wenye makundi na kuchukua watu neutral (wasifungamana na upande wowote) ili chama kifanye kazi ya kurejesha uhai wake, lakini sasa ni kama nafasi hii tumeipoteza," alisema Mkiwa.


Aliongeza kuwa Nyamagana watakuwa na kazi kubwa kurejesha hadhi ya chama kwa kuwa Mwenyekiti na Mjumbe wa NEC wanatoka makundi hasimu kisiasa na kwa maoni yake badala ya kujenga chama kutakuwa na mivutano isiyokoma kila mtu akipigania maslahi ya kundi lake wakati wapinzani wanasonga mbele.


Lakini Mwenyekiti mpya wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Raphael Shilatu, ameliambia Raia Mwema kuwa hajawahi kutofautiana kimsimamo au kimtazamo na mjumbe wake mpya wa NEC Masha na kwamba anaamini malengo yao pamoja ni kujenga na kuimarisha chama wilayani humo na si vinginevyo.


Alikumbusha pia kwamba ameshawahi kufanya kazi na Masha wakati akiwa mbunge na yeye akiwa mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya na hivyo hakuna mahali popote ambapo wamewahi kukwaruzana katika mitazamo ya kisiasa, akisisitiza kuwa uhasimu huo utakuwa unapandikizwa na watu kwa maslahi yao na wasiokitakia chama mafanikio.


"Naomba nikuhakikishie, mimi na Masha tuko karibu sana, nitashirikiane naye katika kila hatua ya kuimarisha chama chetu, hiyo ndiyo kazi yetu kubwa. Hata kabla ya uchaguzi nimezungumza naye sana na hata yeye hana tatizo lolote kabisa, haya ni maneno na mitazamo ya watu tu ambayo haitatuyumbisha katika kujenga chama" alisisitiza Shilatu.


Aliongeza kuwa katika kuhakikisha kwamba wamedhamiria kukiimairsha chama Nyamagana ameunda kamati ya siasa imara inayohusisha watu walio na taaluma na fani mbalimbali ili kuleta mawazo mapya katika kukimarisha chama kukabiliana na wimbi la sasa la upinzani.


Vikao vya chama vyalalamikiwa

Akizungumzia kukosa umakini kwa vikao vya chama vya uteuzi, Kapteni Mkiwa alisema kuwa vikao vya juu vya chama vimekuwa vikibariki kwa namna fulani uvunjwaji wa kanuni za chama kitu ambacho anaamini kitakigharimu chama hicho.

Mkiwa, ambaye pia amewahi kuwa diwani wa Kata ya Nyamagana, amesema kitendo cha Halmashauri kuleta majina ya watu siku mbili na kuitisha uchaguzi ni kielelezo kuwa chama kilibariki watu waanze kampeni mapema wakati kanuni zinakataa.


"Kama chama hakikujua kwamba watu wameshaanza kampeni kinawezaje kuteua majina tarehe 26 na uchaguzi kufanyika tarehe 29, kwa wapiga kura 800? Mtu anawezaje kuwazungukia kata zote kuwafikia hawa ndani ya muda mfupi huo, hii ina maana walijua watu wameshafanya kampeni," alieleza.


Alieleza kuwa chama kimeshindwa kukisimamia kifungu cha 6.8.5 cha Kanuni za Uongozi na Maadili toleo la Mwaka 2002 kinachozuia kiongozi wa CCM kutumia dini kabila, rangi au eneo analotoka kushawishi wapiga kura wamchague au kujenga na kudumisha makundi yanayovunja mshikamano ndani ya chama.


"Chama kimeshindwa kuvunja makundi, badala yake kinayarutubisha. Uchaguzi huu umeonyesha yote aliyokataza Mwalimu (Baba wa Taifa Julius Nyerere) kuwa ndiyo tumeyafanya, hii ni hatari kwa mustakabali wa chama katika zama hizi za ushindani," alisisitiza.


Huku hayo yakiendelea hivyo, mmoja wa wagombea nafasi ya Uenyeviti mkoa wa Mwanza Hussein Mashimba Hussein amewataka wana CCM kuchagua viongozi ambao watawarejeshea heshima waliyokuwa nayo wana CCM na kutembea kifua mbele wakiwa na sare za chama chao kama zamani.


"Mchague viongozi watakaorejesha heshima ya nguo hizi (sare za chama) zamani ulikuwa unaivaa na unatembea kwa madaha, lakini siku hizi ukiwa unaenda mkutanoni unaiweka kwenye begi unakwenda kuivalia ukumbi, jamani nguo hizi zina heshima zake mtumie uchaguzi huu kuzirejeshea heshima hiyo," alisema wakati akiwasalimia wajumbe wa mkutano wa Uchaguzi wa Wilaya ya Nyamagana.


Ilikuwa ni Polycarp Vs Kitwanga Misungwi

Ingawa hawakuwa wanagombea nafasi zozote katika uongozi wa chama Wilayani Misungwi, vigogo wa siasa za wilaya hiyo Mbunge wa Jimbo hilo na Waziri nchi ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Charles Kitwanga na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Polycarp Bernard walikuwa katika ushindani mzito kupitia wapambe wao.

Katika kinyang'anyiro hicho kambi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halamashuri hiyo ambaye chama chake CCM kilifuta udhamini wake kiliomdhamini wakati anagombea uenyekiti wa Halmashauri, na hivyo kutakiwa kujiuzulu uenyekiti hali ambayo imeendelea kuzua utata kwa kuwa bado anajiita ni kiongozi wa Halmashauri hiyo, imeibuka kifua mbele dhidi ya mbunge huyo.


Mwenyekiti mpya wa chama Wilaya hiyo Judith Mlolwa na Mjumbe wa NEC aliyechaguliwa, Jacob Shibiliti aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo wanaelezwa kuwa katika kambi ya Bernard.


Akizungumza na gazeti hili Bernad amesema kuwa kushindwa kwa kambi anayoiita ya hasimu wake kunatokana na wananchi kuelewa nani ni mkweli kati yao na kwamba fitna zina kikomo chake.


"Hii wanatakiwa tu wajue kuwa fitna zina mwisho, wanachama wamechambua, wameamua kuzingatia misingi ya chama kwa kuamua kuwachagua viongozi watumishi wanaoamini watawatendea haki na kuwatumikia kwa uaminifu," alisema.


Kwa upande wake Kitwanga alisema anasikitishwa na mambo hayo yanayozushwa na watu ambao hawakitakii mema chama, hasa katika wakati huu ambao kina kazi ya kujijenga na kujiimarisha zaidi.


"Jamani, haya mambo mengine yanasikitisha sana. Mimi sina kambi, watu wote waliogombea waliteuliwa na chama, sasa kambi zinaingia wapi hapo? Mimi ninakitumikia chama, nitafanya kazi na yeyote na niwaombe wenzagu huu si wakati wa malumbano. Tukijenge chama chetu, ndilo jukumu tunalodaiwa, haya mambo ya kambi yanakivuruga chama," alisema.


Kutoka Mbeya, Mwandishi wetu anaripoti kuwa baada ya kipindi kirefu cha majina mazito kutawala siasa za Mkoa wa Mbeya, hatimaye sasa majina mapya yamejitokeza katika chaguzi za CCM mkoani humo, kwa wanachama wake wengi wasiofahamika kuibuka kidedea katika nafasi mbali mbali za uongozi zikiwemo za uenyekiti wa wilaya na ujumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC).


Wakati hali ikiwa hivyo kuhusu washindi, chaguzi za CCM zinazoendelea nchini kote hivi sasa zimethibitisha kwa mara nyingine tena kwamba fedha haina nafasi mbele ya nguvu ya umma, baada ya wagombea wenye kuabudu matumizi ya fedha kujipatia uongozi, kujikuta wakianguka pamoja na kutumia fedha nyingi kushawishi wajumbe.


Mwamko wa wajumbe dhidi ya rushwa wakati wa chaguzi mkoani humo unaelezwa kuchangia kufanikiwa kwa wanachama wengi wasio na majina kunyakua nafasi za uongozi katika chaguzi za CCM zinaoendelea. Pamoja na mwamko huo, hatua ya baadhi ya vigogo wa chama hicho mkoani Mbeya kutojitokeza kulitoa nafasi kukaa pembeni na kutogombea nafasi kwa vijana na wanachama wasiokuwa na majina mazito kushinda.


Waziri wa Ofisi ya Rais, Profesa Mark Mwandosya, kwa mara nyingine tena amedhihirisha umwamba wake katika siasa za Mkoa wa Mbeya, baada ya kuibuka mshindi katika nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) akimwacha kwa mbali mwanachama mwingine aliyejipatia umaarufu katika siasa za Wilaya ya Rungwe katika miaka ya hivi karibuni, Richard Kasesela.


Profesa Mwandosya aliibuka mshindi katika nafasi hiyo ya Mjumbe wa NEC akiwakilisha Wilaya ya Rungwe kwa kupata kura 1,118 na kumuacha kwa mbali mshindani wake, Kasesera aliyeambulia kura 198.


Matokeo hayo yanachukuliwa na wengi kama pigo kwa mwanasiasa huyo kijana katika maisha yake ya kisiasa mkoani humo, wakizingatia kuwa hiyo inakuwa mara yake ya pili kushindwa katika chaguzi ndani ya wilaya hiyo.


Baadhi ya wanasiasa vijana waliopoteza nguvu zao za kisiasa mkoani humo baada ya kupambana na Profesa Mwandosya ni pamoja na Thom Mwang'onda ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Usalama nchini, Apson Cornel Mwang'onda.


Mwang'onda alipambana na Profesa Mwandosya kuwania nafasi ya Mjumbe wa NEC katika uchaguzi uliopita wa chama hicho, wakati huo nafasi ikiwa ni moja tu mkoa. Baada ya kupingwa chini, Thom amepotea kabisa katika siasa za mkoa huo kiasi cha hivi sasa jina lake kupotea kabisa, hata kwa kutajwa tu kama miongoni mwa wanasiasa wa mkoa huo.


Uchaguzi huo ulikuwa na mvutano mkubwa ambao haujawahi tokea katika siasa za mkoa huo.


Kishindo cha uchaguzi ule kinajionyesha hata kwenye kitabu cha Profesa Mwandosya, "Sauti ya umma ni Sauti ya Demokrasia," ambamo anasimulia hali ilivyokuwa huku akiwataja kwa majina washiriki wote wa kambi iliyoabudu nguvu ya fedha katika chaguzi ndani ya chama hicho.


Mwanachama mmoja ameliambia Raia Mwema kuwa si rahisi kumshinda Profesa. Mwandosya kwa sasa mkoani humo, kwa sababu anachukuliwa kama taswira ya mkoa huo, ni kiongozi mwenye kuheshimika na watu wa rika zote mkoani humo, hivyo kwa mwanachama yeyote anayeamua kupambana naye, huhesabika kama mchafuzi wa mkoa huo, hivyo haishangazi anapopotea kisiasa mara baada ya kushindwa.


Mwansiasa mwingine aliyekumbana, waweza sema "laana za Profesa Mwandosya", ni mfanyakazi wa BOT Tawi la Mbeya, Stephen Mwakajumilo ambaye katika Uchaguzi Mkuu uliopita aliamua kuking'oa kisiki hicho katika Jimbo la Rungwe Mashariki analolishikilia.


Kama ilivyokuwa kwa Kasesela, kijana huyo ambaye pia ni Kamanda wa Vijana, CCM, Mkoa wa Mbeya, alijikuta akiangukia pua baada ya kupata kura zisizozidi 300!


Kama hiyo haitoshi, naye Mwakajumilo, kama ilivyokuwa kwa kijana mwenzake, Thom, amejikuta akiangushwa na Sambwee Shitambala katika kinyang'ang'anyiro cha nafasi ya Mjumbe wa NEC kwa Wilaya ya Mbeya Mjini, katika uchaguzi ambao ulishuhudia Ephrahim Mwaitenda akishinda nafasi ya Mwenyekiti wa Wilaya hiyo.


Mwanasiasa kijana anayekuja kwa kasi mkoani humo, Philip Mulugo ambaye ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, naye alidhihirisha nguvu zake katika siasa za Wilaya ya Chunya pale alipoibuka mshindi katika nafasi ya Mjumbe wa NEC kutokea wilaya hiyo, akipata kura 1034 dhidi ya 314 za aliyemfuatia.


Katika nafasi ya Mwenyekiti wa Wilaya ya Chunya, mtetezi wa kiti hicho Chakupewa Makelele alifanikiwa kutetea nafasi yake hiyo baada ya kumshinda mpinzania wake, Noel Chiwanga.


Pamoja na wengi kutofuatilia kwa karibu uchaguzi huo katika Wilaya ya Kyela, pengine kutokana na majina ya wagombea wengi kutovutia masikio ya watu, bado matokeo katika nafasi ya Mwenyekiti wa wilaya hiyo yamewafurahisha wengi wakiamini kuwa kwa mara nyingine tena, jeuri ya fedha imeshindwa wilayani humo.


Nafasi hiyo iliyogombaniwa na wanachama watatu, Hunter Mwakifuna, Visk Mahenge na Kennedy Koroso ndiyo ilivuta zaidi hisia za wananchi wilayani humo kutokana na kuwepo kwa madai ya matumizi makubwa ya fedha ya mmoja wa wagombea hao akidaiwa kutumia zaidi ya shilingi milioni 30. Hata hivyo, pamoja na matumizi hayo ya fedha bado Hunter Mwakifuna aliibuka mshindi dhidi ya washindani wenzake hao wawili.


Taarifa za ndani kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Mkutano wa Uchaguzi, zinadai kuwa mgombea huyo alianza kwa kutoa shilingi elfu tano kwa kila mjumbe, kisha akaongeza kwa kuwapa shilingi elfu 10,000 kila mjumbe, ambapo inaelezwa walikuwa zaidi ya 2,000.


Matokeo mengine yaliyopatikana hadi jana ni pamoja na Wilaya mpya ya Momba ambako Juma Rashid alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa wilaya hiyo huku Jackson Mbwile akishinda nafasi ya Mjumbe wa NEC kupitia wilaya hiyo.


Mathayo Mwangomo alichaguliwa kuwa Mwenyekiti Wilaya ya Mbarali wakati Godfrey Mwangulumbi alifanikiwa kunyakua nafasi ya Mjumbe wa NEC kupitia wilaya hiyo, ambapo kwa Wilaya ya Mbozi Mwenyekiti aliyekuwepo, Alois Mdalavuma alifanikiwa kutetea nafasi yake hiyo huku nafasi ya Mjumbe wa NEC ikienda kwa George Mwenisongole.


Kwa mara ya kwanza katika chaguzi za CCM mkoani Mbeya, waandishi wa habari wamefanikiwa kupata nafasi mbalimbali za ujumbe katika ngazi ya wilaya, mkoa na taifa, hali ambayo ni tofauti na ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita ambapo walionekana kama wavamizi, na ilihakikishwa kwamba hawapiti.


Miongoni mwa wanahabari waliofanikiwa kupata nafasi za uongozi ndani ya chama hicho ni pamoja na mwandishi wa gazeti la Majira, Charles Mwakipesile, ambaye ameshinda nafasi tatu za uwakilishi ikiwemo ya Ujumbe wa Mkutano Mkuu Taifa.


Wengine ni mmiliki wa Kituo cha Sweet FM jijini Mbeya, Emmanuel Mbuza anayekuwa Katibu wa Siasa na Unezi Wilaya ya Mbeya Mjini, Jackson Numbi wa Generation FM jijini humo anayekuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Mkoa huo, wakati mmiliki wa kituo hicho alichaguliwa kuwa Mjumbe Halmashauri Kuu CCM wilaya.


Kuibuka kwa wanahabari wengi katika kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama hicho kumeamsha swali moja zito, nalo ni kwa jinsi gani wanahabari hao wataweza kuweka katika mizania sawa maslahi ya chama chao waliko na nafasi za uongozi na yale ya umma yenye kukinzana na ya chama chao.


Hata hivyo, tofauti na uchaguzi uliopita, mwaka huu chaguzi zinazoendelea ndani ya chama hicho zinaelezwa kukosa mvuto kwa wananchi wa kawaida kiasi cha watu kutofuatilia kwa karibu kama ilivyokuwa huko nyuma ambapo wananchi wasio wanachama wa CCM waliweza kufuatilia chaguzi za chama hicho ili kufahamu viongozi wanaochaguliwa.


Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa mkoani Mbeya, wanaielezea hali ya sasa kuchangiwa zaidi na hatua ya CCM kupeleka nafasi ya mjumbe wa NEC ngazi ya wilaya, hivyo kupunguza mivutano katika ngazi ya mkoa kama ilivyokuwa huko nyuma.


Hadi tunaenda mitamboni matokeo ya Wilaya za Ileje na Mbeya vijijini yalikuwa bado kutokana na kupiga kura siku ya Jumatatu tofauti na wilaya nyingine, huku nafasi ya Mjumbe wa NEC kwa Wilaya ya Kyela ikisubiri kurudiwa baada ya wagombea wawili, Andilile Mwambalaswa na Asajile Mwambambale kura zao kugongana.


Kwingineko wilayani Chemba Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia alipita kwa kuwashinda, Fredrick Duma na Said Sambala nafasi ya Mwenyekiti ikienda kwa Shaban Kilalo aliyepita bila ya kupigwa.


Wajumbe wengine waliopita ni Msonga Swedi, Mwanaharusi Bato, Mary Mkanya, Halifa Nyasuka na Ally Dosa.



Uyui:
Mlolwa Beatus alishinda kwa kumbwaga Mbunge wa Igalula, Dk Athumani Mfutakamba na Nhumbi Nhumbi.


Mwenyekiti: Alichaguliwa Mussa Ntimizi kwa kuwashinda, Abdallah Kazwika na Hamisi Bundala.


Urambo:
Mbunge wa Viti Maalum CCM, Margreth Sitta alishinda dhidi ya Weston Chokala na Hamis Malunkwi. Wajumbe wa Mkutano Mkuu waliochaguliwa ni Dk. Zakaria Mganilwa, Adamu Malukwi, Emmanuel Gembe, Anna Magoha na Blandina Lawi.


Uchumi na Fedha: aliyeshinda ni Francis Kasanga na katika Uenezi nafasi hiyo imechukuliwa na Paul Shija.


Kibaha:
Rugemalira Rutatina aliwashinda Rashid Bagdela na Kepteni Fratern Kiwango huku wajumbe Mkutano Mkuu Taifa wakiwa ni Catherine Katele, Joseph Chale, Jumanne Mangala, Mohammed Mpaki na Kepteni Fratern Kiwango.


Kilosa:
Nafasi ya Mweyekiti ilikwenda kwa Nassoro Udulele aliyemshinda Christopher Wegga aliyekuwa akitetea kiti chake. Naye Dk. Chisuligwe Kadudu aliwashinda Hamadi Lila na Theophil Nangusu katika nafasi ya ujumbe.


Masasi:
Mwenyekiti wa zamani Kazumali Malilo aliibuka mshindi akitetea kiti chake kwa kumbwaga Andrew Kasawala huku nafasi ya ujumbe wa NEC ikishuhudia mwanasiasa wa siku nyingi Kate Kamba akibwagwa.


Newala:
Ali Sadi aliibuka mshindi nafasi ya Mwenyekiti huku Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika akishinda nafasi ya ujumbe kwa kuwabwaga Abdallah Napinda na Shaibu Namkuna.


Tandahimba:
Abdul Namtula alipita kwa kumshinda Sophia Makonyola kwenye uenyekiti huku Balozi Makame Rashid akichaguliwa kuchukua nafasi ya ujumbe wa NEC kwa kuwashindaNamyundu Salum na Lihundu Samli.


Mtwara Mjini:
Mwenyekiti amekuwa Ali Mussa Chikanwene baada ya kuwashinda Yusuf Mineng'ene, Hawa Mangasala na Bakari Mbwana huku Godbless Kweka akitangazwa mshindi nafasi ya ujumbe wa NEC kwa kuwabwaga Saidi Swalehe, Phiri Makaburi na Ernest Haule.


Mtwara Vijijini:
Mwenyekiti amekuwa ni Ali Komba wa kumshinda Ahmadi Likomba huku nafasi ya ujumbe ikitwaliwa na Salehe Livanga aliyewashinda lhaji Mpeme na Salehe Nandieti.


Nanyumbu:
Muhata Masusa aliwashinda Ali Dua na Chibwana Mtimbe kuwa Mwenyekiti huku Hassan Kambutu akiwaacha Rajabu Mrope, Linga Mpwanya na Mwema Issa katika nafasi ya ujumbe.


Nyasa:
Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kepteni John Komba alimshinda Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Adolph Kumburu katika nafasi ya ujumbe wa Nec huku nafasi ya Mwenyekiti ikichukuliwa na Francis Homanga aliyewashinda Essau Milinga na Severin Kapecha.


Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa waliochaguliwa ni Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Ernest Kahindi, Edna Hyera, Grace Haule, Adam Mhaiki na Erenest Hyera.


Mbarali:
Mwenyekiti aliyechaguliwa ni Mathayo Mwangomo baada ya kuwashinda Ignas Pesipesi Mgao na Benedict Masuhva huku ujumbe wa NEC ukienda kwa Geofrey Mwangulumbi aliyewashinda Paul Kitha na Hanji Godigodi.
 

Sasa hao Mafisadi wakiingia Madarakani atakulaje nao ? na hiyo SAHANI MOJA ? Miaka yote alipokuwa CCM
Hakujua huo UFISADI Mpaka sasa hivi alipokuwa anaparamia CHEO ? ILI AWE RAIS wa NCHI ?
 
huyu mzee fungu la kukosa. Anadhani nani atampigia kura huyu ili awe rais? Huyu hata likiwekwa jiwe. Jiwe linashinda
 
Kwanza huyu ni mmojawapo wa walioitengeneza TAKUKURU feki. Walifanya hivyo makusudi ili wajilinde, leo yupo nje ya system anaanza kupiga mayowe. Hata hawa wanaoshangilia hivisasa, nao utafika muda wao wataanza kupiga mayowe kama Mzee wetu Sumaye.
 
08 OCTOBER 2012

*Akanusha kufanya kuzungumza na CHADEMA

*Adai kuanguka NEC ni tiketi ya mapambano zaidi


Na Willbroad Mathias

WAZIRI Mkuu mstaafu, Bw. Frederick Sumaye, amekanusha uvumi uliosambaa katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa ametangaza vita na Waziri Mkuu aliyejiuzulu Bw. Edward Lowassa kama atachukua fomu ya kuwania urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema taarifa hizo hazina ukweli wowote bali ni za kutungwa kwani hajawahi kuzungumza lolote juu ya Bw. Lowassa, wala kuzungumza na mtu yeyote kuhusu jambo hilo.

Bw. Sumaye aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika mkutano wake na waandishi wa habari ili kufafanua masuala mbalimbali likiwamo suala la rushwa katika uchaguzi wa kuwania Ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC), Jimbo la Hanang', mkoani Manyara.

Alidai kushangazwa na jinsi habari hizo zilipotokea na akawataka waandishi wa habari kuwa makini na wasikubali kutumiwa na wanasiasa wanaosaka urais 2015.

"Kuna baadhi ya magazeti yaliandika Sumaye kulipua bomu, mengine Sumaye kupasua jipu na kibaya zaidi, hivi majuzi gazeti moja likaandika Sumaye atangaza vita na Lowassa, ninachosema mimi sina jipu wala bomu la kulipua.

"Mimi sina ugomvi na Lowassa, hata nikiamua urais 2015 sitafanya hivyo kwa ajili ya mtu bali kwa masilahi ya Taifa," alisema.


Kuteta na CHADEMA

Bw. Sumaye pia alishangazwa na habari iliyoandindwa na gazeti moja (bila kukitaja jina), kikidai alitetea (kufanya mazungumzo), na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

"Sijawahi kuzungumza na CHADEMA kuhusu kuhamia chama chao, hata kama ningetunana nao, ufike wakati wapinzani wasionekane kama maadui.

"Habari hiyo ni ya kutengeneza pamoja na picha iliyowekwa mbele ya gazeti nikiwa na Mbowe ili nionekane nateta naye, namuomba Mwenyezi Mungu jambo hili lifahamike ni uvumi tu ili tusije tukaiingiza nchi katika matatizo," alisema Bw. Sumaye.

Uchaguzi NEC Hanang'

Akizungumzia kuhusu uchaguzi huo, katika Jimbo la Hanang', Bw. Sumaye alisema alipoteza nafasi hiyo kwa sababu uchaguzi huo ulitawaliwa na vitendo vya rushwa hivyo kumuathiri kwa
kiasi kikubwa.

Alisema mbali wajumbe kupewa rushwa pia yalikuwepo makundi aliyoyahita ya 'kiharamia', ambayo yalikuwa yakiwahamisha wajumbe nyakati za usiku ili wasipige kura.

"Mambo yaliyotokea Hanang', yalijitokeza sehemu nyingi lakini tofauti ni kwa ukubwa gani na nani yalimkuta," alisema.

Aliongeza kuwa, pamoja na kwamba vitendo vya rushwa vilikuwepo siku za nyuma, safari hii hali ilionekana kuwa mbaya zaidi kwa sababu ya mitandao iliyokuwa ikisambaza fedha katika maeneo mbalimbali ili kuwang'oa wanasiasa hasa wanaokemea maovu.

Alisema zamani watu walikuwa wakienda wenyewe na kutoa fedha kwa wakazi wa eneo husika ili wachaguliwe lakini sasa hali hiyo imebadilika ambapo baadhi ya watu aliodai kuwa wanasaka urais kinguvu, wamejenga mtandao wa kununua wapiga kura.

"Kwa sasa kuna mtandao wa kuonga wapiga kura tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo mtu alikuwa akienda eneo husika na kuwapa fedha wapiga kura ili wachaguliwe," alisema Bw. Sumaye akinukuu baadhi ya hotuba alizowahi kuzitoa katika matukio mbalimbali akikemea vitendo vya rushwa.

Hata hivyo, alipobanwa na waandishi wa habari kama anaweza kuutaja mtandao huo na eneo ambalo wajumbe walipewa rushwa Bw. Sumaye alikataa kata kata kuzungumzia zaidi suala hilo.

"Pamoja na kufanyiwa vitendo hivi, sitafikisha malalamiko yangu katika vikao vya chama wala kukata rufaa kwani yaliyojitokeza yalikuwa yakifahamika pia itaonekana nipo ndani ya CCM
kwa ajili ya vyeo.

"Mimi ni mwana CCM, nina imani na chama changu ambacho kiliunganishwa na vyama vya TANU na ASP, sipo ndani ya chama kwa ajili ya kutaka vyeo," alisema Bw. Sumaye na kuongeza;

"Rushwa haizalishwi na demokrasia bali tunaizalisha wenyewe kwa sababau zetu za kijinga, nchini Marekani na Uingereza kuna demokrasia, mbona hatusikii vitendo hivi," alihoji Bw. Sumaye.

Alisema kama wapiga kura wasipokuwa makini, Taifa litaambulia viongozi waliochaguliwa kwa nguvu za fedha badala ya utashi wa wananchi wenye haki ya kuchagua kiongozi wanayempenda.

Bw. Sumaye alisema katika nchi zenye demokrasia, wapiga kura huchagua kiongozi wanayempenda na mwenye uwezo lakini katika nchi zilizopondeka kwa rushwa, fedha ndio inayochagua viongozi
na kazi ya wapiga kura ni kupiga mihuri tu.

Alihadharisha hali hiyo na kudai kuwa, nchi nyingi zimeingia katika machafuko kutokana na chaguzi za aina hiyo na kushauri wale wanaopiga kelele kukemea vitendo hivyo vya rushwa waungwe mkono badala ya kusakama.

Aliwashauri viongozi ndani ya CCM, wajirekebishe kabla wananchi hawajachoshwa na hali hiyo na kuamua kuingia mitaani.

"Wananchi watachoshwa na hali hii, hawawezi kuvumilia mambo haya kama yataendelea ipo siku watasema inatosha, wakifikia hatua hiyo hali itakuwa mbaya zaidi," alisema.

Kuteteleka kisiasa na hatma ya kuwania urais 2015

Bw. Sumaye aliulizwa kuanguka kwake NEC, pengine pamemfanya ateteleke kisiasa na kuathirika katika mbio za kuwania urais 2015, ambapo akijibu swali hilo alisema, hali hiyo imemuongezea nguvu na akaahidi kuendeleza mapambano akiwa ndani ya CCM.

"Kuangushwa kwangu ujumbe wa NEC kumenipa nguvu zaidi, wala sijateteleka kisiasa bali nitaendelea kupambana na maovu nikiwa ndani ya chamachangu CCM," alisema Bw. Sumaye.

Alisema hata akiamua kuwania urais 2015, ingawa bado hajatangaza dhamira hiyo, matokeo hayo yamemrahisishia njia kwani kama angepata ujumbe wa NEC, ingemuwia vigumu kujitosa katika mbio hizo.










 
Utamu wa MDOMO wake UMEFYATUKA ? Hana la kusema tena ? Kwahiyo hata hakuongea na CHADEMA sasa MAGAZETI yalichapa kupata PESA na akanyamaza kwa SIKU NNE ? Sasa Anachapa Habari ya kukanusha ? What a delightful statement to hear from former FISADI... STILL GREADY in PRESIDENCY Ukimuuliza UNATAKA KUGOMBEA URAIS ILI UFANYE NINI atasema ni kutekeleza MALENGO YA CCM ... Haujui hata MTOTO MDOGO anaweza kuyatekeleza hayo MALENGO... URAIS sio hayo MALENGO ya CCM
 
"Lowassa ni mwanaume wa shoka" - Sofia Simba. Kiukweli Sumaye hana ubavu wa kupambana na Lowassa. Lowassa for presidency 2015.
 
Back
Top Bottom