Naomba niijadili hoja ya Sumaye, na sio Sumaye mwenyewe. Nakubaliana naye kwamba mchawi wa maendeleo katika jamii yetu ya Tanzania ni rushwa, waweza iita ufisadi. hatuwezi kuendelea kwa kauli mbiu za kilimo kwanza. Natoa ushauri kwa watawala, sijui kama wananisoma na kama wananisoma sijui kama wanajali,kwamba wabadilishe kauli mbiu. Sasa tuanze kuimba "mapambano dhidi ya rushwa kwanza". Uwekwe utaratibu ambamo kila mtanzania akijihusisha na vitendo vya rushwa akamatike. Tukizuia wizi wa raslimali za umma, tutakuwa na uwezo wa kuzielekeza raslimali za umma kwenye miradi itakayozalisha mali kwa wingi na hivyo kuwa na ajira nyingi, mali ikizalishwa, mfumuko wa bei nao utashuka. Kilimo hakiwezi kufanikiwa kama ruzuku ya pembejeo inaliwa na walio na mamlaka na raslimali za taifa zinaelekezwa kwenye miradi ambayo ni rahisi kwa wenye mamlaka kutuibia.
Lingine ni kuhusu urais. Sumaye amesema atapima kama ataona ana ubavu wa kuibuka mshindi ndipo atutangazie kwamba anautaka urais. Kwangu mimi uwezo wa mtu kuwa rais (uwezo wa kuongoza) ni muhimu zaidi kuliko uwezo wa mtu wa kushinda katika kinyang'anyiro cha kuupata urais. ningeridhika kama Sumaye angetwambia atajitathmini na akijiona ana uwezo wa kuwa rais (uwezo wa kuongoza) atatutangazia nia yake ya kuwa rais. Wala ile kuangalia kama wananchi wanapenda uwe rais ndipo utangaze nia, sikubaliani nayo. Unaweza ukawa na mvuto kwa wananchi na ukachaguliwa kwa kishindo kwa zaidi ya asilimia 80, kumbe masikini huna uwezo wa kuwa rais (uwezo wa kuongoza), huna msimamo na uwezo wa kukisimamia unachokiamini kikawa.Hii haitatusidia.