Sumaye Afunguka: Anguko la Elimu Tanzania na Viwango Vipya Vya ufaulu

Kokomili

Member
May 3, 2013
96
20
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye , ameonya kuwa kubadili madaraja na kushusha alama za ufaulu si majibu ya matatizo yanayoikumba sekta ya elimu nchini, bali dawa pekee ni kuboresha mazingira ya utoaji elimu. "Dawa ya matatizo yetu katika sekta ya elimu ni kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu na wala si kucheza na mitaala au kushusha alama za ufaulu," alisema Sumaye. Sumaye alitoa kauli hiyo jana kwenye mahafali ya Shule ya Sekondari Wasichana ya Amani iliyopo wilayani Manyoni mkoani Singida, ambapo alikuwa mgeni rasmi.

Alisema kinachotakiwa ni kuhakikisha shule zina vitabu, vifaa vya kufundishia, maabara yenye vifaa muhimu, walimu wa kutosha kiidadi na kitaaluma na mengineyo kama vyumba vya madarasa na nyumba za walimu. Alisema hayo yakitekelezwa viwango vya ufaulu vitapanda bila kubadilisha viwango hivyo. "Lazima elimu yetu iwe na ubora kitaifa kulingana na mitaala inayokubalika na pia iwe na ubora wa kimataifa," alisema Sumaye na kuongeza; "Tusijitengenezee viwango vyetu wenyewe ambavyo havikubaliki na kutiliwa shaka na watu wengine au hata sisi wenyewe."

Alitolea mfano malumbano yanayoendelea nchini hivi sasa kuhusu viwango vipya vya ufaulu kwa mitihani ya kidato cha nne. Alifafanua kuwa viwango vya elimu vimeshuka na hili tatizo liko katika ngazi zote za elimu si elimu ya sekondari peke yake. Kwa mujibu wa Sumaye, tatizo hilo linahitajika kutatuliwa kwa haraka kwa kuinua kiwango cha elimu na si kwa kubadilisha majina ya madaraja na kushusha viwango vya ufaulu. "Leo tunaanza kulumbana kama matokeo ya kidato cha nne yawe na daraja sifuri au daraja hilo sasa liitwe daraja la tano na kwa kufanya hivyo kiwango cha kufeli sasa kianzie alama 20 badala ya 34 ya huko nyuma," alisema Sumaye.

Alisema tafiti zingine zinaonesha hata kiwango cha ufaulu wa alama 34 yenyewe iko chini sana. "Je, tukikishusha kiwango hicho itakuwaje? Kama badiliko hili litapitishwa basi itaingiza sura mpya kabisa katika shule zetu," alisema na kuongeza; "Sasa mwanafunzi atahitaji kufanya juhudi kubwa ili kufeli kuliko kufaulu kwa sababu kupata alama chini ya 20 kwa 100 kwa mtu aliyehudhuria darasani na kufanya mazoezi ya darasani si kazi rahisi." Alisema, “hakuna mtihani usio na madaraja na daraja la mwisho ni la walioshindwa kufikia kiwango cha kufaulu”. Aliongeza kuwa, “mwanafunzi anapokuwa na daraja F au 0 si kwamba hana chochote kichwani, bali kilichoko hakifikii kiwango kinachotakiwa kwa kufaulu," alisema.

Alisema kwa mantiki hiyo mpya, kama isivyo sahihi kwa mwanafunzi aliyepata alama 34 kupewa daraja 0 basi hata aliyepata alama 5 naye hastahili kupewa daraja 0 maana hata yeye ana kitu japo kidogo kichwani. Sumaye alisema kwa kushusha alama za kushindwa mtihani, kisaikolojia unamfanya mwanafunzi sasa asiongeze juhudi kwa sababu anajua hata akipata alama 20 atakuwa amefaulu kwa sababu sasa kufeli ni kazi ngumu kuliko kufaulu. Aliongeza kuwa wakati umefika sasa elimu inayotolewa iwe na malengo. "Yaani iwe ni elimu inayotoa majibu kwa matatizo makubwa yanayoikabili jamii yetu na nchi yetu na kutuwezesha kuwa washiriki wazuri katika ulimwengu huu wa utandawazi wa karne ya 21," alisema.

Alisema si vema kuwa wanafundishwa watoto ili mradi wameingia chuo kikuu bila kujua kama fani wanazofundishwa ndizo hitaji la jamii na taifa au la. "Elimu yetu kwa kiwango kikubwa ilenge mahitaji ya soko na mahitaji ya jamii," alisema. Alisema hivi sasa kuna tofauti kubwa katika viwango vya utoaji wa elimu baina ya shule za serikali na za binafsi zikiwemo za taasisi za dini na hata kati ya shule za serikali za zamani na shule mpya hasa zilizoko katika kata. "Nataka nisisitize kuwa hakuna anayepinga shule za kata kwa sababu ni sera ya taifa, lakini ni lazima tunapopanua elimu upanuzi huo uendane na viwango vinavyohitajika na kwa kuhusisha sekta zingine zinazobebana nazo, kwa mfano sekta ya uchumi, utumishi kwa maana ya ajira.

Kujenga shule bila walimu na vifaa muhimu vya kufundishia ni sawa na kujenga hospitali bila madaktari na watumishi wengine. Tofauti katika utoaji wa elimu hujenga tabaka mbili ndani ya jamii na ni jambo la hatari sana kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wetu, mshikamano wetu na kwa usalama, amani na utulivu wetu. Eneo la elimu ni nyeti sana hivyo si vyema kulifanyia majaribio kila mara.
CHANZO: GAZETI LA MAJIRA Majira - Gazeti huru la kila siku | news_read_more
 
Mwisho wa siku wa kulaumiwa ni sisi wenyewe, vizazi vijavyo vitatushangaa tulikubalije mambo haya yakatokea?
Ina maana watoto wa siku hizi hawana akili, wanakula vitu gani, uwezo wao mdogo, wajinga.........

Badala ya kuangalia jinsi ya kuboresha kiwango cha elimu, serikali inacheza na matokeo, hata wakishusha daraja la kwanza likaanzia alama 20, kama hawataboresha vigezo na mahitaji mwengine bado wanafunzi watafeli tu.

Hawa wabunge/viongozi watoto wao wanasoma nje ndio maana suala la ubovu wa elimu haliwagusi moja kwa moja.
Matokeo yake watoto wa wananchi walio wengi watakujaonekana hawana vigezo vya kuajiriwa na kujikuta tunaendelea kutaabika na watoto wa wakubwa wakiendelea kushika nyadhifa na kupata ajira kwa sababu wamesoma.
 
Back
Top Bottom