SoC02 Suluhisho la changamoto ya ajira

Stories of Change - 2022 Competition

Erny1165

Member
Jul 31, 2022
8
5
Mpaka sasa nchini mwetu kuna tatizo kubwa sana la ukosefu wa ajira, ni ukweli usiopingika kwamba hakuna taifa lolote duniani sio hata Marekani inayofahamika kuwa na maendeleo makubwa yenye uwezo wa kuajiri watu wake wote, isitoshe watu hawa wasio kwenye mfumo wa ajira za serikali wanahitajika sana ili kukuza uchumi wa taifa husika.


Ni kwa namna gani watu hawa wanasaidia kukua kwa uchumi wa taifa?

Hawa ndio wanaopelekea uwepo wa sekta binafsi ambazo zinapelekea kuongezeka kwa mzunguko wa fedha zaidi kwenye taifa kwani sekta nyingi za binafsi zinalenga zaidi uzalishaji na biashara tofauti na sekta za serikali ambazo mara nyingi zinatoa huduma kwa mtazamo usio wa kibiashara zaidi.

Wimbi la vijana wasiokua na ajira linazidi kuongezeka kwani kila kunapokucha wasomi wanaendelea kuongezeka mtaani, chakushangaza ni kuwa kila kijana analalamika kuwa anasisitizwa kusoma ila haajiriwi sasa swali ni, je "serikali iache kutoa elimu kwa watu wake kwasababu haiwezi kuwaajiri wote?"

Jibu ni hapana elimu lazima iendelee kutolewa hata kama nafasi za kuajiriwa serikalini ni chache kwani ziko njia nyingi za kulisuluhisha hili tatizo.


Ila kutatua ama kusuluhisha tatizo hili inabidi kwanza tutazame chanzo hasa ni nini cha vijana wengi kurandaranda mitaani pasipo ajira?

Kwanza tutazame ajira ni nini? kwa ufupi tunaweza sema ajira ni fursa inayoweza kumpatia mtu kipato ili kukidhi mahitaji yake kwa maisha bora yaweza kuwa katika mfumo wa kuajiriwa ama kujiajiri mwenyewe.
Baada ya kuona ajira ni nini basi tutizame kwanini vijana hawana ajira?

Changamoto ya kwanza juu ya tataizo la ajira ni mifumo ya elimu ambayo imeundwa na mitaala isiyomjenga kijana katika kuziona na kuzitumia fursa zilizopo mitaani kwetu ili aweze kujiajiri na badala yake inawajenga vijana kuwa watu wa maofisini hivyo wanapohitimu wanabaki kulalamikia ajira na si kujiajiri.

Mifumo yetu imekuwa ni ya nadharia zaidi kuliko vitendo na pia haingalii karama ama talanta aliyonayo kijana yenye kuweza kumnufaisha anapohitimu masomo yake

Changamoto nyingine imekuwa ni ukosefu wa mitaji kwa vijana hawa ili kuwawezesha kujiajiri. Lakini hata mitaji ikitolewa na elimu ikabadilishwa bado inabaki changamoto ya ubunifu wa kuziona na kuzitumia fursa nyingi zilizopo mitaani, vijana wengi hususani wasomi bado wana hii shida anaweza lalamika kwamba hana mtaji lakini ukimuuliza anahitaji shillingi ngapi ili afanyie nini bado hajui kwa maana wanakosa ubunifu wa mipango madhubuti ya kujitengenezea ajira.

Lakini pia kumekuwa na tatizo la vijana wengi kukosa moyo wa umoja na mshikamano kwenye suala kujikwamua kiuchumi, kila kijana anatamani kusimama mwenyewe kwenye biashara zake hali ambayo mara nyingi imekua ikiwakwamisha na kuwarudisha nyuma vijana hata kushindwa kujiajiri au biashara zao kutodumu kwa mda mrefu wanapoanzisha.


Ni nini kifanyike ili kutatua tatizo hili?

Suluhisho la kwanza ambalo ndio mzizi wa hili janga ni kubadili mfumo wa elimu na mitaala iliyopo kwa sasa ambayo kwa kiasi kikubwa haitujengei vijana wazalishaji wa ajira bali wakimbiza ajira ambao kutwa hushinda wakilala na kutangatanga wakitafuta ajira ambazo kimsingi zipo kwenye mitaa wanayoishi, yamkini leo hii mtu anahitimu akiwa na taaluma ya usimamizi wa biashara (business management) lakini akipewa biashara inamshinda kuendesha na kuikuza kwani muda mwingi anajifunza nadharia kuliko vitendo.

Uwepo mfumo wa kuwawezesha vijana mikopo rahisi yenye riba nafuu ambayo itaambatana na semina elekezi juu ya suala zima la kujiajiri ili kuwafungua kifikra vijana wengi na kuhakikisha suala la mitaji linakua si changamoto ya kumfanya kijana asijiajiri.

Aidha serikali iwahakikishie vijana mifumo mizuri ya miamala yao kuanzia kwenye mabenki na hata miamala ya mitandao ya simu kwa kupunguza kodi na tozo ambazo kwa namna moja au nyingine zinawavunja moyo vijana kufanya uwekezaji hata mdogo pindi zinapokua kubwa sana.

Aidha sisi wenyewe vijana tubadilike na kubadilisha mitazamo yetu kutoka kwenye kuamini kua kila anaesoma ni lazima aajiriwe na badala yake tuwe tayari na tuwe wenye uthubutu kuhakikisha tunazitumia fursa zilizopo kwenye jamii zetu ipasavyo ili kujiajiri na kujikwamua kiuchumi badala ya kufunga tai na kukimbizana maofisini kulilia ajira na kuilaumi serikali kila kukicha.

Sambamba na jilo vijana tuwe na moyo wa kushikamana na kuinuana kiuchumi kwa kuwa na vikundi makini vya uwekezaji, ili kama inatokea umeona fursa ya kujiajiri na huiwezi pekeyako shirikisha na wengine ili kwa pamoja muitekeleze badala ya kuiacha ikapotea kwa maana wahenga walisema "pekeyako utakwenda haraka, ila kwa pamoja tutakwenda mbali".

Matumizi mazuri ya maemdeleo ya sayansi na teknolojia na kukua kwa utandawazi inaweza pia kuwa fursa ya vijana kujiajiri na kutangaza biashara zao mitandaoni ili kuwavutia wateja na hata kufanya biashara zao kukua zaidi na kutanua masoko badala ya kutumia mitandao kwa vitu visivyo na tija kwao wala kwa taifa.

Sisi kama vijana inabidi tutambue kukaa na kusubiri ajira za serikali ni matumizi mabaya ya elimu na ujuzi binafsi tulio nao tuamke na tuamue kuwa wabunifu tukizifungua na kuzitumia fursa zote za kujiajiri zilizopo kwenye jamii zetu. Kusema tujiajiri simaanishi usijaribu kutafuta ajira serikalini zinapotangazwa ila unapoikosa usikae kijiweni na kulalamika lakini badala yake ulitatue hilo suala kwa kujitengenezea ajira wenyewe.

Kijana FUNGUKA fursa za ajira ni nyingi sana ni wewe tu kuamua ni ipi unaichukua.

Ni mimi mtumishi wa wote
ERNEST MODEST MPIRA
 
Back
Top Bottom