Suleimani Misango: Bajeti imelenga kuwafukarisha wavuvi na Wafugaji nchini

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
617
1,541
Waziri Kivuli wa Mifugo na Uvuvi, Ndugu Selemani Misango, amesema bajeti iliyotengwa kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi haiwezi kukidhi matakwa na matatizo ya Sekta hiyo nchini na kwamba ACT Wazalendo haioni ni kwa nini Sekta hizo mbili zisitowe mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa.

Amesema kuendelea kutenga bajeti ndogo ni muendelezo wa kudumaza Sekta ya Mifugo na Uvuvi kwa lengo la kuendelea kuwafukarisha wafugaji na wavuvi ambao ni kundi kubwa la watanzania na kuitaka Serikali iangalie mnyororo wa thamani wa mazao ya mifugo na uvuvi, ili sehemu kubwa ya thamani imwendee mfugaji na mvuvi na sio matajiri wachache.
Ndugu Misango ametoa kauli hiyo leo tarehe 15.05.2024 wakati akitoa uchambuzi wa Bajeti ya Serikali katika wizara ya Mifugo na Uvuvi iliyowasilishwa Bungeni jana Jumanne.

Aidha ndugu Misango ameitaka Serikali ifungamanishe sekta ya Mifugo na Uvuvi kwenye viwanda na Biashara kupitia TANTRADE Ili vipate viwanda vya kutosha vya Maziwa, Usindikaji wa Nyama na Ngozi pamoja na mazao mengine ya mifugo itakayowawezesha wafugaji kupata masoko yenye uhakika na bei nzuri kwa ajili ya kukuza Uchumi wao.

Kuhusu kufungwa kwa Ziwa Tanganyika ndugu Misango ameitaka Serikali kusitisha hatua ya kufunga Ziwa hilo na badala yake itafute njia mbadala ya kuwawezesha wavuvi wanaotumia ziwa hilo kuendesha Maisha yao kwa kutengewa maeneo maalum ya kufanyia kazi zitakazowaingizia kipato.

Amesema uamuzi wa kufunga ziwa hilo haukuzingatia ushauri wa wadau wala hali za maisha ya watu wanaotegemea uvuvi na limeibua hofu kubwa kwa wadau wa mazao ya uvuvi kwenye mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa ambao kwa sehemu kubwa wanategemea ziwa hilo na uamuzi huo utaenda kuwaacha bila ya kuwa na shughuli mbadala za kujikimu.

Aidha amesema ACT Wazalendo inatambua kuwa Serikali za Tanzania kupitia ofisi ya Makamu wa Rais, Burundi Zambia na DRC (Lake Tanganyika Charter) kwa pamoja ziliazimia kufunga kwa miezi mitatu shughuli za uvuvi kwenye ziwa Tanganyika na kwamba uamuzi huo si njia sahihi ya kushughulikia changamoto zozote zinazodhaniwa kumalizwa kwa kuchukua hatua za kufunga Ziwa Tanganyika.

“Maeneo mengi ya nchi yetu yanayojihusisha na shughuli za uvuvi, wananchi wa maeneo hayo hawana shughurli zingine mbadala za uchumi, kufunga ziwa kunaleta madhara mengi sana ikiwa ni pamoja na kuongezeka matukio ya kiuharifu, kuharibika na kupotea kwa vyombo vya uvuvi, kushuka kwa mapato ya halmashauri na kukithiri kwa Umasikini.”amesema.

Amesema msimamo wa ACT Wazalendo ni kuitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia upya mkataba wake na nchi nyingine za Maziwa makuu na kulinda ziwa Tanganyika kwa kutenga maeneo maalum ya uhifadhi na uvuvi au mbinu mbalimbali za uvuvi kwa kipindi cha mwaka na sio kulifunga ziwa hilo.

Kuhusu Migogoro ya ardhi baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi ndugu Misango amesema Migogoro 8 ya ardhi iliyotajwa na Waziri Abdallah Ulega bungeni kuwa imeshughulikiwa na kutatuliwa inadhihirisha namna Serikali isivyowekeza nguvu ya utatuzi wa Migogoro ya watumiaji wa ardhi nchini kwa kuwa tatizo la migogoro ni kubwa kuliko utatuzi uliotajwa kufanyika.

Amebainisha kuwa moja ya vitu vinavyochangia migogoro hiyo ni Serikali kupitia mamlaka za hifadhi kuchukua maamuzi ya kumega maeneo ya wananchi na kuyatia kwenye Hifadhi jambo linaloacha madhara makubwa kwa kwa jamii inayohitaji maeneo ya matumizi ya ardhi.

Kuhusu Bandari ya Uvuvi ndugu Misango amesema bado miradi ya Bandari za Uvuvi nchini haijapewa kipaumbele na Serikali, na kwamba hali hiyo inadumaza shughuli za Uvuvi katika Bahari kuu na kuzorotesha Sekta ya Uvuvi na kuwaacha wavuvi katika umasikini wakutupwa.

Amesema ACT Wazalendo inaitaka Serikali ijenge bandari za uvuvi Mikoa ya Tanga, Pwani (Mafia) Dar es Salaam, Lindi na Mtwara. Aidha, Serikali inunue meli za Kitaifa za uvuvi pamoja na kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).

Imetolewa na;
Ndg. Abdallah Khamis
Mkuu wa Habari na Mawasiliano-ScaRo
ACT Wazalendo
Mei 10, 2024.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom