Kiza Mayeye: Tunataka Serikali Iwathamini Wavuvi

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
610
1,540
UVUVI ni shughuli kubwa ya Uchumi kwa jamii za watu wanaoishi kando ya bahari, mito na Maziwa. Mpaka sasa watu wanaojishughulisha na mnyororo wa thamani wa Uvuvi ni Takribani watu Milioni 4.5 lakini Uvuvi unachangia Asilimia 1.8 tu kwenye Pato la Taifa.

Hali za wavuvi ni duni licha ya jitihada kubwa wanazofanya. Uduni wa hali zao ni kutokana na ukosefu wa mitaji, matumizi ya zana duni za uvuvi na uvuvi wa kubahatisha hali inayopelekea wakati mwengine kufanya uvuvi usio endelevu. Uwekezaji kwenye sekta ya uvuvi bado ni mdogo sana katika maji ya asili.

Tumekuwa tukisema nchi hainufaiki vya kutosha na jiografia yake ikiwa ni Pamoja na uchumi wa bahari kuu, mathalani samaki waliovuliwa mwaka 2022/23 ni tani 426,555 tu Asilimia 89 ni kutoka maji ya baridi na asilimia 10.7 ni kutoka maji chumvi, hii inaoyesha ni kwa kiasi gani Bado hakuna uwekezaji na uwezeshaji wakutosha kwenye sekta hii muhimu.

Wavuvi kwa Muda mrefu wamekuwa na malalamiko katika utekelezaji wa shughuli zao miongoni mwa changamoto zinazowakabili wavuvi ni;

Ukomo wa Leseni, Leseni za Uvuvi tofauti kabisa na leseni nyengine za uvuvi na biashara ya Mazao ya uvuvi zinadumu kuanzia Januari mpaka Disemba bila kujali imekatwa kwa muda gani hivyo mvuvi akikata leseni mwezi Janauari itafika ukomo Disemba au akikata Oktoba leseni hiyo itakwisha mwezi Disemba na Januari atatakiwa kukata upya leseni husika, hii imekuwa ikiwaumiza sana watu wanaojishughulisha na biashara hii kuna nyakati inawalazimu kukata leseni mbili ndani ya mwaka mmoja wa serikali.

Viwango vya nyavu, Serikali imekuwa ikikamata nyavu mbalimbali zisizokidhi vigezo na kuzichoma. Mpaka sasa Nyavu za kuvulia dagaa zinatakiwa kuanzia milimita (mm) 8 mpaka 12 na za kuvulia Samaki wengine ni kuanzia jicho la inchi 3, bila kujali ni aina gani ya samaki unavua, Mfano, Serikali inatambua Sato na Mgebuka wanaweza kuwa na umri sawa ila umbile tofauti lakini kanuni zinalazimisha namna sawa za kuwavua.

Utafiti uliofanywa katika ziwa Tanganyika umeonyesha kuwa Migebuka inaweza kuvuliwa kwa nyavu yenye jicho la nchi 2.5 na sio nchi 3 kama ilivyo kwenye kanuni. Takwimu zinaonyesha kwamba mwaka 2022 nyavu aina ya nyavu za makila 2,988; nyavu za timba 11,284; kokoro 2,268 ambazo wavuvi wamekuwa wakizinunua kwenye maduka rasmi yanayoagiza kutoka nje au kutengenezwa nchini zilikamatwa na kuchomwa, hii ni kutokana na kanuni kutoendana na uhalisia licha ya baadhi ya wavuvi kutumia zana zisizoruhusiwa.

Vikundi vya Uangalizi wa Fukwe (BMUs), vimeundwa kwa kanuni za Uvuvi mwaka 2007 vikundi hivi huchaguliwa miongoni mwa wavuvi, wenye maboti na wafanya biashara wa vifaa vya uvuvi na watu wanaoishi maeneo ya uvuvi, BMU zimekuwa mwiba kwa wavuvi kwa kuanzisha Michango mbalimbali bila makubaliano, na kufanywa ndio wawakilishi wa Wavuvi kwenye masuala yanayohusu maslahi na masuala ya wavuvi na uvuvi kiasi sheria ama taratibu zinazotungwa na kupitishwa zinapata ukinzani mkubwa kutoka kwa wavuvi licha ya kudaiwa kushirikisha wavuvi.

Mfano Itifaki ya Kufunga Ziwa Tanganyika kwa Miezi Mitatu haukuhusisha wavuvi ila baadhi ya viongozi wa BMU na kusababisha mvutano wakati wa utekelezaji wa Itifaki hiyo. Hata hivyo BMU zinalalamikiwa kutumika kama chombo cha Dola kudhibiti shughuli za uvuvi.

Uwezeshaji wa wavuvi, wavuvi wamekuwa wakipitia changamoto nyingi sana ikiwemo kukosa zana za kisasa, mitaji na vyombo vya vya uvuvi, jambo linalosababisha kuzorota kwa maendeleo yao binafsi na sekta kwa ujumla. Hakuna mikakati ya makusudi ya kuwawezesha wavuvi kama ilivyo kwenye sekta nyengine ndio maana maisha na hali za wavuvi bado ni duni mno. Hasa wavuvi wanaovua kwenye maji ya asili katika maziwa, mito na bahari, tunaona Serikali imeanza kuweka nguvu na jitihada kubwa kwenye Ufugaji wa Samaki (Aquaculture), tunaona ipo haja ya Kufanya hivyo kwa wavuvi wa asili kwani kwao Uvuvi ndio Maisha yao.

Kutokana na changamoto hizo ACT Wazalendo tuna mapendekezo yafuatayo;

1. Tunataka Muda wa uhai wa leseni za uvuvi kuwa miezi kumi na miwili (12) kuanzia siku ya kutolewa Leseni husika kama ilivyo kwa leseni za biashara nyengine.

2. Serikali idhibiti Nyavu zisizokuwa na viwango zisiingizwe nchini ili kuwe na uvuvi endelevu, udhibiti huu ufanyike kuazia Mipakani na Bandarini kwani wavuvi wamekuwa wakinunua nyavu hizo madukani na zinalipiwa kodi. Vilevile Serikali iweke viwango kulingana na mahitaji kwani ukubwa wa Samaki unatofautiana hivyo nyavu za aina moja haziwezi kuvua Samaki aina zote katika eneo husika, ifanye tafiti kuangalia mazingira na aina ya Samaki wanaovuliwa na kuheshimu tafiti hizo.

3. Tunaitaka Serikali Kuanzisha mfumo maalum wa kuwawezesha wavuvi ili kupitia vyama vya wavuvi kuwasajili wavuvi wote na kuwawezesha vifaa na mitaji ili waweze kuvua uvuvi salama na wenye tija. Jitihada kubwa inayofanywa kwenye kilimo na Mifugo ifanywe kwenye uvuvi pia.

4. Tunataka Vikundi vya uangalizi wa Fukwe (Beach Management Unit) vitekeleze majukumu yake ya kiuangalizi na visitumiwe kuwakandamiza wavuvi. Masuala yanayowahitaji wavuvi wahusishwe wavuvi wenyewe kupitia vyama vyao ili wajadili na kukubaliana juu ya masuala na ustawi wao na si kupitia BMU ambazo kwa kiasi kikubwa zinasimamia maslahi ya Serikali.

Mwisho, ACT Wazalendo tunatambua na kuhamasisha Uvuvi endelevu unaozingatia utunzaji wa mazingira na viumbe maji kwa ajili ya vizazi vijavyo, hivyo tunakumbusha Serikali kuwa Uchumi wa Buluu unatakiwa kwenda sanjari na uwezeshaji wa wavuvi na mnyororo wa thamani ya mazao ya Uvuvi. Ni wajibu wa Serikali kuweka jitihada na kuondoa vihunzi kwa wavuvi kwa kuwapa teknolojia, mitaji na zana za kisasa katika shughuli zao.

Imetolewa na,
Kiza Hussein Mayeye
X @Kizamayeye_
Waziri Kivuli wa Mifugo na maendeleo ya Uvuvi.
07 Sptemba 2023.
 
Back
Top Bottom