WARDA...
Tony mshikaji wangu sana tena sana, yule kaka kanisaidia sana kipindi cha chuo, Tony dizaini wakishua ingawa anakataaga kuitwa wa kishua, ila mi nikimchek kwa simu lazma nimuite wa kishuaaaa, hapo jiandae na matusi balaa, we fala nani wa kishua



.... ukitoa weakness yake ya kupenda chini ila alikua mtu poa sana, Tony ana huruma vibaya, mnooo...
Katika wale tuliofurahia na kushangilia boom kuongezeka hadi asilimia 65 mi nilikuwepo, familia yangu ya chini sana , kuna mda wa kufungua chuo nauli tu utata, nilikua na boy friend wangu ndio alikua ananitoa wakati mwingine, ile michezo ya Dulla niliishtukia na Dulla alinilengesha sana ila niliweka nadhiri kua nitajiheshimu, nilikua naogopa sana magonjwa.
Ukiwa umetoka familia za chini, maisha ya chuo lazma yakuchape yaani, isingekua Tony daaah sijui ingekuaje... Tony ni mtu wa bata sana, nilikua namuokoa kwenye assignments, na nilikua nahakikisha kua nimepangwa nae group moja ili nimuokoe, kuna muunganiko
fulani ivi ulikua unakuja kati yangu na Tony maisha yakawa yanasonga kiaina hiyo.
Nikiwa mwaka wa pili ikabidi nibuni biashara ambayo walau itafanya maisha yawe mepesi kwa aina fulani, nikaanza kuuza mikate na sausages, blocks zetu zilikua mpya kwahiyo kuna kipande hadi ufike madukani. Nikawa nanunua mikate kwa bei ya jumla kiwandani mitaa ya Nyerere square kwa nyuma kule, napita maduka ya jumla nanunua sausages...
Sausages nazichemsha kwenye majagi ya umeme, nawauzia na mkate kwa bei ya rejareja, skonsi moja mia mbili, sausage jero. Mungu mwema walau nikawa namudu mahitaji yangu madogomadogo bila ya kumtegemea Tony . Nilikua nawaona mabinti wanavyozuzuka na maisha ya anasa daaah, Dullah alijua kuwauza watoto wa watu, ila it's free world and free market, everything is business , hopefully wapo na maisha bora kwa sasa.
Kale ka boyfriend kakaniletea mambo ya kipuuzi, narudi nyumbani naambiwa story zake , nikaona huyu hanijui nikapiga chini. Nikakomaa na chuo maana najua nikifeli sina kaka anafanya TRA kama Tony wa kuniconnect popote, nilipiga kitabu kama chizi yaani.
Siku hazigandi tukamaliza chuo, mtaa ukatupokea, nyumbani wanakuvumilia mwezi wa kwanza tuu, wa pili wanaanza kukuuliza mbona hutafuti ajira, daah wanafikiri siku hizi ni kama zamani unatembea na bahasha eeh, nikapambana kufanya applications wapii, nikaanza kuomba hadi temporary jobs za kufundisha shule za karibu, naambiwa hapo walipo wana walimu kama wanne wanajitolea, nikaona hii tena balaa.
Nikaanza kuchekecha kichwa, hapo nimeshapotezana na Tony na wadau wengine wa chuo, kila mtu anapambana na hali yake, nasikia tu Tony kashatoboa sio mwenzenu. wakishua yulee, kalamba dume TRA daaah,mi si ndio nilikua namfanyiaga assignments yule, mzee wa bata katoboa .
Nikapambana nikapata nafasi ya kujitolea mahala, nikafanya kama mwaka hivi, yaani pale unaenda kwa nauli yako unarudi kwa nauli yako, maisha ya dar si mnayajua, usafiri changamoto, mjini lazma uwe na hela ya lunch pamoja na breakfast, nikasema hapa nikijifanya mlokole sitoboi, kuna mbaba akajiweka, aliniwekea bill ya breakfast na lunch, walau maisha yakawa na unafuu, ila si unajua mkono mtupu haurambwi, mzee akaanza kudai mzigo, mi kutoa mzigo naogopa magonjwa, nikamuomba tukapime mzee akaruka, kwani huniamini au? nikasema huu ufala nimeukwepa ukimwi udom nije niupate kifala hivi, hapana...nikamkazia mzee.
Hakuna rangi sikuona, mzee alinifanyia figisu yulee balaa, akaanza kugawa ofa kwa rafiki angu, rafiki angu hajuagi kuacha fursa akapita nae, usumbufu ukazidi kwa yule mzee nikakaza. Kuna anko wangu alikuja kwetu kwa ajili ya matibabu Muhimbili, Ni mtu ana vihela walau, nikaona acha nijaribu bahati yangu maana sijawahi kumuomba hata mara moja . Nikamuelezea mazingira yangu ya kazi, nikampa wazo langu pale kua kama ningepata mtaji walau laki moja niwe nafata mashuka Tandika , nayafua, nayapasi , nawauzia watu pale kazini, Mungu tu alikua upande wangu akanipa, maana ana kaubahili balaa.
Walau maisha yakaanza kua na nafuu, nikajiongeza jumamosi nadamkia Karume napoint viatu vya wadada na vya watoto, navifua fresh ,jumatatu huyooo na mizigo yangu kama mwehu , kazini wakawa wanaiita machinga, ni kama Mungu alinipa tu kibali cha kukubalika walahi, nikaanza kuingiza pesa , kinamama wa kazini wakawa wananiunga mkono sana, miezi michache baadae nikapata ajira rasmi, aiseee Mungu acha aitwe Mungu tuu, hachelewi wala hawai.