Somo la 3: uwekezaji kwenye soko la hisa (DSE)

Somo la 3: uwekezaji kwenye soko la hisa (DSE)

Joined
Aug 26, 2022
Posts
64
Reaction score
119
🌀 Kumbuka: Katika somo letu lililopita, tulijifunza mambo muhimu ya kuzingatia kabla hujawekeza — kama kuwa na mfuko wa dharura, kulipa madeni ya riba kubwa, kuwa na malengo, na kujua uwezo wako wako wa kuhimili hatari za uwekezaji.

📍 Leo, tunazungumzia moja ya maeneo maarufu na rasmi ya uwekezaji: Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

1️⃣ Soko la Hisa ni nini?
Soko la hisa ni mahali ambapo kampuni huuza sehemu ya umiliki wake (hisa) kwa umma ili kupata mtaji, na watu huweza kununua au kuuza hisa hizo.

Kwa Tanzania, soko hili linajulikana kama Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na lilianzishwa rasmi mwaka 1998. Mpaka sasa, lina zaidi ya kampuni 25 zilizo kwenye orodha yake.

2️⃣ Kwa nini kampuni huuza hisa?
■ Kupata mtaji wa kukuza biashara.
■ Kupanua shughuli zake kwa kununua vifaa, kuongeza tawi au kuwekeza kwenye teknolojia.

3️⃣ Faida za kuwekeza kwenye soko la hisa

■ Kupata gawio (faida):
Kampuni ikipata faida, inaweza kugawa sehemu ya faida hiyo kwa wanahisa wake.
🧾 Mfano: Kampuni ya CRDB mara kwa mara hugawa gawio kwa wanahisa wake kutokana na faida wanayopata.
■ Ongezeko la thamani (capital gains):
Thamani ya hisa inaweza kupanda kadri kampuni inavyokua.
🧾 Mfano: Kama ulinunua hisa ya kampuni fulani kwa TZS 300, na baada ya muda thamani yake ikapanda hadi TZS 1,000, unaweza kuuza na kupata faida.
■ Umiliki wa kampuni:
Unakuwa sehemu ya wamiliki wa kampuni hiyo. Una haki ya kushiriki mikutano ya wanahisa na kutoa maoni.
🧾 Mfano: Unapomiliki hisa za NMB, unakuwa sehemu ya wamiliki wa benki hiyo na unaweza kushiriki maamuzi kwenye mkutano mkuu wa wanahisa.
■ Dhamana ya kupata mkopo:
Hisa zako zinaweza kutumika kama dhamana unapohitaji mkopo benki.
■ Uwekezaji unaoanza na kiasi kidogo:
Huhitaji kuwa milionea kuanza — unaweza kuanza hata na TZS 5,000.

4️⃣ Changamoto za kuwekeza kwenye soko la hisa
■ Mabadiliko ya bei (volatility):
Bei za hisa hupanda na kushuka kulingana na hali ya soko, taarifa za kampuni, au hali ya uchumi.
■ Kukosa maarifa:
Watu wengi hawaelewi namna soko linavyofanya kazi, hivyo wanaweza kuogopa au kufanya maamuzi yasiyo sahihi.
■ Uvumilivu wa muda mrefu:
Hisa hazikupi faida ya papo kwa papo. Unahitaji kuwa mvumilivu na kulenga muda mrefu ili kuona matokeo.

5️⃣ Mambo ya kuzingatia ukiwekeza kwenye soko la hisa.

■ Fuatilia kampuni kabla ya kununua hisa zake: Soma taarifa za kifedha, angalia historia ya gawio, na matarajio ya kampuni.
■ Wekeza kwenye sekta unayoielewa.
■ Usiwekeze kwa uvumi: Kumbuka, soko linaendeshwa na taarifa sahihi, si maneno ya mitaani.
■ Angalia malengo yako ya kifedha na inafaa uwe na malengo ya muda mrefu.

6️⃣ Jinsi ya kuanza kuwekeza DSE.
■ Kwa sasa uwekezaji umerahisishwa— pakua App ya DSE hisa kiganjani kupitia simu yako ya mkononi, hakikisha una namba ya NIDA na akaunti ya Bank (active) ili uweze kufungua akaunti.

🔄 Hitimisho la somo
Soko la hisa si kwa matajiri pekee, bali kwa mtu yeyote aliye tayari kujifunza na kuwa mvumilivu. Faida zake ni halisi, na zipo wazi kwa yeyote anayetaka kuanza — iwe ni mwanafunzi, mfanyakazi au mfanya biashara.

Swali la siku:

Je, umewahi kufikiria kuwekeza kwenye hisa? Ungetaka kuanza na kampuni gani — na kwa nini?

Usisahau kufatilia somo lijalo 🫵

GODFREY DENIS
Millennium Investors Community Co-founder
0763721523 (WhatsApp)
 
Somo zuri sana ukwel ni kwamb watu wengi ikiwapo na mm atujawa na elimu ya kutosha kuhusu hisa namna ya kununua ni utaratibu upi ufatwe na je unapouza pesa zako unazipata vp hii ni moja kati ya vitu vinavyopelekea watu wengi kutojiusisha na hisa mara nyingi watu uzungumzia namna ya kununua lkn siyo namna ya kuuza hii ni sababu pia inayofanya watu waone kama ni upotevu wa hela mm ni kati yao..wakati wa kuuza kuna mlolongo mrefu sana kuzidi wakati wa kununua
 
Asante.kampuni ya Afriprise na Nicol n nzr kuwekeza?
Ndiyo kaka, zote ni nzuri — ukiangalia taarifa zake za kifedha zinaashiria afya nzuri ya kibiashara lakini hata ukifanya valuation (kutafuta thamani ya hisa) zote ziko vizuri.

Zote ni kampuni ambazo zipo kwenye sekta moja — sekta ya uwekezaji, hivyo unaweza kuchagua moja au kama utaweza kwenda nazo zote.

Sokoni AFRIPRISE ni Tsh 330 kwa kila hisa na NICOL ni Tsh 910 kwa kila hisa.
 
Mkuu nashauri ungeanzisha pia group la whatsapp maana wapo watu wengine ambao hawajajiunga na JF na wanahitaji elimu hii ya uwekezaji.

Thanks.
 
Somo zuri sana ukwel ni kwamb watu wengi ikiwapo na mm atujawa na elimu ya kutosha kuhusu hisa namna ya kununua ni utaratibu upi ufatwe na je unapouza pesa zako unazipata vp hii ni moja kati ya vitu vinavyopelekea watu wengi kutojiusisha na hisa mara nyingi watu uzungumzia namna ya kununua lkn siyo namna ya kuuza hii ni sababu pia inayofanya watu waone kama ni upotevu wa hela mm ni kati yao..wakati wa kuuza kuna mlolongo mrefu sana kuzidi wakati wa kununua
Kweli kaka, kama ulivyosema changamoto kubwa ni maarifa na taarifa sahihi — kununua na kuuza ni jambo rahisi sana, yote hayo yanafanyika kupitia App ya DSE hisa kiganjani, huko unaweza kununua na kuuza hisa — mara nyingi ukishauza hisa ni vema kuwasiliana na broker wako ili akupe utaratibu wa kukutumia pesa yako.

Jambo jingine muhimu ni kujua exit plan (mlango wa kutoka sokoni) kutokana na malengo yako au mwenedo wa kampuni, hii itakusaidia kujua ni muda gani wa kuuza hisa zako. Jambo jingine muhimu ni kujua kuchagua kampuni sahihi kabla ya kuwekeza na kuwa na malengo ya muda mrefu.
 
Back
Top Bottom