Vazi jipya la mfalme.
Muandishi: Hans Christian Andersen, 1837
Kimetafsiriwa na Pictuss.
Email:
pictuspublishers@gmail.com.
Pictuss2021.
Haki zote zimehifadhiwa. Hakuna sehemu yoyote ya tafsiri hii inayoweza kunakiliwa, kutolewa kivuli(photocopy), kuhamishwa, kurekodiwa au kutolewa kwa namna yeyote bila ya taarifa ya awali ya kimaandishi ya mmiliki.
VAZI JIPYA LA MFALME
Hapo zamani za kale kulikuwa na mfalme aliyependa sana mavazi na kuvaa. Alitumia pesa zake zote kununulia nguo. Hakujali kuhusu wanajeshi wake wala kwenda kwenye matamasha ya maonyesho kama wafalme wengine. Alienda iwapo tu alikuwa na nguo mpya za kuonyesha kwa watu.
Alivaa nguo tofauti kila saa ya siku. Wafalme wengi walitumia muda wao mwingi kwenye mabaraza ya kuhukumu na kushauriana lakini yeye almu ya ikuwa akishinda kwenye kabati la nguo.
Siku moja matapeli wawili wakijiita washonaji waliingia kwenye nchi hiyo. Walisema wanaweza kushona nguo nzuri yenye rangi na mapambo ya kupendeza sana. Walisema nguo hiyo itatengenezwa na kitambaa ambacho hakitaonekana na yeyote yule aliye mjinga au asiyefaa kitu. Kifupi, mtu mwenye uelewa mdogo asingeweza kuiona nguo hiyo.
" Bila shaka itakuwa nguo nzuri sana" aliwaza mfalme.
" Kama nikiwa na nguo kama hiyo nitajua mara moja watu gani hawanifai kwenye uongozi wangu. Nitakuwa na uwezo wa kutofautisha wajinga na werevu, inabidi nishonewe nguo hii mara moja".
Akawaita wale washonaji na kuwapa pesa nyingi sana ili wamshonee nguo ile mara moja.
Wale matapeli wakaunganisha mashine ya kufumia vitambaa mara moja. Walifanya kazi kwa bidii sana, japo kiukweli walikuwa hawafanyi kazi yeyote. Waliomba kupewa nyuzi bora za hariri na nyuzi bora za dhahabu. Wakaziweka kwenye mikoba yao.
Wakaendelea kufanya kazi kwenye mashine ya kufumia usiku na mchana lakini hakukuwa na nyuzi zozote kwenye machine.