Soma hapa hotuba ya Waziri Membe katika maadhimisho ya miaka 50 ya Jubilee ya Anglika

Sauti ya Rondo

Senior Member
Aug 1, 2009
127
226
HOTUBA YA MHESHIMIWA BERNARD K.MEMBE, WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KWENYE MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA KANISA ANGLIKANA,DAYOSISI YA DAR ES SALAAM, TAREHE 4 JANUARI, 2015

Mhashamu Baba Askofu Dr.Valentine Mokiwa, Askofu wa Dayosisi yaDar es Salaam; Kasisi Mkuu Kiongozi Canon John Mlekano; Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Dar es salaam- Canon John Senyagwa,Wakuu wa Majimbo mliopo hapa,Ndugu waumini; Wageni waalikwa;Mabibi na Mabwana;Bwana Asifiwe.

Shukrani kwa Mwaliko
Nakushukuru sana Baba Askofu Mokiwa, viongozi wenzako pamoja na waumini wote wa Dayosisi ya Dar es Salaam kwa kunialika kuja kushiriki nanyi katika maadhimisho haya ya kihistoria ya Jubilei ya Miaka Hamsini ya Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar Es Salaam.

Nawapongeza sana waumini wa Dayosisi ya Dar es Salaam kwa kutimiza nusu karne tangu ianzishwe. Miaka hamsini si haba, ni umri wa makamo, na kwa kipimo chochote kile ni umri mrefu. Umri huu ni kipimo cha ukomavu wa Dayosisi ya Dar es Salaam. Ni miaka 50 ya uinjilisti, uponyaji na huduma kwa jamii. Mafanikio haya ya Dayosisi ni kielelezo cha uimara wa Kanisa la Anglikana. Hatuna shaka kuwa mmeweza kudumu kwa muda huo kutokana na misingi imara ya kiroho na uongozi uliojengwa juu ya miamba iliyowatangulia. Hatuwezi kuzungumzia mafanikio ya Dayosisi hii bila kumtaja Baba Askofu John Sepeku na wenzake waliolijenga Kanisa hili.

Kanisa la Kianglikana la Tanzania ni miongoni mwa majimbo mawili tu ya kianglikana duniani kuwa na muungano wa mapokeo mawili ya kanisa Anglikana - yaani High Church (lililokuwa na mrengo wa kikatoliki) na Low Church (lililokuwa na mrengo wa kiinjili). Kanisa la Kianglikana la Tanzania na lile la Burma pekee ndio yaliyoweza kuunganisha mapokeo haya mawili na hatimaye kuwa na kitabu cha sala kimoja, litru- gia moja, na uongozi mmoja wa Askofu Mkuu ambao unasomwa katika parokia zote.

Ndio maana haishangazi kuwa kanisa Anglikana la Tanzania lilisimama imara bila hofu kupinga ndoa za jinsia moja hata pale makanisa mengine ya Anglikana duniani yalipoamua kufanya hivyo. Mlinipa faraja kubwa, maana kupitia kwenu ile sauti ya Serikali, na sauti ya watanzania kukataa shinikizo kutoka nje ya nchi la kukubali ndoa za jinsia moja lilipa- ta nguvu na mwangwi mkubwa. Mlinitia nguvu sana pale niliposimama kidete kuwaambia rafiki zetu wa nje kuwa katika hilo la ndoa za jinsia moja, Tanzania tunaomba tukubaliane kutokukubaliana. Tunapojitokeza kwa kutimiza miaka 50 ya Dayosisi ya Dar es Salaam , hatuna budi kukumbushana kuwa safari bado ni ndefu. Tulipotoka kweli ni mbali, tunapokwenda ni mbali zaidi. Ipo zaidi ya miaka 50

Mingine mbele ya Kanisa hili. Hivyo leo tunaianza safari mpya, katika mwaka mpya na matumaini mapya. Sisi katika Serikali tunayo matumaini makubwa na safari yenu. Katika miaka 50 ya uhai wa Dayosisi, Tumeshuhudia kazi zenu na huduma zenu. Siku zote mmeshirikiana na Serikali katika kutoa huduma za jamii na kuilea amani yetu. Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa la Anglikana pamoja na madhehebu mengine yadini kuboresha maisha ya Watanzania. Tutaendelea kupokea ushauri wenu na kuwashirikisha katika mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Naomba muendelee kushirikiana na Serikali katika kutoa huduma kwa wananchi. Muendelee kutumia mtandao wenu mpana uliopo nchi nzima kwa ustawi na maendeleo ya nchi yetu. Lengo letu libaki kuwa moja daima na milele.

Maombi kwa Viongozi wa Dini

Mhashamu Baba Askofu Dr. Mokiwa, viongozi wa dini mliopo;Mabibi na Mabwana;
Mwaka huu wa 2015 ni mwaka wa kipekee sio tu kwa Kanisa lenu linaloadhimisha miaka 50 ya Dayosisi ya Dar es Salaam, bali pia kwa watanzania wote. Mwaka huu una mambo makubwa mawili yaliyo mbele yetu yaani kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa na uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Kama ilivyo kwa Dayosisi yenu, Taifa letu nalo linaianza safari ya miaka 50 ijayo na kufika kwetu huko ku- tategemea na jinsi tunavyoianza safari yenyewe.

Nchi yetu inapita katika kipindi cha majaribu makubwa na mitihani mikubwa. Tunalo tatizo la mmomonyoko wa maadili katika ngazi zote kuanzia familia, shule, ofisi na serikalini. Tunalo tatizo la ufisadi, ukatili dhidi ya vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi, na tunalo pia tatizo la umasikini. Tunalo tatizo la kupoteza uvumilivu wa kidini na kisiasa. Watanzania wengi wamefika mahala wanaanza kukata tamaa na kupoteza matumaini. Changamoto hizi zinawasumbua pia viongozi wa dini zetu zote. Waumini wamekata tamaa na kupoteza hofu ya Mungu. Kumekuwe- po na wengi sasa wanaokimbilia kwenye nguvu za giza, uganga na unajimu. Tunahitaji kutoka hapa. Tunajiuliza wote, tunatokaje?

Baba Askofu Dr. Mokiwa; Ndugu zangu;
Habari njema ni kuwa, nyakati za majaribu hazidumu. Mashaka na majaribu humfika mwanadamu ili kumuimarisha kila anapoukaribia mwisho mwema. Majaribu ni kipimo cha imani. Tunaletewa majaribu ili tuyashinde sio tuyakimbie. Tunayo fursa muhimu mbele yetu, kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa na muhimu zaidi Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015. Sote tumefuatilia kwa makini mchakato wa Katiba na tumeshiriki kwa hatua mbalimbali. Tumebakiza hatua moja muhimu, nayo ni kupiga kura ya maoni tarehe 31 Aprili, 2015. Sote tujiandae kuipigia kura na sote tutoke tukafanye uamuzi sahihi.

Fursa nyingine muhimu ni uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015. Uch- aguzi wa mwaka huu ni muhimu sana kwani tunachagua Rais mpya atakayeunda Serikali mpya ya awamu ya tano. Rais wa awamu ya tano atategemewa kuendeleza mema ya awamu ya nne na awamu zilizopita, na kutoa majawabu kwa changamoto za sasa na zijazo na kutusogeza karibu zaidi na Tanzania njema tunayoitamani, Tanzania yenye neema tele. Hatuko mbali na nchi yetu hiyo ya ahadi. Serikali ya awamu ya nne imefanya mengi sana makubwa ya kujenga misingi ya kutufikisha huko. Tumepanua nafasi za elimu, afya na huduma za jamii, tumejenga miun- dombinu ya kutuwezesha kufika huko, uchumi umekuwa sana lakini umasikini haujapungua kulingana na kasi ya kukua kwa uchumi. Bahati nzuri tunazo rasilimali zinazoweza kutuvusha katika hatua hii ya mwisho kuifikia neema mbele yetu.

Wengine wetu tumejiuliza sana, nini basi kinasimama kati yetu na neema iliyo mbele yetu ikiwa uchumi unakua na tumewekeza katika mi- undombinu muhimu na rasilimali tunazo? Yako majawabu mengi tofauti. Jawabu moja ambalo linasemwa na kukubalika na wengi ni kuwa,kinachosimama mbele yetu, na kati ya umasikini wetu na neema iliyo mbele yetu ni rushwa na ufisadi. Wako wanaotoboa mtumbwi wetu tunaosafiria pamoja na jitihada zetu za kupiga makasia. Mimi sipendi rushwa na ufisadi. Nashukuru Mungu kuwa rushwa, ufisadi na mafisadi hawanipendi zaidi. Siwaonei wivu wale wanaopend- waa mafisadi, natosheka kupendwa na wale wenye mapenzi mema na taifa letu. Jukumu la kuzuia ufisadi ni la kila mmoja wetu katika kila eneo lake na kwa nafasi yake. Sio jukumu la viongozi pekee, au chama fulani pekee, maana mafisadi wako kote katika ngazi zote.

Naamini, mwaka huu, wengi wetu tukisema hivyo, tukasimama katika mstari huo, na tukaenenda hivyo, ufisadi hauwezi kutushinda. Kila mmoja na asipuuze udogo wa sauti yake,au uchache wetu dhidi ya wale waovu, maana hata mwale mdogo wa mshumaa hufukuza giza.

Baba Askofu,
Kwa kuwa uchaguzi kwa nchi yeyote ile ni jambo kubwa, naomba Kanisa na waumini kwa ujumla waliombee taifa letu ili Mwenyezi Mungu atuongoze kuchagua viongozi wenye uwezo, busara na hekima ya kutatua changamoto zinazolikabili taifa. Tuchague viongozi waadilifu, wazalendo, wachapa kazi, wasio na uchu wa madaraka kwa ajili ya kujinufaisha wao binafsi na marafiki zao. *N*inawasihi viongozi wa dini muongeze juhudi za kuhubiri umoja na kutoa mafundisho ya kuhimiza udugu na mshikamano miongoni mwa waumini na watanzania kwa ujumla. Watu wapendane na washirikiane bila kujali itikadi za vyama vyao au ushabiki walionao kwa wagombea.

Tukumbushane kuwa chaguzi zinakuja na kuondoka lakini amani yetu, usalama wetu, udugu wetu na umoja wetu ndio nguzo kuu za uwepo wa taifa letu. Tusikubali kupoteza kwa gharama yeyote tunu hii ya amani, mshikamano na umoja wetu. Amani ya nchi yetu ikitoweka, umoja na mshikamano wetu ukivunjika, hakuna atakayesalimika itaathiri wote waliokuwamo na wasiokuwamo. Hivyo tunao wajibu wa kuidumisha amani. Nasema hivyo kwa sababu nimeyaona mwenyewe kwa majirani zetu.

Mhashamu Baba Askofu;
Ombi langu lingine kwenu - tuendelee kusaidiana kuilea nchi yetu kiroho na kimaadili. Sisi tutaendelea kuhangaika na afya za miili na akili za watu wetu. Tutaendelea kuwekeza katika afya,elimu na huduma za jamii.

Jitihada hizi za serikali ni kazi bure ikiwa dini zetu zote nchini haz- itawekeza kwenye afya ya mioyo ya watu wetu. Maana binadamu hakami- liki bila afya ya roho.

Mimi naamini kwa dhati kuwa watu wakishika mafundisho ya dini, wakamuogopa Mwenyezi Mungu, maovu mengi yatapungua. Hayawezi kuisha kabisa lakini yatapungua sana. Ninyi viongozi wa dini mnayo nafasi ya pekee kwa vile mnasikilizwa sana na waumini wenu. Ma- neno yenu yanapokelewa vizuri kuliko wanasiasa au watu wengine. Hivyo, tusaidiane kulea taifa letu ili lisiangamie. Hebu kila mmoja alime mrsba wake. Najua ni kazi ngumu hususan katika kipindi hiki cha utandawazi lakini tusichoke. Tuweke mkazo zaidi kwa vijana kwa sababu wao ndio wahanga wakubwa lakini pia wao ndio taifa la leo na kesho, ndio warithi wa taifa letu. Tukiwaandaa vyema, mustakabali wa taifa letu na watu wake utakuwa kwenye mikono salama.

Tukishindwa leo, tutalia na kusaga meno kesho. Taifa letu litakuwa mashakani.

Mwisho
Mhashamu Baba Askofu Dr. Mokiwa, Viongozi wa Kanisa la Anglikana,Ndugu waumini,Mabibi na Mabwana
Nimesema mengi, lakini nilidhani ni vizuri nikayaeleza hayo niliy- oyaeleza kutokana na mazingira na nyakati zenyewe wakati tukishere- hekea miaka 50 ya kanisa hili na tukizitazama nyakati muhimu kwa kanisa na taifa zilizo mbele yetu. Nakushukuru kwa mara nyingine tena Mhashamu Baba Askofu kwa uongozi wenu imara ambao umeliwezesha kanisa katika kupata mafanikio makubwa sana katika miaka 50. Naomba Mwenyezi Mungu awaongezee neema na karama ili kupata mafanikio zai- di siku za usoni . Mimi nitakuwa nanyi bega kwa bega katika safari ya kanisa hili huko mbele tuendako, kama nifanyavyo kwa makanisa na dini nyingine kwa kuamini kuwa sote tunafanya kazi ya Mungu mmoja.

Naomba tuendelee kushirikiana kuleta maendeleo zaidi kwenye Dayosisi yenu na nchi yetu kwa ujumla. Tukiunganisha nguvu zetu, daima ushindi utapatikana. Basi tuamue sasa kuwa washindi.
 
Wakiongea makanisani utadhani watu,ngoja waitane huko wanapokujua,yote waliyoyaongea wanasahau kazi inakuwa moja tu wapi Kuna hela zingine zimesahaulika tuzipige....... Wezi watu wabaya Sana.
 
Izo swagaz za escrow etc. Wachungaji, mashekh na maaskofu wote njaa kali message not sent kwa kondoo ni mchungaji mwenyewe ndio ime delivered.

Hatudanganyiki

cc. Wama project
bcc. Lumumba
 
Back
Top Bottom