Asalam aleikum!!!
Bwana Yesu asifiwe!!
Nimesoma thread ya Lizy kuhusu unyanyasaji wa watoto ikanikumbusha mbali sana, hakika imenitoa machozi!!
Nakumbuka miaka ya nyuma sana wakati nikiwa na miaka 4 tu, mama yangu alifariki kwa ugonjwa wa cancer, hatukukaa hata mwaka baba naye alifariki na ugonjwa wa figo, hapo ndipo nilipotamani dunia igeuke chini juu.
Nakumbuka dada yangu mkubwa alikuwa ndio kwanza yupo 4m3 na kaka yangu ambaye nafatana naye alikua yupo darasa la pili, tulinyang'anywa mali zote za baba yetu, tena tukarudishwa kijijini kabisa ambapo baba aliweka mifugo yake, baada ya muda bb mdg akaja akachukua ngombe wote wakagawana na watoto wa mama mkubwa.
Hakuna aliyetujali, tuliachiwa mbuzi tu pale kijijini, nakumbuka kaka yangu ilibidi aache shule aanze kuchunga hao mbuzi kwa taabu, mimi nilikua nachota maji na kufagia, hakuna aliyejua tunakula nini, tunavaa nini wala tunalala vipi.
Nakumbuka wale rafikize baba wakamlipia dada yangu ada kwa kuchangiwa na kijiji dada akarudi shule, jirani yetu mmoja akasema tuchanganye mbuzi zetu na zake ili kaka asiende kuchunga awe anaenda shule.
kutokana na baridi ya mkoa ambao tulikuwe, na hatukuwa na blanket siku moja nilishikwa na naimonia ikiambatana na homa kali, kaka yangu akapanda gari kwenda mjini kumwambia baba mdogo, baba mdogo akamwambia kama baba yake na mama yake wamekufa yeye anafaida gani, mwache afe akupunguzie taabu na ww!! kaka alirudi kijijini na kuomba msaada ndipo nikapelekwa hospitali na kulazwa, ikimlazimu kufanya vibarua vya kulima wakati akiwa mdogo ili kutupatia fedha za matumizi na kuniuguza.
kaka yangu mtoto wa m.mkubwa akaoa kule kijijini akatuchukua lakini niliona bora tulivyokuwa tunakaa wenyewe maana wifi alitunyanyasa sana, jina langu lilikua mbwa, nakumbuka alikua ananiita hivi, "we mbwa mkubwa njoo hapa" ukifika tu unakibao alafu ndio maagizo mengine yanaendelea!!!
Baada ya muda wale wote waliotudhulumu alikufa mmoja baada ya mwingine, wale waliotunyanyasa kwa chakula leo ndio wanatuomba chakula, waliotulaza chini leo wanatembea wameinamisha vichwa vyao!!
"usimnyanyase yatima wala kumuonea mjane, mkono wa Mungu utakuwa juu yako"