Simulizi: Zawadi ya Adhabu

Simulizi: Zawadi ya Adhabu

Hakwea

Member
Joined
Oct 25, 2018
Posts
16
Reaction score
19
*SIMULIZI YA MAISHA: ZAWADI YA ADHABU*

*MTUNZI: TIMOTHY PETER MSUYA “KIRAKA”*

*Mawasiliano +255 763 305 605*

*Utangulizi*

[Kisha nikarudi tena, na kuona ubatili chini ya jua.
Kuna mtu aliye peke yake, wala hana wa pili wake; naam, hana mwana wala ndugu; hata hivyo amali yake haina mwisho, wala macho yake hayashibi utajiri. Basi asema, Ni kwa ajili ya nani nafanya kazi, na kujinyima nafsi yangu mema?

Hayo nayo ni ubatili, naam, ni taabu kubwa!!

Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua! Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto?

[Mhubiri 4: 7-11]

******
*Nimefundishwa kuwa…*
_“Kuwaza jambo jema ni jambo la kwanza halafu kutenda jema ni jambo la pili tofauti kabisa!! Kuna wakati unawaza jambo jema ukiwa katikati ya kutenda uovu, au ukawa uko katikati ya kutenda mema huku akili yako ikijiwazia uovu mtupu!! Ingawa mara kadhaa nafsi inaweza kukusuta, si mara zote unaweza kuwa imara kiasi cha kuamua kutenda kile chema unachokiwaza. Lakini daima, uamuzi juu ya kutenda jema, uwe umeliwaza ama la, unao mwenyewe.. Ukiamua kutenda jema, hakuna cha kukuzuia!_

*Una hiyari ya kukubali au kukataa….*

*NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU YA KWANZA*

_Alikuwa ndani ya bajaji…_
Jua kali lililoambatana na upepo mkali uliobeba vumbi la kutosha vilishindana kuonyesha umwamba wake! Jua lilimulika kana kwamba lilikuwa likitafuta kitu fulani kilichopotelea ardhini bila mafanikio. Upepo ukashirikiana na vumbi kuichafua hewa kwa makusudi bila kujali kuwa kuna viumbe waliihitaji hewa ile kwa matumizi yaliyohalalishwa. Ulikuwa ni mwanzoni mwa mwezi wa kumi na moja.

Vumbi lilikuwa likitimka bila sababu yoyote ya msingi!!

Kwa wakazi wengi wa Mji wa Singida, hii ilikuwa ni hali ya kawaida kabisa na walikuwa wameizoea na kuifanya sehemu ya maisha yao ya kila siku. Yeye hakuwa na sifa ya kuitwa mkazi mzoefu wa mji huu wa Singida. Vurumai hii ilimkera! Alijikuta akipiga chafya mfululizo huku kamasi nyepesi zikimkereketa puani, akaufikia mfuko wake wa suruali na kukitoa kitambaa safi cheupe, akapenga pua zake asiambulie chochote cha maana.
Akasonya moyoni huku akikunja uso wake uliojaliwa uzuri wa kiume. Ule upepo mkali uliokuwa ukiipuliza bajaji iliyokuwa ikitimka mbio ulimwingia machoni, machozi yakawa yanamchonyota machoni

Alikereka.

Kwa mbali, mawazo yake yalimpeleka Dar es salaam, jiji ambalo pamoja na kukulia na kupatia elimu yake yote, ya darasani na ya maisha, ndilo aliloanzia kufanya kazi. Alitamani sana kuwa Dar es salaam lakini akalipuuza hilo mara moja. Alishaamua kubadili kabisa maisha yake na mojawapo kati ya mabadiliko ya muhimu aliyoyafanya ilikuwa ni kuhamishia makazi yake mkoani Singida. Yaliyomkuta jijini Dar es salaam hakutaka kuyakumbuka hata kidogo, na muhimu kwa wakati ule ilikuwa ni kuyaanza upya maisha yake ambayo almanusura yapotee alipokuwa jijini Dar es salaam. Kwa mbali, ile kero ya vumbi na upepo vilivyokuwa vimemzunguka akavikubali na kujikuta akitabasamu tabasamu hafifu.

Alishaanza kupazoea na kupapenda Singida.

“Tumefika bro” Sauti ilimzindua kutoka mawazoni na akajikuta akishtuka kidogo.
“OK”. Aliitikia huku akishuka kutoka kwenye bajaji ile. Akalipia na kuvuka barabara huku akiiweka sawa tai iliyokuwa imemkaba kooni. Hapo tena, lile timbwili la upepo mkali uliochanganyika na mchanga pamoja na vumbi vikaubusu uso wake na kumuingia kidogo kwenye macho yaliyokuwa nyuma ya miwani aliyokuwa amevaa. Kwa hatua za haraka haraka akalifikia geti la Tanzania Institute of Accountancy ambacho wakazi wengi wa mji ule walipendelea kukiita “uhasibu”.

Bado upepo na vumbi havikumuhurumia msomi huyu, viliendelea kumzomea vikimsindikiza mpaka alipozifikia ngazi za kuingilia ofisini kwake. Hapo vikambusu kwa mara ya mwisho na kumwacha huru.
Naam.. Hapo akawa amefika ofisini kwake. Kule kutembea kwa haraka na kurukaruka kukwepa vumbi na mchanga sasa vikakoma na mwendo wake wa maringo na mikogo ya kisomi vikarejea.

Clifford Chiziza ndilo jina lililokuwapo kwenye vyeti vyake vyote vya shule na vitambulisho vingine vyote. Msomi wa shahada ya uhasibu aliyesajiliwa na bodi ya taifa ya uhasibu na mmiliki mwenza wa kampuni ya Elites Financial Consultants, Clifford aliyependa zaidi kuitwa Cliff alikuwa mkufunzi katika chuo cha TIA tawi la Singida akijikita zaidi katika masomo ya ukaguzi wa hesabu pamoja na uhasibu. Akiwa na miaka 30 tu, alikuwa na sura ya kuvutia iliyotumika pia kuhifadhi tabasamu tamu lililochanua mara kwa mara alipokuwa na watu.

Clifford alitosha kabisa kutumika kumwelezea mwanaume mtanashati. Mavazi yake alijua kuyapangilia vema, mwendo wake wa kiume kabisa, namna alivyozungumza na kupangilia maneno yake pamoja na elimu ya kutosha katika fani yake vilitosha kabisa kumfanya mwanamke yeyote, hata wale walioolewa kumtazama kwa jicho la husuda.
Clifford alikuwa mwanaume hasa!

Haraka aliifikia ofisi aliyokuwa akiitumia kwa kushirikiana na mkufunzi mwingine wa kike aliyeitwa Zulfa Moses. Kwa bahati, alimkuta akiwa amezama katika jitabu kubwa akipekua pekua hapa na pale.
“Hallo Malkia… A very good afternoon to you” Alisabahi huku akimfikia Zulfa na kumpa mkono, kisha akaupokea ule wa Zulfa na kuubusu.
“Afternoon Chiziza.. Za uzima wako?” Aliitikia Zulfa huku kiaibu kikikatiza katika mitaa ya macho yake kwa kule kupokea busu laini kutoka katika papi za midomo ya Clifford..

“There we go again.. Chiziza is that old fella bana.. Mi ukiniita Chiziza nahisi nimezeeka wakati ndio kwanza damu inachemka. Clifford is a name and a half to me” Alisema Clifford huku akiijongea meza yake na kukaa juu yake huku akilegeza tai yake na kutupia kibegi maalumu cha kubebea kompyuta alichokuwa nacho.
“C’moon Cliff.. Umri nao unakwenda bana, na kutumia jina lako naona kama vile nakupa sifa za utoto ambazo zimekupita siku nyingi. Mbona mimi kuna watu wananiita Madam Mosses and I’m jus’ cool with’it?” Alijitetea Zulfa
“You see.. You see… Haya sasa, umeniita Cliff, just the way I like it to be and it sounds really really cool.. Cliff umefupisha Clifford. Hiyo Chiziza ukiifupisha si tunakuwa tunatukanana?” Clifford alilalamika huku uso wake ukichomoza lile tabasamu ambalo alikuwa akilitumia nyakati muhimu hasa awapo na mwanamke mzuri.
Alichokuwa anakitaka akakipata. Kicheko cha kilegevu kikamtoka Zulfa huku akilazimika kukifunika kile kitabu kilichokuwa mikononi mwake. Alicheka kwa sekunde kadhaa huku macho yake yaliyolegea yakimwelekea Clifford.

“Mh.. So you mean Chizi? We mwanaume una vituko kweli” Alisema katikati ya kicheko kile.
Walijadili hili na lile, huku Clifford akitumia muda mwingi kulalamika juu ya hali ya hewa ya mji ule, namna upepo na vumbi vilivyokuwa vikimchachafya na namna usiku alivyokuwa akikosa usingizi kwa kelele za paa la nyumba ambalo lilikuwa likiadabishwa ipaswavyo na upepo ule. Alilalamika pia kuhusu mwenye nyumba kuonekana kutokujali adha ile aliyokuwa akiipata ya kulazimika kukesha akiwa analisikiliza paa lililokuwa likilalamika pasi na msaada wowote. Kwa kusulubiwa na upepo.

“We nawe unadeka sana.. Nyumba uliyopata ni mpya kabisa, na huenda ni changamoto tu za upepo mkali au kuna pahala mafundi hawakuwa makini. Badae nitampigia fundi mmoja mzuri ninaishi naye jirani, we jiandae tu na mwenye nyumba wako aje akusaidie. Umeridhika?” Alimaliza Zulfa.
“Kwakweli hilo limekaa poa, ndio maana nakupendaga mamalake, mmmmmwaaaah” Alichombeza Clifford huku akiachia busu hewani. “Na yule mzee wala sihangaiki kumtaarifu. We nipe namba za huyo jamaa aje anisaidie, mengine tutajua mbele kwa mbele”

“Au kama usumbufu umezidi hamia kwangu basi mpaka atakapotengeneza” Zulfa alisema huku lile jicho lake kubwa lililolegea bila utaratibu akilitumia ipasavyo. Alivaa sura ya utani lakini kwa mwanaume mwerevu kama Clifford alitambua upesi kuwa sehemu fulani ya akili ya mwanamke yule ilimaanisha kile alichokisema.
“Ah.. Wanawake wazuri kama ninyi tena wenye elimu ya kutosha huwa mna wakubwa wanawaweka mjini. Usinitafutie kesi ya mauaji bure mwana wa Chiziza mie.. Hivi una kipindi baadae? Nadhani nitahitaji projector yako, ya kwangu wanaitumia kule procurement” Clifford alibadili mada upesi na aliona waziwazi namna Zulfa alivyokerwa na kitendo kile lakini hakujali.

Hili lilipoisha, wote wakazama katika kujiandaa kwa vipindi vya mchana ule. Mara kwa mara Clifford alikuwa akinua mkono na kutazama saa yake ili kujua muda, na ilipotimu saa nane mchana, akainuka na kompyuya mpakato na kibegi kingine kilichokuwa na projector ya Madam Zulfa na safari ya darasani ikaanza.
Kufundisha masomo ya ukaguzi wa hesabu za fedha na masomo mengine ya uhasibu ilikuwa ni kazi aliyoipenda na aliyoifanya kwa moyo sana huku wanafunzi wake wengi wakimsifia kwa kile kipaji chake kikubwa cha kuweza kufundisha masomo magumu lakini kwa namna iliyowasaidia wengi kumwelewa vema. Pia alikuwa na ukaribu mkubwa na wanafunzi wake, na hakusita kuwasaidia popote walipohitaji msaada wake. Hakika alikuwa kipenzi cha wengi.

Hakuwahi kujua kuwa ufanisi wake katika kazi yake hiyo ungekuja kumgeuka na kumuingiza katika adhabu…
Hakujua kuwa ufanisi huo ungemtunuku zawadi kubwa…

_Zawadi ya adhabu…._
 
*SIMULIZI YA MAISHA: ZAWADI YA ADHABU*

*MTUNZI: TIMOTHY PETER MSUYA “KIRAKA”*

*Mawasiliano +255 763 305 605*

*Nimefundishwa kuwa…*
_Hakuna gharama yoyote unayoitumia kumwamini mtu mwingine. Unachokihitaji ni akili za kujua ni sehemu gani katika wengine unayoiamini. Hii ni kusema tu kwa lugha rahisi kuwa, huwezi kumwamini mtu mmoja kwa kila kitu. Huenda ukamwamini sana katika mwenendo wake, lakini ukakosa imani katika maneno yake. Binadamu mwenye akili isiyoweza kusomeka kutoka nje hawezi kufikia hatua ya kuaminika kwa asilimia mia moja. Acha usiamini hili leo ninapoliandika, halafu kesho, mtu mwingine atapata nafasi ya kukuthibitishia hili kwa vitendo!!_

*Una hiyari ya kukubali au kukataa….*

*NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU YA PILI*

_Sasa alikuwa akiishi Singida…_
Hakuhamia mkoani Singida kutokana na mapenzi yake. Hakuwahi kuwaza kuwa angeishi nje ya jiji la Dar es Salaam katika maisha yake. Alikuwa yuko sahihi kabisa. Maisha yake yote aliishi jijini Dar es Salaam, yeye pamoja na familia yao, yeye akiwa mtoto wa pili kati ya wawili tu wa Kapteni mstaafu wa Jeshi, Mzee Adolph Chiziza na Mama yao, Rabeca Shamte, au Mama Claritha.

Dada yake kifungua mimba alikuwa akiishi Zanzibar na mumewe na watoto wawili mapacha, huku akiwa amejikita kufanya biashara mbalimbali hasa za vipodozi na vifaa vingine vya wanawake huku pia akiwa mwajiriwa wa shirika la bima la Zanzibar.

Kama kuna watoto waliopata bahati mbaya ya kuzaliwa na wazazi wakorofi na waliokuwa na kile ambacho vijana wengi walikuwa wakikiita “ukoloni”, basi Clifford na dada yake Claritha walikuwa na bahati mbaya kwelikweli. Mzee Chiziza hakuwa mtu wa kauli mbili! Awali, wengi walidhani kuwa huenda kule kufanya kazi jeshini ndiko kulikuwa kunamfanya kuwa mbabe kiasi kile, lakini hata baada ya kustaafu akiwa bado na nguvu za kutosha kabisa, ukali wake uliokuwa una kila sifa ya kuitwa udikteta uliendelea kushamiri! Alikuwa akisema jambo mara moja, na ikiwa lisingetendeka, hangesita kumchukulia mtu hatua ambazo zingeweza kumwacha hospitali kwa muda!
Chiziza hakuwa mtu wa kauli mbili!

Ukali wake haukuwa nje tu ya familia. Mara kadhaa alishamsweka Clifford au ndugu mwingine yeyote ndani na kumwacha huko hata wiki nzima kwa kile ambacho alikiita kuwafunza adabu. Kwa kiasi kikubwa alifanikiwa na kweli, yeyote aliyemfahamu vema Chiziza alijitahidi kuitunza nidhamu yake kwa viwango vya juu ili asije akaingia matatizoni pasi na sababu!! Hii ilikuwa ni sababu pekee ya Clifford kupendelea kujita Clifford tofauti na wengine walipotaka kumwita jina lake la pili, Chiziza, jina ambalo kila kona ya jiji lilitambulika kwa ubabe, visasi, ujeuri na fujo za kukata na shoka!

Elimu ya Clifford ilimsaidia kwa kiasi kikubwa kujitenga na ukorofi wa baba yake. Alipohitimu tu chuo kikuu cha Dar es Salaam, alipata nafasi ya kubakishwa ili kufundisha katika chuo kile huku akiendelea na masomo yake ya kuthibitishwa na bodi ya taifa ya Uharibu na ukaguzi wa fedha, NBAA. Hii ikamtenga na nyumbani kwa yule aliyemwona kuwa gaidi, jambo lililosadifiwa ma sura yake amnayo pamoja na ukweli kuwa haikuwa mbaya kama wengi wanavyoutafsiri ubaya wa sura, mzee huyu aliilazimisha kuwa mbaya muda wote kwa kuikunja na kuzuia aina yoyote ya Tabasamu...Ndiyo.. Kuna wakati Mzee Chiziza angekutana na jambo linalomlazimisha kutabasamu au kucheka kabisa, lakini kama ungelikuwa karibu naye, ungelimwona jinsi alivyoamua kwa makusudi kukaza sura kama gumegume na kuishia kutoa aina fulani ya mguno wenye chembechembe ya kejeli, kisha akajikohoza..Kicheko kikapotea, na ile sura ngumu ikaumba tena kunyanzi zito usoni....Mwenyewe ndivyo alivyopenda..Ndani ya mwaka mmoja tu, Clifford akawa amekamilisha masomo yake na kuwa ni mhasibu aliyethibitishwa. Hakutaka kutafuta kazi nje ya kufundisha, hivyo kitabu kikaendelea.

Jua likachomoza na kuzama, akamaliza shahada yake ya pili ya uchumi wa viwanda na biashara za kimataifa.
Hapo sasa akawa ameiva kwelikweli kwenye taaluma. Kwa kushirikiana na mhadhiri mwenzake kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha, IFM, wakaanzisha kampuni ya _Elites Financial Consultants_ huku Clifford akiwa ndiye hasa injini ya kampuni.

Wakaajiri vijana machachari kwenye masuala ya usimamizi wa biashara, biashara za hisa, fedha na sheria za kikodi, na ndani ya muda mfupi wa kuanzishwa kwake, Elites ikawa ni mojawapo kati ya sehemu za kusuluhisha matatizo ya makampuni makubwa ya kibiashara ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam.

Upepo wa mafanikio ukaanza kuipuliza pwani ya maisha ya Clifford, na ule ukorofi wa baba yake ingawa hakuujali sana, uliendelea kama kawaida. Ukwasi alioanza kuupata katika umri mdogo ukampa heshima kati ya watu na ule ugwiji wake katika taaluma yake pamija na kufundisha chuo kikuu cha Dar es Salaam ukamketisha miongoni mwa vijana wachache ambao haingepita dakika kumi bila majina yao kutajwa midomoni mwa watu.
Halafu sasa likazuka jambo…

Kikaja kisa!!

Kisa ambacho kilimweka Clifford katika wakati mgumu na kulazimika kulihama jiji alilolipenda na lililokuwa limemwashia jua la mafaniko na kumpa mwangaza wa mafanikio. Kisa hiki kilipochanganyika na ukali wa Mzee Chiziza likawa kumbo la kuumiza na tufani la kupoteza meli ya mafanikio aliyokuwa ameipanda.
Tufani lilipoisha, akajikuta yuko Mjini Singida, ingawa hakufika kwa meli wala jahazi!!

***

Kungekuwa ni kutokumtendea haki kama ungemwita mwanamke aliyejikatia tamaa ya kimaisha. Ni kweli maisha yake hayakuwa na matumaini, na kwake, usiku na mchana havikuwa na tofauti kubwa. Vyote alivitumia kusaka pesa. Hakuwa na sura iliyomtosha kusimama katikati ya kundi kubwa la wanawake na kujitambulisha kuwa ni mzuri wa kupindukia, lakini alichonacho kilitosha kabisa kumpa sifa ya mwanamke mzuri, na kuwageuza wanaume wakware shingo na kumtazama huku wakimeza mate na kuendelea na safari zao. Pamoja na kutokuwa na uzuri wa kumuingiza kwenye orodha ya wanaoweza kushindania mashindano ya ulimbwende, alikuwa na sifa ya kipekee..

Aibu!!

Hakukuwa na mwenye hakika kuwa sifa ile ilikuwa ni ya kuzaliwa, lakini ilitosha kabisa kumuingiza katika kundi la wanawake wenye aibu. Asingeweza kuongea maneno mengi mbele ya mwanaume bila kujikuta akiwa akafikicha viganja au kutazama chini.

Alikuwa na elimu ya kutosha juu ya mazingira yanayomzunguka, na huenda angefaa kabisa kuwa mkufunzi wa elimu dunia. Aliyafahamu maisha ya tabu, raha, karaha, huzuni, furaha, ugomvi, purukushani na polisi na zingine zinazoendana na hizo. Hakika angeweza kuwa mwalimu mzuri iwapo ingeanzishwa shule ya kuyafundisha hayo, lakini kwa bahati mbaya, shule hiyo haikuwepo.

Akaishia kuyaishi yale aliyoyajua!

Kwa darasani, wala hakuwa anakumbuka hata kilipo cheti chake cha darasa la saba, kiwango cha juu kabisa cha elimu alichokuwa anakitambua duniani. Kuna wakati angetumia hata dakika mbili nzima akijaribu kukumbuka jina la shule ya msingi aliyosomea!. Hakuwa na habari nayo. Kwake, darasa la saba alilohitimu lilikuwa ni zaidi ya zawadi ya mtende kuota jangwani kwa kuwa pia, hakulimaliza kirahisi.

Alipokuwa akisoma, alitamani sana siku moja akamilishe safari ile ya miaka saba ya mateso makubwa. Ungekuwa mtu wa ovyo machoni pake kama ungepoteza muda wako kujadili naye kuhusu maisha ya shule uliyowahi kuyapitia, utamu wa masomo au majina ya walimu wake. Kwake hayo yalikuwa yamesahaulika siku nyingi na wala hakuwa na mpango wa kufanya bidii yoyote kuyakumbuka.

Kwanza ayakumbuke ili iweje kwa mfano?

Mbali na hilo, hakuwa anakumbuka ni lini alifika jijini Dar es Salaam, lakini baadae alielezwa kuwa, baada ya kifo cha mama yao yeye akiwa na miaka mitatu tu, baba yake alipendekeza kuwa ni heri yeye aende akaishi na dada yake wa kwanza ambaye alikuwa akiishi jijini Dar es Salaam. Hili halikuwa na kipingamizi kwa kuwa, msaada pekee wa kimalezi wakati ule ulikuwa ukitoka kwa dada yake huyu ambaye hakukuwa na yeyote kijijini kwao, Isimbira, Sikonge mkoani Tabora ambaye alikuwa akifahamu ni shughuli gani hasa aliyokuwa akiifanya jijini Dar es Salaam, lakini kila alipokuwa akirudi pale Isimbira, kila mmoja alikuwa akimzungumzia yeye. Alikuwa ni kivutio kwa misuko yake ya nywele, mavazi yake, namna alivyozungumza, kutembea na mengine mengi.

Hakika aliwavutia wengi.

Lakini yote haya, yeye alisimuliwa tu. Nunu hakuwahi kukumbuka habari za Isimbira. Dada yake alimlea jijini Dar es Salaam na wakati alipokuwa akipata akili za kiutu uzima, aliishia kuambiwa tu kuwa Mama yao alianza kufariki na baadae, baba yao pia akafuata. Isimbira walibaki ndugu tu wa karibu. Ndugu ambao wala hakuwa anawafahamu.
Isimbira ikazikwa kwenye kaburi la sahau, na Dar es salaam ikawa ndiyo Mwanzo na mwisho wake wa fikira!
Jina lake lilikuwa Nunu.. Nun utu, basi! Kwanza hakuwahi kufika sehemu yoyote ambako alilazimishwa kutaja majina mawili. Kote alisema anaitwa Nunu, akaeleweka! Kitambulisho cha nini kwenye maisha yake? Kwanza atambulishwe kwa nani wakati mdomo wake tu ungetosha kutoa utambulisho wa kutosha?

Naitwa Nunu… Nunu tu, basi! Hujasikia? Nimesema ‘NU’ halafu ‘NU’ tena, yani Nunu.., Ndio…

_NUNU!_

Kama kilikuwa ni kifupi, kirefu, kinyume nyume au vinginevyo, hakuna aliyejua!

Nunu aliendelea kukua akiishi katika chumba kimoja na dada yake aliyeitwa Kalunde Kwera. Labda Nunu naye aliitwa Nunu Kwera, lakini ole wako umwite hivyo… Maisha yao hayakuwa mabaya ingawa hakukuwa na kazi yoyote ya maana ambayo Kalunde alikuwa akiifanya. Kila siku angeondoka majira ya jioni na kurudi alfajiri akiwa fedha pamoja na baadhi ya mahitaji ya muhimu na maisha yakaendelea.

Mara kadhaa alikuwa akirudi akiwa na mwanaume ambaye Nunu aliishia kulazimishwa kumuita “Baba”, naye bila ajizi kwa kukosa ule utamu wa kuita jina hili, akajikuta akitii bila shuruti. Siku kama hii, angelazimika kulala chini huku akisikia purukushani huko kitandani, lakini hakuwa anaelewa chochote!

Kila mwanaume aliyevaa suruali au kaptula, makobazi au mokasi,aliyefunga mkanda au mshipi, alipofika pale alikuwa baba. Wengine walikuwa “baba wema” na wakaitikia kwa bashasha huku wakimpa shilingi kumi au ishirini, na wengine walikaza sura kama magumegume na wakaishia kumuuliza maswali magumu ambayo hakuwa ameyafundishwa shuleni wala popote inapopatikana elimu yoyote kwa umri wake.

Hali ikabadilika baadae. Kalunde angeweza kupotea hata siku mbili au tatu, na baadae hata wiki! Awali alikuwa akijitahidi kuacha matumizi, lakini baadae, hali ikawa tofauti. Kuna siku Nunu angeshinda njaa huku akiwa hana nauli ya kumwezesha kufika shuleni kwa wakati. Akajikuta akilazimika kukabiliana na mwendo mrefu wa kuifikia shule, au kutumia uongo na utapeli kuwasomesha makonda wa daladala ili aende bure. Kushindwa kufika shule kwa wakati kukamjengea urafiki wa kudumu na viboko vya walimu ambao hawakujaliwa kipaji cha kuuliza maswali mara mbilimbili. Alivizoea viboko na adhabu za hapa na pale, na wakati mwingine akajua hata namna ya kuvikwepa kijanja.
Nunu akawa Nunu wa shoka.

Akajifunza yote, kushiba na kusota na njaa.

Lakini yapo ambayo hangeweza kuyavumilia. Ni nani angemweleza kwa ufasaha juu ya vile vilima viwili vidogo vilivyoanza kuchomoza kifuani mwake kwa fujo huku nyonga zake zikitanuka na kuipa miguu tabu ya kubeba kamzigo cha haja cha makalio yaliyotutumuka ghafla kama kitunguu maji kikubwa? Ni nani angemweleza kwa ufasaha kuwa hata kule kuingia kwa siku zake za kila mwezi lilikuwa ni jambo la kumuingiza ukubwani? Ni nani? Nani angemjali kama si Kalunde dada yake?

Lakini kivuli chake kikamtazama na kumcheka kwa nguvu… “Yuko wapi dada yako tangu wiki iliyopita?” Kabla hajakijibu, kikamsaidia kumpa jibu lenye kukera. “Hayupo.. Hayupo na anaweza asirudi leo wala kesho”
Na kweli hilo likawa. Kalunde aliendelea kutokuonekana mara kwa mara, na alipoonekana kwa nadra, angekuja tu kubadili nguo na kuacha pesa kidogo ya matumizi kisha akapotea tena. Nyuma yake akaacha msururu wa wale akina “Baba Nunu” waliokuwa wakija mara kwa mara kumuulizia. Hapo Nunu akawa kwenye mtihani mwingine! Wanaume!
Wakamparamia na kumkumbusha kuwa alishaiva. Wengine walijua kabisa kuwa, wala hakuwa ameiva tayari, lakini wakajipa moyo kuwa, hata embe likiliwa na chumvi linakuwa na ladha tu! Wakamsaidia kulishibisha tumbo lake kwa chakula ambacho Nunu alikipokea kwa furaha bila ya kujua gharama zake. Taratibu wakamwingiza darasani. Darasa lisilo na viboko wala mitihani.

Hili akalipenda kweli kweli! Anafundishwa na kulipwa!!

Nunu taratibu akajifunza hiki na kile, na akiwa darasa la saba, tayari Nunu akawa ni moto wa kupikia kande! Ungemwambia nini Nunu huyu ambaye sasa angeweza kumkuna mwanaume mtu mzima pahala ambapo si kucha wala jiwe vingeweza kukuna? Ungemweleza nini Nunu kuhusu mapenzi ambacho asingekuwa akikijua kinagaubaga?
Lakini bahati ikawa upande wake. Akahitimu hilo la kuitwa darasa la saba salama. Hao wanaojihusisha na kusahihisha mitihani na kupanga matokeo nadhani walipagawa kila walipokamata mtihani wowote wa Nunu, wakaishia kughadhibika na kumchorea kila aina ya kinyago ambacho wangeweza kuchora. Angethubutu kupita mbele yao, nadhani kila mmoja angemmwagia matusi hata yale ambayo hayapo kwenye kamusi ya mtaani!!
Ingemuhusu nini Nunu ambaye wakati huo alikuwa mtaani akikabiliana sasa na maisha ya mtaani huku akiwa mwanafunzi asiye na sare?

Akajifunza maisha! Akafanya kazi za ndani, uhudumu wa bar, kupiga magengeni, kuuza mitumba, kazi za saluni na kwingine kote, lakini kote hakukumlipa. Angefanya kazi ipi nyingine ya kulipa zaidi ya kuuza kile ambacho anacho, na hakipungui wala kuchakaa? Nunu akawa kahaba wa kiwango cha lami! Ile haiba yake ya aibu na ukimya ukawa mtaji wa kutosha kumkutanisha na wanaume wenye fedha za kuchezea, wakamtumia kwa ujira ambao walipanga wao. Kwake yeye la muhimu lilikuwa pesa tu!

Wengine walikuwa wanaume wa shoka, wakampa ujauzito. Angezaa mtoto ili ampeleke wapi? Akazichoropoa kwa kasi bila wasiwasi, na kazi ikaendelea kama awali. Akaachana rasmi na dada yake na kujitafutia makazi yake peke yake maeneo ya Changanyikeni. Biashara sasa ikafanyika kwa uhuru na faida kubwa. Mbinu za kukabiliana na maisha zikaongezeka na akawa na mbinu nyingi za kuhakikisha kuwa halali wala kushinda njaa kama alipokuwa akisoma shule ya msingi.

_Kukuru kakara zake zikamkutanisha na Clifford Chiziza!_

Halafu....
 
*SIMULIZI YA MAISHA: ZAWADI YA ADHABU*

*MTUNZI: TIMOTHY PETER MSUYA “KIRAKA”*

*Mawasiliano +255 763 305 605*

*Nimefundishwa kuwa…*
_Kama kungekuwa an kanuni moja tu ambayo kwa kuifuata maisha ya binadamu yangekuwa ya kuvutia zaidi, huenda ingekuwa ndiyo kanuni ngumu kuliko zote katika masomo, nab ado binadamu wote wangejifunza kwa bidii kubwa mpaka waweze kuielewa kanuni hii. Lakini hata hivyo, bado kuna ambao wangeshindwa!! Maisha ninayoshi leo sio matokea ya kanuni, lakinni bado ninayafurahia. Hata wewe, unayo nafasi ya kuyafurahia kwa kuwa, unachokiishi leo ndicho kilichopo ndani yako, na hayo ndio maisha yako halisi mpaka utakapoamua vinginevyo!!!_

*Una hiyari ya kukubali au kukataa….*

*NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU YA TATU*

Haikuanza kama tufani wala aina yoyote ya mkasa, na wala halikuanza kama tukio la wapendanao wawili kukutana. Ulianza kama msaada kutoka kwa kijana wa kiume msomi anayeshiriki pia kuibua wasomi wengine kila siku huku mwingine akiwa mwanamke msomi wa mtaani mwenye kuijua vema mitaa na madhila yake. Halafu msaada ukageuka kuwa penzi la ghafla tu, lenye ahadi kemkem.

Ilikuwa ni Ijumaa moja wakati Clifford alipokuwa akitoka kazini kwake kurejea nyumbani kwake Kunduchi. Mvua kubwa ilikuwa ikinyesha na mwanamke mmoja alikuwa akihangaika kujikinga na mvua kwa mikono bila mafanikio huku akionekana wazi kuwa na kila nia ya kuomba msaada. Clifford akasimamisha gari na dada yule akapanda huku akiwa ameshalowa sehemu kubwa ya mwili wake.

“Pole sana dada angu.. Hii mvua ya Dar hainaga hata dalili. Dakika mbili jua dakika mbili mvua” Clifford alimpa pole dada yule aliyekuwa anahangaika kuiweka sawa sketi fupi iliyokuwa imemkaa vema ingawa sehemu ndogo ya mapaja yake yalikuwa yakichungulia nje. Kokwa mbili ndogo zilizovimba zilisimama wima kifuani pake na kule kulowana kwa mvua kukazifanya kuwa kama zenye kumdhihaki Clifford.

“Asante kaka” Aliitikia dada yule akiwa kainamisha uso wake chini.
“Sijui unaelekea wapi” Aliuliza Clifford
“Naelekea hapo Mwenge kupanda gari za kwenda Kunduchi” Alijibu.
“Waaaoooo… Kumbe unaishi Kunduchi?” Alihoji Clifford huku akijiiba na kumtazama hasa maeneo ya kifuani. _Akameza mate huku jicho likimtoka._
“Hapana kaka ‘angu.. Nna mteja wangu naenda kumwona mara moja” Alijibu.
“Kumbe niko na mfanyabiashara?” Clifford alijibu huku sasa gari ikishika mwendo
“Ah.. Kubangaiza tu kaka angu” Zile aibu zake akazipachika hapo kwa kukuna kuna vidole huku sasa akianza kuzoea lile joto ndani ya gari na kule kujikunyata kukaisha. Kifua chake kikawa wazi machoni wa Clifford.
Mwanaume akameza mate tena kwa nguvu huku wakati huu jicho akiwa kalikodoa.
“Mimi naishi Kunduchi, kwa hiyo safari yetu inaweza kuwa moja. Ingawa hujaniambia unafanya biashara gani, huenda nami nikawa mteja ukajikuta unapata wateja wawili leo” Clifford alinogesha mazungumzo. Dada yule akatoa tabasamu jepesi la makusudi, na tabasamu lile likawa kama mapigo mawili ya nguvu katika moyo wa Clifford ambao haukuwahi kusukwa sukwa ukasukika vema!
“Ni biashara za wanawake tu.. Nauza vitenge na vitu vingine wanavyotumia wanawake.. Samahani kwa kukuangusha” Dada yule alisema huku akiachia kakicheko cha aibu na kudeka kidogo.

Pigo la tatu la nguvu!

Clifford pamoja na ukufunzi wake wa uhasibu muda huo ungemuuliza sifa ze mdaiwa angekuwa sifa za mdai na zile za mdai akizifanya za mdaiwa!
“Ona sasa ulivyo na ubinafsi. Kwa hiyo bidhaa zako wanaume hatuwezi kununua? Si tuna marafiki, wake, mama zetu na wengine tunaweza kuwapelekea?” Alijikaza na kuuliza. Kwa mbali alianza kuhisi kule kujiamini kwake kukiisha.
“Kwani umeoa kaka?” Aliuliza dada yule huku akijitahidi tena kukwepesha macho yake. Hapo sasa akawa ndio akawa ameutandika teke kabisa moyo wa Clifford. Akajikuta akichekacheka kama bwege.
“Sijaoa kwakweli, siku hizi waolewaji wapo basi? Kupotezeana muda tu” Clifford alijitetea kipuuzi na pale dada yule alipoonesha kutokujali sana kuhusu jibu lile, mara moja Clifford akagundua kuwa alikuwa ametoa sababu ya kipuuzi. Kwanza hakuulizwa. _“Nimekuwaje mimi? Mbona ni kama vile napoteza umakini wangu? What is happening? Mwanaume atapotezewaje muda dada na mwanamke?”_ Alijikemea kimya kimya na kujiweka sawa ili asiendelee kusema vitu vya kitoto mbele ya mwanamke yule.

Lakini hakuna chochote kilichobadilika. Mpaka anamshusha dada yule katika kituo cha London alipokuwa anakwenda, Clifford alikuwa amejiweka mwenyewe miongoni mwa wanaume wapumbavu waliokuwa wanapatikana jijini Dar es Salaam jioni ile. Pamoja na upole wake na aibu zake, dada yule alikuwa fundi kwenye kila idara ya mazungumzo.

Hata pale Clifford alipojitutumua na kuanza kuongelea habari za uchumi wa nchi iliyokuwa ni miongoni mwa fani zake na masomo aliyoyafaulu vema, alikatwa kidomodomo na maswali pamoja na maelezo mafupi mafupi ya Nunu, akajikuta akijiona goigoi asiyejielewa! Mpumbavu kabisa!!
_“Kwani wewe kwako uchumi wa nchi kukua kutakusaidia ikiwa mshahara wako unachelewa kutoka kwa mwezi mmoja na nusu? Hapo sijaongelea kutokuwa na mshahara, ni kwamba mshahara tu umechelewa?”_ Lilikuwa mojawapo kati ya maswali aliyotupia pale alipoanza kujitia mjuaji wa uchumi.

Akajitia mjuaji, akajieleza weeee, NNP, GNP, pato la taifa, utegemezi na mikopo chechefu sijui fedha ambazo Ahazijaiva... mwishowe akajikuta kuzunguka koooote ametokea palepale alipokuwa.. Akaulizwa tena..

“Achana na hizo sijui TLP sijui GNP, pesa mbichi sijui manini.. Uchumi ukikua, na leo ukasikia kuwa uchumi sijui umekuwa kwa asilimia ngapi.. Halafu mshahara wako wewe ukachelewa.. Hapo nimesema umechelewa, sio kwamba umekosa kabisa, umechelewa kwa miezi miwili tu.. Hiyo utaiongeleaje?” Dada yule akakazia swali.

_Mhadhiri wa Chuo Kikuu tena mjuzi kabisa wa uchumi akaufyata mkia. Alikosa lugha rahisi ya kuongelea mambo magumu!_

Wakajadili hili na lile huku binti akiendelea kuwa kiungo mchezeshaji wa mauzungumzo. Mpaka anamshusha, alichokumbuka kuomba kilikuwa ni namba ya simu tu, na wakati alipopewa, akazidi kuingizwa darasani na mwanamke yule.

“Asante sana Clifford kwa lifti kaka angu. Ingawa kwako namba yangu imekuwa ya muhimu kuliko hata jina langu.. Haya baba, Vodacom labda watakusaidia kulipata jina” Binti alisema huku kwa mbali akionekana kulalamika.

_Ama! Hivi leo nimekuwaje mimi? Mbona kama vile nna kapepo kananiandama?_

Clifford alijaribu kukiweka sawa kichwa chake lakini alikuwa ameshachelewa. Nunu alikuwa ameshashuka kwenye gari huku akiwa anajitahidi kuiweka kadi ya mawasiliano aliyopewa na Clifford kwenye mkoba wake mdogo aliokuwa ameupakata. Kama alifikiri kuwa mwanamke yule alikuwa wa kawaida kama alivyokuwa anaonekana, alikuwa amejidanganya vibaya.

Wakati anaweka sawa koo lake na kuyapanga vema maneno kichwani mwake, tayati Nunu alikuwa akivuka barabara kwa mwendo wa kuchuchumia ulionakshiwa na vile viatu virefu alivyovaa. Hapo sasa Clifford akajionea kile ambacho mwanamke yule alipewa pasi na hiyari yake. Mzigo uliofungwa kwa umakini mkubwa ulikuwa ukiihangaisha hewa iliyokuwa imetulia na ule ubaridi wa mvua ambayo bado haikuwa imeanza kunyesha mitaa ile.

Alipokuja kuwa tayari hata kujigusa, alikuwa akitazamana na askari wa usalama barabarani aliyekuwa akimuhoji juu ya kusimama katikati ya barabara. Haraka akajiweka sawa na kuimalizia safari yake huku mawazo yake yote yakiwa yamezama katika bahari yenye upepo mkali.. Bahari ya mwanamke yule wa ajabu.

Ijumaa hiyo ikamuingiza rasmi kahaba kwenye maisha ya mhadhiri wa chuo kikuu!!

***

Kama ungeambiwa yule alikuwa ndiye Nunu yule ambaye alishazoea purukushani za mgambo na maaskari wa jiji basi ingekulazimu kuingia kwenye vitabu kadhaa vya Imani kutafuta sehemu ambako ungeweza kumuingiza huko ili vizazi vijavyo wamsome! Makazi yake yalishahamishwa kutoka Changanyikeni kwenda Makongo. Hayakuwa makazi ya mwanamke asiye na kazi maalumu. Yalikuwa ni makazi ya mwanamke anayefanya kazi yenye kipato kikubwa na marupurupu juu.

Kule kushinda nyumbani muda wote kukaipa nyumba ile sifa ya unadhifu uliopitiliza. Hata nzi, ingawa ni mjinga daima, angejiona mjinga zaidi iwapo angejivika ujasiri wa kijinga wa kuisogelea sebule ile. Wachache waliokuwa na ujasiri wa kuruka na kutua popote, walijikuta wakizomewa na harufu ya kuvutia iliyowakumbusha kuwa yale hayakuwa makazi yao. Wakajiondokea kwa aibu tele huku wenzao wakiwazomea.

Clifford aliaazimia kuyabadili maisha ya Nunu. Alimtambua Nunu kama mwanamke sahihi wa maisha yake, mbangaizaji aliyekuwa akiuza vifaa mbalimbali vya wanawake kutoka ndani na nje ya nchi, na akakazana kumkuzia mtaji kila siku. Ndani ya miezi minne tu ya uhusiano wao, walishaanza kufanana hadi sura. Kila kona walikuwa pamoja huku marafiki kadhaa wa Clifford wakimtambua Nunu kuwa shemeji yao. Hata kama kuna ambao kwa bahati mbaya tu waliwahi kuonana na Nunu huko nyuma, haingewawia rahisi kumtambua Nunu huyu wa sasa aliyepambwa kwa kila aina ya stara na nguo ya heshima. Ule usemi wa duniani wawiliwawili ukawafunga midomo, na maisha yakaendelea.

Lile tufani lililoupiga moyo wa Clifford siku ya kwanza kuonana na Nunu halikutaka kutulia wala kupunguza makali. Siku hadi siku Clifford akaendelea kuwa dhaifu na asiyejiweza kwa Nunu. Akaungwa kwa viungo vyote, akawekwa na nazi ya tui zito la penzi la mnyamwezi ambaye hakuwahi kupajua unyamwezini. Akaongezwa na ladha ya maneno matamu yaliyopangwa vema kutoka katika midomo midogo ya Nunu, akakandamizwa kwa zile aibu za Nunu zilizokuwa zikitoka kwa mpangilio wa aina yake.

Chali!!!

Mwanaume usomi akauweka mfukoni, na haraka akaiulizia gharama ya pete ya uchumba. Wauza magari wakapata mteja, wenye maduka ya kuuza urembo wakawa na mteja wa kudumu, na madalali wa nyumba na viwanja namba zao zikatafutwa na kuhifadhiwa kwenye simu. Aliazimia kumuoa Nunu tena haraka iwezekanavyo.

Mzee Chiziza akapewa taarifa za kijana wake kuadhimia kumvika binti fulani pete ya uchumba. Ule ubabe na ukali wake vikamjia upesi kutaka kujua taarifa zote muhimu za huyo wa kuitwa mchumba wa mwane na mkwewe. Akam’bana kijana wake ili amweleze vema kuhusu sifa za mchumba wake huyo huku akitaka taratibu zote za kifamilia zifuatwe.

Hapo ndipo Clifford akakumbuka kuwa, hakuwahi kupata nafasi hata ya kumuuliza vizuri Nunu juu ya maisha yake hasa ya kifamilia. Angeuliza sangapi wakati kila alipokuwa akifika nyumbani kwake angejikuta wakati wa kukaa kwenye kochi tayari ana baadhi tu ya nguo mwilini? Angeuliza sangapi wakati kila alipotaka kufungua mdomo alikutana na mdomo mwingine ukiwa unamsubiri wakutanishe ndimi zao? Ni wapi angekuwa na wakati wa kuuliza maswali mengi wakati kila mara yeye ndiye alikuwa mwanafunzi na akamruhusu Nunu, pamoja na aibu zake tele, azungumze kila kitu?

“Ona sasa ulivyo mpumbavu. Yani unakutana na jianamke huko linakupumbaza mpaka unataka kuoa lakini hata hujui habari za familia yake? Hivi elimu yako inakusaidia nini fala wewe? Mbona unakuwa bwege namna hiyo?” Alifoka Mzee Chiziza huku akiwa anagonga gonga meza kwa mkono. Tusi zito la nguoni likamtoka bila kujali yule aliyekuwa mbele yake alikuwa mtoto wake wa kumzaa.

“Hapana dady.. Listen.. You know it is the matter of… the matter of…”

“The matter of what you swine? Unataka kuoa mtu ambaye hata kumfahamu tu is the matter of God knows what? Wewe ni mpumbavu Clifford, sorry kama niliwahi kukwambia hili nilikuwa nakutania tu, now I’m telling you from the depth of my heart.. Wewe ni mpumbavu, and I’m ashamed of you, bastard” Alipigilia msumari Mzee Chiziza, akatema mate kwa nguvu ingawa hayakutoka!!

“Dady calm down.. Ndio maana nimekuja tuongee baba angu.. Sasa unapoanza kuja juu….” Alilalmika Clifford

“Unanipanga sio? Unanilainisha, si ndio? Unadhani mimi ni fala wa zamani? Nakwambia hivi, ufala wangu kwako ndio taaluma zote ulizonazo na usizo nazo, kuku kishingo wewe. Eti ‘Nimekuja tuongee’, umekuja tuongee au umeniletea taarifa fala wewe? Lini ulikaa na mimi ukaniambia uko tayari kuoa na kuwa umeshaanza kusaka huyo mchumba? Lini mwanaharamu wewe? Lini umenipigia simu hata kuuliza juu ya mambo ya muhimu ya kufanya kabla ya kuoa, maluhuni mkubwa weye? Umekuwa eeh? Kufundisha wanafunzi wavaa uchi kumekufungua akili umeamua kuoa sio?” Chiziza alimkazia macho mwanae.

“Baba tafadhali usifike huko, na sifundishi wavaa uchi, nafundishha wanafunzi wa chuo kikuu cha…” Clifford alijisemea kinyonge bila kumtazama zaidi baba yake.

“Listern young man… Wenye akili huwa hawaoi wanapodhani kuwa wako tayari kuoa au wanapokutana na watu wanaofaa kuolewa. Wenye akili wanaoa pale wanakuwa tayari kutimiza wajibu wa ndoa.. Jifunze vema hapo, nimesema wajibu, sio majukumu. Sasa kama wewe kufungua na kufunga zipu unadhani kuwa uko tayari kuoa, au kwa vile una kazi inayokusaidia kula kunya na kulala unahisi umeshaweza kutimiza wajibu wa kuoa, sina cha kukuzuia. Nenda kaoe.. Ila kumbuka, baada ya kuoa, Utaitwa BABA, hata kama huna watoto. Halafu nisikie unaniita kwako kuwa ndoa ina shida, “ooh, baba nisaidie”. Hakyamungu namuapia baba yangu mzazi na kaburi lake kama lipo, nakupiga risasi mwanaizaya weee!” Wakati anayasema haya tayari alikuwa ameshalifikia jokofu na kujimiminia glasi nzima ya maji.

“Lakini baba.. Nahisi niko tayari kutimiza wajibu wangu wa ndoa. Nahisi niko tayari kuwa baba. Yaliyobaki ni madogo tu ya kusikia kama wosia wako kwangu” Clifford alijikaza mpaka mwisho kuweza kuyatoa maneno haya. Maneno ambayo hayakumzuia Mzee Chiziza kumaliza glasi yake ya maji, akaongeza na ya pili, kisha akapiga mbwewe kwa nguvu huku akitikisa kichwa.

“Unahisi Clifford.. Unahisi… Wewe mwenyewe unasema unahisi halafu unataka mimi nikuamini? Ngoja nikuulize swali rahisi. Uko tayari kweli kuoa?”

“Ndio baba, na tayari nna mtu amba….”

“Jibu moja kwa swali moja, usinipe majibu ambayo maswali yake nitakuuliza kesho tafadhali. Nimekuuliza, uko tayari kweli kuoa?”

“Ndi… Ndio Mzee.. Nipo tayari” Alijibu kwa kitetemeshi Clifford.

“Well then, very well… Uko tayari kuoa kwa kuwa uko tayari kuoa au kwa vile watu wengine wanadhani kuwa uko tayari kuoa?” Aliuliza Mzee Chiziza huku akiwa amemkazia macho Clifford.

“Vyote baba. Watu wengi wa umri wangu… unaju….”

“Pumbavu kabisa. Siku ukiwa tayari kuoa ndio uje kuongea na mimi. Mbona wengi wanajiuliza utakufa lini ili warithi mali zako ila hujanijia hapa na ombi la kufa? Tumia akili Mwalimu wa chuo kikuu wewe, shenzi wa tabia” Mzee Chiziza alikifunga rasmi kikao kile kibabe huku akisimama na kuanza kuelekea chumbani kwake akimwacha Clifford akiwa ametumbua macho yake, nusu akiwa haamini kilichotokea, na nusu akiwa anamtukana baba ake mzazi kimoyomoyo kwa ule ukorofi wake usio na msingi.

***

Alijiondokea akiwa ameinamisha kichwa chake chini. Hakuwa na mahapa popote pa kuirudisha furaha yake iliyofifishwa na Mzee Chiziza zaidi ya kwa Nunu. Huko alipokelewa na kukalishwa kwenye kochi safi lililokuwa likimtosha peke yake.


Akavuliwa nguo zote na kukandwa hapa na pale huku akiulizwa juu ya kilichomnyong’onyeza. Akajikuta akibwabwaja yote huku akimtupia lawama baba yake kwa ule ukali usio na mfano.

Akabembelezwa na kuwekwa sawa. Akafanyiwa na uhasibu mwingine ambao hakuwahi kuusoma katika kitabu chochote. Nguo zake zote zikafunguliwa akaunti na kuwekwa huko kwa muda. Mguu huu ukatolewa huku na kupelekwa kule, huku mkono huu nao ukafunguka upande mmoja na kujifunga upande mwingine. Akili yake ikawekwa sawa na ndani ya dakika arubaini, hakuwa anakumbuka kuwa kuna Mzee laghai na tapeli aliyekuwa anaitwa Chiziza.

Alimwona tapeli aliyekubuhu aliyekuwa anataka kumpokonya Nunu wake. Akajiapiza kuwa hangeruhusu tapeli yule wa kizazi kipya awaingilie.

Asichokijua ni kuwa, tayari kisu kilikuwa kikikata nyama yake laini na muda sio mrefu kingekutana na mfupa! Angejua kinachomkabili mbele, angempa Mzee Chiziza tuzo ya utakatifu.

Lakini ambacho macho ya kawaida kabisa yangeona waziwazi, ama pua kunusa, au hata sikio kusikia, kwa Clifford kingekuwa ni kitu cha kusadikika kisichokuwepo popote chini ya mbingu.

_Akazidi kujificha chini ya mbawa chakavu za Nunu!!_
 
*SIMULIZI YA MAISHA: ZAWADI YA ADHABU*

*MTUNZI: TIMOTHY PETER MSUYA “KIRAKA”*

*Mawasiliano +255 763 305 605*

*Nimefundishwa kuwa…*
_Historia wanaandikiwa washindi tu! Hakuna historia yoyote ya waliowahi kushindwa. Daudi alipigana na Goliathi, akamshinda, na historia yake ikaandikwa kwa usahihi kuanzia Mwanzo mpaka mwisho. Hakuna anayeijua historia ya Goliathi kwa undani wake!! Hata mawazo yetu tunayopaswa kuyaenzi na kuyaandikia historia ni yale yenye harufu za ushindi tu. Tukipoteza muda kujenga juu ya mawazo ambayo yalishashindwa, huenda tukajikuta tunakuwa upande ulioosahaulika wa historia maisha yetu yote!_

*Una hiyari ya kukubali au kukataa….*

*NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU YA NNE*

_Chiziza nini bwana?_

Ndugu wa karibu wa Nunu walipatikana.
Akina dada wawili waliovutia mno kuwatazama, mama mmoja wa makamo aliyekuwa na lafudhi ya kisukuma, vijana wawili watatu waliokuwa wakibadilika badilika kutokana na mazingira pamoja na msururu mrefu wa marafiki zake wakatambulishwa kwa Clifford, ingawa kila mmoja kwa wakati wake. Huyu akaitwa dada, na huyu mama mdogo, huyu akaitwa ndugu wa yule dada wa siku ile, na huyu mtoto wa yule mama mdogo ambaye dada yake nilikuonesha siku ile.

Karata zikachangwa na kuchangika.

“Cliffie wangu… Huyu ni rafiki wa kaka yangu dear, kaka ambaye baada ya yule dada wa siku iiileee, anafuatia yule dada angu wa siku ile usiku pale Posta, halafu sasa kuna dada yuko Zanzibar, yeye na huyu kaka mama yao ni mmoja ila baba tofauti” Alitambulisha Nunu siku moja wakiwa kwenye matembezi.
Alichoambulia Clifford hapo lilikuwa ni maneno mawili tu…

“Dada” na “Zanzibar” tu, naye akajikuta amesharopoka.

“Oooooh.. Zanzibar… Dada yangu wa kwanza naye yuko Zanzibar, anaitwa Claritha” Alisema huku tayari mkono wa Nunu wenye kucha ndefu za kubandika ukiwa unazihesabu kwa umakini mkubwa pingili za uti wa mgongo wa Clifford aliyeishia kutabasamu kama katuni za Mickey Mouse. Mjadala wa kaka rafiki wa dada na dada ambaye dada ake ni ndugu na kaka yake na dada mkubwa wa Zanzibar ukawa umefikia ukingoni.

Hivyo tu yani!!!

Clifford angehitaji ndugu gani tena wa kumzuia kumvisha pete ya uchumba Nunu? Aliowafahamu walitosha kabisa. Hao wengine kama wazazi wangejulikana taratibu wakati wa michakato ya mahari, ndoa na wengine angewatambua baadae kabisa watakapokuja kusalimia watoto atakaowazaa yeye na Nunu wake. Hivyo ndivyo alivyofundishwa na Nunu kila siku. Kwanza hata yeye Clifford, hakuwa na ndugu wa maana ambao walikuwa anawatambua. Alimfahamu baba na mama yake, dada yake na watoto wa dada yake, kisha ndugu wengine kadhaa wa mama yao… Kwa upande wa baba, aliwafahamu wachache ambao walikuwa wakiwatembelea pale nyumbani…

_“Tena yule gaidi akiniuliza next time nitamuuliza ni ndugu zake alikuwa anawafahamu wakati anaoa, au ni ndugu wa mama wangapi anawafahamu, anitajie na majina kabisa, asilete ubabe wa kizamani hapa”_ Alijisemea siku moja alipokuwa akitoka ofisini kuelekea kwa sonara mmoja maarufu aliyekuwa amempa kazi ya kumtengenezea pete ya uchumba. Mipango yote alikuwa ameiweka tayari kwaajili ya kumvisha Nunu wake pete ya uchumba.
Mwezi mmoja kabla ya siku hii maalumu ya kumrasimisha Nunu kuwa mchumba wake na kisha kupuliza kipenga cha ndoa ilimkuta akiwa ameshakamilisha maandalizi yote muhimu kwaajili ya shughuli ile. Baadhi tu ya marafiki zake ndio aliwapa taarifa huku akiwa amejipanga vilivyo kumkabidhi mpenzi wake yule zawadi kemkem.

Alishakamilisha manunuzi na makabidhiano ya nyumba maalumu aliyoamua kumnunulia mpenzi wake kama zawadi ya uchumba. Hakukuwa na hitaji lolote la kuhesabu fedha alizokuwa ameshazitoa kwaajili ya Nunu, wala hakukuwa na haja ya kuikagua kadi ya gari jipya ambalo sasa lilikuwa mali halali ya Nunu ingawa ni yeye aliyekuwa mnunuzi.
Clifford alishapenda, na kama ungemuuliza kusudi la maisha yake, hangesita kukwambia kuwa, aliishi kumpenda Nunu!

Hakujua kuwa kunguru si wa kumfuga, na kwamba ipo siku angelikimbia jiji la Dar es Salaam mchana kweupe watu wakiendelea na shughuli zao.

***

Jumamosi ilianza kwa utulivu kabisa.

Orodha ndefu ya nyimbo zilizowekwa kwenye mfumo wa muziki ikiendelea kuyakata mawimbi ya chumba kile kwa sauti ya chini kabisa isiyoleta aina yoyote ya bugudha. Nunu alikuwa wa kwanza kuamka na tayari staftahi nzito ilikuwa imeshaweka mezani ikimngoja “baba yake” mwingine aje ajipendelee. Clifford alipoamka, huduma zote zilikuwa pembeni ya kitanda.

Kwanza, alikutana na Nunu akiwa ameshika bakuli kubwa lenye maji pamoja mswaki wenye dawa ya meno ambao hata hivyo hakuruhusiwa kuushika. Akasaidiwa kupiga mswaki palepale huku Nunu akikisafisha kinywa kile kwa ufasaha mkubwa utadhani chakwake. Kisha kitambaa chenye uzito wa taulo dogo kilichomo kwenye maji ya moto kiasi kikatumika kusafisha uso wote kwa umakini, kisha akalazwa katika kochi maalumu lililokuwepo pale chumbani, akafutwa mwili mzima kwa kitambaa safi na sabuni maalumu. Akapakwa na vijimafuta ambavyo hata hakuelewa viliitwaje.

Aliyekwambia eti kuoga ni mpaka maji meeengi kama ya mto yakumwagikie ni nani? Acha ushamba wewe, kamuulize Clifford!!

Akajihisi msafi kuliko alivyowahi kujihisi hata alipooga masaa mawili mfululizo.
Alitakata mwili na roho!!

Mengine yote yakaenda kama yalivyopangwa. Chai ikanyweka na vimichezo vya hapa na pale vikiendelea huku Mhadhiri yule wa chuo kikuu akiwa mwanafunzi wa chekechea akifundishwa namna ya kujificha na kujifichua, namna ya kuchuchumaa na kurukaruka na vingine vingi. Mara akavalishwa jinsi ya kuvaa brazia, akasimama kwenye kioo na kujicheka.. Wakacheka pamoja na kukumbatiana. Mara akajaribu kuvaa nguo za ndani za Nunu, zilipofika mapajani zikagoma..

Wakacheka tena..

Ungewaona ukiwa mbali, usingekawia kuhisi kuwa ni watu wazima wenye mtindio wa ubongo au aina nyingine ya wendawazimu mkubwa. Lakini kwao, yalikuwa mapenzi na tenzi zake!!

Muda sio mrefu, wakajichafua tena makusudi, kisha wakaoga.

Wakacheka na kufinyana kitoto!!

Tukio zima la kuvishana pete lilipangwa lifanyike kuanzia majira ya saa tatu usiku katika ufukwe wa Mbalamwezi. Maandalizi yote yalikuwa chini ya marafiki wateule wachache wa Clifford ambao mpaka inafika saa kumi jioni, walikuwa wameshakamilisha kila kitu. Vyakula maalumu viliandaliwa pamoja na vinywaji, huku shamra shamra zikitarajiwa kuwa chache tu lakini zenye kuvutia sana!

Jambo moja ambalo alikuwa akimpendea mpenzi wake yule ni kuwa, ilikuwa ni nadra sana kwake Nunu kukubali kwenda kulala nyumbani kwa Clifford huku mara zote akisisitiza kuwa, mtoto wa kile kuonekana mara kwa mara nyumbani kwa mwanaume kutaondoa ladha ya kuingia rasmi akiwa mama mwenye nyumba na mke wa ndoa. Alishauri kuwa kule kwake Makongo yaendelee kuwa makutano kwa kuwa watakapooana, makazi yale yatakuwa yamevunjwa rasmi na hakuna kitakachoharibika.

Hata wewe ungekuwa ni Clifford, hapo ungekataa kwa misingi gani? Labda uwe kiburi tu!! Clifford mtoto wa watu hakuwa ana kiburi!!

Majira ya saa saba mchana, Clifford aliondoka nyumbani kwa Nunu na kwenda kujiandaa. Walikubalina na mpenzi wake kuwa, itakapofika majira ya saa moja kamili, watakutana Mlimani City kupata walau chai ya jioni na kisha kuna pahala angependa asindikizwe, na Nunu akakubali bila kusita. Wakakubaliana na aina ya mavazi ya kuvaa huku gauni alilolileta Clifford wiki moja kabla likichaguliwa. Wakaagana kila mmoja akiwa na lake kichwani.

Mmoja aliwaza kujenga…
Mwingine akawaza kubomoa na kuharibu…

Saa moja kasoro dakika ishirini ilimkuta Clifford akiwa nyuma ya usukani akiegesha gari lake katika maegesho ya magari ya Mlimani City. Alishuka na kujipapasa mfukoni, akachomoa poshi yake na kuhesabu kilichokuwepo. Hakuridhika nacho. Akazama katika mfuko wa suruali safi ya rangi ya kijivu aliyokuwa ameivaa. Akaibuka na kibunda cha pesa. Akakihesabu kwa haraka. Laki na themanini.

_Akasonya kwa dharau!!_

Haikutosha kwa siku muhimu kama ile. Vipi kama angepata wageni zaidi?

Akazama kwenye koti la kijivu lililoendana sawia kabisa na suruali yake. Huko akaambulia kitambaa tu. Akasonya tena huku akishuka na kuiweka sawa suti yake. Haraka akapiga hatua na kuifikia mashine ya ATM ya mojawapo kati ya benki aliyokuwa anaitumia. Akaizamisha kadi yake na kuiamuru mashine ile imsikilize kila alichokuwa anakitaka. Ikamsikiliza na akakipata. Makaratasi yenye rangi nyekundu yakaanza kupuputika baada ya mlio uliokera masikio yake kwa sekunde moja au mbili. Yakatoka, yakatoka tena, yakaendelea kutoka. Aliyekuwa anangoja kwenye foleni akalazimika kungoja sana.

Yakatoka.. Kisha…

Kimya!

Kadi yake ikafyatuka na kumchungulia ikiwa imechoka na kuonekana kuanza kupauka ndani ya muda mfupi.
Hakujali. Akatabasamu. Akaichukua na kuiweka mfukoni. Akayakusanya makaratasi yale kana kwamba si chochote cha maana kwa muda ule ukilinganisha na kilichokuwa mbele yake. Hakuyahesabu. Akayafutika kwenye mfuko wake wa koti kwa upande wa kushoto na kuanza kupiga hatua. Huku nyuma, mashine ile ikamkumbusha kuwa ilikuwa na utaratibu wa kuwapa risiti wateja wake. Hakuijali, akaipuuza na kuiacha ikining’inia pale juu kwa fedheha kubwa.

Yanini sasa makaratasi wakati tayari ana hela? Mchumi na muhasibu makini anayewafundisha wengine kanuni za kifedha akajikuta akiwashangaa wataalamu waliokuja na utaratibu wa kuwapa wateja wao karatasi eti wakiziita risiti baada ya kuchukua pesa.

Wapumbavu tu, pesa ndio muhimu katika usiku huu maalumu!

Alirejea garini na kujifungia huku akiruhusu hewa safi iendelee kutembea mule garini kwa kufungua kidogo madirisha. Hakutaka kuonekana na wanafunzi wake ambao walipendelea kuwepo maeneo yale hasa siku za mwisho wa wiki, au watu wengine wowote aliofahamiana nao. Ile haikuwa siku yake na mtu mwingine yeyote isipokuwa Nunu na marafiki kadhaa.

_Waniache mie!!_

Akiwa katikati ya mawazo simu yake ikapata uhai. Alipotazama kioo cha simu, akakutana na jambo ambalo alilitegemea ingawa hakutaka litokee.

*“Captain Chiziza”* Jina lilisomeka.

Hakuwahi kuacha kupokea simu ya baba yake bila sababu ya muhimu. Na jioni hii aliamua asiipokee. Ndio, alikuwa na sababu maalimu! Mzee huyu alitaka kuitumbulia nyongo furaha yote aliyokuwa nayo siku ile. Mzee huyu lazima angekuja na hotuba ndefu kwa kuwa alihisi tayari alishapata taarifa za yeye kuviisha mtu pete.
Dunia ndogo na walimwengu hawana kifua. Mzee yule angeweza kumwita nyumbani muda ule ule kisha aanze kumchezesha “kinyuki chapenyapenya” kwa hotuba zake ndefu zenye maneno ya kejeli. Hakutaka kuipokea. Akaamua kuikata, lakini kabla hata hajaikata, iliacha kuita. Akashusha pumzi kwa nguvu na kujilaza tena kitini akiendelea kuwaza.

Kabla hata akili yake haijakaa sawa, ujumbe ukaingia na haraka akausoma akijua kuwa, ni Nunu aliyekuwa ameutuma. Jina lilelile alilolisoma katika kioo cha simu dakika chache nyuma likazikaribisha mboni zake katika ujumbe mfupi wa meneno.

*“Wala sikutaka upokee baradhuli weee, na kwa kuchelewa kwako tu kupokea unanithibitishia kuwa, niliyosikia kuwa unavisha mtu pete ya uchumba ni kweli. Ningekuwa na nafasi ya kukwambia ‘Ole wako’ ningefanya hivyo, lakini kwakuwa sina, nakukumbusha tu kuwa, ‘Kunya kuna staili moja, sasa wewe endelea kujitia unaweka mbwembwe na manjonjo”.*

Kudadadeki!!

Clifford alikereka. Akamtukana Mzee yule tusi jepesi na kisha akaachana kabisa na habari zake. “Wazee kuna saa inabidi tuwahurumie tu, hata biblia inasema hilo. Yule mzee anahitaji msaada wa kisaikolojia yule”
Jalada la Chiziza likatupwa kando jioni ile.

Saa moja na nusu ilifika.

Nunu hakuonekana.

Hakuhangaika kumpigia simu, akajipa muda zaidi. Saa mbili kamili. Ama! Hapo sasa akatoa simu na kumpigia Mpenzi wake. Akampata. Baada ya salamu za hapa na pale, Nunu akajitetea kuwa amepata dharura na amekwenda Kigamboni kumwona mama yake mdogo kwa kuwa alikuwa akiumwa sana, na kuwa atarudi muda sio mrefu.
Clifford moyo ukampaa.

Alihoji maswali yote ambayo yeyote angehoji. Mama mdogo yupi? Kigamboni sehemu gani? Mbona hukuniambia? Umeenda sangapi? Anaumwa nini? Nani alikwambia? Kwanini? Kwanini? Ni vipi? Na mengine meengi, lakini yote hayo, Nunu aliyajibu kwa ufasaha mkubwa bila kuumauma midomo. Mwalimu wa chuo kikuu aliyekuwa akifelisha wale wote ambao hawako makini kutoa majibu yanayoridhisha kwenye mitihani yake akatoa maksi tisini na nane kwa mwanafunzi Nunu.

_Eee, ndio maana yake.. 98%!!!_

Akatangulia Mbalamwezi huku akithibitishiwa kuwa, ndani ya saa moja Nunu angeungana naye. Akiwa na matumaini tele, akaelekea Mbalamwezi huku njia nzima akiliwazwa na wimbo mtamu alioupenda wa Don Williams uitwao “Love is on the roll”..

_Mapenzi yako kwenye mwendo.._

Saa tatu kasoro dakika tatu akawa ameungana na wenzake. Wakajadiliana hili na lile huku vyakula na vinywaji vikiendelea kunyanyasika. Akamwita mkuu wa sakafu na kuteta naye, akamweleza mabadiliko ya mpango na kuwa Nunu atakapofika shughuli ndio iende kama walivyopanga, na kwa muda ule, maisha magumu yaendelee kunyanyaswa, kuzomewa, kusutwa na kutukanwa!!

Hakuna msamiati uitwao maisha magumu hapa!!

Wa maji walikunywa maji, wakaanza kubadilika rangi kuwa weupe. Wa bia walizigida mpaka wakaanza kushindana kwa kutoa kauli za kimombo. Wale wapenda kula waliyatanua mashavu na matumbo yao kwa soseji, sambusa, kuku na mishkaki ya samaki, wakashushia na mboga za majani na vipande vya matunda. Wakusakata rumba walilisakata mpaka viuno vikaanza kutepeta, lakini si Nunu wala picha yake aliyetokea!

Maisha magumu yakaanza kumnyanyasa Clifford..

Saa sita kasoro ikawakuta wale wapenda pombe wakiwa hoi taabani huku wale wengine waliojidai mabingwa wa pombe kali wakiwa wameshajiondokea kitambo huku wakiacha baadhi ya vitu vyao pale pasipo na uelewa. Clifford koti lilikuwa mezani na kitambaa cha jasho mkononi. Nunu hakuwa anapatikana kwenye simu wala kwenye mtandao wowote wa kijamii!
Ni kama vile Nunu alikuwa ametoweka katika uso wa dunia!!

Clifford akaaga akiwa amepandwa na hasira na kuelekea nyumbani kwa Nunu ili kujua ni nini kilichompata. Donge zito lilikuwa limemkaa kooni. Akafanya malipo yote yaliyokuwa yakihitajika huku fedheha kubwa ikiwa imemjaa usoni. Zile fedha alizokuwa nazo mfukoni alitamani awaite wote waliokuwa mbele yake awagawie ili tu wakamlete Nunu wake. Alipoingia garini, zawadi alizomnunulia Nunu zilizokuwa kwenye kiti cha nyuma zikamkodolea macho kama vile zinamuuliza; _“kulikoni, mbona hujatufikisha tunapokwenda?”_

Alizitazama kwa hasira, akazisonya na kuzitukana kwa tusi zito la nguoni..
Akaridhika kidogo…

Safari ya Makongo kwa Nunu ikaanza.

Laiti angelikuwa na pua ya kunusa ya kesho, angejiunga na wale walevi pale ili japo alewe ingawa haikuwa tabia yake, kisha aende akalale nyumbani kwake hadi asubuhi ndipo aanze kuhangaikia habari za Nunu.


Lakini pua haikunusa, jicho halikuona, ingawa akili iliamuru mwili kwenda, na mwili ukatii. Ndani ya dakika arubaini, Gari ya Clifford ikaegeshwa mbele ya nyumba aliyokuwa anaishi Nunu, nyumba ambayo ni yeye aliyekuwa amempangishia na kuilipia kwa mwaka mzima, na kwa haraka akaanza harakati za kuingia ndani…

We Clifford wewe!!

Wewe!!!

Maskini!!!
 
*SIMULIZI YA MAISHA: ZAWADI YA ADHABU*

*MTUNZI: TIMOTHY PETER MSUYA “KIRAKA”*

*Mawasiliano +255 763 305 605*

*Nimefundishwa kuwa…*
_Waliosema kuwa hakuna ajuaye kesho wala hawakutumia akili kubwa kiiiivyo kulitambua hilo. Hata dakika tano tu zijazo hakuna azijuaye. Hili si la kujadili. Lakini, maisha ya baadae, ni mwendelezo wa maisha ya sasa. Kile ambacho unakiishi leo, utakapoenda kulala, unajiandaa tu kuamka nacho kesho na kuendelea kukiishi, mpaka utakapiamua vinginevyo. Na labda ni kutokana na ukweli huu, wenye busara wanajifunza kuitumia hali njema au mbaya wanayoijua sasa kuweza kujiandaa kwa hali ambayo hawaijui baadae au hata kesho._

*Una hiyari ya kukubali au kukataa….*

*NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU YA TANO*

_Alifika Makongo…_
Taa zote za nje pamoja na ile ya sebuleni zilikuwa zikiwaka. Hapo hofu iliyokuwa ikikatiza mara kwa mara katika kichwa cha Clifford yakayeyuka kwa kiasi kikubwa.

_“Atakuwa yuko salama tu”_ Alijisema huku akiufikia mlango na kuugonga mara mbili, kisha akakishika kitasa na kukikunja kwa kujiamini. Ile harufu tamu ya marashi aliyoachana nayo mchana wa siku iliyotangulia ikamfunika mwili mzima na kumpa msisimko wa ajabu. Ingawa alikuwa anainusa mara kwa mara, hakuweza kuizoea. Ilikuwa mpya kila mara. Hasira zake zote zikaanza kupotelea kusikojulikana lakini ile sifa yake ya kuwa Mwanaume ikampiga konzi na kumkumbusha..

_“Acha kuwa laini laini wewe, huyu mwanamke amekudhalilisha mbele ya rafiki zako, lazima umuulize maswali ya kipelelezi na kihasibu mpaka aseme kinagaubaga alipokuwa, na asiposema mpige chini haraka sana, hakufai!”_ Sauti nzito iliyosadifu sauti yake ilimnong’oneza sikioni.

Akaisikiliza na kuafiki huku akitikisa kichwa. Akaruhusu uso wake kujenga matuta kadhaa ya hasira. Akaikagua sebule ile. Hakuona kipya. Akashusha pumzi na kuelekea chumbani huku sauti ile ikiendelea kumtia moyo wa kisasi na hamu ya kujua ukweli wa lile lililotokea.

Mlango wa chumbani ulikuwa wazi pia, lakini taa ilikuwa imezimwa. Akausukuma kwa hasira na kuingia mzimamzima, kisha akawasha taa. Akasimama akiwa ameduwaa. Nunu alikuwa amejilaza kifudifudi kitandani huku akilia kwa kwikwi. Ule mzigo uliokuwa ukimchanganya Clifford kila siku ulikuwa umesitiriwa na kanga nyepesi na kufuli ambalo Clifford alionekana kulitambua, huku ukitikisika kwa nguvu kila mara mwanamke yule alipovuta kamasi kwa kilio.

Mwanaume chali!!

Clifford akanyong’onyea. Ile sauti sasa akaiona ni sauti ya usaliti. Zile hasira akaziona kuwa ni kutaka kumkosanisha na Nunu wake, Nunu ambaye sasa alikuwa akilia mwenyewe pale Kitandani. Akaitukana sauti ile kimoyomoyo na kuionya kuwa isirudie tena kumshauri ujinga!!.

Shabash!!

Anawezaje kuendelea kuuliza maswali ya ufahamu, ya kihasibu na kipelelezi wakati Nunu Analia? Amewezaje kumlaumu mpenzi wake njia nzima na kumbe mpenzi wake huyu alikuwa peke yake nyumbani akilia kwa kwikwi?
Clifford akajiona mkosaji. Akamwomba Mungu amsamehe na kumuahidi kuwa hatarudia tena. Akajiapiza kuwa, atakapokwenda tena kuungama kwa padre, atakumbuka kuungama dhambi ya kumuwazia mwenzake mabaya!
Akamsogelea Nunu wake pale kitandani na kumgeuza. Akakutana na ile sura nzuri ikiwa imekolewa na kilio.

“Pole mpenzi.. Nini tatizo mama? Mama mdogo ame… Amefariki? Aliuliza Clifford na hilo ndilo la kwanza lililomjia kichwani.

“Ha….. Hap…. Ha… Aaaaagh.. Hapan… Hapana baba… Huwez… Huwezi kuelewaaa… Nenda tu Cliff.. N…Nen.. Nenda” Nunu kilio kilikuwa sasa kinafikia kilele cha mafanikio yake. Alikuwa akilia haswa!

“Niende? Niende wapi Nu? Niende wapi mama yangu? Cameon, tell me what is not working.. Tell me what is not happening.. Nieleze” Maneno yalimtoka Clifford huku akihangaika kuilegeza tai yake na wakati huo huo akimweka Nunu sawa.

“Nen… Hu… Huwezi… Siwezi.. Ah.. Nu… Cliff nendaaaa…. Huwezi nielewa baby.. Huwezi…” Nunu alizidi kulia.
Kama Nunu alihisi kuwa kile alichokuwa anakiongea au kutaka kuongea kilikuwa kinaingia masikioni mwa Clifford basi alikuwa anajidanganya kwa kiwango kikubwa. Clifford alikuwa akijishughulisha na kupunguza nguo zake mwilini. Dakika mbili tu zilimtosha kumwacha akiwa kifua wazi na chini akiwa na boxer yake tu. Akampandisha vema Nunu kitandani na kumvutia kifuani pake.

Nunu naye hakusita!! Akajisogeza!!

Akalihisi vema joto lake la kike haswa huku akiyaacha yale machozi yatiririke juu ya kifua chake bila kuhangaika nayo. Ahangaike na machozi wakati Nunu wake yupo? Akamsugua taratibu mgongoni huku akitamani kumwimbia wimbo mzuri utakaomnyamazisha ili wazungumze. Nyimbo tamu hakuwa nazo, lakini maneno yakamjia. Elimu yake ya chuo kikuu na uzoefu wa kitaaluma ulimkumbusha kuwa ilikuwa ni vigumu kwa mtu kuzungumza akiwa na hasira, huzuni au akiwa analia. Akaliweka hilo katika vitendo.

Akaongea.. Akasema.. Akazungumza.. Akabembeleza…

Wewe, acheni bwana, kuna wakati hata pikipiki inaweza kutoa mlio wa Scania au buldoza!! Kuna mtu atasema eti kitaalamu hilo halipo…
Achana na wataalamu asee, nisikilize mimi asee!!!

Dakika thelathini zikamkuta Nunu akiwa anahema tu juu juu huku ile mito ya machozi ikiwa imekutana na ukame katika kifua cha Clifford na kukaukia humo. Alikuwa amenyamaza. Ukimya ule haukuwakumbusha kuwa walikuwa na la kujadili. Ukawakumbusha kuwa, wao walikuwa mume na mke watarajiwa, na kuwa haikuwa hatia yoyote kwao kushiriki yale ambayo walikuwa wakiyatarajia.

Hakuna aliyewaambia ‘anzeni sasa’!

Wakajikuta tu wakiwa katika kukurukakara zisizo na mshindi wala mshindani.. Kijasho kikiwa kinawachuruzika bila wao kujua. Kisha ghafla, kama vile dunia nzima iliamua kuwazomea, kishindo kikubwa kikasikika!

Baang!!

Mlango ukawa wazi!

Wazi kabisa!!!

Mwanaume mrefu mwenye sura iliyokosa matumaini ya kusifiwa kwa uzuri alisimama mbele yao akiwa na vijana ambao hesabu za haraka za Clifford zilitambua kuwa walikuwa wanne. Na hakukosea, yeye si mwalimu wa hesabu za kihasibu? Wote wakatawanyika mle chumbani kwa fujo na papara nyingi.

“Nyie.. Aargh! Weezii.. Ah, nyie vipi bana?” Aliropoka Clifford huku akihangaika kutafuta shuka ajisitiri. Mmoja wa wale walioingia akamsogelea na kumkamata vema mkono. Akamvuta na kumtandika ngumi safi chini kidogo ya sikio. Kuna baadhi ya kanuni za hesabu, kanuni za kisayansi pamoja na matukio mbalimbali ya kihistoria ambayo Clifford alivisoma akiwa kidato cha pili vikamjia kichwani na akavikumbuka kwa ufasaha wake kabisa!!

_Ile Archimedes Principle ilitiririka vema kichwani kwake!_

“Taratibu kijana.. Kama utakaa sawa na kukiweka vema kichwa chako, utagundua kuwa wewe ndio mwizi na unapaswa kutueleza udokozi wa wake za watu umeanza lini”. Kidume kile ambacho sasa kilikuwa kimesimama kwenye kona moja kule chumbani kilikoroma kwa upole huku kikimkazia macho Clifford.

Sura yake ilikuwa mbaya, lakini sauti yake ilikuwa mbaya kuliko ubaya wenyewe!!

Ama!! Wake za watu? Hawa jamaa vipi hawa??

Haraka akasimama akiwa anajiamini. Hakujali kuwa yu uchi, umbile lake likiwa limenywea na kubaki kuangalia chini kwa soni kubwa. Aliamua kupambana. Hawezi kumruhusu mtu acheze na hisia zake kwa Nunu kiasi kile.
“Jamani tafadhali.. Kama ni pesa semeni niwape, najua ninyi ni majambazi tu. Tafadhalini tuachieni uhuru na mke wangu.., please guys. Na hamjui tu mnaongea na mtu mkubwa kiasi gani hapa, huu mchezo…..” Aling’aka Clifford lakini hakuweza kumaliza.

“Hebu kaniletee maji ya kunywa Agatha” Lile pandikizi la mtu likatamka huku likimgeukia Nunu. Ajabu hii!! Tayari Nunu alikuwa amejisitiri kwa upande wa kanga na machozi yalikuwa yakimtoka bila utaratibu.

“Agatha?? Ndio nini wewe? Ah.. We Bwege vipi? Ni nini hiki mnanifanyia ninyi? Mchezo ga…..” Alijaribu kulalamika Clifford.

“Mchezo?? Yani unakuja kwangu, unakaribishwa ndani. Unaparamia kitanda change. Hata muda wa kutazama ukutani kujua umeingia nyumba yenye picha za mwanaume mwenzako hutaki, unaishia kuangalia makalio ya mke wangu tu na kuyashika shika. Halafu nakuja kukufumania kisha unauita huu mchezo? Sasa hapo mchezaji ni nani, mimi au wewe?” Jitu lile lilisema huku likisogea karibu na Clifford. Kofi zito likakutana na kisogo kisichozoea shuruba cha Clifford.

Akarudia kuwahesabu wale waliokuwepo chumbani kule.

Inawezekana mwanzo alikuwa amekosea. Walikuwa nane sasa!

Akarudia tena kuwahesabu…

Walikuwa sita!! Eeeeh.. Hapana.., sio sita…

Tisa!!

Hesabu za kujumlisha na kutoa zilikuwa zimegoma kabisa!

Kama vile aliyepewa ishara, kijana mmojawapo akachupa na kubembea katika uume wa Clifford.. Loh!! Dunia nzima ilikuwa inamjia machoni.. Akaziona sayari zote kwa ukubwa wake sahihi.. Akazihesabu kwa haraka haraka.. Wanasayansi walikuwa wanadanganya kwa kusema ziko tisa. Zilikuwa kumi na mbili huku zikiwa zinagongana gongana kwa fujo..

Akamwachia na kumkandamiza ngumi ya tumbo iliyokuwa na lengo la kumtapisha vyote alivyokula siku ile. Ilikuwa ni bahati tu kuwa hakuwa amekula chochote jioni ile. Akaishia kutema hewa iliyoambatana na damu.

Ndani ya nusu saa, hakuna rangi ambayo Clifford hakuwa ameacha kuiona. Nunu alikuwa amekiri mbele ya wote waliokuwepo mule chumbani kuwa alimweleza Clifford kuwa yeye ni mke wa mtu lakini wakakubaliana kufanya kwa siri, na katikati ya kilio akaomba msamaha kwa “mumewe yule”. Clifford alipotaka kuja juu akaonyeshwa vyeti halisi vya ndoa. Ndoa ya kikatoliki baina ya AGATHA MBISE na MARTIN BAZU. Bado haikumuingia akilini. Akajitahidi kukurupuka hadi sebuleni. Huko sasa akajua idadi kamili ya nguvu kazi ile.

Wanaume watano walioshiba vema walimweka mtu kati na wakamsaga kwelikweli. Jicho moja ndilo pekee lililoachiwa nafasi ya kuona, huku lile lingine likitiwa uvimbe kwa makusudi bila sababu yoyote ya msingi. Akiwa karibu na kupoteza fahamu, macho yake yakatua katika pembe mojawapo mule sebuleni. Ilikuwepo picha moja kubwa ya wana ndoa wawili waliokuwa na mavazi yao rasmi ya harusi.

Nunu ndiye aliyekuwa bibi harusi na yule bazazi mwenye sura mbaya aliyekuwa akimchachafya kwa ngumi nzitonzito akiwa bwana harusi. Alipoiweka sawa sasa shingo yake, juu ya kabati ambalo alitengeneza kwa gharama zake mwenyewe na kumwekea mpenzi wake Nunu kulikuwa na picha nyingine kubwa ambapo mwanaume yule alikuwa amesimama peke yake akiwa na mavazi nadhifu ya kijeshi.

Picha hizi hazikuwepo wakati anaingia pale.. Na hazikuwahi kuwepo kabisa!!

Fahamu zikaondoka bila kusubiri walau mazungumzo mafupi na bosi wake!

Akazimia!!!

***

Hakukumbuka alitumia muda gani akiwa mbali na fahamu zake. Hakujua ilikuwa bado ni jumapili au vinginevyo. Hakukuwa na chochote mwilini mwake kilichokuwa kinamsikiliza hata kidogo. Alipotaka kunyanyia mkono, aliishia kuchora chini bila kujua alichofanya. Alipotaka kufumbua macho, yaligoma makusudi! Akajitutumua ili ateme mate walau kusafisha kichwa.. Yote yakaishia kidevuni. Lakini kwa mbali akahisi kuwa ubongo wake bado ulikuwa ukifanya kazi. Akaujaribu..

_“Revenues are recognized when… When… Argh.. Wheeeeen….”_

Hamna kitu!! Hata akili ya Clifford ilikuwa imeyumba vibaya mno. Hakuwa anakumbuka chochote. Hata angepewa mwanafunzi wa chekechea wakati huo, angeishia kumwambia moja na moja jibu nane!! Kiza kikaendelea kujenga urafiki na macho yake.

Alipokuja kushtuka tena, alihisi kwa mbali sasa akipata afueni kidogo. Aliweza kufumbua macho yake yaliyokuwa yamevimba. Hakupatambua alipokuwa lakini sura ngumu ya Martin Bazu ilikuwa imemkodolea macho.

“Umeamka mhadhiri wa wake za watu?” Alimsemesha Bazu huku akimshika kidevu na kumvuta karibu. Akamcharaza kofi, la haja. Kuna hali ilimjia Clifford kwa wakati mmoja.. Alihisi kucheka na kulia, akabaki ameegesha uso katikati ya tabasamu na kilio. Akagumia kwa maumivu. “Mbona sasa mke wangu hujamfundisha zaidi namna ya kupangilia mambo yenu ya uhasibu sijui uchumi na badala yake nimekukamata kirahisi tu panyabuku wewe?”

“Mkuu… Basi yam.. Yameisha kaka…Nimekos.. Nimekosa mimi, nimekosa… Kama.. kama… kama mmeamua kunifanyia uhuni kiasi hiki sawa tu, nakubali yaishe. Niachieni roho yangu nikaanze maisha yangu na Nun…, I mean.. Ah… Maisha yangu kivyangu.. Peke yangu” Alisema Clifford kwa sauti uliyokata tamaa.

“Mbona hueleweki sasa.. Yani bado unahisihisi kuwa tumekufanyia uhuni? Kwanini usithibitishe kwanza?” Cheko baya lilimtoka Bazu.

Akili ikamkaa sawa Clifford. Hapo sasa ndipo akagundua kuwa pamoja na maumivu makali aliyokuwa nayo mwilini, kuna jambo lisilo la kawaida lilikuwa limemtokea. Akataka akae vema kwa kuwa hakuwa amefungwa popote. Zoezi likaishia katikati. Alikuwa na maumivu makali sehemu zake zote za siri.

“Aaah.. Yan… yani… Yani mme…. Aaah.. Yani mmenilawiti kweli?” Clifford alisema huku uchungu mkubwa ukimtambaa kooni hadi kwenye tumbo. Kichefuchefu kikali kikamkata! Hakuwa na cha kutapika, akaishia kukodoa!

“Sio kukulawiti tu, na ushahidi tumeweka. Kama unafikiri kutembea na mke wa mtu ni jambo jepesi jepesi tu, basi sasa umeingia pabaya dogo. Na ukitoka hapa nataka niwe nimehakikisha hauna kabisa hicho kilichokufanya uitwe Clifford” Alikoroma Bazu huku yale macho yake makavu yakiwa yamemwelekea Clifford. Bila kuambiwa na mtu, Clifford akashusha mikono yake kufunika sehemu zake za siri. Bazu na wengine wakacheka, na hapo ndipo Clifford akajua kuwa kulikuwa na zaidi ya watu wawili mule ndani.

Itoshe tu kusema, Clifford hakuwahi kupitia wakati mgumu katika maisha yake kiasi kile. Mijitu ile ilimwachia baada ya kupukutisha zaidi ya milioni thelathini zilizokuwepo katika akaunti yake ya benki. Kwa mkono wake mwenyewe, alipelekwa benki na kujaza fomu za kutoa pesa, akapewa na kuwakabidhi.

Alitishwa!!

Aliambiwa kuwa, ikitokea akaleta usumbufu wowote ule, picha zile chafu zingekuwa ni mabango ya matangazo ya mtandao mmoja maarufu wa simu Tanzania nzima. Kuongeza mkwara, kidume kile kikatoa kabisa na kitambulisho kilichoonesha kuwa, alikuwa mtu mkubwa sana wa usalama wa taifa. Clifford akanywea.. Hapa na pale, bazazi lile likapokea simu huku na kule huku kila mara likiongelea kuhusu “kuua”, “kutesa”, “serikali”, “usalama”, “gerezani” na mada nyingine za kutishia tishia tu!!

Picha zake akishiriki michezo michafu ya kuingiliwa kinyume na maumbile zilimuweka pabaya zaidi. Hakuwa na nguvu ya kudai chochote kwa Nunu. Yote, hata gari lake, simu zake na vingine vilibaki kwa Nunu. Angemfwata nani amwambie kilichomtokea? Angeweza vipi kuificha aibu ile? Akaamua kufa kiume. Lakini mibazazi ile haikumuachia.
Kila siku ilikuja na maombi mapya. Mara tunataka milioni mbili, mara laki tano, mara kuna dada tunataka umfaulishe mitihani, mara kuna mkopo tunataka utudhamini na mengine mengi.

Alipojitutumua kudai uhuru, akakumbushwa juu ya picha zake chafu. Akajikuta akingia katika mtihani wa maisha. Hata kazi sasa hazikuwa zinaenda tena! Clifford yule mtanashati akaanza kuingia katika madeni yasiyoeleweka huku maisha yake yakiishia katika hofu kubwa.

Bila kuambiwa na mtu, akaomba apumzika kazi mwenyewe!! Ingekuwa ni aibu ikiwa picha zake zingeanza kusambaa chuo kikuu cha Dar es Salaam huku naye akiwepo. Ni afadhali akimbie upesi!! Kibaya zaidi, Nunu yule aliyekuwa akimtambua kama mpenzi na mke mtarajiwa aliendelea kumpita barabarani akiwa hajali lolote.
Kibaya zaidi, siku ya siku ikaja ikiwa na picha zingine.

Picha za ajabu zaidi!!!

Katika picha hizi, Clifford mwenyewe, (au mtu mwingine aliyefanana sana naye) alikuwa akisimama akiwa amevaa suti nzuri, huku mkononi akiwa ameshika ua! Pembeni yake, dume la kizungu lililokuwa na umbo kubwa kama wacheza mieleka wa kimarekani lilikuwa limesimama likiwa limetabasamu. Hata mtoto mdogo angejua moja kwa moja kuwa, hawa walikuwa mke na mume!! Picha zingine kadhaa zikawaonesha watu walewale wakiwa uchi wa mnyama wakiwa katika mikao tofautitofauti.

Basi bwana, basi!! Sitaki tena!! Imetosha!!

Clifford alichoka, na moyoni, sauti yenye mamlaka ikamwambia tena kuwa, IMETOSHA!! Kimbilio pekee lilikuwa kwa mwanaume mmoja tu aliyemuamini kuwa ni mbabe kuliko wote duniani…

Mwanaume ambaye huko nyuma hakuwa akimwelewa hata kidogo!!

Gaidi Captain Chiziza!

“Potelea mbali.. Najua ataniadhibu.. Au atanitukana. Au ataniambia “Nilikuonya”, lakini sijali.. Hayo si zaidi ya adhabu wanazonipa hawa nyamaume!” Alijisemea huku akilisogelea geti la nyumbani kwao, nyumba ambayo hakuwa amefika toka alipotoka siku alipolumbana na baba yake juu ya yeye kupata mchumba.

Haikuwa rahisi hata kidogo kuuelezea upuuzi ule kwa Mzee Chiziza. Ilimtumia Clifford zaidi ya masaa matatu kujieleza kwa kina huku mara kwa mara akikabiliana na maswali yasiyo na majibu kutoka kwa baba yake. Hapa na pale, ilibaki kidogo mzee yule amtandike ngumi hasa pale alipokuwa akimweleza kuwa alimpenda Nunu kwa dhati..

“Kupenda?? Kupenda?? Unajua nini kuhusu kupenda Malaya mvivu wewe usiyejifunza hata kwa Malaya wenzako? Unampenda mtu anakupangia Kiswahili kuhusu hata nduguze halafu unaniambia ulimpenda kwa dhati? Mjaa laana wewe..” Aling’aka Mzee Chiziza kabla ya kumruhusu Clifford kuendelea.

Walipojadili kwa kina, mwisho wakawa hawana namna. Tayari suruali ilikuwa magotini na suluhisho pekee lilikuwa ni kuchutama na kuirudisha kiunoni. Hapakuwa na mwafaka, lakini Clifford akaruhusiwa kwenda kupumzika.
Utu uzima dawa, na umwamba wa Chiziza ukaonekana!!

Haikupita hata wiki moja, ile hofu ikamtoka Clifford. Hakuna polisi ambaye alihusika, wala mwanajeshi. Jeshi la Chiziza peke yake lilituliza tufani. Ile mibazazi ikapotea katika uso wake asiione tena. Ni kama vile ilikuwa imefutika kwenye uso wa dunia!!! Nunu yeye hakupotea, lakini kila alipokutana na Clifford, alionesha hofu ya waziwazi, huku mwendo wake ukionekana kama vile una shida fulani. Ilisemekana tu kuwa kuna wachache waliwahi kuziona picha zile chafu za Clifford, lakini hakukuwa na madhara makubwa.

“Sasa bwana mdogo…We ujitie una moyo wa kupenda tena. Nije nisikie tena umejiingiza kwenye misukosuko ya kipumbavu. Hakyamungu utanishuhudia nikisimama kutoa ushahidi kuwa ulifumaniwa na kukuweka ndani mwenyewe kwa gharama zangu. Sitaki litoto la kuvunja heshima niliyoijenga kwa miaka mingi nchi hii… Clifford Chiziza, nakwambia tena, OLE WAKO!” Alijisema Mzee Chiziza huku akiwa hampi kabisa umakini Clifford.


Naam.. Maisha ya Clifford yakaanza upya. Hakutaka tena kukaa jijini Dar es Salaam. Alihisi kuwa, ipo siku ile mibazazi itarudi tena. Lakini pia, alihisi ipo siku angeweza tena kumsamehe Nunu na kurudiana naye, jambo ambalo hakutaka kabisa litokee… Akaamua kufanya maamuzi magumu. Kampuni akamwachia rafiki yake ili aendelee kuiendesha, huku akiwa na wazo la kufungua tawi popote atakapokuwepo ili kuiendeleza. Akaomba kazi upya. Alitaka kuwa mbali na nchi, lakini akahisi kuwa alihitaji kwanza kuwa karibu na Mzee Chiziza ili aendelee kusafisha sifa zake na jina lake. Mungu akamsaidia, akapata kazi ya mkataba kufundisha Tanzania Institute of Accounancy, tawi la Singida…

*

Hayo yote yalitokea miezi kumi na nne iliyopita.. Na sasa alikuwa ameufikia mlango wa chumba namba 116 alipokuwa akihitajika kwa kipindi cha _‘Cost and Management Accounting’_ mchana ule…


Kama alidhani yale ya Dar es Salaam yalitosha kumfunza adabu, hakuwa ametambua kuwa ya Singida yangemfanya kuwa mwanafunzi mdogo tu asiyeijua ‘aa’ wala ‘bee’..


Clifford Chiziza alikuwa katikati ya bahari yenye mkondo mmoja tu..


Bahari imsafirishayo kuelekea katika kisiwa cha majuto na Ardhi ya Majanga, kushiriki mashindano ambayo, iwe isiwe, ni lazima angeshinda. Alipaswa kushinda kwa kuwa hakuwa na wakushindana naye. Na kweli alishinda na kupewa zawadi..


_Zawadi ya adhabu…!!_


***
 
ZAWADI YA ADHABU
SEHEMU YA SITA

******
Nimefundishwa kuwa…
Hakuna kisichowezekana kabisa duniani.. Kule kukifikiria kit utu hata kisichokuwepo ni dalili kuwa kuna nafasi ya kukifanya kiwepo. Lakini, kuna gharama katika kile unachotaka kiwezekane. Ni pale tu tunapoogopa gharama za kuvifanya vitu viwezekane, au tunapozikwepa gharama hizi tunaanza kuzuia yale yanayowezekana kufanyika. Mfano, hata wewe unaweza kuwa mtu bora wa kuwaonyesha wengine njia ya kupita. Lakini ni wengi wamekusa njia kwa kuwa, mar azote umekuwa ukifikiria gharama utakazohitaji kufikia lengo lako.
Una hiyari ya kukubali au kukataa….
******
*** NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU YA SITA ***
“Good afternoon” Alisalimia darasa lenye wanafunzi 38 wa mwaka wa tatu na wa mwisho wa masomo yao yatakayowawezesha kupata shahada ya kwanza ya uhasibu. Wachache waliitikia kwa kusimama kwa kusitasita na kabla hata hawajafikia nusu ya kusimama, Clifford aliupunga mkono kuwaashiria wakae.
“Well well… CR I asked you to collect your papers from my office earlier. Hope that you did..” Aliongea huku akimsogelea kiongozi wa darasa ambaye mara moja aliitikia
“Yes sir”. Mwanafunzi mmoja ambaue tayari alikuwa akijishughulisha kuunganisha computer ya Clifford na projector ili kuanza kipindi alijibu.
“Hamjafanya vizuri sana kwenye test ya mwisho. Sijui ni wapi hapakueleweka vizuri. Nitajaribu kuwa na nafasi jumamosi hii ili kama kuna yeyote ambaye anahisi hakuelewa nionane naye. Next week tutaandaa Markup test kwa watakaohitaji. Otherwise leo tutaenda hatua moja mbele.. We’ll be talking on ‘Cost accumulation for inventory valuation and profit measurements’.
“Well then.. At the end of today’s session, you will be able to…..”
Ufundi ukaanza. Kurasa ziliendelea kupepea katika ubao maalumu ulionururishwa na mwanga wa kifaa kile maalumu kilichokuwa kikichukua maandishi kutoka katika computer huku hapa na pale Clifford akiendelea kuusulubu ubao mwingine wenye rangi nyeupe kwa kalamu maalumu ili kuelezea vema zaidi yale aliyokuwa anayaelezea kwa ufasaha mkubwa.
Mwanafunzi mmoja aliyekuwa amekaa katikati ya wengine alikuwa ametumbua macho kwa umakini, hapa na pale akiukunja na kukuna kichwa chake. Ni wazi kuwa alikuwa akijitahidi kusikiliza na kuelewa kile kilichokuwa kinafundishwa bila mafanikio. Clifford ni kama aliliona hilo na hapa na pale akawa anapunguza mwendo wa kufundisha na kurudia rudia baadhi ya vipengele. Darasa zima likawa limechangamka na ni wazi kuwa walikuwa wanaanza kuelewa kwa ufasaha kile kilichokuwa kinafundishwa.
“Now please… Can someone here differentiate a payroll and a labour cost accounting?” Aliuliza kwa utulivu Clifford huku akitabasamu kirafiki na kalamu yake akiiweka juu ya meza. Nusu ya darasa mikono ikawa juu.. Hakujali sana, akasimama akimtazama mwanafunzi yule aliyeonekana kujawa na hofu wakati wote.
“Neema… Can you?”
“Eeeh.. Sorry sir.. Can you repeat the question?”
“Neema.., Can you please, and kindly, tell the difference between payroll and labour cost accounting?” Aliuliza Clifford huku kwa mara nyingine tena akitabasamu, akijipindapinda mbele na nyuma kwa mbwembwe, wakati huu macho yake akiwa ameyakaza kwa Neema.
“N…. No.. Sir… I can’t”. Alijibu Neema kwa huzuni huku nusu ya macho ya wanafunzi wenzake yakiwa yamemwelekea.
Aibu iliyochanganyika na hofu vilimjaa.
“Well well… Lets try something different then… Can you briefly remind us all Material Recording Procedures in a well defined store?”
“Material recording what in a well defined what?” Alihoji Neema huku akianza kuonekana kutokwa na jasho kwa mbali. Zaidi ya nusu ya darasa wakacheka kwa nguvu. Hata Clifford naye alijikuta akicheka huku akitikisa kichwa. Hakuonekana kusikitika hata kidogo. Akarudisha kurasa nyuma na kukifikia kile alichokuwa amemuuliza Neema. Akarudia kukifundisha taratibu huku macho yake yote mawili yakiwa yamemuelekea Neema. Alitumia dakika ishirini akirudia rudia huku akitoa mifano mingi zaidi. Wengine wakaonekana kuchoka kwa kuelewa zaidi na hapa na pale wakawa wanajibu haraka hata kabla Clifford hajauliza.
Mpaka kipindi kinaisha, Neema aliweza kuyajibu maswali yale kwa ufasaha mkubwa huku akionekana kuchangamka zaidi ya alivyokuwa Mwanzo.
Kwa Clifford hii ilimpa moyo na akajikuta akiondoka darasani akiwa na hali nzuri zaidi. Alitamani sana anaowafundisha wamwelewe kwa kina, na hili alilitimiza kwa gharama yoyote ile.
Narudia hapa.. “Gharama yoyote ile”
***
Ilikuwa jumamosi ambayo walimu wengi waliitumia kupumzika na kufanya mambo yao nje ya chuoni, lakini haikuwa hivyo kwa Clifford Chiziza. Saa mbili kamili ilimkuta ofisini kwake akiwa anakabiliana na vitabu akijiandaa kuanza kuonana na wanafunzi wake wenye mahitaji muhimu na maalumu. Hakutaka amwache yeyote nyuma, hasa wale wa mwaka wa mwisho aliokuwa akiwafundishwa kwa namna ya kuwaandaa zaidi kuingia katika soko gumu la ajira.
Hamu hii iliongezeka kwa kuwa, ndio kwanza walikuwa wameingia mwaka wa tatu, na aliamini kuwa kama angewajenga vema Mwanzo kabisa mwa mwaka ule, huenda wangefanya vizuri na kusahihisha makosa yao yote ya nyuma.
Aliamua maisha yake apigane kufa na kupona kuandaa wasomi wa darasani na sio wahuni wanaosoma mtaani na kuwa waovu kama Nunu!!
Siku hii alikuwa na miadi na wanafunzi tisa ambao walijiandikisha siku moja iliyotangulia, huku wengine akiwatengea siku nyingine. Kama ilivyokubaliwa, saa tatu kamili walianza kuingia. Wapo walioingia wawili wawili na wengine mmoja mmoja. Mpaka kufikia majira ya saa saba, tayari alikuwa ameshaonana na wanafunzi nane ambao wote walitoka wakiwa na tabasamu huku wakiwa wamepewa kazi maalumu ya kufanya ambayo wangetakiwa kuikabidhi wiki iliyofuatia.
Kisha.. Saa saba na dakika kumi na nne, akaingia Neema.
Aliingia akiwa mnyonge na alionekana wazi kuwa na wasiwasi kama alivyokuwa wakati hajaelewa kule darasani.
“Good afternoon sir” Alisalimu huku akiangalia chini.
“’Afternoon Neema.. ‘Course you can sit down” Aliitikia Clifford. “Well.. Tell me Neema.. Muda mwingi unaonekana ukiwa na hofu sana.. Whats wrong with you?”
“Si…Sir… Sielewi. Yani najitahidi sana kuelewa lakini mara nyingi najikuta sikuelewi vizuri. Masomo ni magumu sana na baba hatanielewa nikifeli. Dady ni mkali sana, yani zile supplementary za last semester zilisababisha anipunguzie hadi kiasi cha matumizi. Anataka nifanye vizuri ili nisipoteze hela yake. Sijui nikifeli kama atanisamehe. Anaweza kunifukuza hata nyumbani kwake. Sidhani kama umewahi kukutana na mtu mkorofi kama baba yangu”. Neema aliongea huku akionekana wazi kulengwalengwa na machozi.
“Ungemjua Mzee Chiziza ungenyamaza we binti.. Ila kwa kuwa humjui endelea kufikiri baba yako ni mkorofi” Clifford alijisemea kichwani kwake huku uso wake ukiumba lile tabasamu lake tamu. Kidogo Neema akaonekana kuanza kuzoea kuwepo pale.
“Sikiliza Neema… Unafeli kila mara unapokubali kuwa kuna kufeli. Forget about your father.. This is between your books, your lecturers and you. Huu ni muda wako wa kujithibitishia mwenyewe kwanza kuwa, You will make it. Yani una maanisha kuwa baba yako akikubali kukupokea hata ukiwa failure ndio utakuwa na furaha?” Aliuliza Clifford akiwa amemtazama Neema.
“Hapana.. Sipendi kufeli” Alijibu Neema kwa sauti ya chini.
“There you are.. That is what will take you through.. Jiambie ‘sitaki kufeli’, tena jikumbushe kila mara. Baba awepo au asiwepo, kataa kufeli.. Akulipie ada au asikulipie, kataa kufeli.. Anza kukataa sasa hivi kabla hatujafanya chochote.. Mkatae ‘kufeli’ na mambo yake yote, na fahari zake zote” Clifford alisema huku akiachia tena lile tabasamu lake.
E bwana ee.. Neema alisimama wima, akakunja ngumi moja na kuipigapiga kwenye kiganja chake cha mkono..
“Nakataa kufeli.. Nasema sitaki kufeli, na sitafeli.. Nitafaulu. SITAKI KUFELI”
Shabash!!
Tabasamu likachanua kwenye nyuso zao. Kipindi kikaanza. Walianza tangu somo la kwanza alilofundisha Clifford siku ya kwanza ya muhula ule. Akampitisha taratibu kwenye barabara pana ya taaluma, huku akimpa na mifano kedekede ya hiki na kile, hapa na pale akamruhusu kuuliza maswali ya uelewa, akayajibu kwa majibu rahisi lakini yenye maana kubwa. Hapa wakaenda mbele, pale wakarudi nyuma. Sehemu fulani wakasimama kwa zaidi ya dakika ishirini, wakarudia tena na tena, hesabu ndogondogo za mara kwa mara zikawekwa sawa na maelezo magumu magumu yakatafutiwa lugha nyepesi..
Yakaeleweka!!
Ni kule kuzama kwa jua ndio kuliwakumbusha kuwa muda ulikuwa umekwenda sana. Clifford akatazama saa yake. Saa kumi na mbili kasoro dakika chache, hakuhangaika kuzihesabu. Si Neema wala yeye aliyeonekana kuchoka. Neema alifurahia somo na Clifford alifurahia kazi yake inayomlisha na kumvalisha.
Jembe jipya lilikuwa limepata mpini imara.
Mpaka wanaachana majira ya saa kumi na mbili na nusu, Neema alikuwa na tabasamu pana lililoashiria kiasi alivyoelewa somo. Wakaagana na Neema akaelekea hosteli alizokuwa akiishi mitaa ya Sabasaba na Clifford akipanda bajaji na kuelekea mitaa ya Mwenge, Karakana alipokuwa akiishi katika nyumba kubwa aliyopanga zaidi ya mwaka uliopita alipohamia tu Singida.
Alikuwa na Amani kwa kazi aliyoifanya siku ile.
***
Hali ya kimasomo ya Neema iliimarika. Alikuwa akishiriki kikamilifu kujibu maswali popote yalipoulizwa kwa ufasaha mkubwa. Alijitahidi kuwa karibu na Clifford kama wanafunzi wengine, na mara kwa mara, hakusita kumfuata ofisini na kumwomba amwelekeze kile ambacho kilikuwa kikimshinda. Kuna wakati akawa anafundishwa hata yale ambayo darasani Clifford angeweza kuyasahau. Hii ikajenga urafiki hata wa nje ya masomo baina yao.
Kwa Clifford hili halikuwa na tatizo. Alipokuwa chuo kikuu cha Dar es Salaam, mara kwa mara alikuwa na utaratibu wa hata kualikwa kwenye sherehe za kuzaliwa za wanafunzi wake, au kualikwa kupata chakula cha mchana au usiku. Hii haikumpunguzia umakini wake wa kazi na badala yake, akajijengea heshima zaidi kwa kuwa, wanafunzi wale hawakumwomba upendeleo wowote katika masomo yao, bali walizidi kumtumia vema kuelewa kile walichokuwa wakifundishwa.
Neema naye akawa miongoni mwa wanafunzi wa Clifford walioondokea kuwa marafiki zake wa karibu.
Waliposhindwa kuonana chuoni kwaajili ya kueleweshana jambo fulani, wakakutana hata katika mikahawa nje ya chuo, barabarani au pahala pengine popote ambapo wangeweza kutimiza kiu yao ya kitaaluma. Kiu ya mwanafunzi kusoma na mwalimu kufundisha.
Hamadi! Neema akafika hata nyumbani kwa Clifford.
Kitabu kikasomwa kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho.. Mwalimu akafundisha na mwanafunzi akafundishika.
Lakini sasa, vitabu karibu vyote walishavimaliza. Mtaala wa muhula ule uliisha ndani ya muda mfupi tu. Wakasoma na magazeti, yakaisha. Hekaya za Zee la Kale na za abunuwasi, zikamalizika. Wasome nini sasa?
Wakakosa cha kufundishana.
Wakaanza kufundishana yasiyo kwenye mtaala.
Kizaazaa kikazaliwa, na kikaanza kukua…
Kikakaa, kikatambaa na kisha kikasimama kwa miguu yake…
Ama kweli!!
******
 
ZAWADI YA ADHABU

SEHEMU YA SABA

******
Nimefundishwa kuwa…
Kama vile nywele ziotavyo pasipo sisi wenyewe kujua mwenendo wake, au kama vile tunavyoendelea kukua pasipo kuweza kuamua ni kasi gani tuitumie, ndivyo hivyo mawazo yetu yanavyokua. Ujinga mdogo unaoupalilia leo unaendelea kukua taratibu, bila wewe kujua ni kwa kiasi gani unaongezeka. Tabia mbovu halikadhalika, hata kama ni kwa kiasi kidogo, inaendelea kukua taratibu taratibu tu. Ipo siku, kama unavyoshangaa nywele zako kuwa ndefu, utagundua kuwa, ujinga au tabia mbovu ulivyokuwa unavipalilia vinakudai uvifanyie sherehe ya kutimiza miaka hamsini!!!
Una hiyari ya kukubali au kukataa….
******
*** NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU YA SABA ***
Walikutana.. Wakapendana!!
Wala haikuchukua muda mrefu baina ya Clifford na Neema kujenga ngome imara ya mapenzi baina yao. Walipendana kwa dhati na Clifford aliazimia kuwa, yule angekuwa mke wake wa ndoa. Lile doa ambalo liliingia katika maisha yake kwa mkono wa Nunu likaanza kufutika taratibu. Lakini sasa akaapa kuwa atakuwa makini. Alitaka kufuata taratibu zote za kitamaduni kumuoa Neema. Hakutaka tena kupumbazwa na jinamizi liitwalo ‘kupenda kwa dhati’.
Taalumua yake ya ualimu ikatumika kwa makini kabisa.
Kwanza, hakuwa kiherehere wa kumuhudumia Neema kwa kila kitu kama alivyodanganyika kwa Nunu. Alijibakiza kwa sehemu yake! Alikuwa mwalimu na msaada mkubwa aliopaswa kuutoa haukuwa fedha wala zawadi nyingine yoyote zaidi ya elimu. Wakaweka vikao, wakayaandika mapenzi yao katika karatasi na namna watakavyoyaficha ili yasije yakawaharibia machoni pa watu. Kila mmoja akapewa jukumu lake la kutimiza ili kulinda mapenzi yao.
Wakakaa macho…
Kila mmoja akiwa makini kabisa na mwenzake!!
Haikuwa ngumu kwa kuwa, pamoja na ule woga wake na aibu zake; aibu ambazo Clifford alizifananisha na zile za Nunu ingawa za Neema zilikuwa za dhati; Neema alikuwa msichana mwenye misimamo chanya na isiyotikisika. Mara kwa mara aliendelea kumzungumzia baba yake kuwa ni mtu mkorofi, na hii ikawa kete yake ya kujitunza vema. Alienda nyumbani kwa Clifford kwa machale sana, na popote alipokwenda, kwanza alitanguliza masomo na kisha mengine ndipo yakafuata.
“Utakapomaliza chuo.. Tutafanya mpango twende kwenu kwanza. Niwajue baadhi ya ndugu ingawa kwa kificho. Halafu sasa hapo nitakupeleka kwa Mzee mmoja anaitwa Chiziza. Unajisifia sana kuwa baba yako ni Mkali, ila kuna kiumbe kinaitwa Chiziza sina haja ya kuzisema sifa zake hapa. Utakapomuona ndipo wewe mwenyewe utathibitisha kuwa baba yako anaweza kuwa Malaika Mwema kabisa mbele ya Malaika mtoa roho aitwaye Chiziza” Clifford aliongea kwa utani akizichezea kucha za Neema baada ya kumaliza kumfundisha.
“Mh.. Karibu sana Kanda ya ziwa.. N’tafurahi ikiwa hilo litatimia. Mh! Sema watu watashangaa! Yani mwalimu kumuoa mwanafunzi wake???” Neema alisema kwa aibu..
“Kwani ubaya uko wapi? Tena ndio vizuri, tukizaa watoto nakuwa nawasimulia kuwa mama yenu alikuwa kilaza mimi ndio nikawa namfundisha” Alisema Clifford huku akianza kucheka..
“Cliff.. Cliff umeanza uchokozi.. Bwana mi staaaki.. Staki nakwambia, staaki.. Mi sio kilaza bwana, nilikuwa tu na hofu.. Na ukiwaambia mi nanuna” Alisema Neema huku akiigiza kununa. Uzuri wa binti yule wa kisukuma ukatutumka usoni pake! Akajidai kununa zaidi, lakini mikono iliyokuwa ikimfundisha muda mfupi uliopita ikawa ikimtambaa kila kona ya mwili wake.
Kule kununa kukabadilika, kukawa kuguna na kujipinduapindua kama joka lililoogeshwa mafuta ya taa. Kukuru kakara za hapa na pale zikaendelea. Vitabu vilivyowafanya wakajuana wakavisaliti, wakavisukuma kwa miguu mbali na upeo wa macho yao, navyo vikatii, hiki kikaangukia kule na kingine kikajificha chini ya uvungu kwa aibu. Hakukuwa na joto lolote lililowalazimu kupunguza nguo katika miili yao, lakini wakajikuta wakiwa uchi wa mnyama.
Mwalimu akawa mwalimu kweli, na mwanafunzi akabaki kukubali kila somo alilokuwa akifundishwa. Wakajikuta katika sakafu yenye marumaru zilizopoa kwa ubaridi mkali, lakini jasho likiwa limewaenea mwili mzima. Kwa dakika thelathini nzima hawakuwa kwenye dunia ya masomo ya kihasibu, bali pembezoni kabisa mwa dunia yenye raha na Amani isiyoeleweka.
Huyu alikaa vile na mwenzake akaiga na kukaa vilevile bila yeyote kuwafundisha chochote. Baada ya “kuzozana” kule, aibu ikawarudia. Walikuwa uchi huku wakitwetwa. Kama vile waliopeana ishara, wakaamka kwa haraka na kukimbilia chumbani huku maungo yao nyeti yakipata shida ya kuogelea katikati ya hewa iliyokuwa ikiwazomea.
Wakajikuta bafuni wakiwa wamekumbatiana huku maji yakiisalimu miili yao. Waliporidhika na usafi ule, wakarudi chumbani. Hakuna aliyemuangalia mwenzake machoni ingawa Clifford alijikaza na kujaribu kumtazama Neema. Naye alipotaka kufanya hivyo, wote wakaangalia pembeni kwa pamoja.
Penzi likatunga tenzi!, Neema akalala kwa Clifford kwa mara ya kwanza!
***
Ikawa usiku, ikawa alfajiri.
Wiki zikageuka Mwezi… Wa kwanza na wa pili, kisha wa tatu.
Neema akamaliza muhula wa kwanza wa mwaka wa tatu, na ilimpasa kwenda kwao kwa mapumziko mafupi ya mwezi mmoja. Lakini angeendaje amuache Clifford wake mwenyewe? Haikuwa rahisi. Walishaamua kupendana na kuwa pamoja muda wote, ingawa kwa usiri ambao si Clifford wala Neema aliyeusaliti. Uongo ukatungwa, Neema yuko field Singida.. Hakwenda kwao!!
Zulfa, mkufunzi mwenza wa Clifford waliyekuwa wakitumia ofisi moja alihisi jambo, lakini haraka upepo ukageuzwa kisomi. Yeye mwenyewe alikuwa ni miongoni kati ya wanawake waliotamani kuwa karibu na Clifford, tena ukaribu wa kimapenzi. Hapa na pale alimualika Clifford nyumbani kwake na yeye kumtembelea, mara nyingine nyakati za usiku na kujibaraguza baraguza kuwa alikuwa na mambo ya kitaaluma ya kujadili.
Taaluma gani ijadiliwe baina ya Mhadhiri wa masomo ya Rasilimali watu na gwiji wa Uhasibu na usimamizi wa fedha? Alikuwa na lake jambo, na Clifford alishalijua, na hivyo haikuwa kazi ngumu kumkwepa.
Neema alishamtosha!
Likizo ambayo ilishamirishwa na harakati za kimapenzi pamoja na masomo hapa na pale ikaisha. Neema akarejea darasani na Clifford akarejea ubaoni. Vipindi vikaendelea bila matatizo. Kule kuonana kwao mara kwa mara hakukuathiriwa sana na ratiba ngumu zaidi ya masomo aliyokuwa nayo Neema, lakini ule uwepo wa Clifford ukamsaidia kwa kuwa alikuwa akipata pia muda wa ziada kusoma masomo ya ziada.
Masomo ya ziada chuo kikuu!!
Halafu sasa likazuka jambo!!!
Tena ghafla tu!!
***
Hakuwa na elimu kubwa. Kidato cha nne na kisha chuo cha ualimu, na kisha kurudi uraiani akiwa mwalimu aliyeipenda kazi yake kuliko chochote katika maisha yake. Alifundisha kwa makini masomo ya hesabu na lugha, na akawa kipenzi kwa wanafunzi wake kutokana na umahiri wake wa kufundisha masomo yale, hasa kwa darasa la nne na darasa la saba yaliyokuwa madarasa ya mitihani ya taifa. Shule ya Msingi Nyakato ndiyo iliyompokea na hapo ndipo makali yake yakaonekana.
Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu alikuwa mwalimu aliyeelewa maana ya ualimu! Alikuwa ni msaada mkubwa kwa wanafunzi wengi waliopitia Shule ya msingi Nyakato. Mitihani yake ilijizolea umaarufu mkubwa Mkoani Mwanza na kanda nzima ya ziwa kwa kubeba maswali ambayo yangetoka pia katika mitihani ya taifa.
Mwanafunzi wa darasa la saba ambaye hajapata mitihani ya kutosha yenye herufi “MKM” hakujiona kuwa aliye tayari kufanya mtihani. Waliobahatika kufaulu na kujiunga kidato cha kwanza walikiri kuwa, nusu au robo tatu ya maswali waliyokutana nayo kwenye mtihani wa taifa, yalikuwa yamechukuliwa neno kwa neno, namba kwa namba kutoka kwa fundi yule ambaye hata shuleni walishazoea kumuita “MKM”.
Lakini pamoja na sifa isiyoisha ya umahiri wa kufundisha hisabati na lugha, Masagida Kaswalala Masalu alikuwa ni mwalimu aliyeogofya!! Kisingekuwa kile kipaji chake kisichoelezeka cha kufundisha, hakuna mwanafunzi ambaye angetaka hata kuwa naye karibu! Alikuwa ni mkali wa kupindukia na hakutaka kabisa urafiki usio na tija na yeyote katika maisha yake. Muda wote aliokuwa peke yake, alijitenga na dunia nzima na kuhangaika na madaftari ya wanafunzi wake tu!
Lakini hakuna mkate mgumu mbele ya chai. Hatimaye akafunga pingu za maisha ya binti aliyekuwa muuguzi katika hospitali ya Bugando. Maisha yake yakaendelea huku ile sifa yake ya ukali ikifichwa chini ya ule mwavuli wa umahiri wake wa kufundisha pamoja na ule upole wa mkewe Beatrice Budodi. Mwaka wa kwanza na wa pili ukakatika, wakajaliwa mtoto wa kike waliyemuita Neema.
Neema akayamulika maisha yao! Ili kumlea vema, Masagida akazidisha juhudi mara dufu. Akafanya kazi kwa bidii zaidi na jina lake likazidi kujengeka. Hatimaye akapandishwa cheo na kuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyakato.
Neema alipokuwa na miaka minne, mama yake akapata ujauzito mwingine. Furaha ikayafunika kabisa maisha ya Masagida. Alikuwa ni mwalimu mwenye furaha zaidi duniani. Miezi tisa ikatimia na mkewe akaingia kwenye chumba cha kujifungulia.
Haikuwa kama walivyopanga.
Haikuwa kama walivyotegemea.
Beatrice hakutoka chumbani mule akiwa hai. Mtoto alikuwa amekalia nyonga na hivyo jitihada za kujifungua kawaida zikagonga mwamba. Mama alikuwa ameshachoka sana wakati wataalamu walipoamua kumfanyia upasuaji! Walifanikiwa kumtoa mtoto mkubwa na mzuri wa kiume aliyekuwa na afya tele. Wakati wakilishona tumbo la Beatrice, walikuwa wakilishona tumbo la Maiti yake tu.
Beatrice mwenyewe alikuwa anayajongea malango ya muumba wake!
Alifariki dunia!!
Kifo chake kiliacha uwazi usiozibika katika maisha ya Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu. Kifo kilichomwacha na jukumu la malezi ya Neema aliyekuwa na miaka minne tu na mdogo wake wa kiume aliyemwita Machimu, akimaanisha Mikuki. Ni kweli kabisa mtoto yule alikuja kama mkuki ulioutoboa moyo wake na kuyachukua maisha ya mama yake.
Hakutaka kuoa tena..
Akaamua kuwalea watoto wake kwa mapenzi makubwa huku mdogo wake wa kike na ndugu wengine kadhaa wakimsaidia pale nyumbani.
Neema na Machimu wakakua katika upweke wa kumkosa mama yao. Kuna wakati sura ya aliyeitwa mama yao ilikuwa ikimjia Neema kwa mbali sana, lakini hakuweza kukumbuka chochote. Kwake yeye, baba yao mwalimu Masagida Kaswalala Masalu ndiye alikuwa mama na baba. Ukali wake ukamjenga na kumuandaa vema kuwa binti aliyemfurahisha baba yake.
Kisha sasa, hili linatokea akiwa mbali na baba yake…
 
ZAWADI YA ADHABU

SEHEMU YA NANE

Nimefundishwa kuwa…
Kesho ni siku nzuri sana.. Huenda ikawa ni kweli au isiwe kweli, na hilo si la muhimu sana. Lililo la muhimu ni kuwa, kesho; ingawa inaweza ikawa ni nzuri au vinginevyo, lakini itafika. Ikiwa itafika ikiwa nzuri, tutaifurahia na ikiwa itakuja ikiwa mbaya, tutaipokea. Ukweli utabaki kuwa, hata kesho; ikiwa tutakuwepo, ni lazima tutaendelea kuishi. Sasa tukiwa na Imani kuwa hata kesho maisha yataendelea, ina faida gani kuishi leo huku tukiiharibu kesho yetu au kesho ya wengine kwa makusudi?? Yafaa nini kuishi leo kwa furaha inayoiharibu kesho yetu? Kwangu, huu ni uzembe wa fikra!!
Una hiyari ya kukubali au kukataa….
******
*** NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU NANE ***
Hili hawakulipanga, wala kulitamani…
Ingawa Mwanzo ilikuwa ni hofu tu ya kawaida, Mwanamke yule mrefu aliyekuwa amevalia koti refu kiasi jeupe huku macho yake makubwa na mazuri akiwa ameyaficha nyuma ya mawani makubwa ya macho aliithibitisha hofu ile kuwa ulikuwa ndio ukweli sahihi kabisa. Bila kupepesa macho, aliwaangalia wote wawili usoni na kutabasamu.
“Hongereni sana.. Muda sio mrefu mnaenda kuwa wazazi vijana kabisa” Aliwaambia huku akitabasamu kwa mbali na kuacha uwazi mdomoni mwake ulioonesha ule mwanya mpana aliokuwa nao. Alivutia pamoja na kuwa mtu mzima sana.
“Asante sana dada” Alitikia Clifford huku mwili ukimsisimka kwa ukweli ule. “Muda sio mrefu naenda kuwa baba. Nami nakuwa baba jamani, dah!!” Haya aliyasema mwenyewe tu kwenye mawazo yake bila kuyaacha yatoke kupitia mdomo wake. Lakini cha kushangaza, mama yule akacheka.
“Ndio unaenda kuwa baba. Hukuwa umetegemea au hujiamini?” Aliuliza huku akimtazama kwa chati. Aibu ikamfunika usoni Clifford kwa kuropoka kule ambako wala hakuwa ametarajia. Akamgeukia Neema haraka. Hakuwa ametabasamu wala kununa. Ni kama vile alikuwa amening’inia baina ya vyote viwili, hofu na furaha.
Alikuwa amepigwa na bumbuwazi!
Mengine yote yaliyopangwa kufanyika yakafanyika pale. Wakapima vipimo vyote vya muhimu, wakapata majibu na kupewa ushauri wa hapa na pale, kisha wakapangiwa tarehe ya kuanza kliniki, na wakaondoka wakiwa kimya kabisa. Muda wote huo hawakuwa wamepata nafasi ya kujadiliana juu ya jambo lile.
Haraka wakaagiza bajaji huku sasa Clifford akiazimia kuwa, muda wa kutafuta gari lingine baada ya lile la kwanza kuporwa na ile mibazazi iliyomtengenezea kisa wakishirikiana na Nunu. Bajaji ikaamrishwa kuwapeleka mpaka nyumani kwake, Mwenge, Karakana. Walipofika na kuhakikisha wameshajifungia ndani, ndipo sasa Neema akapata nafasi ya kufanya kile ambacho hakuwa amekifanya muda mrefu sasa.
Alianza kulia kwa uchungu mkubwa.
“Nitamwambia nini yule mwalimu, Clifford? Nitamweleza nini Masagida Kaswalala Masalu? Yani kweli Napata mimba kabla ya ndoa, tena hata kabla ya kumaliza masomo? Ni kipi tutamweleza atuelewe Cliff? Ooh Mungu wangu, Neema mimi nitafanyaje?” Katikati ya kilio kikali Neema alijisemea. Ingawa alikuwa akiongea na Cliff, ni kama yote alikuwa akijiuliza na kujijibu mwenyewe.
“Hebu acha utoto Ney.. Acha kujiliza kwa maswala ya kipuuzi” Alisema Clifford akimsogelea Neema wake.
“Ya kipuuzi? Ya kipuuzi? Cliff we ni wa kuniambia hivyo kweli? Sasa mi ntaenda wapi jamani? Nitaenda wapi mimi?” Neema aliendelea kulia kwa uchungu.
“Come on Ney, uende wapi kufanya nini? Nini ambacho ulitaka nifanye na sikukufanyia? You are my wife, full stop. Hayo ya Masagida Kaswalala Masalu niachie. Nitaenda mwenyewe kwa miguu yangu, nimkabidhi ng’ombe wake hata kama ni mia, nimwombe baraka zake nawe uwe wangu wa maisha. Mbona swala rahisi tu hilo? Si ni ku’credit account ya Masagida na ku’debit account ya Clifford, shida ikwapi?” Clifford aliongea huku akiwa amepiga magoti mbele ya Neema.
“Au hutaki kuolewa na mimi Neema? Neema don’t you love me?” Aliuliza Clifford.
“Ooofcoourse I love you Clifford.. Nakupenda sana Mume wangu.. Its just… Just… just…” Neema alikosa cha kuongeza.
“Hakuna cha just, everything is just so long as we want it to be that way. I will marry you.. Na hii sio ahadi hewa. Inuka sasa hivi twende kwa mkuu wa mkoa, na mkuu wa wilaya, na ustawi wa jamii, na kwa paroko, na kwa kwa wale wafanyabiashara wote pale sokoni, niahidi mbele yao kuwa nitakuoa.. Namaanisha. Inuka twende. Nampigia kabisa na Swai aniandalie lile gari lake la matangazo. Twende” Alisema Clifford akiwa tayari amesimama akimnyooshea mkono Neema ili waondoke.
Neema akacheka katikati ya kilio..
“Staki bwanaaa… Hebu toka hukoooo.. Mkuu wa wilaya na mkoa sijui na wamachinga wanahusikaje sasa?” Alisema huku kukiwa na dalili za kudeka, lakini akasimama. Hawakwenda kwa mkuu wa mkoa, wala kwa kamanda wa polisi, wala kwa mkuu wa kikosi cha mbwa..
Walijikuta tu chumbani wakiwa uchi! Mkuu wa mkoa na wilaya ambaye alishuhudia makubaliano yao walikuwa ni kitanda na yale mashuka ambayo nayo kwa bahati mbaya yalijikuta chini bila huruma.
Mjadala ukawa umefungwa!
******
Mapenzi yao sasa yalishamiri. Neema alibakiza miezi miwili tu amalize masomo yake, na ni tumbo lake lilimpa ushirikiano wa kutokuchomoza upesi. Zulfa sasa hakuhisi tena, bali alitambulishwa rasmi kuwa, Neema ndiye mchumba wa Clifford. Akakubali na kutii huku kwa mbali kiwivu kikimtafuna. Masomo yaliyoendelea kuwa magumu kila siku pamoja na ile hali mpya ya ujauzito vikawa vikimwelemea Neema, lakini uwepo wa Clifford aliyekuwa mwanaume mwenye kujali na kumtunza vema vikampa unafuu.
Hawakuwa na haja ya kujificha kama Mwanzo. Pete ya uchumba ikaveshwa kidoleni mwa Neema kimya kimya na akawa akila na kuamkia nyumbani kwa Clifford. Mpango wao ulikuwa mzuri kabisa. Walitaka kwanza Neema amalize mitihani yake, kisha wangeanza rasmi taratibu za kwenda kwao kwaajili ya kuiweka wazi nia yao. Kwa hatua ile, Clifford hakutaka kabisa kumshirikisha Mzee Chiziza juu ya lile. Alimjua vema baba yake na namna ambavyo angeanza kumkumbusha habari za Mwanzo.
Wakauchuna!
Neema akaingia na kutoka kwenye mtihani wa kwanza, na wa pili na mingine yote mpaka masomo yote nane aliyokuwa nayo kwa muhula ule yakakamilika. Alifanya vizuri sana kwenye muhula wa kwanza, kwa mara ya kwanza katika miaka mitatu akiwa na GPA ya 4.2. Hii ilimpa amani sana wakati akifanya mitihani yake ya muhula wa pili, ambayo alikuwa amejiandaa vizuri sana.
Akamaliza salama! Alikuwa muhitimu mwenye furaha zaidi kuliko wote. Kwanza anamaliza chuo akiwa na maarifa kichwani, pete kidoleni, mume moyoni na mtoto tumboni! Nini kingine alikihitaji mwanamke wa umri wake? Hakika alikuwa na furaha!
Ujauzito wake ulikuwa na miezi mitano sasa. Sasa hakuwa na uwezo wa kuuficha tena. Ulichomoza mbele kwa fujo na kumlazimisha kubadili mavazi yote na kuanza kuvaa mavazi mapana mapana.
Lakini Amani yake ikakatizwa mara kwa mara na maswali kutoka kwa Masagida Kaswalala Masalu ambaye alijua wazi kuwa, binti yake alishamaliza masomo yake na alimuhitaji mara moja nyumbani. Ulitafutwa uongo, ukasakwa kwa kila namna, na lengo lilikuwa jema tu. Walitaka sasa walau kwanza Neema ajifungue. Ndio. Hii ingewasaidia kwanza kupokelewa bila maswali, na wakati mchakato ukiendelea, ingejulikana tu kuwa kilichotokea kimetokea, na wakati huo, mahari ingeshakuwa imelipwa, na ndugu wa pande zote mbili kuonana.
Kizuri zaidi, ndugu wenyewe walikuwa mbalimbali. Mzee Chiziza alikuwa Dar, na mzee Masagida Kaswalala Masalu alikuwa Mwanza, huku wao wakiwa Singida. Vikao vingefanyikia Dar au mwanza. Nani angeyajua kwa undani ya Singida bila wao kusema? Na si tayari walishaamua kutokusema? Ilikuwa rahisi sana. Lilikuwa swali la muda tu!
“Nimepata kazi ya muda mfupi baba. Hapa nilipokuwa nasoma wamenibakisha ili nisaidie kwenye idara ya fedha kule kama mhasibu msaidizi. Wananilipa kidogo lakini walau hutahangaika kunitumia tena….” Hakumaliza.
“Nini wewe? Wamekuajiri namna gani wakati hata matokeo bado? Umeshaanza uhuni wako?” Alifoka Mzee Masagida bila kusubiri maelezo ya ziada.
“Baba.. Najiheshimu sana mwanao.. Na kweli nilishakataa kwa kuwa hata mimi nimepakumbuka sana nyumbani. Ila walisisitiza kuwa ni vema nikabaki kwa kuwa hata ajira siku hizi zinasumbua. Hapa naweza kuunganishiwa nikapata kazi serikalini au kwenye taasisi binafsi upesi kuliko kurudi tu nyumbani” Alijitetea Neema.
“Lakini kwanini usingenipigia simu kuomba ruhusa unaamua kujiamulia tu mwenyewe? Kakwambia nani una nguvu kiasi hicho cha kuamua mwenyewe, eeh? Nasemaje, nimekataa.. Staki.. Staki!! Rudisha kiuno hapa!!” Alifoka Mzee Masagida
“Baba.. Nathamini sana juhudi zako za kunilea. Sitaki kukuvunjia heshima. Nikirudi na kukaa tu nyumbani naweza kukutana na vishawishi baba. Wewe mwenyewe umenifundisha kuwa akili isiyo na majukumu ni kiwanda cha shetani. Nataka nijibidiishe ili kuilinda heshima yako na heshima ya marehemu mama yangu aliyepambana ili niwe hai leo”. Neema alijua pa kumshika baba yake.. Alijua anapomtajia marehemu mkewe anakuwa ameshamaliza kazi..
“Aaah.. Ni sawa.. Ni sawa lakini… Kwanini wasingekupa hata wiki moja ukaja mama angu? Unajua wewe ndio jicho langu kwasasa. Wewe ndio mke, ndio mama, ndio binti, ndio dada, ndio kila kitu kwangu sasa. Muhula wa kwanza ulisema unafanya field, nikakubali. Sasaaaa tena…. Ah., sawa. We fanya kazi mama, ndio heshima ya mwanamke hiyo. Ila ukipata muda hebu uje walau mwisho wa wiki utusalimie. Na Machimu si unajua atakuwa na mahafali ya kidato cha nne mwezi wa kumi? Uje mwanangu” Alimaliza mzee Masagida kwa sauti yake yenye utajiri mkubwa wa lugha ya kisukuma.
Miezi ikakatika na furaha ikazidi kutawala nyumbani kwa Clifford. Pamoja na kutokuwa na kipaji cha kuimba, Clifford alikuwa mpenzi mkubwa wa kwaya. Katika kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu alipokuwa akisali, alikuwa ni rafiki na mfadhili wa kwaya ya Watakatifu Mashahidi wa Uganda, na akawa pia rafiki wa karibu wa wanakwaya mbalimbali. Mara kwa mara walikuwa wakimtembelea nyumbani kwake na Neema ndiye akawa mama mwenye nyumba aliyewakaribisha na kuwahudumia kwa mapenzi makubwa.
Hawa ndio wakawa marafiki zao wa karibu, na mara kwa mara wangesikika wakijadili namna watakavyohakikisha kuwa harusi ya mfadhili wao yule itakavyofana. Walimu walishaanza kufikirifikiri juu ya hata nyimbo za kutumbuiza siku ya harusi.
Kila mmoja alitamani kufika siku hiyo.
Halafu..
Miezi tisa ikatimia. Kelele za Mzee Masagida kumtaka bintiye zikiwa katika kilele huku akitishia kumfwata mwenyewe huko Singida, Neema polepole akaanza kupatwa na uchungu wa kuzaa. Maandalizi yote yalishakuwa tayari na walipanga akajifungulie Hospitali ya Makiungu iliyokuwa kilometa kadhaa kutoka Mjini. Kwa kuwa tayari wakati huo Clifford alishapata tena usafiri, haraka akamuwahisha mkewe hospitali akisindikizwa na marafiki zake wawili ambao wote walikuwa wanakwaya. Njia nzima alikuwa akiendesha gari huku mara kwa mara akimsemesha mkewe ambaye uchungu haukuwa umemfika hatua ya kushindwa kuongea.
Alimtania na kumchekesha, na safari ikawa fupi kuliko walivyotarajia.
Wakafika Makiungu hospitali.
Neema akapokelewa na kuingizwa chumba cha kujifungulia.
Clifford Chiziza na wenzake wakangoja..
Walingoja…
Wakangoja tena…
Wakangoja sana...
Halafu…. Ah!
******
 
ZAWADI YA ADHABU

SEHEMU YA TISA

******
Nimefundishwa kuwa…
Sio wote utakaokutana nao na kuwatendea mema watayakumbuka mema hayo maisha yao yote. Na tena, sio wote wote ambao utawaonesha ukarimu wako siku moja watakulipa kwa kukuonesha ukaribu utakapohitaji. Kukumbuka fadhila nacho pia ni kipaji, na sio wote wanacho. Lakini hii iwe tu ni sehemu ya wewe kujifunza kuwa, wajibu wako kwa wengine ni kuwatendea mema. Ukielewa vema hili na ukaanza kulitenda, dunia nzima itakuwa na binadamu wanaotendeana wema tu!! Kila jema linaanza na wewe!!!
Una hiyari ya kukubali au kukataa….
******
*** NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU TISA ***
Masaa matatu yalipita.
Sasa mishale ya saa ilikuwa ikiwaaminisha kuwa, ilikuwa saa mbili na dakika kumi na moja za usiku. Clifford alishatembelea maeneo yote muhimu katika hospitali ile kuanzia vyooni, kwenye wodi za wagonjwa, sehemu za kuuzia vyakula, maegesho ya magari na hata nje kabisa ya geti. Sasa alishamaliza kote na ni sehemu moja tu ilikuwa imebaki ambapo alitamani sana kuingia.
Chumba kile alipoingizwa Neema wake.
Rafiki zake Laurent na Thobias walikuwa naye bega kwa bega, wakajadili kuhusu hili, likaisha, wakahamia kwenye lile, nalo likaisha, zikaja na mada zisizo na mvuto wowote, wakazimaliza. Sasa wote macho walikuwa wameyatumbulia kwenye korido ndefu ambapo ndipo alikokuwa amepelekwa Neema. Ni Mungu pekee aliyejua ni nini kila mmoja alikuwa akikiwaza kichwani mwake.
Naam..
Mlango ukafunguliwa.
Kijana mrefu mwenye sharubu nyingi na mawani kubwa akatoka akionekana kuchoka kwelikweli. Akavuta hatua haraka haraka kuelekea upande mwingine wa korido ile mbali na walipokuwa wamekaa Clifford na wenzake. Lakini hakumaliza hata hatua kumi, Clifford tayari alikuwa naye bega kwa bega.
“Yes Dr. Mark, poleni sana” Alimsalimu daktari yule ambaye alikuwa ameshakutana naye zaidi ya mara tatu alipomleta Neema kuhudhuria kliniki.
“Njema.. Oooh, bwana Cliff.. Twende ofisini mara moja” Alisema Dr. Mark bila ya kupunguza mwendo wala kumtazama Clifford usoni. Clifford alisimama ghafla na kumtazama Daktari yule ambaye hakugeuka nyuma. Alitazama ingawa hakumwona! Kisha akanyanyua tena hatua na kuanza kumfuata nyuma nyuma kama kondoo aliyekwenda machinjoni.
Tayari alishaanza kuwa na majibu mengi kwa swali moja, na yote yalionekana kuwa sahihi.
Walifika katika chumba kidogo ambacho Clifford alishaingia zaidi ya mara mbili wakati wa matembeleo ya kliniki, lakini chumba kilionekana kuwa kigeni kabisa kwake. Alihisi kukichukia na wala hakutaka kuwa pale muda ule. Alimtaka Neema wake na mtoto wake awe amempakata mikononi akijaribu kucheza naye. Alikuwa akiyaona mashavu ya Neema katika uso wa mtoto wake. Alikuwa akiutazama uso wa kuvutia katika mtoto wake. Alitaka muda ule ule awe amemshika mtoto wake. Ni vipi sasa Dr. Mark anamleta katika hiki anachokiita ofisi huku hakina dalili yoyote ya kuwa na kitanda kitakachompokea Neema na mtoto wake watakapotoka huko walipo?
“Enough Dr. Mark!! This isn’t a joke anyhow. Please speak out, how is my good wife and a baby? Are they fine? Is everything alright?” Aliuliza Clifford huku akionekana wazi kughadhibika hasa kwa kuwa, Dr. Mark aliendelea kujishughulisha na kifaa hiki au kile akimwacha Clifford akiwa amesimama dede!!
“Yes yes Clifford.. Just have a sit brother.. We need to talk” Alijibu Mark huku akijipangusa uso na kuiweka sawa mawani yake. “We need to talk? Talk on what you swine?” Alijisemea Clifford ndani ya kichwa chake. Akamtemea kohozi zito kimawazo na akajiapiza kuwa, hatazungumza tena na daktari yule akishatoka hospitalini na Neema wake na mtoto wao.
Akaridhika kiasi. Hasira zikampungua.
Akaketi kishingo upande huku akimtazama Dr. yule usoni. Alikuwa mbaya!!Alimchukia na kushangaa ikiwa ni yuleyule kijana mwenye sura nzuri ambaye alikuwa akimuhudumia mkewe! Akamtukana tena tusi la nguoni kimoyomoyo, akaridhika zaidi, akatulia na kumkazia macho.
“Kuna vitu inabidi tuviweke sawa…” Alianza Dr. Mark.
“Vitu gani? How much? Sema, pesa ngapi nikupe mwanaume? Sema upesi, au nikupe……” Kihoro kilikuwa kimempanda Clifford.
“Clifford you must learn to listern and listern good!” Mark alijibu kwa mkato kwa sauti ya upole lakini kwa mbali, ilionekana kuwa na msisitizo fulani unaolazimisha jambo fulani. Clifford akatulia tuli.
“Imekuwa ni ajabu kidogo. Mkeo alihudhuria kliniki zote na kila kitu kilikuwa sawa kabisa.. Hata wakati wa tembeleo la mwisho nilimpima mwenyewe na hali yake ilikuwa sawa na ingempasa ajifungue kawaida. Lakini tuligundua kitu tunakitita “abnormal Presentation”. Mkao wa mtoto haukuwa sahihi na wakati tunajiandaa kufanya upasuaji, kulitokea hali nyingine ambayo tunaiita “Amniotic Fluid Embolism”, ambapo katika namna isiyo ya kawaida, kuna fluid tunaiita Amniotic Fluid ilianza kupenya kwenye mfumo wa damu, na fluid hii hupelekwa hadi kwenye mapafu na kusababisha hali tunayoiita kitaalamu “Arteries contractions” ambapo…
“Dr Mark get to the business buda, get to the damn thing!!.. Ningependa zaidi utumie lugha nyepesi tu, MKE WANGU NA MWANANGU WANAENDELEAJE? Achana na habari za amphibia, flomborism, autopia na mamalia, nitakuita wiki ijayo uje unifundishe nikiwa na kalamu na daftari. Nataka kujua hali ya Neema bana.. Amniotic arteries na Manini nini sijui huko utaniambia siku nyingine”. Alikuja juu Clifford.
“Clifford.. Wewe ni mwanaume, na unapaswa kujikaza. Mtoto ametoka salama na tayari wauguzi wanamuandaa. Lakini mke wako…. Neema ame…. Ametutoka Clifford. Haikuwa rahis….” Alisema Mark huku akijaribu kuiweka sauti yake kuwa ya kubembeleza.
Lile kofi la kisogo alilowahi kubamizwa na Martin Bazu likarejea tena kwa fujo kwenye mawazo yake, likambabatiza kwa nguvu. Lakini hili halikuambatana na maumivu, lakini madhara yalikuwa yaleyale. Na tena, Aliwaona akina Dr. Mark wanne wanaofana wakimtazama.
“Whaaaat?? Nini wewe? Unasemaje Mark? Neema ame.. Amefanya nini?” Clifford alishajikabidhi mwenyewe chini kwa kishindo! Hakuwa tena anajua kinachoendelea.
Vijana wa Kiswahili wangesema amekata moto!
***
Ulikuwa usiku wa hekaheka kwa Laurent na Thobias. Taarifa za kifo cha Neema ziliwatia ganzi na kule kupoteza fahamu kwa Clifford kukawaingiza katika tanuru ambalo halikuonekana. Walifuta jasho, wakapanda na kushuka. Haraka, mwili wa Neema ikaburuzwa kwa machela na kuingizwa katika chumba cha maiti. Shemeji ambaye walikuwa wakitaniana naye masaa kadhaa yaliyopita alikuwa kimya..
Kimya cha daima!!
Kitoto kichanga cha kike kilikuwa kikitumia mikono yake midogo kupangua hewa na kulia kwa bidii. Watawa wa kanisa katoliki ambao walikuwa wakiihudumia hospitali ile wakakanyakua juu juu na kukapeleka katika chumba maalumu na kuanza kukahudumia.
Ulikuwa ni uchungu usiovumilika kwa Clifford baada ya kupata fahamu. Alidumu katika hali ya kutokujitambua kwa saa moja na nusu ndipo alipofungua tena mboni zake na kuanza kuweweseka. Clifford alilia, akasimama, akakaa, akagaragara chini, akajipaka na vumbi, lakini sauti pekee aliyoisikia haikuwa ya Neema wala mwanae yule.. Sauti pekee ilitoka kwa Thobias aliyekuwa akitoa maneno yote kutoka katika biblia, tenzi za rohoni, katekisimu za kanisa na hata sala alizozifahamu yeye.
Zote hazikuwa na msaada wowote kwa Clifford.
Taarifa zikafika Singida mjini. Majirani, marafiki pamoja na jamaa wa karibu na Clifford wakayasikia yaliyomtokea. Usiku uleule, wakarudi mjini huku wakimwacha Neema akipigwa na ubaridi usiomithilika na kichanga kile kikiwa chini ya uangalizi wa wataalamu.
Usiku ule ule, tayari kikundi cha wanakwaya pamoja na majirani wengine wa Clifford walishafika nyumbani kwake. Nyumba ikaendelea kujaa kila baada ya dakika chache na mpaka kufikia siku iliyofuata asubuhi, tayari na turubai lilitundikwa juu ili kuwasitiri watu kwa jua. Clifford hakuwa na nguvu ya kuongea chochote. Alikuwa amejiinamia huku akiliona jinamizi kubwa la kifo likimjia na kumzomea. Ni wazee wachache na marafiki zake hasa wale wanakwaya waliokuwa wakishughulika kila kitu.
Hakika aliuona upendo wa watu!
Lakini wote wale walikuwa wakihangaika bure tu. Hakuna hata mmoja kati yao aliyeonekana yuko tayari kumpa msaada wa kupata majibu magumu ambayo yalikuwa yakitembea kichwani mwake..
Angemweleza nini Mzee Chiziza?
Angemweleza nini Mzee Masagida Kaswalala Masalu?
Angempeleka wapi Neema?
Angempeleka wapi yule mtoto asiye na jina ambaye hata alikuwa hajamtia machoni?
Kamasi zilimchuruzika na wala hakuona umuhimu wa kuhangaika nazo. Alikuwa na mambo ya msingi ya kuwaza kuliko kuwaza zile kamasi na machozi yaliyokuwa yanamtoka bila kibali maalumu. Tayari alishaonekana kuchoka kuliko kawaida. Hakuwa mtu wa kuzungumza, na wote waliokuja kumpa pole aliwaona wanafki na wazandiki wakubwa.
Jua likawaka na kupunguza makali. Jioni ikafika. Wenye busara wakaona kimya, na kwa kuwa utu uzima wao ulishawakutanisha na mambo makubwa kuliko lile, wakaamua kuweka kikao kwa nguvu.
“Sasa Bwana Clifford.. Yaliyotokea yameshatokea. Neema ametutoka, Innallilah Wainai Lillah rajiun. Waislamu sisi tunasema Kul nafsin zakatul Maut, nadhani hana nanyi ndugu zetu katika Imani mnalikiri hilo, tumetoka kwake na kwake tutarejea”. Alianza kuzungumzwa Mzee Ibrahim Upodo, moja kati ya wazee ambao Clifford aliheshimiana nao mno pale Singida.
“Acha uongo wewe.. Neema hajafariki” Clifford alisikia kitu kikimuwaka ndani yake, na kwa mara ya kwanza akamchukia Mzee Upodo. Bahati tu ilikuwa upande wake kwa kuwa maneno haya yaliishia katika kichwa chake tu. Mzee Upodo akaendelea.
“Alhamdullilah Mwenyezi Mungu ameweka mkono mtoto amemnusuru. Kuna Ibra katika hili ndugu zangu.. Kuna mazingatio hapa na ni vema tukayashika na kuendelea kumcha M’nyaaazi Mungu mwingi wa reh’ma. Ni vema tukamshukuru M’nyaaz Mungu Subhannahu Wataalah wandugu. Lakini sasa, kule kwetu Tabora huwa tunasema Msiba haukosi pa kuingia. Na sasa kwetu umeingia. Nadhani labda kama umeshaongea na wazee ungetupa mrejesho ili walau tujue tunafanyaje bwana Clifford” Alimaliza Mzee Upodo na zaidi ya watu nane waliokuwepo pale sebuleni wakaafiki.
“Kwa kweli… Kweli sijui nianzie wapi.. Nashindwa… Nashindwa kujua ni balaa gani ili limenigongea hodi asubuhi na mapema.. Mi sijui kwakweli, sijui” Kilio cha kwikwi kikaanza kumtoka Clifford. Mzee Upodo akahisi kuwa lipo jambo, na upesi akawabagua waliopo pale ndani. Wakabaki wanaume wanne pekee, na haraka, Mzee Upodo kama vile ajuaye yanayomsibu Clifford, wala hakuhangaika kumbembeleza.
Akatoka nje na kuagiza vijana kadhaa kwenda huku na kule, wakati huo huo simu yake ikifanya kazi. Dakika arubaini baadae, sebule ile ikawa kama kikao cha ukoo. Wazee kadhaa wenye heshima pamoja na marafiki wa karibu zaidi wa Clifford wakawa wamekaa kwa kuelekeana, idadi yao ikiwa watu kumi na sita. Mzee Upodo ni kama vile alishajipachika cheo cha mwenyekiti na kila mara alikuwa akikagua kagua ili kujirishisha kuwa akidi imetimia, kisha sasa akafungua mjadala.
“Naam wazee wenzangu na vijana wangu wachache. Nimeona tuitane mara moja kuwekana sawa kwa yale yaliyompata kijana wetu. Nadhani wote hapa tunakiri kuwa huyu kijana amekuwa ni kijana wetu sasa. Heshima yake na utii kwetu vimempa jina jema miongoni mwetu. Huu ndio ujana wenye manufaa, pamoja na elimu kubwa aliyonayo lakini bado anatuheshimu sisi wazazi wake kwa kituo.
Sasa yamemfika mambo. Ana msiba. Ukimya wake tangu msiba ulipomfika umenishitua kama mtu mzima na nikaona muwepo watu wenye vifua ninaowafahamu. Tafadhali kama kuna anayejua hana msaada hapa, na labda nimemuita kimakosa, ajiondokee mara moja” Alianza Upodo na kimya kilipozidi kuzizima akaendelea.
“Haya bwana mkubwa.. Clifford, ulipojaliwa hayo maumbile hapo katikati ya miguu ulipewa na zawadi nyingine kubwa. Zawadi ya uanaume. Mwanaume si mtu legevulegevu, hata yamfike makubwa yepi, huangalia kwanza namna ya kuyakabili halafu ndipo aanze kulia. Sasa tumekutana hapa kusaidiana nawe kuyakabili hayo. Hebu funga fundo gumu kooni, kisha liteme hapa lililo moyoni mwako. Nakuapia hata liwe na uzito wa dunia, tutalibeba mabegani na kutembea nalo kwa madaha kabisa” Upodo alisema huku akiweka kifua mbele.
Ujasiri ukamuingia Clifford.
Kwa mara ya kwanza akatamani Upodo angekuwa ndiye baba yake mzazi!
“Acha ujinga wewe, baba yako ni Chiziza…, Chizi Chiziza ambaye akisikia uliyoyafanya atakuachia laana ya kudumu” Ile sauti ikamjia tena lakini akaipuuza. Alifungua kinywa chake na kwa zaidi ya saa zima aliendelea kuwasimulia waliokuwa wakimsikiliza habari za Mzee Chiziza, kisha Neema na jinsi walivyokuwa wamepanga, na namna ujauzito ule ulivyowalazimisha kungoja, na juu ya uwepo wa Mwalimu korofi aliyeitwa Masagida Kaswalala Masalu ambaye wakati huo labda alikuwa akihangaika kumtafuta binti yake bila mafanikio kwa kuwa alikuwa na kawaida ya kuongea nae kila siku mara mbili au mara tatu.
Mpaka anafika mwisho wa simulizi yake, sebule nzima ilikuwa imezizima kwa ukmya usiomithilika. Hakuna hata mmoja aliyenyanyua kinywa kuhoji wala kushauri.
Wote walikuwa wamesawajika!
“Mmmmh… Ama kweli ‘pachonge pangali panene’. Babu yangu aliwahi kunifundisha msemo huo miaka mingi iliyopita. Hiki kweli kizaazaa. Lakini bado sijaona dalili za kushindwa. Kwanza, nadhani wa kwanza kumuarifu habari hizi ni baba mzazi wa kijana. Mpigie simu Mzee Chiziza nami nitaongea nae taratibu na kwa kituo. Yeye akshatuelewa, nadhani tutakuwa na karata ya kwanza ya kututoa katika mtego huu” Alisema Mzee Upodo kwa kauli iliyokosa ule ujasiri wa awali.
“Halafu imekuwa ajabu kweli. Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu anayeongelewa mimi namfahamu vema sana. Mzee wangu aliwahi kufundisha naye pale Nyakato lakini yeye baadae akahamishiwa Geita. Nadhani naweza pia kumwomba baba yangu atusaidie upesi kuwasiliana na Mzee mwenzake ili walau tuone msimamo wake”. Joshua Tegu ambaye alikuwa rafiki wa Clifford akachangia.
“Unaona sasa Clifford? Haya mambo bwana ukikaa na watu wanayamaliza. Haya bwanaaa…. Nani vile?” Alihoji Upodo
“Tegu.. Tegu.. Mr. Joshua Tegu” Alijibu Tegu ambaye alikuwa mhandisi wa maji.
“Naam Tegu.. Hebu wewe na Mzeeee…. Makambaaaa, Nyonzo naaaa… Mmole.. Wewe, Makamba na Mmole chukueni jukumu la kuwasiliana na Mzee wako pamoja na kuhakikisha kuwa mpaka saa mbili kamili tunapata mrejesho juu ya huko nyumbani kwao marehemu kwa huyo Mzeeeee” Alisema na hakungoja mtu amkumbushe.. Alikuwa akipitia karatasi ambalo muda wote wa masimulizi alikuwa akiandikaandika mambo ya muhimu.
“kwa mzee Masalu”. Alimaliza.
“Mimi, Clifford, Mzee Babudiii.. naaaa…, nani mwingine jamani? Tujitokeze..”
“Mimi hapa” Aliitikia mtu wa makamo aliyekuwa ameegamia ukuta.
“Hewalaaa.. Mimi, Clifford, Babudi na Lasway tunajishughulisha na mawasiliano na Mzee Chiziza na upande mzima wa Clifford. Kama kawaida, mbili kamili tunakutana hapa kuweka vichwa pamoja tuone tumefikia wapi. Wengine wote tuliobaki, chini yaaaa… Oh, ndio.. Ningepitiwa hapa.. Chini ya Bwana Kimati.. Ambaye mimi napendekeza awe mwenyekiti wa kamati ya mazishi. Ninyi anzeni mipango mara moja. Wekeni sawa bajeti zote, angalieni kama tuna fedha ya kutosha na kila kitu kiwe sawa. Sisi tukija na majibu tu tunaendelea kutoka mlipoishia” Alimaliza Upodo na kuangalia kama kuna aliyekuwa na nyongeza.
“Sawa.. Mi nakubali. Na napokea jukumu hilo mara moja. Ila kwa kuwa shughuli hii itahitaji pesa, nashauri hapa kuwa mwenye nacho aanze kukiahidi au kukiweka kabisa mezani ili tujua tunaanzia wapi. Mimi nitachangia taslimu Milioni nne, na magari matatu” Alisema Kimati.
Hoja ikapita mara moja. Huyu akaahidi hiki na huyu kile. Ndani ya dakika tano tu, Milioni sita na nusu zikapatikana pale pale ingawa nyingine zikiwa ni ahadi. Kikao kikakamilika na watu wakasambaa wakikubaliana kukutana tena saa mbili na nusu.
Walikuwa na masaa mawili tu ya kufanya kazi ngumu kwelikweli!
Kazi ambayo hata hivyo…
Mh!!
 
ZAWADI YA ADHABU

SEHEMU YA KUMI

******
Nimefundishwa kuwa…
Sio lazima ujichanganye na watu wote muda wote. Kila binadamu ameumbwa na namna fulani ya hali inayomfanya wakati fulani atake kuwa peke yake tu. Hii ni kawaida kabisa hata kwa sisi wengine, sio kwako tu!! Unapoona kuwa inakulazimu kujitenga na wengine, fanya hivyo. Lakini daima jijengee hali ya “kufikika”. Wafanye wengine wakuone kuwa mtu wanayeweza kumfikia katika hali walizonazo. Unapojenga aina ya kisiwa cha kukaa mwenyewe, kuna wakati unajitenga na fursa ambazo huenda hata wewe unazihitaji sana!!
Una hiyari ya kukubali au kukataa….
******
*** NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU KUMI ***
Hali sasa ilikuwa tete!!
Kama Clifford alidhani alikuwa anaufahamu vema ukali wa baba yake, alikuwa amejidanganya vibaya sana! Mzee Chiziza alimsikiliza huyo wa kuitwa Upodo kwa umakini mkubwa tangu Mwanzo wa simulizi yake mpaka mwisho. Hapa na pale, Mzee Upodo alikuwa akitumia muda mwingi kuelezea busara za Clifford na namna alivyokuwa na heshima kwa watu anaoishi nao, na Mzee Chiziza alikuwa kimya tu akimsikiliza kwa umakini. Kwa mbali, timu ile ya watu wanne wakaanza kuhisi kuwa walikuwa wanaelekea kufanikisha jukumu lile kirahisi kabisa.
Mzee Upodo akamaliza.
“Umemaliza mzazi mwenzangu?” Sauti kavu ilisikika kwenye simu.
“Naam Mzee mwenzangu. Na nikaona hili nililete mimi kama…”
“Huwa napenda jibu moja kwa swali moja, huenda Clifford hakukueleza hilo. Msamehe tu, huenda hajakueleza mengi bado.. Nipe jibu la swali langu tafadhali” Sauti ile kavu na yenye wingi wa mamlaka ikamkatiza Upodo.
Wajumbe wale wanne wakatazamana, lakini haraka Clifford akatazama chini. Alishajua balaa linalokuja.
“Naam.. Nimemaliza Mzee mwenzangu” Upodo alijibu kinyonge.
“Sawa. Kwahiyo huyo bwana mdogo alikuwa akiishi na mwanamke, akampachika mimba na kuendelea kuficha akiamini kuwa baada ya kujifungua ndipo napaswa kupigiwa simu ili tu kutoa jina la mtoto, sio?” Aliuliza Chiziza.
“Eeeh.. Nadhani ndiyo ilikuwa maana yake, na huenda kulikuwa na….”
“Unaonekana nawe unaanza kuwa mzee mpumbavu mwenye kusahau sahau mambo. Nimesema swali langu moja huwa linahitaji jibu moja tu.. Hayo majibu yako yatunze, maswali yake ninayo pia” Hapa hasira zilionekana wazi wazi kwenye sauti ya Chiziza. Lakini tofauti na matarajio ya wengi, Mzee Upodo wala hakukasirika, alizidi kuwa mpole na uso wake kuwa makini zaidi.
“Nahisi hivyo bwana” Alijibu Mzee Upodo.
“Clifford ni mwalimu mzuri sana darasani. Naona amefika Singida amepata na wanafunzi wazee watu wazima ambao nao amewafundishwa somo linaloitwa “kuhisi”.. Kwahiyo utaacha muda gani “kuhisi” ili unipigie tuanze kuongea vitu halisi na sio hisia?” Aliuliza Chiziza huku akiweka msisitizo fulani kwenye baadhi ya maneno.
Clifford tusi zito likamtoka lakini jicho kali la mzee Upodo likamtuliza jazba!
“Mzee mwenzangu.. Lililopo mbele yetu ni tatizo kubwa, na wewe kama baba mzazi…” Upodo alijaribu kujitetea.
“Angalia bwana, nilisema nikiuliza swali lijibiwe kwa jibu moja, hayo maelezo kuna wakati ntakuja kuyahitaji halafu usiwe nayo bure. Jifunze kuwa na akiba ya maneno. Na kwa kukukumbusha tu ili usije ukakosea mara nyingine, Mimi sio “kama baba mzazi wa Clifford”, mimi ni “Baba mzazi wa Clifford”.
Simu ilikatwa!!!
Bumbuwazi ikatawala.
Mzee Babudi na Laswai walitazamana, wakatikisa kichwa kwa pamoja. “Hivi baba yako ni kabila gani?” Aliuliza Mzee Babudi macho yakiwa yamemwelekea Clifford. Kabla hata hajajibu, Mzee Laswai akajibu kwa hasira.. “Huyu lazima atakuwa kabila mbovu tu.. Mali mbovu.. Mswahili sana huyu Mzee, doh”
“Tulizeni jazba, bado tuna nafasi kubwa kwenye hili. Hebu nipatie hiyo namba nimpigie kwa simu yangu, kuna jambo nimejifunza hapa” Upodo akapatiwa namba na dakika mbili baadae, alikuwa tena kwenye mazungumzo.
“Naam.. Nakupongeza kuwa kuacha kuhisi ndani ya muda mfupi tu. Haya sasa, hebu nieleze. Wewe ndiye uliyeyabariki hayo mahusiano ya huyo barazuli kuishi na mtoto wa watu, kumjaza mimba na kuendelea kuficha akiamini kuwa akishajifungua ndio anaweza kuwaambia wazazi wake?” Alikuwa ni Mzee Chiziza aliyeanzisha mazungumzo.
“Kwakweli hakuna mzee au mtu mzima yeyote anayeweza kubariki jambo kama hili. Kilichofanyika ni kosa na kilikuwa kosa tangu awali. Tatizo ni kuwa, vijana wetu kuna wakati wanafikiri kuwa wana dunia yao peke yao, na ni busara tukawaacha waamini hivyo. Lakini ni dunia hiyo hiyo inapowafunza, yatupasa tuwarudi na kuwakumbusha kuwa, njia uijuayo panapo mwanga huwezi kuiendea vema palipo na kiza” Hakukuwa na hofu wala mashaka yoyote katika sauti ya Upodo.
Alishaanza kuonesha ujabali wake!!
“Anhaa.. Kwa maana nyingine unamaanisha kuwa, Clifford, aliiona njia mchana wa jua kali. Akaipitia mara mbili mara tatu, na kiza kilipotua akajiaminisha kuwa njia ile anaifahamu vema, akafumba na macho kabisa na akapita tena, na mwishowe alipofungua macho amejikuta amepotea, sio?’ Alihoji Chiziza.
“Naam ndugu yangu.. Nadha…, Hapana, naamini kuwa kijana kwenye hili, sio kwamba tu amepotea. Lakini ametupoteza hata na sisi ambao inatulazimu sasa tumtafute, tumpate na kwa pamoja turudi hadi Mwanzo wa safari. Tumfundeshe tena namna ya kutembea gizani” Upodo alizidisha Kiswahili.
“Sasa mimi neno langu ni moja… Neno langu ni moja tu…” Alianza Chiziza.
“Naam”
“Na huwa nina utaratibu mmoja. Clifford atakueleza vema kama akiamua kufanya hivyo. Nikishafanya uamuzi juu ya jambo moja, natamani ufuatwe kama ulivyo, bila kupakwa rangi wala kupuliziwa uturi…, tuko pamoja?”
“Naam.. Nakusikiliza bwa’mkubwa”
“Na katika hili, neno langu ni moja. Na nikishamaliza tu kulisema, nitakata simu. Kama unatamani heshima yangu, usinipigie simu mpaka utakapolitimiza, tuko pamoja?”
“Eeeh… Nakusikiliza bwana, na naamini…”
“Achana na Imani yako bwana, nisikilize mimi. Kwanza usiamini usichokijua bwanaaa.. Nani vile ulisema?”
“Mzee Upodo”
“Ndio Upodo.. Usiamini usichokijua.. Sasa neno langu ni hili. Clifford, na mkipenda ninyi pia kushirikiana naye, malizeni huo upuuzi mliokuwa mnaulea pamoja. Kama mtazika, au mtaishi na maiti, au mtamrudisha mtoto wa watu kwao, hilo mimi sihusiki nalo. Sijafundishwa kusaidia watu wazima wanaochezea moto namna ya kuuguza majeraha yao, nilifundishwa kuwaelezea madhara ya moto. Huyo bazazi yalishamkuta makubwa, nikadhani amejirekebisha, na badala yake kaenda kuchuma makubwa zaidi. Sasa malizeni huo upuuzi, mkishamaliza tu, nipigie simu, nitakueleza nini kifuatacho. Nimekuheshimu sana kukupa nafasi hii, na sikumbuki mara ya mwisho niliitoa mwaka gani. Msiba Mwema”.
“Aah.. Lakini Chiziza… Unajua bwana hali iliv…..” Upodo alikuwa akiongea mwenyewe. Simu ilikuwa kimya. Tusi la kiarabu likamtoka kwa uchungu!
Kikao hakikuwa na maana tena, kikavunjika na wote wakaendelea kungoja majibu ya upande wapili.
***
Ilikuwa rahisi sana kumpata Mzee Tegu ambaye mara moja aliwasiliana na mzee Masalu. Bila kukawia, Mzee Masalu akaungwa na waliokuwa Singida na mara moja mawasiliano yakawa baina yake na wao.
Kwa zaidi ya dakika ishirini walijaribu kumuelezea kilichotokea lakini maswali mazito mazito yalikuwa yakirushwa mfululizo. Haraka wakaamua kumshirikisha na Clifford aliyekuwa ametoka kwenye kikao cha kuzungumza na baba yake. Akajieleza kwa kirefu kwa Mzee yule ambaye aliishia kuguna kila alipokuwa akisimuliwa.
“Kwahiyo wewe ulikuwa mwalimu wake wa chuo, sio?” Aliuliza Masalu
“Ndiyo baba”
“Na ulimpa mimba akiwa bado mwanafunzi hapo chuoni?”
“Lakini tulishaanza uchumb…”
“Unalikumbuka swali langu?”
“Ndio baba”
“Naomba jibu”
“Ndiyo, Neema alipata mimba akiwa anakaribia kumal..”
“Akiwa mwanafunzi, acha kuremba mwandiko, kumbuka unaandika imla”
“Nakubali baba, akiwa mwanafunzi”
“Maadili ya ualimu yanasema nini kuhusu mahusiano baina ya mwalimu na mwanafunzi?”
Jasho lilikuwa likimtoka Clifford. Aliona dalili za kupoteza kila kitu maishani mwake.
“Ni kweli si sahihi kuwa na mahusiano ya kimapenzi. Lakini mimi na mwenzangu tulishakubaliana kufunga ndoa, na hata…”
“Wewe ndiye uliyemtafutia kazi chuoni?”
“Hapana baba, hakuwa anafanya kazi.”
“Jibu zuri kabisa. Wewe ndiye uliyemwambia anidanganye kuwa anafanya kazi ili uendelee kumlaza akiwa uchi kufuani pako, sio?”
Clifford angejibu nini sasa hapo? Alinyamaza kimya.
“Halafu.. Ni sheria ipi inamruhusu mwanaume kuishi na mtoto wa mtu kwa karibu mwaka mzima bila kutoa taarifa kwao? Au ndio ujana huo?”
“Tumekosea baba.. Tumekos..”
“Sema umekosea kijana, sema nimekosea”
“Nimekosea baba”
“Sawa.. Sasa mimi ninachojua, binti yangu Neema sio mjamzito wala hajafa. Yuko chuo cha uhasibu Singida akiwa anafanya kazi. Kama utamleta nimwone kuwa ndiye au siye hiyo ni juu yako, lakini binti yangu yuko hai!”
Simu ilikatwa!!
******
Saa mbili kasoro dakika nane wajumbe walikuwa tena pahala pamoja. Yaliyojadiliwa yakawekwa wazi. Kulikuwa na ugumu pande zote mbili, lakini unafuu ukaonekana upande wa Mzee Masalu. Ile kauli yake kuwa apelekewe mwaneye akamwone ilitafsiriwa na wazee kuwa ni kauli ya kiungwana na kishujaa. Huenda Mzee Masalu angeamini kuwa bintiye amefariki baada ya kumuona. Mipango ya kusafirisha ikaanza mara moja.
Kamati zikawekana sawa na marafiki wote wa Clifford wakawa tayari kwa safari. Mwili wa Neema ukaandaliwa na kurudishwa hospitali ya mkoa na mchana wa siku iliyofuata, kila kitu kilikuwa tayari. Pamoja na mchango wake katika kanisa, haikuwezekana kuwepo kwa ibada maalumu ya mazishi. Clifford alihesabiwa kuwa, kwa muda wote alishi suria, na kwa sheria na kanuni za kanisa katoliki, isingewezekana kuwepo kwa ibada ya misa takatifu. Zikasaliwa sala za hapa na pale, wanakwaya wakaimba na kuomboleza, na saa kumi kamili, safari ya mwanza ikawadia.
Gari sita zenye waombolezaji zikaanza safari, huku mkuu wa msafara akiwa Mzee Upodo huku akiwa bega kwa bega na wazee wenzake zaidi ya nane ambao wote waliamua kushiriki kukamilisha shughuli ile ambayo wangeendelea kuiwekea masihara, ingeweza kumwendea vibaya kijana wao Clifford. Tayari mawasiliano yote ya kumwomba Mzee Tegu awe Mwanza mapema ili kushirikiana na wazee wenzake kuupeleka msiba kwa Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu yalikwishafanyika, na tayari Mzee Tegu alikuwa njiani kuelekea Mwanza.
Shughuli ilikuwa imepamba moto kwelikweli..
Ziliimbwa nyimbo, machozi yakatiririka, mafuta yakaungua, Mwanza wakatua. Saa sita na robo usiku, msafara wa magari ukawasili jijini Mwanza. Lakini tofauti na ilivyo ada ya misiba, usiku huo isingewezekana kuufikisha mwili wa Marehemu nyumbani kwao.
Nani angewaelewa ikiwa hakukuwa na maandalizi yoyote?
Wazee wakaitana, majadiliano yakafanyika na ikakubaliwa kuwa, alfajiri ya siku iliyofuata, Tegu na wazee wengine kadhaa waende kwanza nyumbani kwa Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu na baada ya kuwekana sawa na kupima kile ambacho angewajibu ndipo sasa mwili upelekwe na msiba upate pa kufikia.
Walipitia tena mipango yao, wakachambua chambua na mila za kisukuma, wakauliza na kujibiana juu ya faini ambazo wangeweza kukabiliwa nazo ili mwili ule kupokelewa. Wakapigiwa simu wenyeji kadhaa na kuulizwa hili na lile. Baada ya masaa mawili ya kupanga na kupangua, mpango kamili ukawa umekamilika na ukakabidhiwa kwa wazee watano..
Upodo akiwa mwenyekiti, Tegu kama rafiki wa Masagida, Mzee Babudi, Makamba na Laswai kutoka Singida, na Mzee Urubani Ng’wanzalima aliyekuwa rafiki mkubwa wa Tegu na Masagida.
Wakakaa wakipiga soga na kunywa gahawa kuingoja alfajiri.
Mipango ikiwa barabara kabisa..
Hawakujua kuwa yooote waliyopanga yalikuwa ni kuteka maji kwenye kapu, waliyachota kisimani na kuyaweka kichwani, lakini walipofika nyumbani walikuwa wamelowa..
Walikuwa wakipanga na kupangua ujinga mtupu!!!
******
 
ZAWADI YA ADHABU

SEHEMU YA KUMI NA MOJA

imefundishwa kuwa…
Mambo mengi yanayotuponza ni yale ambayo tunayafanya kwa kuwa ni ya hiyari. Kama mambo yote yanayotuzunguka yangalikuwa ni sheria, tena zisizotupa hiyari ya kuzitii ama la, huenda, narudia tena, huenda, kila kitu kingekuwa tulivu zaidi ya sasa. Lakini haiku hivyo. Tuna hiyari ya kuchagua katika kila kitu tunachokifanya. Mbaya zaidi, tuna hiyari ya kusema kweli au kuikataa kweli, na pale tunapoisaliti kweli na kuamua kuunda urafiki na uongo, tunajikuta kuwa, jambo dogo tunalolifanya kwa hiyari linajenga misingi ya matatizo makubwa yatakayotukuta kwa lazima!!
Una hiyari ya kukubali au kukataa….
******
*** NINAWAANDIKIA HAYA KATIKA SEHEMU YA KUMI NA MOJA ***
Alfajiri ilifika..
Ni kama kila mmoja alikuwa akimtegea mwenzake aongoze njia.
Lakini ule utu uzima wao ukawasuta na kuwakemea. Wakainuka kwa pamoja, kisha wakaingia kwenye gari moja dogo wakiwaacha waombolezaji wengine wakiwa wamesambaa huku na kule. Wapo ambao toka walipofika walikuwa wamejikita katika ulevi na kupoteza mawazo, wengine walikuwa wamelala tu garini na wengine huku na kule wakijadiliana. Clifford yeye alikuwa amejikunyata garini akiwa mgonjwa wa ugonjwa ambao haujapatiwa damu ya kuponya wala kinga ya kuuzuia.
Ugonjwa wa hofu!
Wazee walishamwonya kabisa kuwa hata kama wangekubaliwa, asingepaswa kuonekana eneo la karibu na msibani kwa kuwa angezusha tafrani isiyo ya lazima. Kule kushindwa hata kushiriki kumzika Neema wake kulizidi kumpa homa isiyotibika.
Wazee watano wakafika kwa Mzee Masalu. Ile hali waliyoikuta tu kwanza ikaanza kuwatia ubaridi. Nyumba ilikuwa katika utulivu wake na hakukuwa na dalili yoyote ya kupokea mziba. Wakatazamana na kuulizana kwa kutumia macho, lakini hakuna aliyeonekana kuwa na jibu.
Wakafika na kugonga hodi!
Naam… Kidume cha futi tano unusu kikatoka kikiwa kimevalia suruali na shati huku kikiwa na kijitabu kidogo mkononi.
“Ohoooo… Bwana Tegu… Doh, Ng’wanzalima… Nawiwa nini nanyi hata mwanijia mapema yote hii?” Aliwalaki Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu huku akiwa na uso wake ule ule ambao hata alipotabasamu, ilikuwa ni vigumu kujua kuwa alitabasamu.
“Mgeni aambiwa karibu bwana, tena mwenyeji amwekee na kifua aangukiepo” Alijibu Tegu huku akitabasamu kwa kijilazimisha.
“Tangu lini Tegu akamwomba Masagida kifua aangukiepo? Tegu si wa kuangukia popote atakapo? Labda kama kuna kingine bwana” Alisema huku akijaribu kuwatazama wengine.
“Yapo mengi dunia ya leo bwana, na tena….” Alianza Ng’wanzalima
“Wala si mengi ya kuwakurupua asubuhi yote tena na wageni watu wazima kwangu. Kama ni posa jamani si mngeniarifu niwaandae na ndugu zangu? Au bado mnataka kuniletea huo utani wa msiba?” Alijibu Mzee Masagida huku sasa akiwa amesimama dede.
Hapo akakaribishwa Mzee Upodo. Akajitambulisha, yakafuatia maneno mawili matatu ya utani wa msukuma na mnyamwezi, kisha akaingia kazini. Itoshe tu kusema kuwa, Upodo alikuwa fundi wa kujieleza. Alipangilia kwa umakini mkubwa kauli zake, akayapekua vizuri maneno kabla ya kuyatoa. Akapanga semi na tamathali zake, penye kuweza kutumia neno la kinyamwezi au kisukuma akafanya hivyo. Jambo ambalo asiye mwerevu angetumia dakika mbili tu kulielezea, yeye akatumia saa moja na dakika kadhaa.
Akaweka kituo huku wale wazee wenzake wanne wakitamani wampigie makofi, lakini wakakumbika pale hawakuwa kilabuni wala kwenye minakasha ya gahawa. Walikuwa nyumba ya mfiwa, tena mfiwa asiye na uhakika. Wakaungana naye kwa kutikisa vichwa tu.
“Umemaliza maelezo yote mzee Upodo?” Alihoji Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu
“Naam.. Kwa tuo na kituo. Kama kuna lililobaki basi si la…”
“Sijauliza swali lingine, nadhani jibu lako la kwanza linatosha” Alijibu Masagida, kisha akawageukia wale wengine.
“Kuna mwenye maelezo mengine yanayokinzana na haya?” Alihoji.
“Hapana, Hapana bwana” Walijibu kwa pamoja kwa haraka kuliko walivyotaka.
“Vema sana. Hicho mnachokiita mwili wa Neema kiko wapi?” Alihoji tena
“Tumefika hapa jana usiku na tuli….”
“Nimeuliza swali moja tu.. Kiko wapi?” Akikatisha Mzee Masagida.
Jasho lilimtoka Mzee Upodo, akajiapiza kuwa angekuwa makini tangu muda ule kujibu maswali ya Mzee Masagida kama ilivyo kwa Mzee Chiziza.
“Penguin Hotel.. Ndipo magari ya waombolezaji yalipofikia kwa muda kuingoja alfajiri” Alijibu Upodo.
“Mzee.. Haya sasa, ngoja uone.. Kwanini mlifikia Penguin Hotel??” Akamkazia macho mzee upodo ambaye alikosa jibu la haraka.. “Ni wazi kuwa utajikuwa kuwa mlifikia hapo kuingoja alfajiri. Jifunze kuwa, kila swali unaloulizwa, toa jibu laka na uishie hapo. Acha kutoa majibu ya maswali ya kesho.. Utafeli” Mwalimu alirudi darasani, kisha kwa haraka akaanza kuongoza njia huku akisema,
“Vema sana. Twendeni” Aliongoza Masagida na kuanza kuelekea kwa mguu kwenye njia iliyokuwa ikiiacha nyumba ile.
“Lakini Mzee… Kwanini… Sisi… Eeh, si tungekuja tu moja kwa mo….” Alijaribu kujieleza Tegu.
“Tegu.. Unajua vile tunaheshimiana Mzee mwenzangu. Hebu usicheze michezo ambayo hukujifunza ujanani ukiwa mzee.. Utajavunja mgongo ukose wa kukuokota.. Acha tuliocheza ujanani tumalizie uzeeni” Alimjibu na haraka akapotea machoni pao.
Waliduwaa!!
Kengele za hatari zikaanza kupiga makelele masikioni mwao.
***
Walirudi upesi Penguin Hotel na walipokuwa njiani, Mzee Upodo alimpigia simu Clifford na kumwomba atafute pahala pa kwenda kwa muda na awe mbali na pale kwa wakati ule. Walifika na kupokelewa na waliokuwepo lakini hawakusema chochote badala ya kuwaomba muda kidogo wa kujadili jambo. Lakini hawakutumia hata dakika kumi, wazee watatu wakawasili pale wakiongozwa na Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu.
Wazee wale wale watano wakawapokea na kuweka kikundi kidogo cha wazee pembeni. Wakajadiliana huku hapa na pale wakionekana kuvutana na kuelewana, na baada ya muda, vijana kadhaa wakaombwa kushusha jeneza lililokuwa limeuhifadhi mwili wa Neema. Wazee wale watatu wakaingia garini na kukaa huko kwa dakika kadhaa, na baada ya muda wakatoka. Kimya kikuu kilikuwa kimetawala na hakuna hata mmoja aliyezungumza na mwenzake.
Wakajadiliana tena kwa muda.
Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu akiwa na nduguze hawakusema neno. Wakaomba waende nyumbani kwa mazungumzo ya muda mfupi na kisha watatoa jibu.
Wakaondoka!!
******
Saa nne kamili.. Kimya!!
Saa tano kamili.. Hola!!
Saa sita kamili.., Hamna kitu!!
Saa nane na nusu, waapi!!
Tisa kamili, kumi kamili, kumi na nusu.. Malikiti!!!
Joto likageuka kuwa baridi.. Kila mmoja alitetemeka. Njaa iliuma lakini hakuna chakula kilichonunuliwa kikalika!
Macho ya watu wote yaliwaelekea wazee watano. Wao kwa wao pia, kila mmoja akimgeukia mwenzake, lakini kama vile walionong’onezana, kila mmoja akamgeukia Upodo!! Upodo yule mwerevu wa maneno ni kama alikuwa kwenye dunia ya peke yake huku wengine wote wakimtupia mawe.
Saa kumi na moja kamili, simu ya Mzee Tegu ikaita, na alipoangalia, herufi tatu zikajitokeza mbele yake zikimsanifu…
MKM!!!
“Masagida Kaswalala Masalu…” Alinong’ona huku akiipeleka simu yake sikioni.
“Halo Mwalimu” Alianza kusema lakini akagundua kuwa koo lilikuwa limekauka.. Akameza mate kwa nguvu ili kulilainisha lakini hakuwa na mate mdomoni. Akaishia kunong’ona tu.
“Hebu nizungumze na Upodo” Alisema mara moja Masalu. Mzee Tegu akatii na kumpa simu.
“Sasa bwana Upodo. Familia nzima imekutana na kujadili kwa kina. Ni kweli huo ni mwili wa Neema.. Hatuwezi kuutesa mwili wa binti niliyemzaa na kumlea kwa tabu kubwa kama Neem….” Ni wazi Mzee Masalu alikuwa akilia moyoni ingawa sauti yake ilijitahidi kubaki katika muhimili wake bila mafanikio.
“Sasa bwana.. Huyo kijana sijui Cliff nani huyo, mimi sina shida nae. Huenda kweli mwanangu ndiye alikuwa mbwa wa kujirahisi kwa wanaume.. Lakini nataka mnitendee heshima moja… Namtaka Mzee mwenzangu hapa.. Namtaka baba wa huyo kidume cha mbegu aliyenizalishia mwanangu na kupelekea kifo chake. Namtaka na huyo kiumbe aliyekuwa tumboni mwa Neema.” Alianza na kuendelea
“Nataka na taarifa ya daktari kuthibitisha kilichomuua Neema.. Vikipatikana hivyo hata sasa hivi, njooni na msiba tuzike. Pasi na hayo matatu, wala msijali. Nendeni makaburini, chimbeni, mfukieni Neema.. Ipo siku Neema wangu atarudi…” Alimaliza Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu na kubaki kimya kama vile aliyetaka kusika kutoka upande wa pili.
Damu iliwasisimka wale wazee!!
Ama kweli hili lilikuwa ni tukio la mwaka..
Mwili, upo, hii haina shaka.
Taarifa ya daktari na kibali cha mazishi, ipo, haina maneno!
Kichanga cha marehemu, hiki kipo pia.. Ila kiko mbali, ingawa kinaweza kuletwa..
Shida sasa…
“Chiziza” Alijisemea Upodo pasi na kujua kuwa simu bado ilikuwa hewani… Akaiweka mezani, akavua kikofia kidogo alichokuwa amekibandika kichwani, akakuna upara wake ulikuwa umezungukwa na mvi kwa mbali. Akashusha pumzi ndefu zilizotoka na aina fulani ya mlio kama wa vuvuzela.
Alichodhani kipo, sicho alichokikuta!
******
Simu ilipigwa…
Mazungumzo yakafanyika… Zulfa akaombwa asaidiane na kina mama wengine wawili, mmoja aliyekuwa rafiki mkubwa wa Clifford akifanya kazi kama muuguzi wa afya katika hospitali ya Mkoa wa Singida, kuwa wafanye juu chini kumchukua yule mtoto kule hospitali na kuja naye Mwanza upesi. Kazi ile ikafanywa kwa upesi na mpaka kufikia saa nne ya usiku, walikuwa wanaanza safari ya kutoka Singida kuelekea Mwanza.
Mwili wa Neema ukashushwa na kupelekwa tena chumba cha maiti katika hospitali ya Rufaa ya Bugando ili usije kuharibika wakati ule wa sintofahamu. Waombolezaji wale wakagawana majukumu na namna ya kujikimu ikawekwa sawa, na ikaonekana kuwa, wengi walikuwa na ndugu, marafiki au jamaa pale Mwanza. Wakaenda kujisitiri huko.
Kazi ikabakia moja tu..
Kumshawishi Chiziza!!
Ee bwana wee!!
Upodo aliongea, Tegu akasema, Laswai akadakia, Ng’wanzalima naye akaweka neno, Makamba akaweka na uswahili kidogo, lakini ngoma ilikuwa inadundwa bila kutoa mlio. Mtu pekee aliyebaki kuwa na msaada akaonekana kuwa ni Clifford mwenyewe.
Usiku kucha wazee wale walifanya walichoweza lakini hakukuwa na matumaini. Asubuhi ya siku iliyofuata ikafika.
Siku ya nne tangu Neema aage dunia!!
Clifford alifanya maamuzi magumu!!
“Nataka niongee na Baba mimi mwenyewe, tafadhali wazee hebu niruhusuni” Alisema Clifford macho yakiwa mekundu kupita kiasi.
“Aah. Lakini Clifford, kwanini tusinge…” Aliingiliza Mzee Babudi
“Hapana.. Hebu tumpe nafasi.. Mwacheni ajaribu.. Damu nzito kuliko maji kumbukeni” Alishauri Upodo akiwa anaonekana mchovu kupita kawaida.
Simu ikapigwa, ikaita!!
“Shkamoo baba” Alisalimu Clifford akionekana kulemewa na machozi
“Ningekuwa namfahamu baba anayedharaulika kama mimi ningemtafuta ili tuunde umoja wa kina baba wapumbavu Tanzania” Alijibu Chiziza.
“Baba.. Sijawahi kuacha kukuheshimu Baba yangu” Alijieleza Clifford
“Iambie maneno hayo maiti ya huyo binti wa watu.. Iambie kuwa wewe Clifford, ulimuheshimu sana baba yako mzazi na ulimshirikisha hata juu ya mpango wako wa kuoa.. Iambie, iambie baradhuli mkubwa weye…” Chiziza alinguruma.
“Siwezi kushindana na wewe hata kwenye ujinga baba yangu.. Hata kwenye kuchezea matope ni wewe ndiwe ulikuwa mwalimu wangu, siwezi kukushinda. Wewe umenizaa na umenifikisha hapa nilipo. Kujifunga mkanda na kutaka kushindana na wewe ni kuiambia dunia kuwa elimu yangu haijawahi kunisaidia. Ujanja wangu kwako ni upumbavu mtupu, na hamna chochote kinachonifanya kuwa bora kuliko wewe baba angu” Clifford alisema huku chozi likimtoka.
Kwa mara ya kwanza kwenye maisha yake, alikuwa amemjibu mzee Chiziza jambo na kisha mzee huyo akaacha kusema. Ikamlazimu kuendelea.
“Mimi ni mtoto mjinga ambaye daima sitakua mwerevu mbele yako. Baba, si kwamba dunia nzima ina akili kama ulivyo wewe. Mimi ni mtoto, na huenda hata wewe hungependa kunikumbatia chini ya mbawa zako daima. Kuna wakati unaniacha niende huku na kule kuokota okota kama kifaranga. Si yote ninayokutana nayo yanafanana na yale unayonipa wewe baba. Sio akina baba wote wana busara kama za kwako. Lakini ni wewe wa kunifanya nijione niko salama tena baba yangu. Hata pale kila mtu anaponifungia mlango, nakuwa na Imani kuwa upo mlango mmoja ambao haujafungwa. Na mlango huo ni wewe baba” Clifford machozi yalikuwa yakimtoka.
“Anhaaa.. Kwahiyo unafanya upuuzi wako kwa vile unajua kuwa Mzee Chiziza ataelewa tu, si ndio? Sasa imekula kwako fala wee.. Malizia mwenyewe ujinga uliouanza, fisi maji wewe” Alijibu Chiziza lakini ni wazi kuwa , hakuwa na hasira kama awali.
“Hapana baba.. Hapana hata kidogo. Kama leo nikiulizwa nimtaje baba aliye bora kuliko wote duniani, bado Mzee Chiziza anabaki kuwa the best. Ni wewe uliyenizaa na kila kitu chema ninachokifanya kimetoka kwako. Haya mabaya yooote ninayoyafanya nakiri tu kuwa nimetoa kwingine, lakini sio kwako baba yangu. Mimi sit u fisi maji.. Ni zaidi ya hata hayawani wote wa mwituni, majini nan chi kavu” Alijieleza Clifford.
“Acha kuniremba hapa. Kila mtu anakosea duniani..” Chiziza alijibu. Ilikuwa ni mara ya kwanza katika maisha yake Clifford kusikia kauli ile kutoka kwa Chiziza!!! Damu ikamsisimka. Bila kujielewa akajikuta akisema.
“Umesema sawa baba, daima najua kuwa kila mtu anakosea. Lakini napiga magoti yangu mbele yako leo baba, sio ili kuanza kukumbushana kuwa nani alikosea wapi, na kwanini. Leo hii, kuna baba ambaye mtoto wake yupo kwenye jokofu kwa siku ya nne leo. Kuna baba ambaye yeye pia anajua kuwa kila mtu anakosea, na anaugulia kifo cha mtoto wake.. Sitaki awepo baba mwingine atakayeumia kwa kupoteza mtoto wake Mzee Chiziza!” Clifford alisema kwa utulivu uliowatisha wenzake.
Hewala!! Wazee wale nywele za shingo ziliwasimama!! Hakuna hata mmoja aliyetegemea kauli nzito kama ile kutoka kwa Clifford. Mzee Upodo akafuta chozi!
“Kwahiyo unanitisha kuwa nawe unaweza kufa sio? Unataka ujiue ili nami niwe baba mwingine anayelilia mtoto sio?” Sauti kavu ya Chiziza ilihoji.
“Hapana baba.. Siwezi kukutisha kwa kujiua hata siku moja. Nikifa leo ili kukukomoa, sitakuwa nimejifunza chochote. Kama niliwahi kukuita baba kwa kumaanisha, nadhani wakati huu nakuita baba nikiwa namaanisha mara mia zaidi. Sikuwahi kujua jukumu lililopo mabegani mwa baba. Wakati huu ninapoongea na wewe, na mimi ni baba. Nami ni baba wa mtoto mmoja. Kuna kiumbe sasa kinaniangalia na kusema “baba, baba”. Nitakuwa baba wa ajabu zaidi duniani kama nitakiacha kiumbe hiki kiendelee kuchekwa na dunia wakati mimi baba yake nikiwa hai!” Alimaliza Clifford.
Halafu…
Kimya!!!
“Mwili wa marehemu mmeuhifadhi wapi?” Katika hali isiyo ya kawaida, Mzee Chiziza alibadili uelekeo wa mazungumzo baada ya kimya kifupi.
Ndani ya dakika arubaini, Mzee Chiziza, Mkewe pamoja na dada mkubwa wa Clifford aitwaye Claritha ambaye kwa bahati tu alikuwa jijini Dar es salaam kibiashara walikuwa njiani kuelekea uwanja wa ndege ili kuelekea jijini Mwanza.
Joto lilirejea.
Taarifa ilitolewa kwa Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu juu ya ugeni ule ili taratibu za msiba zianze mara moja. Kweli kabisa. Nusu saa tu tayari nguvukazi ilikuwa ikishambulia majukumu kama mchwa. Ilipangwa kuwa, siku hiyo jioni kifanyike kikao kikubwa cha familia zote mbili na kuweka mambo sawa, na panapo majaliwa, kesho yake mazishi yafanyike.
Naam..
Walikuwa wakimngoja Chiziza…
Na wakati huo, kumbe walikuwa wakingoja kizaazaa kingine cha karne!!
Ama kweli likiandikwa, litatimia!!
******
 
ZAWADI YA ADHABU

SEHEMU YA MWISHO

Nimefundishwa kuwa…
Si lazima uanze kila jambo likiwa katika ubora mkubwa. Hata magwiji wa elimu wanaamini kuwa, awali yaweza kuwa na changamoto zake nyingi tu. Lakini, daima lenga kuhitimisha kila jema unalolifanya kwa mafanikio makubwa. Azimia kuwa, ni muhimu kukamilisha kila unachokifanya kwa namna ambayo watu wote wataamini kuwa, daima ulikuwa ukilenga kufanikisha kwa mafanikio. Hatima nzuri sio tu inakupa moyo wa kuanza tena kwa nguvu, lakini inawajengea wengine Imani kuwa, misukosuko ya njiani haiwezi kuzuia mwisho Mwema wa safari!!
Una hiyari ya kukubali au kukataa….
******
*** NAWAANDIKIA HAYA KATIKA TAMATI ***
Jua liliwaka, likafika utosini…
Adhana ya alasiri ilimkuta Chiziza na familia yake wakiwa wamewasili jijini Mwanza, na wakafikia Charity Hotel. Ingawa alishawaeleza mkewe nab inti yake juu ya yaliyomkuta Clifford, bado yeye pia alitamani amwone Clifford na amweleze mwenyewe kwa kinywa chake Mwanzo mpaka mwisho wa kisa kile. Waliyozungumza asubuhi ile yalionekana kumuingia moyoni mwake na hapa na pale alitamani kumwona Clifford.
Kwa mara ya kwanza katika maisha yake, Chiziza alisikia uchungu usio wa kawaida!!
Naam.. Kikao cha kwanza kikakubaliwa kufanyika Charity Hotel. Wazee wale wale watano wakaongozana na Clifford hadi hotelini na baada ya hatua zote za utambulisho, mazungumzo yakaanza.
Wale wazee watano walikuwa wakimtumbulia macho Mzee Chiziza na familia yake kama vile walikuwa wakiwatoka sayari nyingine. Hapa na pale, walionekana wakinong’ona peke yao lakini ule ukali na uimara wa Chiziza uliwatisha! Ingawa hakuoneka kuwa mkubwa sana kuwazidi, alikuwa akiongea kwa mamlaka na kuhoji hapa na pale. Walizungumza kwa zaidi ya saa moja na hapo wakakubaliana kuanza safari ya kuelekea kwa mzee Masalu. Wakati huu, Clifford naye akaruhusiwa kuambatana nao!
Safari ya kwa Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu ikaanza. Njia nzima, wazee wale watano walikuwa wakikonyezana na kuzungumza kwa ishara, lakini ni kama kila mara Mzee Chiziza alikuwa akiwanyima uhuru. Mzee Upodo akanyanyua kinywa ili kusema jambo, lakini Mzee Tegu akamuwahi na kumkanyaga kwa nguvu huku yeye mwenyewe akipaza sauti na kuuliza.
“Vipi hali ya hewa ya Mjini bwana Chiziza.. Kule joto majira yote bwana” Alihoji Mzee Tegu.
“Umefanya vema kujiuliza na kujijibu bwana mkubwa” Jibu rahisi lilimtoka Chiziza.. Tegu akafikicha mikono na kuegamia kiti… Uso umemshuka na joto kali likimpita kwenye makwapa na sehemu nyingine muhimu.
Aliishiwa kauli!!
Kimya kikatanda hadi walipofika kwa Masagida Kaswalala Masalu..
******
Giza lilikuwa linaanza kubisha hodi kwa mbali, na nyumba ilikuwa na pilika pilika kiasi. Gari mbili zikawasili kwa pamoja. Moja walishuka Chiziza, Clifford aliyekuwa akiendesha, Tegu, Upodo na Claritha. Gari jingine wakashuka Mkewe Chiziza, Mzee Ng’wanzalima, Mzee Lasway, Mzee Makamba na Mzee Amri. Wajumbe wengine kutoka Singida walipaswa kufika baadae baada ya mazungumzo ya awali. Wageni wakapokelewa sebuleni, ingawa kila walikopita, miguno ilikuwa ikibaki nyuma huku wao wakisonga mbele.
Kuna jambo halikuwa saw ahata kidogo..
Hata kidogo, Hapana!!!
Sebule pana ilikuwa tayari na watu nane.. Watu kumi wakazidi kuinyanyasa kwa kuingia na kusambaa. Ilikuwa ni bahati kubwa kwamba, Masagida Kaswalala Masalu hakujenga nyumba ile kichoyo.. Ilikuwa sebule pana iliyoweza kuwachukua wote ingawa wengine walilazimika kuketi kwenye mkeka uliokuwa chini.
Kimya kikuu kikatanda…
Alikuwa anangojwa baba mwenye mji, Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu ili afike na mnakasha uanze.
Akafika!
Halafu!!
Kila mtu alibaki kimya…
Kioo kimoja kilikuwa kimesimama mbele ya kingine..
Kama vile walioambiwa na mtu, Mzee Chiziza na Mzee Masagida Kaswalala Masalu wakasimama na kutazamana.
Kilikuwa kituko cha mwaka!!
Alikuwa ni mtu mmoja aliyevalia mavazi tofauti… Walifanana kuliko mayai ya kuku wa kisasa yanavyoweza kufanana. Walikunja sura kwa pamoja, hapo wakazidi kuwashangaza waliokuwa wakiwatazama..
“Wewe … Ndiye mwenye nyumba?” Alianza Chiziza huku akimtazama vizuri mwenyeji wake.
“Naam.. Karibu.. Kwani wewe ni…” Alijibu Masagida Kaswalala Masalu
“Nimeuliza swali moja.. Ningependa lijibiwe kwanza” Chiziza alijibu haraka.
“Ndiye haswa.. Kwani wewe ni nani? Aliuliza tena Masagida..
“Mzee Chiziza.. Ni baba yake na …” Alianza Mzee Chiziza.
“Kuwa mstaarabu.. Habari za umezaa watoto wangapi nitakuuliza baadae” Masagida akajibu kwa haraka.
“Lakini.. Nahisi kama vile…..” Chiziza alianza tena, lakini akakatizwa.
“Kuhusu hisia zako tutaongea tukiwa na muda, keti tujadili uhalisia” Masalu alijibu huku akiketi.. “Nilikuwa na wazo.. Nadhani tuanze na…” Aliendelea Masalu, lakini naye hakumaliza.
“Habu tuachane na wakati uliopita.. Kama ulikuwa na wazo sio pahala pake hapa. Nadhani kama una wazo ndio tuanze nalo” Chiziza alisema huku akiketi.
Upodo, Makamba, Lasway, Tegu, Babudi na Ng’wanzalima waliangaliana kwa haraka. Hali ya sintofahamu ilikuwa imetawala.
Utambulisho ukaanza mara moja na baada ya utambulisho, mazungumzo yakaanza. Lakini hakuna aliyetaka kujadili kuhusu msiba kwanza. Wazee wale wawili wakawa ndio wa kuzungumziwa pale. Hata wao walionekana kuwa na sintofahamu, lakini upesi, Chiziza akasafisha koo lake na kujiweka sawa, kisha akasimulia.
***
Anasimulia Chiziza
Kwakweli nashindwa kuelewa ikiwa hiki ninachokipitia ni ndoto ama la, lakini naona kuna jambo fulani zito hapa. Mimi jina langu la kwanza ni Adolph.. Sijui ni nani hasa alinipa jina hili, lakini ninachojua ni kuwa, nilikuwa mtoto pekee wa Mzee Aidani Chiziza na mkewe Anastella. Mzee Chiziza alikuwa ni mfanyabiashara maarufu sana jijini Dar es Salaam, lakini hakuwa kuniambia hasa asili yake ni wapo ingawa baadae nilikuja kujua kuwa, alikuwa mgogo wa Dodoma.
Nilikuwa peke yangu nyumbani kwetu, na nililelewa kwa ukwasi kiasi kutokana na hali ya kiuchumi ya Mzee Aidani.
Hata hivyo, wakati nilipokuwa na akili timamu kabisa, mara kwa mara nilikuwa nikimsikia mama akilalamika kwa baba kuwa, kuna watu walikuwa wanamsema na kumcheka kuwa amebaki kuokotaokota watoto, lakini sikuelewa chochote. Wakati nilipofika darasa la saba, mama yangu alifariki kwa ugonjwa wa kansa ya kizazi. Nikabaki na baba yangu ambaye alinilea kwa upendo mkubwa mpaka nilipoingia kidato cha kwanza.
Pengo la mama yule halikuniathiri mimi peke yangu. Hata baba alionekana mara kwa mara akiwa na mawazo kupita kiasi na kuna wakati alikuwa akiniangalia kwa huzuni sana na kutoa machozi. Sikujua nini hasa kilimliza baba na kuna wakati mimi nami nilijikuta nikilia pamoja naye.
Siku moja usiku, baba aliniita na tuliongea naye kwa muda mrefu sana. Kwenye mazungumzo yake, alikuwa akiomba sana kuwa, siku moja nikiwa mtu mzima, niende nikaishi Mwanza. Sikuwa namwelewa kwa kuwa hakuniambia kwanini alitaka nifanye vile, lakini nilimkubalia na baadae akaniruhusu nikalale.
Siku iliyofuata, nakumbuka ilikuwa siku ya jumapili, nilimwamsha baba ilitujiandae kwenda kanisani kama kawaida yetu. Lakini baba hakuamka. Nikahisi huenda kule kuchelewa kulala kulikuwa kumemchosha, hivyo nikaamua kwenda peke yangu na kumwacha. Hata niliporudi, hali ilikuwa vilevile. Bado alikuwa amelala.
Baadae, iligundulika kuwa, Mzee Aidani alikuwa amefariki dunia. Nilihisi dunia nzima ikiniacha peke yangu!! Ingawa ndugu walikuja na kunifariji, sikuwa nimewazoea na sikuwahi hata siku moja kwenda kwa ndugu!!
Tukazika salama! Lakini baada tu ya mazishi, ndipo kikao cha familia kikaambiwa ukweli. Kwamba wakati mimi naletwa pale nyumbani, mama yangu hakuwa na mimba yoyote na baadae akasema kuwa amejifungua. Ndugu walipotaka sana kujua ukweli, baba yangu aliwajibu kuwa,nilitolewa kwenye kituo cha watoto yatima kwa kuwa yeye (baba yangu) na mama yangu walikuwa wameshatumia miaka ishirini ya ndoa bila kuwa na mtoto, na hivyo waliamua kupata mtoto hata kwa kuasili.
Niliumia sana siku ile!! Niliwaza sababu ya baba yangu kuniambia nije Mwanza. Familia ile ikanitenga, lakini sikuwa hata kwangu pia ilikuwa na nafuu. Sikutaka tena kuishi kinyonge. Nikaendelea kujibana bana pale nyimbani mpaka nilipomaliza kidato cha nne. Nafasi zikatoka na nikaenda jeshini, na tangu wakati huo, sikuwahi kujua habari zao tena!!!
Nilipokuwa jeshini, kuna bwana mmoja kutoka Mwanza alikuwa akipenda sana kuniita Teacher.. Siku moja nilipomuuliza, alinicheka na kuniambia.. “Mwalimu hata kama umekimbia chuo cha ualimu na kuingia jeshi, wewe ni mwalimu tu”..
Nilipuuza kauli ile na kuendelea na maisha yangu ya jeshi. Nikahitimu na kulitumikia jeshi hadi nilipostaafu kwa hiyari ili nifanye mambo yangu. Lakini maisha yangu yote, nimekutana na zaidi ya mtu mmoja ambao kila mara wanaishia kuniangalia sana na kuondoka bila kusema neno, au pale ninapowagombeza kwa kuniangalia ovyo!!
Sasa nashindwa kujua huyu aliyesimama mbele yangu leo ni nani hasa
******
Kikao kilizizima!
Kila mmoja mdomo ulikuwa wazi!!
Ni mtu mmoja tu ambaye alionekana kuwa na cha kusema lakini hata hivyo alikuwa na wasiwasi mwingi..
“Kwa kweli sijui kama hiki ninachokiona ndicho ama naota.. Lakini nakumbuka nilikuwa binti mwenye ufahamu wakati wifi alipokuwa mjamzito. Akiwa hospitali ambako alilazimishwa kwenda baada ya kanisa kujenga hospitali pale kijijini, kuna taarifa zilikuja kuwa wifi yetu ameleta mkosi nyumbani”.
“Tuliambiwa kuwa, amepata watoto wawili. Wazee walikusanyika na kuanza kupanga nini cha kufanya. Watoto hatukuruhusiwa kusogelea karibu na watu wazima walipokuwa wanajadili.. Lakini baadae, tulisikia kutoka kwa kina mama kuwa, watoto wale wangeuwawa baada ya kufika nyumbani” Alizungumza mama mmoja mtu mzima kabisa ingawa kwa mbali alionekana na nguvu kiasi”.
“Tulingoja wifi arudi na watoto wawili kwa kuwa hatukuwahi kuona watoto wawili wachanga kwa pamoja, lakini baadae alipokuja, haikuwa hivyo. Alikuwa na mtoto mmoja tu.. Basi ile habari iliishia pale. Sasa leo hiki nnachokona….” Alimaliza mama yule.
******
Mjadala uliendelea mpaka karibu saa sita usiku.. Ya Adolph Chiziza na Masagida Kaswalala Masalu yalikuwa pasua kichwa. Kwanza kuna saa wao wenyewe walikuwa wakibadilikiana kupita maelezo.
“Nimeuliza swali Mzee, maelezo yako ni mazuri lakini siyahitaji” Chiziza alianza
“Swali la jibu hilo ninalo, tafadhali tunza jibu lako utalitoa baadae” Masalu naye akalipuka
“Nisikilize bwana, hata wanasayansi wanasema…” Alijaribu Masalu
“Achana na wanasayansi, nisikilize mimi” Chiziza akadakia!
Hata kama wasingekuwa mapacha wa kuzaliwa, tabia zao tu zilitosha kuwaita mapacha!!
***
Mwili wa Neema ulizikwa!!
Kila mtu alikuwa akiongea lake!
Juu ya nini kilitokea hata Chiziza na Masalu wakatenganishwa utotoni hakuna aliyekuwa na haja ya kukitafuta. Ukweli kuwa jamii nyingi zamani zilikuwa na utamaduni wa kuamini kuwa mapacha ni dalili ya laana ilijadiliwa, na kukawa na uwezekano kuwa, huenda wakati wakiwa hospitali pale, mtoto mmoja aliruhusiwa kuondoka na mama yake na mwingine akabaki na kutafutiwa malezi sehemu nyingine.
Hakuna aliyetaka kujua sana. Wazee wawili wakorofi walikuwa wamekutana, na kwa mara ya kwanza kwa ndugu zao, walionekana muda mwingine wakiongea na kucheka huku wakijitenga na watu wengine.
Damu nzito kuliko maji..
Halafu sasa kuhusu damu…
Ilishatokea.. Watoto wa ndugu wawili wamekutana na kuzaa mtoto.. Ndugu wawili waliopotezana wamekutana.. Alimuradi kila mtu alizungumza la kwake. Lakini ukweli ukabaki palepale.
Hakukuwa na haja ya DNA kupima undugu wa Adolph Chiziza na Masagida Kaswalala Masalu!
Matanga yalivunjwa na taratibu za kumpa jina mtoto wa Clifford zikafanyika. Hakukuwa na jina jingine zaidi ya kumwita Neema, na familia ambayo sasa ilikuwa umeunganika na kuwa moja, ikaridhia. Taratibu zote za kimila zikafanyika. Ndugu wakaitwa na wakatambuana. Wa kupigwa faini akapigwa na wa kusemwa akasemwa.
Watoto wakakumbushwa tena umuhimu wa kufuata taratibu hasa katika mambo muhimu kama vile kuoa, wakakumbushwa ubaya wa kuamua tu kuishi na mtu pasipo kuwafahamu vema ndugu zake, wale waliokuwa wakiishi pasi na ndoa wakanyooshewa vidole na kupewa muda wa kufanya maamuzi upesi pamoja ne mengine mengi. Wazazi nao wakakumbushana yaliyowahusu. Chiziza na pacha wake wakapanga ni lini wanakwenda kuyatembelea makaburi ya wazazi wao huku Chiziza kwa mara ya kwanza katika maisha yake akiuhisi sasa uchungu hasa wa kutokuwa na wazazi.
Ni wakati huu ndipo alipokumbuka pia, pamoja na vifo vya wazazi waliomlea na kumpa jina, moyo wake ulikuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuwahifadhi japo kwa kumbukumbu ya picha tu wazazi wake halisi!!
Wakaonyana na kuwekana sawa, wakapena mikono na kubadilishana namba za simu. Wakapiga na picha za familia pamoja na “selfie”.
Chiziza akarejea Dar es Salaam akiwa na Amani ya kumjua ndugu yake, familia yake na ukoo wake.
Clifford alirudi Singida na kuendelea na majukumu yake kwa muda. Moyoni mwake alishaamua kuwa, sehemu iliyobaki ya maisha yake angeitumia akiwa Singida kwa namna wakazi wale walivyokuwa faraja wakati wa dhiki kuu iliyomfikia. Ingekuwa ngumu kwake kumchukua mwanae Neema na kuishi naye, hivyo familia nzima ilikubali kuwa, Neema aende akaishi kwa shangazi yake Claritha, dada yake na Clifford mpaka Clifford atakapokuwa tarayi kumchukua na kuishi naye.
Baada ya miezi miwili tangu mkasa wa kifo cha Neema, Clifford alikuwa jijini Dar es Salaam kumsalimu Baba yake..
“Kijana… Nadhani sasa umejifunza nini maana ya ukali wangu juu ya maswala yahusuyo familia. Ujinga ulioufanya awali, na labda unaoendelea kuufanya hata sasa maana inawezekana bado hujajifunza, wa kukutana tu na mwanamke na kuzoana ulitaka kuitoa roho yako. Lakini hakuna kosa kubwa kama kuishi na mtoto wa mtu bila kutoa taarifa kwa ndugu. Unaweza kuingia matatizoni mpaka ukahisi dunia hii ni chungu..” Mzee Chiziza alieleza.
“Ni kweli baba.. Unakumbuka nilichokuambia mara ya mwisho kabla hujaja Mwanza?”
“Naam.. Nakumbuka”
“Well.. Wakati wa nyuma, sikuwa nakuelewa vizuri ulipokuwa ukizungumza kama Baba.. Lakini sasa, najifunza kuwa, nitakapoamua kuoa, sipaswi tu kuangalia kuwa ni kiasi gani niko tayari kuoa peke yake, au watu wengine wananiambia nini kuhusu kuoa.. Napaswa kujichukulia kwanza kama Mume, lakini zaidi, bila kujali iwapo nina mtoto au la, nijichukulie kama BABA!!
“Na ndio maana niliamua kukupa adhabu ili akili ikae sawa. Na ole wako urudie Clifford.. Hakyamungu nakuapia nakunyongelea mbali, mbulula weye” Ingawa aliyasema kiutani, kulikuwa na chembe za hasira katika kauli yake.
“Mzee Chizi.. Wala hujanipa adhabu.. Hii imekuwa ni zawadi kubwa sana kuipokea kutoka kwako. Umenipa zawadi ya adhabu. Zawadi ambayo imeukomaza moyo wangu na kunifanya imara. Hakika zawadi ya adhabu uliyonipa imenibadili. Ikiwa hili halijanibadili, hakuna lingine lolote chini ya jua litakalonifundisha baba angu” Alimaliza Clifford.
******
Geti kubwa la nyumba ya Mzee Chiziza lilikuwa likigongwa kwa nguvu. Haraka, Clifford alinyanyuka kwenda kufungua huku kule kukatishwa mazungumzo na baba yake kukimkera waziwazi.
“Nahisi kama Janeth ameenda kufungua, ama?” Alisema Mzee Chiziza huku naye akionekana kutamani kukaa karibu na mwanae.
“Achana na hisia mzee na rudi kwenye uhalisia, Janeth na mama wameenda mjini kitambo tu. Umekuwa msahaulifu tena?” Alisema Clifford huku akiufikia Mlango.
“Pumbavu kabisa. Clifford nitakupiga risasi we chalii. We sio wa kunijibu jibu kisanii mimi” Chiziza alisema huku akisimama kwa utani.
“Nilikuuliza swali mzee, hilo tusi ungeliweka akiba, utalihitaji baadae. Halafu sikujua kuwa nawe huwa ni msanii unayewajibu wenzako kisanii” Clifford alibamiza mlango huku akikwepa mto mdogo wa kochi aliorushiwa na Mzee Chiziza na kuelekea getini.
Alifungua mlango na kuchungulia nje.
Gari yake nyeusi ambayo mara moja aliitambua kuwa ni ile iliyopotea kihuni ilikuwa imepaki ikiwa tupu ndani, huku mtu fulani akionekana kuanza kuondoka eneo lile.
“Oyaa.. Vipi? Nani?” Aliuliza Clifford..
Mtu yule akageuka na kumtazama kwa macho yaliyolegea na kuonekana kuchoka.. Alitia huruma
Alikuwa Nunu!

*************** MWISHO***************
Mungu ni mwaminifu na kazi zake ni takatifu!
Nunu atarudi tena!!
***********
Nakushukuru sana msomaji na msikilizaji wa simulizi hii kwa kuwa sehemu ya kazi hii tangu mwanzo mpaka kituo cha mwisho. Sijajua imekuwa ni safari ya aina gani kwako, lakini kwangu imekuwa ni neema ya nguvu ya Mungu kunipa nafasi ya kuyabadili mawazo yangu kuwa simulizi hii. Ni faraja kwangu pia kujua kuwa, huenda kuna sehemu ya maisha ya mtu fulani imebadilika baada ya kusoma au kusikiliza simulizi hii.
Ni wazi kuwa, hata nawe umejifunza jambo. Lichukue na kulihifadhi moyoni. Kama halitakufaa siku ya mvua, litakusitiri siku ya jua. Na kama halitakunufaisha katika maisha yako, ligawe kwa mwenzako, huenda likawa ni Mwanzo mpya wa maisha ya mtu mwingine.
Kwa uzito wa kipekee pia,
Izingatiwe kuwa simulizi hii ni kazi ya Sanaa. Iwapo mazingira, majina ya wahusika au mfululizo wa matukio unafanana na tulio lolote halisi, tafadhali ichukuliwe kuwa imetokea hivyo kwa bahati mbaya tu na kama matokeo ya kazi ya sanaa na wala haikukusudiwa.
Endelea kuwasiliana nami kwa nambari ya simu +255 763 305 605 kwa ushauri na maoni.
 
ZAWADI YA ADHABU

SEHEMU YA MWISHO

Nimefundishwa kuwa…
Si lazima uanze kila jambo likiwa katika ubora mkubwa. Hata magwiji wa elimu wanaamini kuwa, awali yaweza kuwa na changamoto zake nyingi tu. Lakini, daima lenga kuhitimisha kila jema unalolifanya kwa mafanikio makubwa. Azimia kuwa, ni muhimu kukamilisha kila unachokifanya kwa namna ambayo watu wote wataamini kuwa, daima ulikuwa ukilenga kufanikisha kwa mafanikio. Hatima nzuri sio tu inakupa moyo wa kuanza tena kwa nguvu, lakini inawajengea wengine Imani kuwa, misukosuko ya njiani haiwezi kuzuia mwisho Mwema wa safari!!
Una hiyari ya kukubali au kukataa….
******
*** NAWAANDIKIA HAYA KATIKA TAMATI ***
Jua liliwaka, likafika utosini…
Adhana ya alasiri ilimkuta Chiziza na familia yake wakiwa wamewasili jijini Mwanza, na wakafikia Charity Hotel. Ingawa alishawaeleza mkewe nab inti yake juu ya yaliyomkuta Clifford, bado yeye pia alitamani amwone Clifford na amweleze mwenyewe kwa kinywa chake Mwanzo mpaka mwisho wa kisa kile. Waliyozungumza asubuhi ile yalionekana kumuingia moyoni mwake na hapa na pale alitamani kumwona Clifford.
Kwa mara ya kwanza katika maisha yake, Chiziza alisikia uchungu usio wa kawaida!!
Naam.. Kikao cha kwanza kikakubaliwa kufanyika Charity Hotel. Wazee wale wale watano wakaongozana na Clifford hadi hotelini na baada ya hatua zote za utambulisho, mazungumzo yakaanza.
Wale wazee watano walikuwa wakimtumbulia macho Mzee Chiziza na familia yake kama vile walikuwa wakiwatoka sayari nyingine. Hapa na pale, walionekana wakinong’ona peke yao lakini ule ukali na uimara wa Chiziza uliwatisha! Ingawa hakuoneka kuwa mkubwa sana kuwazidi, alikuwa akiongea kwa mamlaka na kuhoji hapa na pale. Walizungumza kwa zaidi ya saa moja na hapo wakakubaliana kuanza safari ya kuelekea kwa mzee Masalu. Wakati huu, Clifford naye akaruhusiwa kuambatana nao!
Safari ya kwa Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu ikaanza. Njia nzima, wazee wale watano walikuwa wakikonyezana na kuzungumza kwa ishara, lakini ni kama kila mara Mzee Chiziza alikuwa akiwanyima uhuru. Mzee Upodo akanyanyua kinywa ili kusema jambo, lakini Mzee Tegu akamuwahi na kumkanyaga kwa nguvu huku yeye mwenyewe akipaza sauti na kuuliza.
“Vipi hali ya hewa ya Mjini bwana Chiziza.. Kule joto majira yote bwana” Alihoji Mzee Tegu.
“Umefanya vema kujiuliza na kujijibu bwana mkubwa” Jibu rahisi lilimtoka Chiziza.. Tegu akafikicha mikono na kuegamia kiti… Uso umemshuka na joto kali likimpita kwenye makwapa na sehemu nyingine muhimu.
Aliishiwa kauli!!
Kimya kikatanda hadi walipofika kwa Masagida Kaswalala Masalu..
******
Giza lilikuwa linaanza kubisha hodi kwa mbali, na nyumba ilikuwa na pilika pilika kiasi. Gari mbili zikawasili kwa pamoja. Moja walishuka Chiziza, Clifford aliyekuwa akiendesha, Tegu, Upodo na Claritha. Gari jingine wakashuka Mkewe Chiziza, Mzee Ng’wanzalima, Mzee Lasway, Mzee Makamba na Mzee Amri. Wajumbe wengine kutoka Singida walipaswa kufika baadae baada ya mazungumzo ya awali. Wageni wakapokelewa sebuleni, ingawa kila walikopita, miguno ilikuwa ikibaki nyuma huku wao wakisonga mbele.
Kuna jambo halikuwa saw ahata kidogo..
Hata kidogo, Hapana!!!
Sebule pana ilikuwa tayari na watu nane.. Watu kumi wakazidi kuinyanyasa kwa kuingia na kusambaa. Ilikuwa ni bahati kubwa kwamba, Masagida Kaswalala Masalu hakujenga nyumba ile kichoyo.. Ilikuwa sebule pana iliyoweza kuwachukua wote ingawa wengine walilazimika kuketi kwenye mkeka uliokuwa chini.
Kimya kikuu kikatanda…
Alikuwa anangojwa baba mwenye mji, Mwalimu Masagida Kaswalala Masalu ili afike na mnakasha uanze.
Akafika!
Halafu!!
Kila mtu alibaki kimya…
Kioo kimoja kilikuwa kimesimama mbele ya kingine..
Kama vile walioambiwa na mtu, Mzee Chiziza na Mzee Masagida Kaswalala Masalu wakasimama na kutazamana.
Kilikuwa kituko cha mwaka!!
Alikuwa ni mtu mmoja aliyevalia mavazi tofauti… Walifanana kuliko mayai ya kuku wa kisasa yanavyoweza kufanana. Walikunja sura kwa pamoja, hapo wakazidi kuwashangaza waliokuwa wakiwatazama..
“Wewe … Ndiye mwenye nyumba?” Alianza Chiziza huku akimtazama vizuri mwenyeji wake.
“Naam.. Karibu.. Kwani wewe ni…” Alijibu Masagida Kaswalala Masalu
“Nimeuliza swali moja.. Ningependa lijibiwe kwanza” Chiziza alijibu haraka.
“Ndiye haswa.. Kwani wewe ni nani? Aliuliza tena Masagida..
“Mzee Chiziza.. Ni baba yake na …” Alianza Mzee Chiziza.
“Kuwa mstaarabu.. Habari za umezaa watoto wangapi nitakuuliza baadae” Masagida akajibu kwa haraka.
“Lakini.. Nahisi kama vile…..” Chiziza alianza tena, lakini akakatizwa.
“Kuhusu hisia zako tutaongea tukiwa na muda, keti tujadili uhalisia” Masalu alijibu huku akiketi.. “Nilikuwa na wazo.. Nadhani tuanze na…” Aliendelea Masalu, lakini naye hakumaliza.
“Habu tuachane na wakati uliopita.. Kama ulikuwa na wazo sio pahala pake hapa. Nadhani kama una wazo ndio tuanze nalo” Chiziza alisema huku akiketi.
Upodo, Makamba, Lasway, Tegu, Babudi na Ng’wanzalima waliangaliana kwa haraka. Hali ya sintofahamu ilikuwa imetawala.
Utambulisho ukaanza mara moja na baada ya utambulisho, mazungumzo yakaanza. Lakini hakuna aliyetaka kujadili kuhusu msiba kwanza. Wazee wale wawili wakawa ndio wa kuzungumziwa pale. Hata wao walionekana kuwa na sintofahamu, lakini upesi, Chiziza akasafisha koo lake na kujiweka sawa, kisha akasimulia.
***
Anasimulia Chiziza
Kwakweli nashindwa kuelewa ikiwa hiki ninachokipitia ni ndoto ama la, lakini naona kuna jambo fulani zito hapa. Mimi jina langu la kwanza ni Adolph.. Sijui ni nani hasa alinipa jina hili, lakini ninachojua ni kuwa, nilikuwa mtoto pekee wa Mzee Aidani Chiziza na mkewe Anastella. Mzee Chiziza alikuwa ni mfanyabiashara maarufu sana jijini Dar es Salaam, lakini hakuwa kuniambia hasa asili yake ni wapo ingawa baadae nilikuja kujua kuwa, alikuwa mgogo wa Dodoma.
Nilikuwa peke yangu nyumbani kwetu, na nililelewa kwa ukwasi kiasi kutokana na hali ya kiuchumi ya Mzee Aidani.
Hata hivyo, wakati nilipokuwa na akili timamu kabisa, mara kwa mara nilikuwa nikimsikia mama akilalamika kwa baba kuwa, kuna watu walikuwa wanamsema na kumcheka kuwa amebaki kuokotaokota watoto, lakini sikuelewa chochote. Wakati nilipofika darasa la saba, mama yangu alifariki kwa ugonjwa wa kansa ya kizazi. Nikabaki na baba yangu ambaye alinilea kwa upendo mkubwa mpaka nilipoingia kidato cha kwanza.
Pengo la mama yule halikuniathiri mimi peke yangu. Hata baba alionekana mara kwa mara akiwa na mawazo kupita kiasi na kuna wakati alikuwa akiniangalia kwa huzuni sana na kutoa machozi. Sikujua nini hasa kilimliza baba na kuna wakati mimi nami nilijikuta nikilia pamoja naye.
Siku moja usiku, baba aliniita na tuliongea naye kwa muda mrefu sana. Kwenye mazungumzo yake, alikuwa akiomba sana kuwa, siku moja nikiwa mtu mzima, niende nikaishi Mwanza. Sikuwa namwelewa kwa kuwa hakuniambia kwanini alitaka nifanye vile, lakini nilimkubalia na baadae akaniruhusu nikalale.
Siku iliyofuata, nakumbuka ilikuwa siku ya jumapili, nilimwamsha baba ilitujiandae kwenda kanisani kama kawaida yetu. Lakini baba hakuamka. Nikahisi huenda kule kuchelewa kulala kulikuwa kumemchosha, hivyo nikaamua kwenda peke yangu na kumwacha. Hata niliporudi, hali ilikuwa vilevile. Bado alikuwa amelala.
Baadae, iligundulika kuwa, Mzee Aidani alikuwa amefariki dunia. Nilihisi dunia nzima ikiniacha peke yangu!! Ingawa ndugu walikuja na kunifariji, sikuwa nimewazoea na sikuwahi hata siku moja kwenda kwa ndugu!!
Tukazika salama! Lakini baada tu ya mazishi, ndipo kikao cha familia kikaambiwa ukweli. Kwamba wakati mimi naletwa pale nyumbani, mama yangu hakuwa na mimba yoyote na baadae akasema kuwa amejifungua. Ndugu walipotaka sana kujua ukweli, baba yangu aliwajibu kuwa,nilitolewa kwenye kituo cha watoto yatima kwa kuwa yeye (baba yangu) na mama yangu walikuwa wameshatumia miaka ishirini ya ndoa bila kuwa na mtoto, na hivyo waliamua kupata mtoto hata kwa kuasili.
Niliumia sana siku ile!! Niliwaza sababu ya baba yangu kuniambia nije Mwanza. Familia ile ikanitenga, lakini sikuwa hata kwangu pia ilikuwa na nafuu. Sikutaka tena kuishi kinyonge. Nikaendelea kujibana bana pale nyimbani mpaka nilipomaliza kidato cha nne. Nafasi zikatoka na nikaenda jeshini, na tangu wakati huo, sikuwahi kujua habari zao tena!!!
Nilipokuwa jeshini, kuna bwana mmoja kutoka Mwanza alikuwa akipenda sana kuniita Teacher.. Siku moja nilipomuuliza, alinicheka na kuniambia.. “Mwalimu hata kama umekimbia chuo cha ualimu na kuingia jeshi, wewe ni mwalimu tu”..
Nilipuuza kauli ile na kuendelea na maisha yangu ya jeshi. Nikahitimu na kulitumikia jeshi hadi nilipostaafu kwa hiyari ili nifanye mambo yangu. Lakini maisha yangu yote, nimekutana na zaidi ya mtu mmoja ambao kila mara wanaishia kuniangalia sana na kuondoka bila kusema neno, au pale ninapowagombeza kwa kuniangalia ovyo!!
Sasa nashindwa kujua huyu aliyesimama mbele yangu leo ni nani hasa
******
Kikao kilizizima!
Kila mmoja mdomo ulikuwa wazi!!
Ni mtu mmoja tu ambaye alionekana kuwa na cha kusema lakini hata hivyo alikuwa na wasiwasi mwingi..
“Kwa kweli sijui kama hiki ninachokiona ndicho ama naota.. Lakini nakumbuka nilikuwa binti mwenye ufahamu wakati wifi alipokuwa mjamzito. Akiwa hospitali ambako alilazimishwa kwenda baada ya kanisa kujenga hospitali pale kijijini, kuna taarifa zilikuja kuwa wifi yetu ameleta mkosi nyumbani”.
“Tuliambiwa kuwa, amepata watoto wawili. Wazee walikusanyika na kuanza kupanga nini cha kufanya. Watoto hatukuruhusiwa kusogelea karibu na watu wazima walipokuwa wanajadili.. Lakini baadae, tulisikia kutoka kwa kina mama kuwa, watoto wale wangeuwawa baada ya kufika nyumbani” Alizungumza mama mmoja mtu mzima kabisa ingawa kwa mbali alionekana na nguvu kiasi”.
“Tulingoja wifi arudi na watoto wawili kwa kuwa hatukuwahi kuona watoto wawili wachanga kwa pamoja, lakini baadae alipokuja, haikuwa hivyo. Alikuwa na mtoto mmoja tu.. Basi ile habari iliishia pale. Sasa leo hiki nnachokona….” Alimaliza mama yule.
******
Mjadala uliendelea mpaka karibu saa sita usiku.. Ya Adolph Chiziza na Masagida Kaswalala Masalu yalikuwa pasua kichwa. Kwanza kuna saa wao wenyewe walikuwa wakibadilikiana kupita maelezo.
“Nimeuliza swali Mzee, maelezo yako ni mazuri lakini siyahitaji” Chiziza alianza
“Swali la jibu hilo ninalo, tafadhali tunza jibu lako utalitoa baadae” Masalu naye akalipuka
“Nisikilize bwana, hata wanasayansi wanasema…” Alijaribu Masalu
“Achana na wanasayansi, nisikilize mimi” Chiziza akadakia!
Hata kama wasingekuwa mapacha wa kuzaliwa, tabia zao tu zilitosha kuwaita mapacha!!
***
Mwili wa Neema ulizikwa!!
Kila mtu alikuwa akiongea lake!
Juu ya nini kilitokea hata Chiziza na Masalu wakatenganishwa utotoni hakuna aliyekuwa na haja ya kukitafuta. Ukweli kuwa jamii nyingi zamani zilikuwa na utamaduni wa kuamini kuwa mapacha ni dalili ya laana ilijadiliwa, na kukawa na uwezekano kuwa, huenda wakati wakiwa hospitali pale, mtoto mmoja aliruhusiwa kuondoka na mama yake na mwingine akabaki na kutafutiwa malezi sehemu nyingine.
Hakuna aliyetaka kujua sana. Wazee wawili wakorofi walikuwa wamekutana, na kwa mara ya kwanza kwa ndugu zao, walionekana muda mwingine wakiongea na kucheka huku wakijitenga na watu wengine.
Damu nzito kuliko maji..
Halafu sasa kuhusu damu…
Ilishatokea.. Watoto wa ndugu wawili wamekutana na kuzaa mtoto.. Ndugu wawili waliopotezana wamekutana.. Alimuradi kila mtu alizungumza la kwake. Lakini ukweli ukabaki palepale.
Hakukuwa na haja ya DNA kupima undugu wa Adolph Chiziza na Masagida Kaswalala Masalu!
Matanga yalivunjwa na taratibu za kumpa jina mtoto wa Clifford zikafanyika. Hakukuwa na jina jingine zaidi ya kumwita Neema, na familia ambayo sasa ilikuwa umeunganika na kuwa moja, ikaridhia. Taratibu zote za kimila zikafanyika. Ndugu wakaitwa na wakatambuana. Wa kupigwa faini akapigwa na wa kusemwa akasemwa.
Watoto wakakumbushwa tena umuhimu wa kufuata taratibu hasa katika mambo muhimu kama vile kuoa, wakakumbushwa ubaya wa kuamua tu kuishi na mtu pasipo kuwafahamu vema ndugu zake, wale waliokuwa wakiishi pasi na ndoa wakanyooshewa vidole na kupewa muda wa kufanya maamuzi upesi pamoja ne mengine mengi. Wazazi nao wakakumbushana yaliyowahusu. Chiziza na pacha wake wakapanga ni lini wanakwenda kuyatembelea makaburi ya wazazi wao huku Chiziza kwa mara ya kwanza katika maisha yake akiuhisi sasa uchungu hasa wa kutokuwa na wazazi.
Ni wakati huu ndipo alipokumbuka pia, pamoja na vifo vya wazazi waliomlea na kumpa jina, moyo wake ulikuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuwahifadhi japo kwa kumbukumbu ya picha tu wazazi wake halisi!!
Wakaonyana na kuwekana sawa, wakapena mikono na kubadilishana namba za simu. Wakapiga na picha za familia pamoja na “selfie”.
Chiziza akarejea Dar es Salaam akiwa na Amani ya kumjua ndugu yake, familia yake na ukoo wake.
Clifford alirudi Singida na kuendelea na majukumu yake kwa muda. Moyoni mwake alishaamua kuwa, sehemu iliyobaki ya maisha yake angeitumia akiwa Singida kwa namna wakazi wale walivyokuwa faraja wakati wa dhiki kuu iliyomfikia. Ingekuwa ngumu kwake kumchukua mwanae Neema na kuishi naye, hivyo familia nzima ilikubali kuwa, Neema aende akaishi kwa shangazi yake Claritha, dada yake na Clifford mpaka Clifford atakapokuwa tarayi kumchukua na kuishi naye.
Baada ya miezi miwili tangu mkasa wa kifo cha Neema, Clifford alikuwa jijini Dar es Salaam kumsalimu Baba yake..
“Kijana… Nadhani sasa umejifunza nini maana ya ukali wangu juu ya maswala yahusuyo familia. Ujinga ulioufanya awali, na labda unaoendelea kuufanya hata sasa maana inawezekana bado hujajifunza, wa kukutana tu na mwanamke na kuzoana ulitaka kuitoa roho yako. Lakini hakuna kosa kubwa kama kuishi na mtoto wa mtu bila kutoa taarifa kwa ndugu. Unaweza kuingia matatizoni mpaka ukahisi dunia hii ni chungu..” Mzee Chiziza alieleza.
“Ni kweli baba.. Unakumbuka nilichokuambia mara ya mwisho kabla hujaja Mwanza?”
“Naam.. Nakumbuka”
“Well.. Wakati wa nyuma, sikuwa nakuelewa vizuri ulipokuwa ukizungumza kama Baba.. Lakini sasa, najifunza kuwa, nitakapoamua kuoa, sipaswi tu kuangalia kuwa ni kiasi gani niko tayari kuoa peke yake, au watu wengine wananiambia nini kuhusu kuoa.. Napaswa kujichukulia kwanza kama Mume, lakini zaidi, bila kujali iwapo nina mtoto au la, nijichukulie kama BABA!!
“Na ndio maana niliamua kukupa adhabu ili akili ikae sawa. Na ole wako urudie Clifford.. Hakyamungu nakuapia nakunyongelea mbali, mbulula weye” Ingawa aliyasema kiutani, kulikuwa na chembe za hasira katika kauli yake.
“Mzee Chizi.. Wala hujanipa adhabu.. Hii imekuwa ni zawadi kubwa sana kuipokea kutoka kwako. Umenipa zawadi ya adhabu. Zawadi ambayo imeukomaza moyo wangu na kunifanya imara. Hakika zawadi ya adhabu uliyonipa imenibadili. Ikiwa hili halijanibadili, hakuna lingine lolote chini ya jua litakalonifundisha baba angu” Alimaliza Clifford.
******
Geti kubwa la nyumba ya Mzee Chiziza lilikuwa likigongwa kwa nguvu. Haraka, Clifford alinyanyuka kwenda kufungua huku kule kukatishwa mazungumzo na baba yake kukimkera waziwazi.
“Nahisi kama Janeth ameenda kufungua, ama?” Alisema Mzee Chiziza huku naye akionekana kutamani kukaa karibu na mwanae.
“Achana na hisia mzee na rudi kwenye uhalisia, Janeth na mama wameenda mjini kitambo tu. Umekuwa msahaulifu tena?” Alisema Clifford huku akiufikia Mlango.
“Pumbavu kabisa. Clifford nitakupiga risasi we chalii. We sio wa kunijibu jibu kisanii mimi” Chiziza alisema huku akisimama kwa utani.
“Nilikuuliza swali mzee, hilo tusi ungeliweka akiba, utalihitaji baadae. Halafu sikujua kuwa nawe huwa ni msanii unayewajibu wenzako kisanii” Clifford alibamiza mlango huku akikwepa mto mdogo wa kochi aliorushiwa na Mzee Chiziza na kuelekea getini.
Alifungua mlango na kuchungulia nje.
Gari yake nyeusi ambayo mara moja aliitambua kuwa ni ile iliyopotea kihuni ilikuwa imepaki ikiwa tupu ndani, huku mtu fulani akionekana kuanza kuondoka eneo lile.
“Oyaa.. Vipi? Nani?” Aliuliza Clifford..
Mtu yule akageuka na kumtazama kwa macho yaliyolegea na kuonekana kuchoka.. Alitia huruma
Alikuwa Nunu!

*************** MWISHO***************
Mungu ni mwaminifu na kazi zake ni takatifu!
Nunu atarudi tena!!
***********
Nakushukuru sana msomaji na msikilizaji wa simulizi hii kwa kuwa sehemu ya kazi hii tangu mwanzo mpaka kituo cha mwisho. Sijajua imekuwa ni safari ya aina gani kwako, lakini kwangu imekuwa ni neema ya nguvu ya Mungu kunipa nafasi ya kuyabadili mawazo yangu kuwa simulizi hii. Ni faraja kwangu pia kujua kuwa, huenda kuna sehemu ya maisha ya mtu fulani imebadilika baada ya kusoma au kusikiliza simulizi hii.
Ni wazi kuwa, hata nawe umejifunza jambo. Lichukue na kulihifadhi moyoni. Kama halitakufaa siku ya mvua, litakusitiri siku ya jua. Na kama halitakunufaisha katika maisha yako, ligawe kwa mwenzako, huenda likawa ni Mwanzo mpya wa maisha ya mtu mwingine.
Kwa uzito wa kipekee pia,
Izingatiwe kuwa simulizi hii ni kazi ya Sanaa. Iwapo mazingira, majina ya wahusika au mfululizo wa matukio unafanana na tulio lolote halisi, tafadhali ichukuliwe kuwa imetokea hivyo kwa bahati mbaya tu na kama matokeo ya kazi ya sanaa na wala haikukusudiwa.
Endelea kuwasiliana nami kwa nambari ya simu +255 763 305 605 kwa ushauri na maoni.

Safi sana... inafundisha...

Chapter Closed...


Cc: mahondaw
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom