*DORCAS-22*
Sikuelewa sababu ya Barton kuendelea kuniangalia badala ya kuondoka, nilijiuliza kama aliyekuwa akipigwa au kuwa katika hali ile angekuwa dada yake Bite au Monica angevumilia kuwaangalia.
Jambo la kushangaza, mama hakujali aliendelea kunishambulia mpaka Bite na Monica walipoamka na kuhoji sababu za kuadhibiwa namna ile.
“Huyu msichana ni jeuri sana, mimi namwuliza badala ya kunijibu ananikunjia sura, hivi hanijui eh?” mama aliwaambia mabinti zake.
Wakati akinizushia uongo huo nilifanikiwa kuvaa sketi yangu na kuzidi kumuomba msamaha mama japo sikuwa na kosa, lengo langu lilikuwa anisamehe ili aache kunishambulia.
“Bahati yako umelitambua kosa lako, ukirudia tena nitakufukuza hapa nyumbani kwangu,” mama aliniambia.
Nafsi yake iliporidhika, alimwambia Bite aende akachukue fedha za matumizi alizoziweka juu ya meza chumbani, zilipoletwa aliniambia niende sokoni nikanunue mboga na viungo.
“Muone kwanza, hebu kamalizie chai yako ila usirudie tena upuuzi wako wa kuamua kunywa chai bila kupewa maelezo na wenye nyumba,” Dorcas anasema yule mama alimwambia.
Nikiwa sina amani, licha ya kujongea pale mezani nilishindwa kunywa chai nikabaki nimejiinamia na kumkumbuka marehemu mama.
“Hivi kama mama na baba yangu wangekuwepo sidhani kama ningepitia mateso haya, hivi ni lini nitaishi kwa amani kama watu wengine, lini nami nitakuwa na furaha hapa duniani?” niliwaza.
Wakati nawaza hivyo, mama aliniambia kama sikuhitaji kunywa chai niende sokoni nikanunue mboga kisha nipike ili wasijechelewa kula.
Niliinuka na kuelekea chumbani kwa lengo la kubadili siketi na kujiweka sawa,nilipoingia niliwakuta Monica na Bite wakiwa wameketi kitandani ndipo Bite akaniambia nisimfanyie ujeuri mama yao.
“Dorcas,unaona huo ujeuri wako umesababisha mama akuchape makofi na kama hutajirekebisha anaweza hata kukufukuza hapa nyumbani,” Dorcas anasema Bite alimwambia bila kujua sababu ya mama yao kumchapa.
Aliponiambia hivyo, sikumjibu chochote,nilibadili nguo nikaenda jikoni nilikochukuwa kikapu na kuelekea sokoni.
Niliporejea nikatakata nyama na kuiinjika jikoni, wakati huo akina Bite walikuwa wanajiandaa ili waende mjini.
Walipokunywa chai waliacha vyombo walivyonywea mezani kisha wakaondoka.
Kwa kuwa niliwazoea,nilivikusanya na kwenda kuviosha huku nikiwa nina msongo wa mawazo. Kufuatia hali hiyo nilisahau kama nilikuwa nimeinjika nyama.
Aliyenishtua alikuwa Barton aliyenifuata na kuniambia ilikuwa ikiungua nikatoka mbio kwenda jikoni na kukuta sehemu kubwa ya kitoweo ikiwa imeungua na harufu ya kuungua ikiwa imetanda jiko zima.
Nilichofanya ni kuipua lakini kabla sijafanya chochote mama aliyesikia harufu ya nyama kuungua aliingia, kama alivyofanya asubuhi alijishika kiunoni na kuniuliza nilikuwa nimefanya nini!
Kwa hofu nilishindwa kumjibu ndipo akaniuliza nilifanya nini nikamwomba msamaha kwa kuunguza nyama kwa bahati mbaya, akatoka mle jikoni. Moja kwa moja nilijua anakwenda kufuata fimbo.
Kabla hata sijachukua hatua ya kutoka nje aliingia akiwa amefura kwa hasira, kabla hajaanza kunitandika nilipiga magoti na kumwomba msamaha kwamba nyama iliungua kwa bahati mbaya hakunielewa, alinitandika bakora ya mgongoni.
Baada ya kunitandika, alinyanyua tena fimbo ili anichape begani nikakinga mkono, hapo nikawa nimemuongeza hasira akanimbia kumbe nilikuwa najua kukinga fimbo yake!
Alipotoa kauli hiyo alinizaba kibao cha nguvu upande wa kushoto nilipojishika kufuatia maumivu niliyopata alinizaba tena kibao upande wa kulia, nikasikia masikio yakivuma.
Mama aliniambia hapendi kuishi na mtu jeuri akaitupa fimbo chini, akaniambia nitafute fedha zangu nikanunue nyama nyingine. Kwa kuwa sikuwa na fedha niliomuomba msamaha, akanisonya.
“Kumbe unajua kuunguza tu wakati huna hata hela mjinga wewe, hivi huko ulikotoka ulikuwa unakulanyama?” mama aliniambia kwa kebehi.
Wakati akiniambia hivyo, bado masikio yangu yalikuwa yakivuma, alichokifanya alimtuma biti akanunue nyama na kuniambia niipike na ole wangu iingue tena.
Siku hiyo nilikosa raha kwa maumivu na uchungu wa kupigwa bila sababu, nilipokula nilishindwa kabisa kufanya kazi yoyote nikaingia chumbani kulala. Kufuatia kipigo cha mama nilipoteza uwezo wa kusikia vizuri kutokana na makofi aliyonipiga masikioni.
Nilipomwambia mama akanieleza nimuondolee upuuzi wangu na kusema kama sikusikia vizuri yeye afanyeje.
Kauli hiyo iliniumiza sana, kulipokucha kabla hawajaamka nikaenda mtaa wa pili alipokuwa akiishi dada aitwaye Stellah niliyekuwa naelewana naye sana na alijua mambo yangu mengi.
Nilimwelezea suala zima la kupigwa na manyanyaso niliyopata na kumuomba anisaidie fedha ili niende Mbeya kwa mama, mkubwa.
Stellah aliyekuwa akifanya biashara alihuzunika sana, alinipatia shilingi 30,000 kisha alinifahamisha kwamba jioni ya siku hiyo angehamia kwenye nyumba yake huko Kimara, akasema kabla sijaenda Mbeya alitaka nikapafahamu.
Alinieleza kuwa sikutakiwa kabisa kuendelea kuishi kwa yule mama, akasema nikifika nyumbani nikusanye vitu vyangu halafu niende pale kwake kisha twende Kimara.
Nilifurahi sana, nilipofika nyumbani wote walikuwa wamelala, nilichukua begi langu na vitu vyangu vyote nikaenda kwa dada Stellah.
Kuhofia kuonekana tuliondoka na kuelekea Kimara, nilimpongeza kwa kujenga nyumba nzuri alishukuru kisha aliniacha kwa jirani yake hadi jioni alipohamia.
Alfajiri dada Stellah alinisindikiza Ubungo akanikatia tiketi ya kwenda Mbeya, nikiwa safarini niliwaza mambo mengi la kubwa ni kumsimulia mama mkubwa masaibu yaliyonikuta.
Safari yangu ilikuwa nzuri kwani niliwasili Mbeya saa 12.15 jioni, nilipoteremka Mwanjelwa nilipanda daladala za kwenda Soko Matola nikashuka Kituo cha Sido na kukatisha njia ya mkato kuelekea kwa mama mkubwa.
Nilipokaribia mtaa aliokuwa akikaa mama mkubwa mama wa kwanza kukutana naye alikuwa mama Ambokile, alishangaa aliponiona na kunipongeza kwa kuwa mkubwa.
Licha ya kuzungumza mawili matatu na mama huyo alionesha alikuwa na jambo moyoni mwake,nilipomuuliza mama mkubwa hajambo aliniambia hajambo.
Hata hivyo, alinifahamisha kwamba alihamia Usangu hivyo twende nikalale nyumbani kwake ili kukicha nianze safari ya kwenda Usangu alikohamia, nilipopewa taarifa hiyo nilikosa raha.
Tulipofika kwa mama huyo ambaye alipoongea name nilikuwa simsikii vizuri, aliniandalia maji ya kuoga pamoja na chakula, lakini moyo wangu ulikosa utulivu kabisa.
Usiku tukiwa tumekaa jikoni tukiota moto,mama huyo aliyekuwa mjane aliniambia kuna jambo alitaka kuniambia lakini niwe jasiri kwa sababu hakuona sababu ya kunificha.
Nikiwa mwenye shauku ya kujua jambo hilo alinifahamisha kwamba mama yangu mkubwa alifariki dunia kwa ajali ya kugongwa na gari miezi mitano iliyopita.
Taarifa hiyo ilinifanya nianze kulia kwani sikujua hatima ya maisha yangu ingekuwaje,mama alinipa pole.
Nilipomuuliza alizikwa wapi japo nikalione kaburi lake akaniambia alizikwa kijijini kwao Tukuyu.
Hakika niliona dunia imenitenga, nililia sana lakini hakuna kilichobadilika ukweli ulibaki mam mkubwa kipenzi cha mama yangu alifariki dunia. Nilikaa Mbeya siku tatu ndipo yule mama akanipa nauli nikarudi Dar kwa dada Stellah aliyenipokea kwa upendo.
Nikiwa naishi kwa dada Stellah aliyekuwa ananipenda sana na kuahidi kuishi name katika maisha yake yote, kadiri siku zilivyokwenda masikio yangu yalipoteza uwezo wa kusikia.
Baada ya kuhangaikia tiba bila mafanikio alinipeleka Muhimbili ambapo nilifanyiwa vipimoa kugundulika masikio yangu yalipata matatizo makubwa hivyo nisingweza kupona.
Siku hiyo nililia sana na kumuuliza Mungu kwa nini niliandamwa na matatizo katika maisha yangu, wakati nazungumza hivyo dada Stellah aliyenishawishi niandike kisa changu ili jamii ijifunze jambo alinisikia na kuniambia nisiseme hivyo kwa sababu misukosuko katika maisha ni jambo la kawaida.
Nilimwambia sikatai lakini kwangu ilikuwa imezidi akanimbia niwe na amani ipo siku nitapona na kusahau yote yaliyonitokea na nitakuja kushangaa siku nitakayokutana na baba pamoja na ndugu zangu.
Kutokana na msongo wa mawazo niliokuwa nao, licha ya kupata kila kitu kwa dada Stellah nilijikuta nashindwa kula na kupoteza kabisa uwezo wa kusikia yaani nikawa kiziwi nikawa nazungumza kwa ishara.
Jambo hilo liliniumiza nikajikuta nadhoofu kadiri siku zilivyokuwa zikisonga mbele, siku moja nilipatwa na malaria kali nikapelekwa Hospitali ya Muhimbili ambapo iligundulika nilipungikiwa dawa na maji nikalazwa.
Mpenzi msomaji, taarifa mbaya ya kuumiza niliyopewa na dada Stellah aliyekuwa akiishi na Dorcas ni kwamba mpendwa wetu huyo alifariki dunia Desemba mwaka jana siku ya tano baada ya kufikishwa Muhimbili ambapo msiba huo ulikuwa nyumbani kwake.
Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.
*MWISHO.*