Sehemu ya 24.
Haraka sana akasimama na kumwambia Maggie alijisikia kunywa pombe hivyo anakwenda baa na angerudi baada ya dakika kadhaa.
“Sawa bebi,” alisema Maggie, akajigeuza upande mwingine na kuendelea kulala.
Haraka sana Gosling akatoka, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuonana na Mike na kumuuliza kuhusu msichana huyo, alichukua namba au alikataa.
“Alinipa!”
“Wasiliana naye, ninataka nionane naye, yule msichana amenivuruga sana, Mike, umeona alivyokuwa mrembo lakini?” aliuliza Gosling.
“Ndiyo bosi. Halafu ana mwili!”
“We’ acha tu! Hebu mpigie simu umuite niende naye sehemu kuzungumza,” alisema Gosling na kumwambia akachukue chumba kingine ambacho yeye angekwenda kulala na Catherine kwa saa moja
“Sawa, haina shida,” alisema Mike, akaenda kuchukua chumba, akampa funguo bosi wake na kisha kumpiga simu Catherine ambapo ilipopokelewa tu, akamwambia kuwa bosi yule aliyehitaji namba yake alihitaji kuonana naye.
“Sawa. Nakuja hapo baa!” alisema Catherine.
“Hapana! Nenda chumba namba 22, utakutana naye,” alisema Mike.
“Sawa. Haina shida,” alisema Catherine na kukata simu.
Kule ndani alipokuwa, Gosling hakuwa akijiamini, alitetemeka huku kijasho chembamba kikimtoka. Hakuamini kama alikuwa akienda kukutana na msichana ambaye alimuona mara moja tu na kumpenda kutoka moyoni mwake.
Alikumbuka jinsi alivyokuwa, alilikumbuka umbo lake, mapaja yake yaliyonona na kiwowowo kilichomchanganya mno, aliona kabisa siku hiyo ingekuwa Vita Kuu ya Tatu ya Dunia.
“Hivi ni mimi kweli ndiyo nakwenda kulala na yule msichana ama? Mbona sijiamini? Gosling hebu tulie, jiamini, una pesa hutakiwi kuogopa...tulia baba...” alijisemea huku akishusha pumzi ndefu.
Mule chumbani hakutulia, wakati mwingine alikuwa akikaa kwenye kiti, mara asimame na kukaa kwenye kitandani, alipoona haitoshi, akaanza kutembea huku na kule, mara aende bafuni, mara chooni, kwa kifupi hakuwa akitulia.
Baada ya dakika chache akasikia mlango ukigongwa, moyo wake ukapiga paaa kwani alijua kabisa mtu aliyekuwa akiugonga alikuwa yule msichana mrembo, Catherine aliyekuwa amemuona mchana wa siku hiyo.