SIMULIZI: Tembele la uwani (EDGAR MBOGO)

SIMULIZI: Tembele la uwani (EDGAR MBOGO)

TEMBELE LA UWANI
SEHEMU YA THEMANINI NA NNE
MTUNZI Mbogo EDGAR
ILIPO ISHIA SEHEMU YA THEMANINI NA TATU : “hivi we una nini lakini, ina maana unadhani watu hawajuwi kama tunachokifanya mwisho wake ni kupata mimba na kuzaa?” aliuliza Soraya, na Higgno akamtazama Soraya kwa mshangao, Soraya akazidi kumshangaa Higgno ambae ghafla aliangua kicheko kikubwa sana, “lione kwanza kumbe lina nitania” alisema Soraya akimpiga kijikofi cha mgongoni mpenzi wake.
Naam wakati wanaendelea na matembezi yao huku wanaongea na kucheka kwa furaha, wakiwa wanakatiza barabara ya mtaa wa wahindi, maarufu kama mtaa wa Veris, mara wakashangaa kuliona gari la polisi linasimama mbele yao, polisi tena! Duh!..... ENDELEA ……..
Likiwa na askari kama sita nyuma ya gari hilo wote wakiwa na bunduki zao aina ya smg, wapo walio valia na vijikoti vifupi vya rangi nyeusi vyenye mikono mifupi, nazani kwa ajili ya kuzuia upepo, pia wapo walio ongezea na miwani nyeusi, wote walikuwa wanawatazama wakina Higgno, lakini macho ya mlenga Soraya, ambae alianza kuogopa, maana wote wawili hawakuelewa kwanini lile gari la polisi limesimama mbele yao namna ile, na ukizingatia hata ule mpango wao wa kuwapigia simu polisi ulikuwa bado haujafanyika, “Higgno nasikia polisi waonevu sana, si unaweza kupigana nao” aliuliza Soraya, kwa sauti ya chini ya kunong’ona, huku taratibu akirudi nyuma na kusimama nyuma ya Higgno, “mh! we huoni zile bunduki” aliuliza Higgno, akimaanisha kuwa ingekuwa vigumu wao kupambana na wale polisi kama kweli walikuwa wanalengo la kuwa nyanyasa, ikiwa ni imani potofu ya watu wengi juu ya chombo hiki cha ulinzi na usalama wa raia.
Akiwa amesimama kwa uoga nyuma ya mpenzi wake Higgno aliekuwa amesimama analitazama kwa umakini lile gari la polisi, ambalo lilikuwa limesimama mbele yao pasipo wale polisi nyuma ya gari kushuka, na baada yake ukafunguliwa mlango wa mbele upande wa kushoto, ambao hukaliwa na abiria, na akashuka polisi mmoja alievalia sale zake pasipo jacket wala miwani na bunduki, kisha akaanza kuwasogelea Soraya akatoa macho ya uoga.
Lakini kila yule askari polisi mwenye nyota moja alipo wasogelea akashangaa kumuona anatabasamu, Soraya akamtazama Higgno akamuona nae pia anatabasamu, “hoooo! brother Kiwili, kumbe uliingia jeshi la polisi?” Soraya alimsikia Higgno akiuliza kwa mshangao, “haaa! kwani baba yako hajakuambia, nilikutana nae juzi kule mabatini alikuja kutoa reprt ya kuunguliwa kwa duka lenu, nikamuambia kuwa mimi ni rafiki yako” alisema Kiwili akionyesha kushangazwa na kutokupata taarifa kwa Higgno juu yake, mpaka hapo tayari Soraya alishaelewa kuwa hakukuwa na tatizo lolote wala uadui kati yao na polisi zaidi ya urafiki, “baba alitingwa sana kuhusu duka, sema nashukuru amesha jenga jingine hivi leo ilikuwa nikamsaidie kupanga vitu ndani ya duka jipya” alisema Higgno kwa sauti yake ile ile ya upole, “dah! poleni sana bwana, hivi bado hamuja muona huyo mshenzi tuje tumfundishe adabu?” aliuliza Kiwili, ambae ni yule ambae alikuwa anasoma nae Luhuwiko secondary, na pia aliamua kumfundisha karate kule kwenye kambi ya jeshi la ulinzi, “bado hatuja mpata na alie muona ni baba peke yake, jamaa anadai kuwa nilimvulugia mipango yake, sijajuwa ni mipango gani?” alisema Higgno na wakati huo Soraya alikuwa anawasikiliza kwa umakini kabisa, na kugundua kuwa hawa wawili sio tu kuwa marafiki ila ni marafiki wa toka zamani waliopoteana muda mrefu, ikiwa ni rafiki wa kwanza wa Higgno ambae yeye amemuona, “lakini vipi kuhusu wakina Talib na wale wenzake, hujakorofishana nao hivi karibuni?” aliuliza Kiwili na hapo ndipo Soraya na Higgno kila mmoja akamkumbuka Talib, kivyake vyake, wakati Soraya anajiuliza kwanini Talib hakuonekana kwenye ile shughuri pale nyumbani kwao, Higgno nae akajiuliza kuwa kama kweli Talib ni mtoto wa Mahamud, mbona hajamuona pale nyumbani kwao, “yule jamaa bwana amesumbua kama wiki mbili zilizopita hivi, alikuja nyumbani na Hilda kunifanyia fujo, lakini sikufanya lolote” alisema Higgno, akishindwa kuongea zaidi kwa kuchelea Soraya yupo pale japo alikuwa anajuwa kuhusu vurugu ile aliyo ifanya Talib, “vipi kuhusu dojo (sehemu ya mazoezi ya karate) unaendelea lakini?” aliuliza Kiwili, ambae sasa alianza kumtazama Soraya, “bado naendelea lakini nafanya mwenyewe nyumbani, si unajuwa majukumu muda unakuwa mdogo” alisema Higgno, na hapo Kiwili akauliza kuhusu Soraya, “vipi naona upo na ….. sijui ni shemeji au…?” aliuliza Kiwili kwa namna ya utan, huku anasita sita, baada yake Higgno alicheka kidogo,na kumtazama Soraya ambae alionekana kucheka cheka, “ndiyo ni mchumba wangu bado sijaoa” alisema Higgno sasa alicheka cheka, “ok! ni wapale pale Luhuwiko au …” aliiuliza Kiwili japo hakuwa na kumbu kumbu ya mschana wa kiarabu pale shuleni, labda alianza form one wakati yeye amemaliza, hapana huyu alikuwa anasoma songea girls” alijibu Higgno, “ok! ni wakule Luhila au?” aliuliza Kiwili, ambae ni kama hakuamini alicho kiona na kukisikia toka kwa Higgno, kuwa anamiliki mschana wa kiarabu, ambao pale mjini songea walikuwa wachache sana, “hapana mimi na kaa kwa Mahamud si unamfahamu?” alijibu Soraya mwenyewe, “ndiyo napafahamu, inamana wewe ndie Soraya mtoto wa Mahamud” aliuliza Kiwili kwa mshangao, “ndiyo mimi shemeji polisi, tena kuna kitu tunataka tukuambie” alisema Soraya na Kiwili huku akiwa bado kwenye mshangao akasema, “hakuna tatizo, kama ni la kutoa msaada nipo tayari siwezi kumuangusha rafiki yangu Higgno” alisema Kiwili, huku macho yake yakiwa bado kwa kuto kuamini kama kweli rafiki yake Higgno anammiliki Soraya Mahamud, mtoto mzuri wa kiarabu, mtoto wa tajiri mmoja mkubwa sana pale mkoani na tanzania kwa ujumla, “mpe namba yako ya simu Higgno tutakupigia baadae maana kuna mtu tuna mtilia mashaka” alisema Soraya ambae daima sauti yake huwa ni nyororo na tamu huku akiwa ameukumbatia mkono wa mpenzi wake Higgno, “mh! unaweza kunifafanulia kidogo ili nijiandae, maana nina weza kuja na nguvu kubwa kumbe inshu ni ndogo na pia ninaweza kuja na nguvu kidogo kumbe inshu ni kubwa sana” alisema Kiwili ambae licha ya kukutana na rafiki yake pia alitamani kuiona sura ya shemeji yake Soraya, maana licha ya kuwahi kumuona siku moja akiwa shuleni kwao, miaka mingi iliyo pita lakini akuwahi kumuona kwa ukaribu kama hivi.
Hapo wakina Higgno wakamsimulia Kiwili mambo wanayo yatilia mashaka kuhusu ujumbe ulioingia kwenye simu ya watekaji na Kiwili hakuwa na kipingamizi, “hakuna shida Higgno chukuwa namba yangu ya simu, kama mukiwaona tu we nijulishe mimi leo nipo doria, nitafika mara moja” alisema Kiwili na hapo wakaongea mawili matatu kisha wakaagana na kila mmoja akaingilia njia yake, huku Kiwili akishinda kuelewa Higgno alimpatapataje mschana yule mtoto wa Mahamud, “kumbe unarafiki askari polisi” aliuliza Soraya wakiwa wanaendelea kutembea pale mjini, wakipandisha upande wa soko kuu wakiifuata barabara ya delux, ili wazunguke upande wa pili ( kutokea mtini pub) ili washukie nyumbani kwao kama sehemu ya matembezi yao, tayari wakiwa wamesha peana namba za simu na Kiwili kwaajili ya kama wata baini lolote uski ule.******
Naam saa mbili za usiku ndio muda ambao, mama Hilda aliachiwa na mwenyekiti wa kijiji ili aende nyumbani kwake, wakiwa wamemtafutia kanga za kujihifadhi zilizo azimwa kwa mke wa mwenyekiti, maana nguo aliyo kuwa ameivaa mwanzo ilikuwa imechanika vibaya sana, ni sawa na kuwa kama hajavaa nguo yoyote.
Mama Hilda alitembea kwa kujificha ficha mpaka nyumbani kwake, ambapo alishangaa kuona moto unawaka, na alishangaa kwasababu kwa mida ile ni vigumu kuona moto unawake nyumbani kwake, kwasababu yeye na Hilda mida kama hii huwa wanakuwa kwenye ulanzi, hata mtoto wa Hilda ameshazoea kula kwa majirani, mama Hilda alipo tazama vizuri aligundua kuwa aliepo nyumbani pale ni wifi yake, hakushangaa tena kwasababu ni yeye ndie aliempelekea ujumbe kuwa aje kusaidia kuuguza kaka yake.
Mama Hilda akiwa anaamini kuwa wifi yake hajui lolote lililotokea mchana akapitiliza kuelekea ndani bila kumsemesha wifi yake huyu, “habari wifi” lakini kabla hajaufikia mlango akasalimiwa na yeye hakuitikia akaendelea na safari yake, “sasa wifi unaninunia mimi kwani mimi ndie niliekufumania?” aliuliza shangazi yake Hilda kwa sauti ya ukorofi, hapo mama Hilda akasimama na kugeuka, “naomba ufuate ya kwako hayo mengine haya kuhusu” alisema mama Hilda kwa sauti ya shari pia, “yasinihusu kwanini, kwani unayomfanyia kaka ni maziri, unamtelekeza hospital halafu wewe unaenda kuinamishwa vichakani” alisema shangazi kwa sauti ile ile ya kikorofi, ilionekana wazi kuwa wawili hawa hawapikwi chungu kimoja, sawa na chumvi na sukari, “sasa wifi unanitaka la rohoni, nasema nitakubomoa sasa hivi” alisema mama Hilda huku anageuka na kumsogelea shangazi, “nani umbomoe Malaya mkubwa wewe, tena ukome kuniita wifi kwa kaka yangu yupi aliekuoa wakati unamtelekeza hospital na kwenda kufanya uchafu wako” alisema shangazi na wakati huo huo mama Hilda akamzabua kofi la mgongoni.
Naam na hapo mama Hilda ni kama alikuwa ameuwasha moto, maana shangazi aliinuka na kipande cha kuni alicho kichomoa jikoni na kukivurumisha kichwani kwa mama Hilda, ambae bado maumivu ya teke la kitumbuani alilopigwa mchana yalikuwa yanasikika kwa mbali, ile anataka kujitetea akashtuka ukuni mwingine ukija kichwani hivyo akakwepa na kukinga mgongo, hapo kikasikika kishindo cha puuuh!, sambasamba na kilio kikuu, “mama na kufaaaa” alipiga kelele mama Hilda huku anakimbilia alikotoka na shangazi hakumuacha, alizidi kumshushia kipigo cha mbwa mwizi.
Kelele za mama Hilda zilisikika kwa watu waliokuwepo nyumba za jirani na kuwafanya waje eneo la tukio na kumuamulia mama Hilda ambae alichomoka na kupotelea gizani, hakujulikana ameenda wapi, “mshenzi sana na usirudi tena hapa” alisema shangazi kwa hasira, “na nina msubiri huyo Malaya mwenzio nae arudi yeye si anajifanya TEMBELE LA UWANI sasa leo namtandika na ataenda kugawa vizuri hilo papa lake” alisema Shangazi kwa hasira, huku anarudi kwenye jiko alilokuwa ameliwasha kwa kutumia kuni kwaajili ya kuandaa chakula cha mgonjwa baada kudhaminiwa na nurse akakope kwenye moja ya magenge pale kijijini, kwa ahadi ya kulipa siku inayo fuata, “afadhari, maana huyu mama hajielewi kabisa, yaani mambo anayo yafanya utadhani mwanga” walisikika baadhi ya watu kati ya wale waliokusanyika wakimsifu shangazi kwa kitendo alicho kifanya, wakati huo mtoto wa Hilda alikuwa anakimbilia nyumbani kwao baada ya kuona leo moto unawaka mapema, ikiwa ni ishara ya kuwa kuna mtu.*******
Naam saa mbili za usiku pikipiki mbili zilisimama nje ya bar ya mtini, karibu na Toyota collola jeupe, zikiwa zime beba watu watatu kila pikipiki moja, wote wamevalia makoti meusi na kofia za sox nazo pia nyeusi, na waliposhuka toka kwenye pikipiki zao mmoja wao alitoa simu na kupiga, “oya tumeshafika mtini tupo hapa nje” alisema yule mwenye kuongea na simu” alisema yule mwenye kuongea na simu na pasipo kusikia alicho ongea mwenzao, wakasikia tena anasema poa poa fanya faster basi” alisema yule mwenzao na kukata simu, “vipi Vutus anasemaje huyo?” aliuliza mmoja kati yao, “anasema anakuja, tumsubiri hapa hapa” alijibu Vitus, “tumsubiri kivipi, si aseme tuzame ndani na sisi tukashtue na bapa kisha tuzame kazini” alisema yule alieulizia, “dah! Zido bwana, usiwe na haraka, we unadhani yeye yupo hapa anafanya nini, si anapiga vitu?” alisema Vitus, huku wakiendelea kumsubiri walie mpigia simu ambae ni Talib.********
Naam baada ya Laylah kuwafikisha nyumbani baba na mama Higgno, yeye akarudi mjini, kwenda kuungana na wakina Soraya akitumia gari la mzee Frank alilopewa na baba yake Soraya aina ya suzuk escudo, huku wakipanga kuwa siku inayofuata atakuja kuwa fundisha kuendesha gari lile ambalo leo angelala nalo nyumbani kwao kule Makambi, lakini ni baada ya kumaliza kuweka mtego wao, maana sms ilielekeza kuwa kesho yaani leo wasifanye makosa na kiukweli walisha ona kuwa funguo moja haipo pale mlangoni, akiwaacha baba na mama Higgno wakielekea zahanati kumtazama mzee Komba,huku njia nzima wakiongea kwa furaha wakimsifu Higgno kwa mambo aliyoifanyia familia ya Mahamud na kumpata mschana mzuri kama Soraya, ambae anakwenda kuwa mke wake, na katika maongezi yao hawa kuwahi kuzungumzia familia ya mzee komba wala kuisimanga kwa yote waliyo wafanyia, na pia hawa kuikumbuka baiskeri yao waliyoisahau nyumbani kwa Mahamud.
Pale Hospital walimkuta Nurse alieshinda mchana kutwa akijiandaa kuondoka, baada ya mwenzie kuja kumpokea, “naona mjini kulikuwa na mambo mengi sana jamani, ndio munarudi sasa hivi?” aliuliza kwa utani yule nurse, “yaani we acha tu, mambo yaliyotokea huko ni zaidi ya kushtukizwa, mpaka sasa tupo hoi” alisema mama Higgno akionyesha tabasamu pana la furaha, huku mzee Komba nae akionekana kutabasamu kwa kufurahia ujio wa wawili hawa, “kama mambo ni mazuri basi tuna shukuru, naona mumekuja kukutana na mgonjwa kama mulivyo ahidi” alisema nurse akionekana kuwa na tabasamu la matumaini, baada ya kuwaona wakina Frank, “ndio bwana maana mzee Komba alinisisitiza sana nije hapa” alisema mzee Frank, huku akimtazama mzee Komba, na wakati huo huo wakamuona dada yake Komba akiingia pale Hosptal akiwa ameongozana na mtoto wa Hilda yaani mjukuu wa mzee Komba, “kwa kweli kaka maisha yako na familia yako unayajuwa wewe mwenyewe, alisema shangazi aliebeba sahani mbili za plastic, moja ikiwa imefunikwa juu ya mwenzie, “vipi dada yangu mbona hivyo, kuna jambo gani tena” aliuliza yule nurs alieshinda mchana, huku wote wakigeuka na kumtazama shangazi, “shikamoo babu, shikamoo bibi” alisalimia mtoto wa Hilda, huku kijipapatua toka kwa shangazi ya mama yake na kumfuata mzee Frank, akienda moja kwa moja na kumshika mkono akionyesha kuwa bado anawakumbuka, “babu, naona ulinitoroka moja kwa moja” alisema mzee Frank, ambae siku zote ambazo Hilda na mtoto huyu walikaa nyumbani kwake, hakuwahi kuonyesha wazi chuki juu ya mtoto huyu, “mama mwenyewe hanileti” alisema mtoto wa Hilda, kwa kisauti cha kuchangamka huku mzee Komba akiwa ana watazama kwa macho ambayo yalionyesha machungu ya wazi, maana aliweza kuona upendo wa wazi kati ya wawili hawa, yaani mzee Frank na mjukuu wake, “kwani wewe huwezi kuja mwenyewe?” aliuliza kwa kutania mzee Frank, ni wazi aliishinae vizuri.
Naam baada ya maongezi mawili matatu ya mzee Frank na mjukuu yule ndipo shangazi alipoeleza kilichotokea nyumbani kwa kumtandika mama Hilda mpaka kukimbilia kusiko julikana, hadithi ambayo ilitoa mwanga wa kile kilicho mtokea mama Hilda mchana na kuwaacha midomo wazi wakina Frank na mke wake, “bwana Frank, hakika wewe ni mtu mwenye moyo wa pekee sana, siwezi kuamini kuwa licha ya yale yote yaliyo tokea leo hii umesaidia kuni kimbiza na kuokoa maisha yangu kwa kugharamia matibabu yangu hospital” alisema mzee Komba mara baada ya simulizi ya dada yake juu ya mama Hilda, “haaa! mzee Komba tufanye yamepita hayo, kuna mambo yakitokea hatuwezi kukumbuka kuwa tuna ugomvi, baada yake tunaweka tofauti pembeni na kutatua tatizo” alisema mzee Frank kwa sauti iliyojaa upole na urafiki, na kwa kuthibitisha hilo kwanza alimpatia dada yake Komba kiasi cha elfu kumi shilingi za kitanzania kwaajili ya huduma kwa mgonjwa, akamueleza dada yake Komba kuwa atapohitaji kitu chochote kwa kipindi kile atakacho kuwa ana muhudumia mgonjwa anaweza kwenda nyumbani kwake kumueleza mkewe, vivyo hivyo alimueleza nurse kuwa kama kuna gharama za dawa zitakazo kuwa zinahitajika wasisite kumueleza ilimradi mzee Komba apate matatibabu, mwisho wakaaga na kuondoka zao kueleka nyumbani kukagua zawadi zao.******
Tayari watu walikuwa wamesha tawanyika, nyumbani kwa Mahamud na tayari mama na baba Soraya walisha swali Insha na sasa walikuwa mezani wanapata chakula cha jioni, huku wanajadili mawili matatu kuhusu tukio lililotokea leo mchana pale nyumbani kwao, “sijui Talib ana maana gani kutuambia kuwa Higgno aliusika na tukio la utekwaji wa Soraya?” aliuliza mama Soraya kwa sauti masikitiko, “tena ume nikumbusha hivi huyu atakuwa wapi ina maana kutwa nzima ya leo hajagusa hapa nyumbani” aliuliza mzee Mahamud kwa sauti ya kutia shaka, hapo hakukuwa na wenye jibu, sio mama Soraya wala baba Soraya mwenyewe.*******
Naam Soraya na Higgno walipokuwa wanakatiza eneo la mtini pub, ni kama Soraya alikumbuka jambo fulani, “mh! hivi Higgno sijawahi kukuuliza kama unakunywa pombe” alisema Soraya huku akiitazama bar ile , na hapo akawaona watu sita waliosimama pembeni ya gari jeupe na pikipiki mbili wakiwa wamevalia makoti meusi, situmii pombe ya aina yoyote…” kabla Higgno hajamaliza kuongea, mara Soraya akambinya mkono, “Higgno hebu ona kule” alisema Soraya kwa sauti ya kunong’ona, na Higgno akatazama upande ule aliokuwa anatazama Soraya, yaani upande wa maegesho ya mtini pub upande wa nyuma, “unakumbuka zile pikipiki ni kama zile walizokuja nazo wale majambazi kule shambani” alisema Soraya, huku wanatazama kule kwenye maegesho, “mh! kama zinafafa japo siku zitazama vizuri siku ile, halafu walejamaa ni kama wale wale waliokuwepo kule shamba” alisema Higgno, ambae baada ya kutazama vizuri akamuona Vitus, “halafu yule jamaa ni rafiki yake Tali..” Higgno hakuweza kumalizia kuongea alicho taka kuongea maana aliganda ghafla, huku wote wakitazma upande ule ambao ni mita kama ishirini na tano toka walipokuwepo wao, wakiwatumbulia macho watu wawili waliokuwa wanatoka kwenye mlango wa nyuma wa mtini pub, “hawa tokea lini wamekuwa marafiki?” aliuliza Soraya kwa sauti ya chini iliyojaa mshangao.
Kwa macho yao waliweza kuwaona Talib na Idd wakitoka ndani,huku wakiwa na sigara zao mkononi, wanatembea kuwafuata wale vijana sita waliovalia majaket meusi wakisimama karibu na pikipiki zao, hapo Soraya na Higgno wakatazamana kwa macho ya ung’amuzi, kama vile waliambizana “tume wabamba”..... ITAENDELEA
 
Back
Top Bottom