TEMBELE LA UWANI
SEHEMU YA THEMANINI NA MBILI
MTUNZI
Mbogo EDGAR
ILIPO ISHIA SEHEMU YA THEMANINI NA MOJA: alisema Soraya, huku akiwashangaza watu hasa Higgno ambae alikuwa anamtazama Soraya kwa umakini kabisa, “na Soraya ambae Higgno anamtaja kuwa mchumba wake ndie mimi” alisema Soraya huku anavua niqab yake usoni na kuacha uso wazi, kila mmoja aliweza kuliona tabasamu pana lililotawaliwa na aibu. Naam ghafla Higgno akajikuta ameshasimama bila kuambiwa, huku ameyatoa macho kwa mshangao, akamtazama Soraya kisha akamtazama mzee Mahamud, “sikujuwa kama Soraya ni binti yako” alisema Higgno kwa sauti ya upole iliyo jawa wasi was …… ENDELEA…….
Japo ilikuwa ya chini ambayo ilisikika masikio mwa baba yake peke yake aliekuwa nae karibu, lakini kila mmoja aliweza kuona ishara ya midomo iliyokuwa inacheza na kuona macho ya mshangao na wasi wasi usoni kwa Higgno mwenye sura ya upole, ambae bado alikuwa amemtazama mzee Mahamud, ambae pia alisimama na kunyoosha mikono kwa Higgno, akimuonyesha ishara Higgno ya kuwa aende pale alipokuwepo, nae akamtazama kwanza baba yake ambae alimuonyesha ishara ya kuitikia kwa kichwa kwamba aende, kisha Higgno akamtazama Soraya ambae kiukweli sio kupendeza tena ila aliogopesha kwa uzuri aliokuwa nao, kiasi cha kwamba Higgno hakuweza kuamini kuwa huyu ndie yule mschana ambae usiku wa jana ametoka kukesha nae kule kwenye kibanda chake shambani, nae akamuonyesha ishara ya kuitikia kwa kichwa kuwa ande kwa baba yake.
Watu walikuwa kimya, wakimtazama Higgno ambae alianza kutembea taratibu kumfuata mzee Mahamudpale alipokuwa amesimama, huku music wa qaswida pekee uliokuwa unasikika, “hakika mema ya mtu hayapotei” alinong’ona mama Soraya, huku kwa midadi akimshika mkono mama Higgno ambae pia alikuwa amezama kwenye furaha ya moyo, huku wote wawili vimachozi vya furaha viki wachuruzika machoni mwao, na kulowesha mashavu yao.
Soraya akiwa mwenye kusisimkwa na furaha iliyo sababishwa na tukio lililokuwa linatokea mbele yake, tukio la mapokeo ya wazazi wake juu ya kijana Higgno, aliweza kuona jinsi mpenzi wake huyu alivyomsogelea baba yake ambae moja kwa moja akampa mkono na kumvutia kwake, wakakumbatiana, “nime juwa maana ya swali la Soraya, aliniuliza kama ninaweza kuwa mshenga wa binti yangu” alisema Mahamud, huku akicheka kwa uchungu wa furaha, maana mwanae alimchezea mchezo wa busara kubwa sana, Higgno nae akimsaidia mkwe wake kucheka, kicheko kama kile kile huku wakiwa wamekumbatiana, wakitumia nusu dakika wote wawili wakizuia machozi na kuruhusu tabasamu midomoni mwao, hata mama Soraya nae alijikuta akitoka mbio kuwasogelea wakina Higgno na baba mkwe wake, kisha na yeye akajiunga nao kwa kuwa kumbatia wote wawili, “nisamehe mwanangu yaani nilivyo kufikiria sivyo ulivyo, pole sana mwanangu” alisema mama Soraya kwa sauti ya chini, ambae alishindwa kuficha hisia zake na kujikuta akiachia kilio cha chini chini pasipo watu wengine kujuwa kwanini analia, zaidi walijuwa kuwa ni kilio cha furaha, hata walipoachiana watu walipiga kelele za shangwe, “naam sasa nadhani tunaweza kuongea vizuri, naona muafaka umesha patika, sijui nani ataanza kuongea?” aliuliza mjomba huku akimtazama Mahamud aliekuwa amesimama karibu na mama Soraya na kijana Higgno ambae alikuwa amemshika mkono, “kwa kweli nitaongea mwishoni, ila kwa sasa naomba kijana aongee machache kisha awatambulishe watu alio ambatana nao” alisema Mahamud, ambae ni wazi kabisa alionyesha kuwa mwenye furaha kubwa, huku mama Soraya anamkonyeza mwanae Soraya kwamba awasogelee pale waliposimama, kwanza akamtazama Higgno ambae pia alikuwa anamtazama wakatabasamuliana, huku wote wanatazama chini kwa aibu, huku Soraya anatembea kuwasogelea na moja kwa moja na kusimama kati kati ya baba na mama yake.******
Naam Talib na Idd wakiwa wanaendelea kunywa pombe huku wanapanga jinsi safari yao, ambayo wameipanga kuanza siku mbili mbele itakavyo kuwa, mara Idd akachomekea swali nje ya mada waliyo kuwa wanaiongelea, “hivi huyo fala anae mchumbia Soraya ni yupi?” aliuliza kwa sauti iliyojaa chuki na kuto kupendezwa na jambo lile la Soraya kuchumbiwa, ni wazi kabisa aliumia sana na kujiona kuwa ameshindwa na kijana ambae hata muonekano wake ni wakishamba shamba, “mjinga mmoja hivi anakaa bushi huko Luhila, sijui kama unamfahamu” alijibu Talib kwa sauti iliyojaa dharau, “ningemjuwa mapema nilikuwa na mzimisha kabisaaaa, halafu ningechukuwa mzigo” alisema Idd huku anainuwa glass yake ya pombe kali na kuigugumia mdomoni, “tena umenikumbusha, unajuwa tunafanyaje? kabla yakuondoka tumfanyie kitu mbaya yule boya kisha tuondoke, ninavyo mjuwa Soraya hatoolewa mpaka tukirudi unajibebea mzigo” alisema Idd, akieleza mpango ambao sio waajabu tu, pia wa hovyo pegine kuliko mipango yote aliyowahi kuipanga Talib, “ila Talib unajuwa nilikuwa na kudharau sana, kumbe jiniaz kiasi hicho, kwa hiyo unapajuwa anapokaa huyo fala?” aliuliza Idd, akionyesha kupendezwa na mpango wa Talib, “sio kupafahamu tu! juzi nimechoma duka lao, nilikuwa nasubiri wafungue tena nilichome” alijisifu Talib, “halafu Soraya nae kwanini anakubali kuolewa na huyo fala?” alisema Idd kwa sauti iliyojaa chuki na wivu, “ila Idd sijui kama mjomba atakubari, unajuwa jamaa ni mkristu” alisema Talib, na hapo Idd akachanua tabasamu la mshangao wa kuto kuamini, “weeee! sema kweli kumbe jamaa ni mkristu?” aliuliza Idd huku anatoa simu yake toka mfukoni, “sasa je we ulisha wahi kusikia kuna muisilamu anaitwa Higgno, jamaa mbona anajisumbua” alisema Talib ambae kila dakika alikuwa anazidi kulewa kama ilivyokuwa kwa Idd, “hapo hapo ndipo adui mkuu anapo jiingiza na kuharibu mchezo mzima” alisema Idd kishujaa wa ulevi ulevi, huku anaandika sms kwa baba yake, “mzee Mahamud anamuozesha Soraya kwa kafiri (mtu asie muislamu )” alipomaliza akaituma kwenda kwa mzee Mahadhi, najuwa lazima atakianzisha tu!” alisema Idd huku anasubiri jibu toka kwa baba yake.
Naam sekunde mbili kumi mbele, simu ya Idd ikaita nae alipoitazama ilikuwa ni kutoka kwa baba yake, “hallow usiniambie weye, habari hizo umezitoa wapi?” aliuliza Mahadhi kwa sauti ya mshtuko wakimbea mbea, “hooo! Huamini, wenzio kwa Mahamud sasa watu wamejaa kibao pananukia mapilau tu” alisema Idd, kwa sauti ya kichochezi, “kwahiyo wataka kusema huyo kijana aliemsema Mahamud kuwa ni mchumba wa bintiye kumbe ni kafiri?” aliuliza Mahadhi kwa sauti ya mshangao, “ndiyo anaitwa Higgno anakaa Luhila huko, tena mshamba mshamba tu!” alisisitiza Idd kwa sauti ya dharau za hali ya juu, “aiseee, kama ni kweli basi analo hilo, nasema kaisha huyooooo” alisema Mahadhi kwa sauti ya kishabiki na kushangilia, kisha akakata simu, “sasa mdingi wako anahusika nini na mchongo huu” aliuliza Talib ambae muda wote wamaongezi alikuwa kimya kabisa akiwasikiliza, “we subiri moto wake kutoka kwa wazee wabaraza” alisema Idd, kwa sauti ambayo ilionyesha amepatwa na furaha ya ghafla.**********
Huko mtaani habari za kufumaniwa kwa mama Hilda ziliendelea kuzagaa kwa speed sana, kama ingekuwa miaka hii ya sasa nadhani video zake zinge zagaa kwa fujo Luhila nzima, karibu sehemu zote kuanzia sokoni, mtaani kwenye majumba ya watu, mpaka kwenye vilabu vya pombe, ambako zilimfikia Hilda ambae alikuwa amaeshapata mfadhiri aliekuwa anamnunulia ulanzi, ambao waliunywa taratibu huku wakisubiri giza waingie kichakani wakapeane dudu.
Baada ya Hilda kuzinasa habari hizo, huwezi kuamini, ukweli alizipotezea na kudharau, “shauri zake nani alimuambia aingie kichakani mchana wote huu?” alijiongelesha Hilda aliekuwa anaendelea kunywa pombe yake ya ulanzi, ambayo na yeye angeenda kuilipia kama alivyo ilipia mama yake, sio kwamba Hilda hakuwa na kumbu kumbu juu ya baba yake, lakini aliona kuwa kumhudumia baba yake sio jukumu lake.
Shangazi yake Hilda akiwa amesha shuhudia kila kilichotokea kwa wifi yake, yaani mke wa mzee Komba kama tunavyo mfahamu kuwa ni mama Hilda, na alipoona watu wanatawanyika na kumuacha mama Hilda akiwa amefungiwa ndani ya ofisi ya mwenyekiti wa kijiji huku mgambo wakiingia porini kwenda kumsaka bwana Njogopa, yeye akaondoka zake na kuelekea zahanati alikomuacha kaka yake, “vipi umewakuta” aliuliza mzee Komba, ambae hata sauti yake ilionyesha wazi kuwa katika tatizo la kiafya, sijawakuta, nitaenda tena baadae kwasababu nadhani nitahitajika kukaa huku kwa siku kadhaa ili kukuhudumia” alisema shangazi huku anajitabasamulisha, ila moyoni mwake alikuwa ana nusu furaha kwa kile kilicho mkuta wifi yake mzinzi, ambao umemfanya kutelekeza mume wake hospital, pia alikuwa na nusu huzuni kwa kaka yake kuchagua mke wa aina ile huku familia yake ikizidi kumvuruga, sio mama alie fumaniwa porini wala binti yake ambae amebatizwa jina anaitwa
TEMBELE LA UWANI msaada kwa wenye njaa, kilicho muumiza kichwa shangazi ni namna ambavyo angeweza kumuhudumia kaka yake hapa hospital maana wenyeji wake hawaeleweki, na mmoja ndiyo huyo tayari alikuwa amefungiwa ndani kwa usalama wake, akiwa amesha tembezwa uchi na kushuhudiwa karibu nusu ya wanakijiji wenzake.
Wakati anaendelea kuwaza na kuwazua huku akishindwa kumsimulia kaka yake juu ya kilichotokea huko mtaani mara akaingia mzee Nyoni pale hospital, huku anatoa harufu ya pombe aina ya ulanzi, kitendo kilichomshangaza hata yule nurse, maana ni mmoja kati ya wale waliomleta pale zahanati na kumtelekeza, “pole sana bwana Komba, nime kutana na ngonyani akanieleza kuwa umeletwa hapa” alisema Nyoni, huku anataka kukaa kwenye kitanda cha pembeni, maana mule ndani kulikuwa na vitanda viwili tu! “samahani mzee wangu, haturuhusu kukaa kwenye kitanda” alisema Nurse, akionyesha wazi hakupendezewa na ujio wa mzee yule, “ndiyo bwana Komba za toka juzi, maana tuliona tu ghafla umeingia ndani halafu shemeji anapiga kelele, tukajuwa mnapigana, mara hoo msaada msaada, hivi kilitokea nini?” aliuliza nyoni, huku akiacha kukaa kwenye kitanda kama alivyo ambiwa na kubakia amesimama, lakini Komba hakujibu kitu, “kwani kaka huyu ni rafiki yako pia?” aliuliza dada yake Komba, kama nyoni angekuwa na akili za akiba basi ange gundua kuwa swali lile lilikuwa ni la mtego, “ndiyo mimi ni rafiki yake wakushibana kabisa, unadhani hapa hospital aliletwa na nani” alisema Nyoni kwa majisifu, “kwahiyo toka ukutane na Ngonyani asubuhi ndio unakuja sasa hivi?” safari hii aliuliza Nurse, “kulikuwa na tukio huko mtaani ndio lilinichelewesha, maana kosa mimi shemeji angekuwa amesha kufa” alisema Nyoni, akijisifu, huku Komba akiwa hajaelewa kinachoendelea, kama ilivyokuwa kwa nurse na shangazi, “we! kaka wewe acha uongo wewe umesaidia nini pale, tena hata sura yako sikuiona, au ndio umbea umekuleta hapa hospital” aliuliza shangazi kwa sauti ya kusuta, “tena mtu mbaya sana huyu mzee, wewe na wenzako mulimkimbia mwenzenu hapa hospital leo umesikia umbea ndio unakuja kuuleta hapa, tafadhari naomba utoke hapa hospital mgonjwa anataka kupumzika” alisema nurse na kabla hata hajamaliza kuongea tayari Nyoni alishatoka kwa hasira na kuwaacha wakina shangazi wanacheka, “jamani kwani kime tokea nini huko nyumbani?” aliuliza mzee Komba na hapo ambae alikuwa anaona picha picha, shangazi hakuwa na jinsi akaanza kusimulia kama ilivyo kuwa na mwisho wa simulizi mzee Komba akasema, “kwa niliyo ya sikia mwanzo kwa sasa siwezi tena kuzimia.******
Naam baada ya hapo, Higgno akapewa nafasi ya kuongea, “kwanza niombe msahama, kwa kilichotokea mwanzo, siwezi kumlaumu Soraya kunificha kuwa ni mtoto wa Mahamu, pengine…..” alisita kidogo Higgno, ni kama alipatwa na kihoro cha furaha “pengine alidhania nisinge kuwa nae, lakini ukweli ni kwamba toka mwaka tisini na nane, sikuwahi kujuwa wala kuwaza kuwa Soraya ni mtoto wa Mahamud, naomba msamaha kwa usumbufu uliojitokeza kwa kukataa kwangu kuwa simjui mtoto huyo wa mahamud, lakini pia naomba musinilaumu kwa jilo, mwisho ningependa kuwaambia kuwa hapa nimekuja na baba yangu na mama yangu” alimaliza Higgno na mjomba akadakia, “baba na mama Higgno wasimame waje hapa mbele”alisema mjomba na ikawa hivyo baba na mama Higgno wakasogea pale walipokuwepo wakina Higgno huku nyuso za furaha zikiwa zime tawala miongoni mwao, “karibu sana katika nyumba hii, na tunaomba mutueleze malengo yenu kwa binti yetu” alisema Mjomba na hapo kila mmoja alitulia kusikiliza, “asante sana jamani, kwa kweli mimi hapa nizaidi ya nyie muliokuwa munajuwa kilichokuwa kinaendelea, kwasababu kwa upande wangu, nilikuwa najiandaa kuwa mshenga, labda Higgno mwenyewe aeleze mipango yake” alisema mzee Frank, kwa sauti ya upole kama mwanae, huku anatabasamu akionyesha kupendezwa na tukio lililokuwa limetokea mahali pale kwa kijana wake kumpata mchumba, tena mtoto wa Mahamud, ukiachilia utajiri wa baba yake pia mschana huyu mwenye moyo wa huruma alikuwa ni mzuri sana, “mipango yangu ni kutafuta kazi ili niweze kupata nyumba ya kukaa na Soraya ndipo nifunge nae ndoa” alieleza kwa kifupi Higgno, jibu ambalo kila mmoja alilipenda.
Naam sasa uliwadia sasa wa Mahamud mwenyewe kuongea jambo, lakini kabla hajaongea lolote mara simu yake ikaita na alipoitazma alikuwa ni mwenyekiti wa baraza la wazee wakiislam, “samahani kidogo jamani” alisema Mahamud na kupokea simu, “hallow asalam alaykum mwenyekiti” alisalimia Mahamud, huku watu wakiendelea na maongezi ya chini chini, wakisifu kile kilichokuwa kinaendelea kutokea ndani ya nyumba ya Mahamud, “waalaykum salaam Mahamud, naona nimeingilia shughuri yako, pole kwa hilo” alisema mwenyekiti, huku Soraya akisikia kwa mbali sauti hiyo toka kwenye simu ya baba yake.
Ukweli Mahamud alishangaa kusikia kuwa mzee wa baraza alikuwa anafahamu shughuri iliyokuwa inaendelea mule ndani mwake, “hooo! hakuna tatizo mwenyekiti, tunaweza kuongea” alisema Mahamud ambae sasa mapigo ya moyo yalianza kuongeza kasi, maana hakujuwa ile simu inataka kuleta ujumbe gani na mwenyekiti alijuwaje kama leo kuna shughuri nyumbani kwake, “Mahamudu, hivi umeshindwa kuowaona vijana wote wakiislam mpaka unataka kumkabidhi binti yako kwa kafiri?” swali lile gumu sio tu lilisikika kwa Mahamud peke yake hata kwa soraya aliekuwa amesimama karibu na baba yake, pia alisikia……. labda wasomaji niwaambie tu, ghafla ni nzuri kuliko ahadi… (surprise is better than promise) pia asanteni sana kwa msaada wenu na mchango ambao unaendelea kutuletea burudani, hivyo endelea Kufuatilia mkasa huu hapa hapa JamiiForums