TEMBELE LA UWANI
SEHEMU YA SABINI NA SITA
MTUNZI
Mbogo EDGAR
ILIPO ISHIA SEHEMU YA SABINI NA TANO: “hata mimi sijui, na jana ametuma sms anasema tayari amesha chukuwa funguo, na kwamba wasifanya makosa kama waliyo yafanya kule shamba” alisema Soraya, ambae pia hakuonyesha kama anatambua maana ya funguo ile, “kwahiyo anataka wavamie nyumbani kwenu?” aliuliza Laylah kwa mshangao uliochanganyika na uoga, “pengine wanataka kuvamia ndani, si unakumbuka zamani alikuwa anaiba vitu vya ndani anaenda kuuza?” alisema Soraya akimkumbusha Laylah, matukio ya nyuma ya Talib, “sasa wewe umeamua nini?” aliuliza Laylah, wakati huo alikuwa amesha kanyaga mafuta mengi kueleka mjini……ENDELEA NAYO
Kwanza Soraya alitulia kidogo kama anatafuta jibu, kisha akajibu “naenda kuwaeleza wakina mama, wakiwa wabishi shauri zao” alisema Soraya ambae kiukweli alishaona kuwa wazazi wake wanamuamini sana Talib, “sikia Soraya usiwaambie kwanza, maana ninavyo wajuwa wale watakurupuka kumuuliza Talib, bora tuweke mtego mpaka wakamatwe halafu unautoa ushahidi” alisema Laylah, na hapo Soraya akaonekana kuvutiwa na mpango wa Laylah, “sasa mtego gani tuna weza kuuweka?” aliuliza Soraya akiwa mwenye hamu ya kusikia mtego wa Laylah, Sasa walikuwa wanalipita eneo la soko kuu, kisha Laylah akakata kushoto, kuingia barabara ya kwenda kwa kina Soraya, “wala usiwe na haraka tutapanga ukiwa unaenda kazini, ngoja kwanza ukajiandae maana tumechelewa” alishauri Laylah ambae hakuwa na wazo jingine zaidi ya kuwashirikisha polisi katika swala hili, maana hakuwa na njia nyingine ya kuwadhibiti hao watu kama kweli walikuwa na mpango wa kuvamia, “sawa lakini inabidi tutumie akili” Soraya aliunga mkono swala lile na wakati huo tayari walikuwa wanasimamisha gari mbele ya geti la nyumbani kwao, ambalo lilifunguliwa mara moja.
Lakini ile linafunguliwa tu! wakaliona Nissan Patrol linataka kutoka, “usiingie kwanza msubiri atoke” alisema Soraya kwa sauti ya chini iliyojaa tahadhari, akionyesha kuwa hakutaka kukutana na baba yake Asubuhi ile, sijui kwanini lakini haikusaidia, kwasababu ndio kwanza wakaliona Nissani linarudi nyuma kuwapisha wao, “pita lakini usisimame” alisema Soraya ambae ni wazi kabisa hakutaka kuongea na baba yake, na hapo Laylah akaingiza gari ndani, lakini tayari Mahamud alisha shuka toka kwenye gari na kusimama kwenye njia ambayo wao ilibidi wapite, hawakuwa na ujanja, Laylah akasimamisha gari, karibu na aliposimama Mahamud, “Assalam alaykum” walisalimia wote wawili yaani Soraya na Laylah,huku Soraya akishindwa kumtazama baba yake usoni “Waalaykum Salaam, naona leo mumeniwahi vipi huko mutokako?” aliitikia Mahamud ambae uso wake ulionyesha kuwa mwenye uchangamfu “salama tu baba, nimewahi ili nisichelewe ofisini” alisema Soraya akijitahidi kuchangamsha sauti yake, lakini ili onyesha wazi kujishtukia, “kuhusu ofisini we leo usije bakia hapa nyumbani ili ushirikiane na mama yako kuwaandalia wageni,si unajuwa wakwe zako wanakuja?” alisema Mahamud akiingiza utani kidogo, wote watatu wakacheka huku Soraya akionekana mwenye kujawa na aibu, “hivi baba wakija nani atawatambulisha mi siwezi” alisema Soraya, na hapo wakacheka tena, “atatutambulisha Laylah, najuwa anawafahamu vyema kabisa” alisema Mahamud wakacheka tena, “kaka Talib umesha muambia kuwa kuna ugeni?” aliuliza Soraya, ambae mpaka sasa koo ni kama lilikuwa linamkereketa kwa kutamani kueleza kilicho tokea, “mh! sijamuambia, ila nadhani atakuwepo, “mimi mwenyewe siendi kukaa sana huko ofisini narudi sasa hivi kuwasubiri wageni” alisema Mahamud ambae kiukweli alikuwa anatamani kule alikoenda Talib arudi na jibu kamili la upelelezi wake ili awaumbue wageni wake.
Naam baada ya maongezi mawili matatu wakaagana, lakini Mahamud alipotaka kuondoka akaonekana kusita ghafla, halafu Soraya nilisahau kukueleza jana kuwa ile nafasi ya yule kijana, tayari nimeshampata mwenyewe, hivyo wafanyakazi wote wameshatimia” alisema Mahamud pasipo kujuwa tayari Soraya alikuwa anafahamu swala hilo, “hooo! alikuja ofisini?” aliuliza Soraya ni kama alikuwa anamchota akili baba yake, “nilikutana nae mjini, kilichotokea ni maajabu kwa kweli, nimeona vijana lakini huyo ni kiboko” alisema Mahamud kwa sauti ya kusifia, kitendo ambacho kilimfanya Soraya atabasamu, huku moyoni akishangaa sifa alizo mwaga baba yake, maana ni kama Higgno hakumueleza kitu chochote cha kustaajabisha, “kwanini baba, mbona unamsifia sana huyo kijana, amefanya nini?” aliuliza Soraya kimtego mtego, “kwa kweli yule kijana ni mtu wa ajabu sana” alisema Mahamud na kuanza kueleza kuhusu kilicho mtokea, baada ya kuingia kununua vocha na kujikuta hakuwa na wallet, “ile nimechanganyikiwa nikamuona yule kijana anakuja na kukabidhi, kumbe nilidondosha wakati naiweka mfukoni, hapo nikaambatana nae mpaka msikitini” alieleza Mahamud jinsi walivyoongea mpaka walipo agana na yule kijana, “sema nilisahahu kumuuliza jina, ila amechukuwa namba yangu” alisema Mahamud, “hukumueleza kuhusu kunichumbia” aliuliza Soraya ambae alifarijika kwa simulizi ya baba yake na sifa alizo zimwaga kwa Higgno, huku akiwa hajuwi kuwa huyo kijana ndie Higgno wa Soraya.
Kwa swali hilo la Soraya Mahamud akainamisha kichwa chini, “yaani katika vitu vizuri ambavyo nimeshindwa kukupatia mwangu ni huyo kijana, ambae amesema tayari ana mchumba na mimi ameomba niwe mshenga wake” alisema Mahamud akamsimulia kila kitu hata jinsi alivyo mshawishi kwa magari na nyumba pia na fedha ya mtaji wa biashara atakayo itaka, “lakini huwezi amini alikataa katakata, ila aliongea jambo la msingi” alisema Mahamud hakueleza majibu ya Higgno, “kwani baba wewe unaweza kuwa mshenga wa Higgno?” aliuliza Soraya mara baada ya baba yake kumaliza kusimulia, “mh! we uliona wapi hiyo, yaani nijiletee barua mwenyewe?” aliuliza Mahamud huku anacheka kweli kweli na kueleka kwenye gari lake akaingia na kuondoka zake, na wao wakaelekea sehemu ya kuegeshea gari, kwasababu hakukuwa na safari yoyote ya kutoka pale nyumbani, “kwanini ulimuuliza vile baba yako” aliuliza Laylah, “nilitaka nijuwe kama ana fahamu kuwa Higgno ndie huyo kijana au laa” alijibu Soraya, huku gari linasimama sehemu ya maegesho, “sasa Laylah, twende chumbani kwangu tuka pange mpango wa kupata ushahidi” alisema Soraya, kisha wakashuka na kuingia ndani ile wanafika sebuleni na kupokelewa na mama Soraya ambae alikuwa anaelekea jikoni kutoa maagizo, “hooo! walaykum salaam Soraya, kumbe umesharudi, anasemaje mkwe?” aliitikia mama Soraya na kuuliza hali ya mkwe wake, maana alionyesha wazi kuwa anafahamu alikolala Soraya, “yupo tu anakusalimia, atakuja baadae na baba yake” alijibu Soraya huku anatembea kuelekea chumbani kwake akifuatiwa na Laylah, “umesha nogewa hata nyumbani hapalaliki” alisema mama Soraya kwa sauti ya kusimanga, Soraya hakuwa na jibu zaidi ya kupiga hatua kuelekea chumbani kwake, na wakati anafungua mlango akamsikia mama yake akitoa maagizo, “na ujifungie huko chumbani hakikisha unajiandaa vizuri, Laylah hakikisha Soraya anavaa vizuri anapendeza” alisisitiza mama Soraya.*******
Mzee Komba akiwa kitandani hawezi kuamka na kujisongea hata hatua moja, alikuwa ametulia kimya anasubiri gari ambalo litampelekea Zahanati ya shule ya sekondari ya wavulana ya songea, huko mtaani kwao Luhila, huku machozi yakimtiririka machoni mwake na kushuka mashavuni, sio kwamba jakutaka kurudishwa Luhila au kuna maumivu alikuwa anayasikia kwa wakati huo, la hasha, hakika mzee Komba alikuwa katika mawazo ya kuumiza zaidi ya jipu la kwapa au jino lililo toboka.
Ukweli ni kwamba ilishapita siku nzima pasipo kuwaona mke wake wala mwanae Hilda, achana na wakina mzee Ngonyani ambao kwa habari za juu juu hawakuweza hata kusubiri apande gari kuletwa hospital ya mjini, hawakusubiri hata azinduke na kumuuliza tatizo nini, “kwahiyo urafiki wetu ni wa bure” aliwaza mzee Komba, ambae hakutaka kukumbuka maneno aliyoyasikia katika maongezi ya mkewe na binti yake, “hata mimi kanifanya tena kote kote” hakika ni maongezi ambayo kila alipoyakumbuka alihisi kizungu zungu kilikuwa kina mnyemelea, “hebu ona, mtu niliemkusudia mabaya ndiyo huyu kanisaidia, na anaendelea kunisaidia” aliwaza mzee Komba, ambae alikumbuka vyema kabisa kuwa sababu ya mke wake na mwanae kurudi wakishindwa kutembea vizuri ni sababu sehemu zao za uke, zilisulubiwa vibaya sana, kitendo ambacho hakuwahi kukifanya hata kipindi cha cha ujana wake akiwa na nguvu zake, na mbaya zaidi ni kwamba mkewe na mwanae waliingiliwa na mwanaume mmoja, ambae ni kibabu kikongwe, (mbuya mundu) na mbaya kuliko mbaya zaidi, ni kwamba aliwatuma yeye mwenyewe kwenda kumloga mtu ambae mtu huyo ndie aliemsaidia kumleta hapa hospital na bado mtu huyo huyo na familia yake wanaendelea kumsaidia, hata swala la kusongezwa karibu na huduma ni ombi la familia hiyo hiyo ambayo yeye aliifanya adui zake pasipo kukumbuka sababu ilikuwa nini, “sijui nita mtazama bwana Frank?” aliwaza bwana Komba, ambae alikumbuka jinsi walivyo shangilia duka la bwana Frank lilivyoungua moto, huku wakinywa pombe na kuimba nyimbo za mafumbo, sasa aliokunywa nao pombe hakuonekana hata mmoja, yaani hata mke wake aliemsababishia matatizo pia hakuwepo karibu yake, “ni washenzi sana watu hawa” alijisemea Komba, ambae alikumbuka mema yote ambayo binti yake alifanyiwa na Higgno, kuanzia wakiwa wanasoma shule ya msingi hata kuweza kwenda sekondari wakiwa ni vijana pekee wa kutoka Luhila kwa mwaka ule, na licha ya binti yake kumfanyia Higgno mambo yasiyofaa, lakini bado kijana yule aliweza kumsaidia fedha ya matibabu, mwishoe wakamlipa ubaya kwa kumsingizia ndoa ya mkeka, “ambayo iliisha kwa kwenda kumfanyia fujo akiwa na yule mvuta bangi” alisema kwa masikitiko mzee Komba, huku machoz yakimtiririka kama maji kwenye bomba bovu, “Ee mungu mwenyezi mzidishie bwana Frank, mjalie kila lililo jema na neema” mwisho mzee Komba alijikuta anasema hivyo, kwa moyo kunjufu kabisa.*******
Kijana Idd leo pia aliamka mapema sana, kulikotokana na kukatika kwa usingizi wake mapema sana, maana adhana ya saa kumi na moja alfajili ilimkuta yupo macho kwa kuwa alishaacha utaratibu wa kuswali, basi alibakia kitandani huku akiwaza hili na lile kuhusu mambo yaliyomtokea jana kule kwenye baraza la wazee, “yule demu nuksi kweli kweli, yaani ameharibu kila kitu” aliwaza Idd akiwa bado kitandani ana jigeuza geuza kama vile kitanda kina kunguni, “hebu ona amesababisha nimesha daharaulika, na hizi habari zikizagaa nitaonekana wa ajabu hapa mjini” aliendelea kuwaza Idd, ambae kiukweli alisha jiaminisha kuwa ange mnasa Soraya, ambae ukiachilia uzuri aliokuwa nao pia angekuwa na fedha nyingi sana, “halafu ikibainika kuwa sisi ndio tume sambaza ile messeji yule mzee ana tutupa ndani, maana ana hasira huyo?” hapo Idd akajikuta anavuta picha ya gerezani, na kuhisi mwili unamsisimuka kwa kile anacho kisikia kina fanyika mahali huko, “duh! bora nifanye mchongo nipate fedha kisha nisambae zangu ni kajichimbie hata Malawi au Zambia, nikishindwa hata Gado(mashariki kaskazini, mwa msumbiji” aliwaza Idd, “na hapa nimcheki dingi anipatie hela kidogo nikatulie mtini pub, nitafute demu mmoja mkali nile nae bia” aliwaza Idd ambae kiukweli akiwa hapa Tanzania baba yake ndie alikuwa chanzo chake cha fedha
Naam kulipo kucha Idd alitoka chumbani kwake na kumvizia baba yake aliekuwa anatoka kwenda dukani na kumuomba fedha, ambae alimkabidhi elfu arobaini, “ujipange vizuri, inabidi tukaombe msamaha kwa Mahamud na wazee wa baraza kwa kitendo chako cha kutoka kikaoni bila adabu” alisema mzee Mahadhi wakati anamkabidhi mwanae fedha hiyo, hakujuwa kuwa fedha hiyo ndiyo chanzo kibaya cha kumponza mwanae.*******
Talib nae alifika kwa kina zido na kuwakuta wakiwa wametulia uwani wakivuta bangi, huku wanapanga jinsi watakavyo vamia nyumbani kwa tajiri Mahamud na jinsi mgao utakavyo kuwa, “lakini inabidi tupate gari la kuondoka nalo eneo la tukio” hilo ndilo swala ambalo hata Talib alilikutia, japo hakuangaika nalo kwanza yeye aliliza vidole vyake ikiwa ni ishara ya kuomba apewe msoko wa bangi uliokuwa unavutwa na wenzake, nao wakamtembezea kisha akaanza kuivuta kwa pupa, akionyesha kuwa alikuwa na kiu kali kweli kweli, “Talib tunafanyaje kuhusu gari?” aliuliza Vitus na wote wakasubiri jibu la Talib, “lile gari langu halina mafuta hata kidogo, vinginevyo tunge litumia hilo” alisema Talib na wezake wakatazamana kwa mshangao, “yaani gari lile lile la mjomba wako litumike kuiba nyumbani kwake, hata akitokea mtu kwa bahati mbaya akaliona si atajuwa kuwa wewe unahusika” aliuliza Zido kwa mshangao, “unadhani hilo tatizo basi, sema tatizo ni mafuta tu” alijibu Talib huku akiwa anajitahidi kubana moshi alioujaza mdomoni, “Talib acha kuzingua, we inawezekana vipi likatumika gari la mjomba wako, hata kama lingekuwa na mafuta” aliuliza Vitus, ambae alianza kuona Talib bangi inamchanganya, “tatizo we hujausoma mchezo, yani wale si wanaingia kulala mapema tu!?” aliongea Talib, na kuweka kituo ambacho alikitumia kuvuta tena bangi yake, kisha kuuzuwia moshi kwa ndani na kumfanya aongee kwa shida, “yaani mida ya saa Tano tu! tayari wanakuwa ndani, mimi wakisha ingia tu nitawatumia messeji kuwa julisha, kisha nyie munaenda getini, muna mkamata mlinzi munamfunga kwenye gunia kisha muna mtupia barabarani agongwe na gari halafu nyie munazama ndani kupitia ule mlango wa nyuma kama nilivyowaambia, munafungua mlango kisha munaingia ndani kwenye lile korido munaenda mpaka mlango wa tatu upande wa kulia, mnafungua na kuingia ndani uwa afungagi ule mlango” kufika hapo Talib akaweka tena kituo na kuvuta tena bangi, “mukifika mule ndani munatazama kwenye ukuta wa kushoto kwenu, munaona picha munaitoa ile picha” alieleza Talib akieleza namna ya kufungua lile kabati la ukutani ambalo hata siku ile alimuona mjomba wake anafungua, “halafu muna toka kiulaini kabisa, yaani hata kama lingekuwa Hyundai, hakuna wakuuliza, maana tayari mlinzi alishazimwa kitambo” huo ulikuwa ndio mpango wa Talib, nao wakauona ni wa ukweli, “kweli bwana ingekuwa poa sana, sasa inabidi tufanye mchongo wa gari” alisema Zido, akionyesha kuukubali mpango wa Talib.
Naam waliendelea kupanga mipango yao huku wanavuta bangi zao walitumia masaa zaidi ya matatu mpaka kufukia muafaka, “ok! hilo niachieni mimi, wacha niende nikafanye mpango wa mafuta ili tulitumie Hyundai” alisema Talib huku anainuka nakujiandaa kuondoka zake akichukuwa kiasi flani cha bangi ambayo angeenda kushinda nayo anaivuta pale nyumbani kama alivyopanga ili mjomba na shangazi yake wasiweze kumshtukia kama anajusika na tukio litakalo tokea, na mwisho wakakubaliana na Talib, kuwa akafanye mpango wa kupata hela ya mafuta aweke kwenye lile gari la nyumbani, kisha watumie kwa kuondokea baada ya tukio, “ila jamani hee! mi naona Talib afanye mpango wa kutafuta gari nyingine, kwasababu kwa vyovyote vile gari likiwashwa lazima watu wataamka na kusanukia mchongo” alishauri mmoja kati ya wale vijana wanne, “ni kweli jamani, au kama vipi tukishindwa kupata gari basi tutumie pikipiki tu!, maana zipo zile mbili tukiongeza moja wote sita tunaenda” alishauri mwingine na hapo wakampa jukumu Talib kutafuta gari dogo ambalo lita wasubiri nje ya uzio wa Mahamud, wakisha maliza kazi waondoke nalo, huku wengine wakitumia pikipiki kama ilivyo kuwa kule shamba,
Hatimae Talib aliaga na kuondoka zake, huku njia nzima akiwaza na kupanga jinsi atakavyo tumia mamilioni ya fedha ambazo atazipata baada ya wenzake kuiba nyumbani kwa mjomba wake, na kikubwa ni lile wazo lake la kwenda dar es salaam kupumzika kwa siku kadhaa, huku akiwa amechagua mschana mrembo ambae atatumia nae kiasi fulani cha fedha na mwisho anunue gari zuri na kurudi songea kuanzisha biashara kubwa sana ambayo itahitimisha maisha ya kuwa tegemezi.*******
Baada ya kufika ofisini kwake mapema bwana Mahamud na kuwakuta wafanya kazi wake wakina Jamal wakiwa wanaingia pale ofisini, na wao walishangaa kidogo kumuona boss wao akiwa amewahi sana pale ofisini, “Jamani leo ni dharula ya wageni nyumbani, hivyo sitakaa sana hapa ofisini nitarudi nyumbani kwaajili ya ugeni huo” alieleza Mahamud, akiwa ofisini kwake anatoa maagizo ya mambo ambayo inabidi yafanyike, na mgawanyo wa kazi kwa wale fanyakazi wapya, “cha msingi wawe chini ya ungalizi mkubwa, maana kuna mambo mengi ya kuelekeza na kuwachunguza” alisisitiza Mahamud, ambae baada ya kumaliza kutoa malekezo akaanzisha mada nyingine, “hivi Jamal, unamfahamu kijana mmoja anaitwa Higgno, na baba yake anaitwa mzee Frank wanakaa huko Luhila, au Matogoro?” aliuliza Mahamud, kabla hajaondoka pale ofisini, swali lilikuwa gumu kidogo, maana Jamal ambae aliwahi kueleza sifa za Idd, ambazo baadae Mahamud alibaini kuwa ni za kweli, aliwatazama wenzake kama vile anawauliza kama wanawafahamu watu hao, lakini hakuona alieonyesha dalili za kuwa fahamu, “labda boss ungefafanua, ni watu wa aina gani na wamefanya nini, maana wakina Higgno na wakina mzee Frank wapo wengi sana hapa Songea” alisema Jamal, akimtaka mzee huyu kutoa sifa tabia na uwezo wa watu hao, “sijui nianzie wapi, labda ngoja niwasimulie kwa ufipi” alisema Mahamud, na kuanza kuwasimulia habari ya binti yake na kijana Higgno, ambae hapo mwanzo waliwahi kumuita kijana mpole .
“nadhani niliwasimulia juzi kuhusu habari za kijana aliewahi kumsaidia Soraya mara tatu, lakini leo kuna utofauti kidogo” alisema Mahamud ambae alieanzia kusimulia mkasa wa Higgno na Soraya, akianzia miaka zaidi ya mitano au sita iliyopita, wakati binti yake akiwa kidato cha pili pale alipovamiwa na wanafunzi watukutu wa shule ya wavulana ya Songea na kutaka kumubaka, kisha kutokea kijana yule na kumsaidia kwa kupambana na wanafunzi wale akimfanya Soraya apate mwanya wa kutoroka, na kumuacha kijana yule anapambana, na hata alipofika yeye akiwa na polisi waliwakuta wanafunzi wanne wakiwa katika hali mbaya ya majeraha makubwa miilini mwao, huku kijana yule akiwa amesha toweka na kushindwa hata kumpa pongezi au shukrani, kwa kile alicho kifanya, Mahamud alisimulia pia matukio mawili yaliyotokea kwa Soraya na kusaidiwa na kijana huyo huyo, ambae baba yake ameunguliwa na duka na binti yake ameamua kumsadia, akiwa hajui kama ni baba wa kijana huyo, maana wao walifahamiana baada ya yule mpuuzi Idd kumpamia mzee wa watu na gari, “sasa jana yule mpwa wangu amesema kuwa huyo mzee ni tapeli, na pengine waliomchomea duka ni watu ambao aliwahi kuwatapeli, pia kuhusu Higgno kumsaidia Soraya ule ulikuwa ni mchongo ambao umepangwa na kijana yule ili kumuweka Soraya karibu yake na pengine kumchumbia kabisa akiwa na nia ya kufuata fedha na mali” alisema Mahamud huku akisimulia kwa mapana jinsi ilivyokuwa siku ya tukio, akilazimishwa kutoa fedha na alipotaka kujaribu kuweleza polisi kabla sijapiga simu kwa RTO, nikapigiwa na watekaji wakasema niache mara moja kuwashirikisha polisi, vingenevyo wangemuua Soraya” alimaliza Mahamud, kutoa simulizi yake, ambayo muda wote aliisimulia kwa sauti iliyojaa mashaka na shuku kwa kijana huyo Higgno na wazazi wake Frank, “samahani boss, labda nikuulize swali, sasa baada ya kusikia hivyo ulichukuwa uamuzi gani?” aliuliza Ayub, ambae pia ni mmoja wa wafanyakazi pale ofisini, “kiukweli sijui mpaka sasa natapa tapa tu!, na nikitazama Soraya amezama kweli kweli kiasi cha kuanza kuandaa washenga, lakini nimemtuma Talib afanye uchunguzi wa kina apate ushahidi ili tuwabaini watu hao” alisema Mahamud, kisha akawatazama wakina Jamal kuona watachangia nini katika habari ile inayowahusu wakina Higgno na baba yake, “boss hapo kweli kuna utata, kama kweli ulikuwa ni mpango umepangwa na Higgno, ambae kiukweli sijawahi kumsikia kabisa, basi pia kuna mtu wako wa karibu alihusika katika swala la kumteka Soraya” alisema Jamal, na hapo Mahamud akashtuka kidogo, huku moyoni akimpuuza Jamal, huyu nae, kama amekosa cha kusema si aseme tu” alijisemea kimoyo moyo, bwana Mahamud, “hata mimi nilitaka kusema hivyo hivyo, yaani boss kama ilikuwa hivyo inabidi uwe makii sana katika uchunguzi wako?” alisema Ayubu, na hapo Mahamud akaanza kutilia maanani kauli zile mbili zinazo fanana, “kivipi hebu nifafanulieni” alisema Mahamud kwa sauti ya kuchanganyikiwa na jambo lile……. ITAENDELEA MUWE NA USIKU MWEMA