Sehemu ya 96
Kwa kweli nilikuwa mwanaume mpumbavu sana.
Siku hiyo tulilala vizuri, ingawa mara kwa mara usiku nilikuwa nikijiwa na ndoto za ajabu ajabu. Asubuhi kulipokucha, nilikwenda bafuni kuoga tayari kwa kuendelea na shughuli zangu za kila siku.
Wakati natoka bafuni, ile namaliza kushuka ngazi za bafuni, nikasikia sauti nzito ya mwanaume ikiniita ndani ya bafu, wakati nageuka kutizama, sijui nilikanyaga wapi, nikateleza na kupiga mweleka.
Nilianguka kidogo tu, ajabu nilipata maumivu makali sana ya kwenye goti, nilipotaka kusimama nikashindwa kabisa. mfupa wa mguu ulikuwa umevunjika.
Toba!!
****
Ni siku ya tatu nilikuwa nimelazwa kwenye hospitali ya Kitete ya mjini Tabora. Mguu wangu uliovunjika baada ya kuanguka bafuni ulikuwa umefungwa hogo.
Katika zile siku tatu zilikuwa ni siku za mateso makubwa, mguu ulikuwa unauma kana kwamba, kulikuwa na mtu anakwangua mfupa kwa kisu ndani kwa ndani.
Muda wote nilikuwa nalia kwa maumivu makali hadi madaktari wakashangaa.
“Itabidi afanyiwe kipimo cha X- ray upya, inawezekana kuna mahali kwenye mguu wake kuna tatizo.” Dokta aliamwambia Lawalawa aliyekuwa akiniuguza hospitalini hapo.
“Inawezekana kweli?”
“Kabisa.”
Mwanamke huyo hakuwa na tatizo, alilipia gharama za vipimo, muda mfupi badaye nikachukuliwa na kupelekwa maabara. Huko nikafanyiwa upya kipimo cha X- ray.
Majibu yalipotoka hayakutofautiana na yale ya awali, sehemu mfupa ulipovunjika ilikuwa ni palepale.
Sasa maumivu hayo yalitokana na nini?
Siku hiyo nililala nikiugulia maumivu makali. Pamoja na kuchomwa sindano za ganzi na maumivu, lakini wapi, niliendelea kuteseka usiku kucha.
Asubuhi ya siku ya pili, siku ya nne tangu nilazwe hospitali ya Kitete, tofauti na siku zingine hadi inatimu saa sita mchana, sikuwa nimemwona mpenzi wangu Lawalawa.
Kwa kuwa hapakuwa na mtu mwingine aliyekuwa akiniuguza zaidi ya Lawalawa, nilijikuta nakosa chakula. Kwa kudra zake Jalali. Kulikuwa na chakula cha msaada, siku hiyo kikanifaa. Hadi inatimu saa kumi jioni bado sikumwona Lawalawa.