SEHEMU YA 33
Hapo akili yangu ikapiga kengele. Jina hilo halikuwa geni, niliwahi kulihisi kabla. Siku ile nilipokuwa nikila chakula na Scaila, namba hiyo ilipiga kwenye simu yake, sikuwa na uhakika kama jina lilikuwa Alfred ama Albert, ila leo nikapata uhakika kwamba mtu aliyepiga alikuwa huyo Alfred, ila yeye aliniambia alikuwa Janeth.
Hapo nikashikwa na machale zaidi, nikahisi kabisa kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea, ila kwa sababu nilikuwa mwanaume, sikutaka kujali sana, nikajifanya kupotezea na hapo ndipo nilipoanza kazi rasmi ya kumchunguza huyu Scaila.
Niligundua inawezekana alikuwa na michezo mingi nje ya kumi na nane aliyokuwa akiicheza ila sikuwa nikiijua kwa undani. Ilikuwa ni lazima nifanye kila linalowezekana kuhakikisha naujua ukweli kabisa.
Scaila hakuwa demu, alikuwa mchumba wangu ambaye nilipanga kufunga naye ndoa, hivyo kupoteza muda wangu kwa lengo la kumchunguza halikuwa tatizo hata kidogo.
“Akitoka Alfred ndiyo anaingia Scaila,” aliniambia mama yake bila kuona aibu hata kidogo.
“Nimefurahi kumfahamu!” nilisema huku nikiwa nimetoa tabasamu pana kweli, yaani sikutakiwa kuonekana nikiwa na shaka hata kidogo.
Basi tukaongea mambo mengi, muda mwingi nilikuwa na furaha mno, nilihitaji kuwaaminisha kwamba sikuwa na wasiwasi na Alfred hata kidogo, hivyo ilikuwa ni lazima nionekane nipo kawaida kumbe upande wa pili niliamua kuanza kazi yangu ya kumpeleleza huyu Scaila, alikuwa nani na alijishughulisha na nini?
Nikamchukua na kuanza kurudi naye nyumbani.
Nilimletea unafiki mwingi, stori zilikuwa nyingi mno, nilichangamka kupita kawaida kumbe moyo wangu ulikuwa na maumivu makali mno.
Tukafika nyumbani na kuelekea sebuleni. Tukaingia na kuendelea kupiga stori, tulicheka pamoja na kula kisha kuelekea chumbani.
Siku hiyo nilihitaji kujifanya kuwa bize na mambo yangu kumbe nilihitaji kufanya jambo fulani kubwa. Nilijua kuhusu mambo ya kompyuta, jinsi application ya WhatsApp ilivyokuwa ikifanya kazi kwenye kompyuta kupitia kitu kiitwacho WhatsApp Web.