15
Nilikitolea macho kile kitu, sikuweza kukifahamu lakini alipokichukua na kukifunga mkononi mwake, nikagundua kwamba ilikuwa ni hirizi iliyofungwa kwa kitambaa chekundu.
Mchungaji yule aliendelea kukaa pale makaburini huku akizungukazunguka huku na kule, ghafla, likaja kundi la wachawi wengi, walikuwa na muonekano kama aliokuwa nao yeye, walimfuata na kuanza kuzungumza naye maneno mengi ambayo sikuweza kuyasikia.
Miongoni mwa watu wale waliokuwa wamemfuata, alikuwepo mtu ambaye nilimfahamu sana kwa sura, hakuwa mgeni kabisa machoni mwangu, alikuwa mchungaji mwingine ambaye naye nitakupa stori yake hapo baadae nikimalizana na hawa watu niliowaona kule kuzimu.
“Ninataka kuwa na washirika wengi zaidi,” nilimsikia mtume yule akisema kwa sauti ya juu huku wengine wakimsikiliza.
“Kingine?” aliuliza mchungaji yule.
“Ninataka niwe na mvuto mkubwa,” alisema mtume.
“Hakuna tatizo, subiri.”
Aliposema hivyo, watu wote wakainamisha vichwa vyao chini akiwemo huyo mtume mwenyewe.
Ghafla nikaanza kuona moshi mkubwa ukianza kufuka kutoka katika sehemu iliyokuwa na giza totoro, nilibaki nikiangalia na sikutaka kuyaamisha macho yangu.
Mara akatokea mzee fulani, alionekana kuwa dhaifu na mwendo wake ulionyesha aliumia mguu. Kwa kumwangalia tu, isingekupa wakati mgumu kugundua kwamba mzee yule alikuwa mchawi.
Alimsogelea mchungaji yule huku akiwa ameshika tunguli moja kubwa ambayo kwa juu aliifunga kwa kitambaa cheusi. Alipomfikia, akamwambia apige magoti, mchungaji akatii na kumuwekea tunguli ile kichwani mwake.
Alizungumza maneno ambayo nayo sikuyaelewa na mwisho wa siku kumgawia kisu mtume yule na kumwambia akichomeke kaburini, katika lile kaburi la mtoto mdogo, akafanya hivyo.
“Ninataka utoe kafara,” alisema mzee yule.
“Hakuna tatizo, nipo tayari bwana wangu,” alisema mchungaji.
“Chukua hii tunguli, kuna damu ndani yake, nyunyizia katika kaburi hilo.”