Simulizi : Safari Ndefu Kuelekea Kaburini

SEHEMU YA 68

kama alikuwa amebeba mzigo mkubwa moyoni mwake, kwa kipindi kile akajiona kama ameutua mzigo ule.
Tabasamu pana likaanza kuonekana usoni mwake. Hakujua ni hali gani ambayo ilimpelekea kutabasamu, ila alijihisi kufanya hivyo moyoni kwa kuwa alikuwa akijisikia huru kupita kawaida.
Mchungaji White akaanza kumsogelea Bwana Jonathan ambaye bado alikuwa akiendelea kupiga kelele huku akiendelea kuleta vurumai kitendo ambacho kwa kiasi fulani kilitaka kuharibu ibada nzima. Alipomfikia Bwana Jonathan, akamuwekea mkono kichwani.
“Who are you? (Wewe ni nani?)” Mchungaji White alimuuliza.
“Jethro. I am Jethro. We are one thousand in here (.Jethro. Mimi ni Jethro. Tupo elfu moja hapa)” Sauti ambayo ilikuwa ni tofauti na sauti ya Bwana Jonathan ilisikika kinywani mwa mzee huyo.
“Ok! Do you know this place? (Unaifahamu sehemu hii?)” Mchungaji White aliuliza.
“The Church. This is the church (Kanisani. Hili ni kanisa){
“So you have to keep quite. In the name of Jesus Christ (Kwa hiyo unatakiwa kubaki kimya. Kwa jina la Yesu Kristo)” Mchungaji White alimwambia.
Hapo hapo mchungaji White akawaambia wale watu ambao walikuwa wamemshika Bwana Jonathan kumuachia. Kuanzia hapo hakukuwa na vurumai zozote zilizoendelea zaidi ya utulivu mkubwa uliowekwa na Bwana Jonathan. Mchungaji White akaendelea kuhubiri huku Bwana Jonathan akiendelea kubaki kimya huku akiwa amesimama kanisani pale.
Alipomaliza kuhubiri, maombezi yakafanya na kanisa zima na kisha kuanza kumfuata Bwana Jonathan ambaye alikuwa katikautulivu mkubwa. Alipomfikia, akaupeleka mkono wake kichwani kwa Bwana Jonathan.
“Let him free...in the name of Jesus Christ (Mwacheni huru....kwa jina la Yesu Kristo)” Mchungaji White aliamuru.
Bwana Jonathana akaanguka chini, akaanza kutupa miguu yake huku na kule, kelele zikaanza kusikika tena kutoka kinywani mwake huku zikilalamika kwamba kulikuwa na moto ambao ulikuwa ukiwaunguza mahali pale. Washirika wengine hawakubaki kimya, walikuwa wakizidi kuomba.
“Let Jesus finish His work (Mwacheni Yesu amalize kazi yake)” Mchungaji White aliliambia kanisa huku yeye akiifuata madhabau ambapo akamimina
 
SEHEMU YA 69

maji katika grasi yake na kunywa huku tabasamu pana likiwa usoni mwake.
Bwana Jonathan bado alikuwa akiendelea kupiga kelele mahali pale, baada ya dakika tano, akabaki kimya. Watu ambao walikuwa wamemleta mahali pale wakaambiwa wambebe na kumuweka kwenye kiti kwa ajili ya kupumzika hata kabla mambo mengine hayajaendelea.
Bi Leticia alibaki akilia, hakuamini kile ambacho alikuwa amekiona kwa macho yake. Kitu ambacho mganga mkubwa Moodinho alikuwa ameshindwa kukifanya, kanisani pale kiliweza kufanyika, mumewe alikuwa mzima kama siku za nyuma. Huku akionekana kuwa na furaha, akaanza kumfuata mchungaji White, machozi ya furaha yalikuwa yakimtoka.
“Thank you (Asante)
“Glory to God. I am not the one who healed him. Jesus is the one who healed him and let him free (Utukufu kwa Mungu. Mimi siye ambaye nimemponya. Yesu ndiye ambaye amemponya na kumuweka huru)” Mchungaji White alimwambia Bi Leticia ambaye alikuwa akilia na kuomboleza.

Watu hawakuamini kile ambacho walikuwa wamekisikia katika vyombo mbalimbali vya habari juu ya msanii Martin kuamua kufunga ndoa na msichana ambaye alikuwa amelala kitandani kwa muda wa miaka mitatu. Watu wakaanza kufuatilia kwa ukaribu zaidi kwa taarifa zile ambazo wala hazikuonekana kuaminika masikioni mwao.
Mpaka pale ambapo Martin alipohojiwa na kukubaliana na tetesi zile ndipo ambapo watu wakaamini kwamba taarifa zile zilikuwa na ukweli na wala hazikuwa tetesi zozote zile.
Watu wengi walikuwa wakimshangaa Martin ambaye alikuwa ameamua uamuzi mkubwa ambao kamwe usingeweza kufanya namtu yeyote yule kama asingekuwa na mapenzi ya dhati. Watu wakaanza kumuona Martin kama mtu ambaye alikuwa amekosea kufanya uamuzi huo kwa sababu tu kulikuwa na wanawake wengi wazuri na wazima ambao walikuwa wakitamani kuwa nae.
Kwa wasichana hao wengine wote, Martin alikuwa hajawaona, kwake, msichana ambaye alikuwa amepooza kitandani ndiye ambaye alikuwa ameonekana machoni mwake.
Taarifa zile zikaanza kusambawa kwa kasi, watu wengi wakawataarifu
 
SEHEMU YA 70
marafiki zao katika mitandao ya kijamii kama facebook, Twitter na mitandao mingine. Kila mtu ambaye aliisikia taarifa ile alionekana kushangaa na kushtuka.
“Mapac huyu huyu ndiye anataka kumuoa Patricia?” Jamaa mmoja aliwauliza wenzake huku akionekana kushangaa.
“Ndio”
“Yaani pamoja na kumsaliti kote kule kwa kutaka kuolewa na mcheza kikapu?”
“Kwani alisalitiwa! Hapana. Wakati msichana yule alipokuwa akiondoka nchini Tanzania hakuwa na uhusiano wa kimapenzi na Mapac, walikuwa ni marafiki tu” Jamaa mwingine alijibu.
“Lakini si walifanya”
“Kufanya sio ishu. Unajua msichana yule alikuwa amelelewa kiulaya ulaya tu, kwa hiyo kufanya ni jambo la kawaida kwake”
“Acha kunitania wewe”
“Kweli. Unamjua Angelina Jolie?”
“Amefanya nini sasa?”
Mbona yeye alikuwa akifanya mapenzi na marafiki zake wa kawaida kila alipojisikia kufanya mapenzi. Sisi Waafrika ndio tunachukulia jambo hili kubwa, ila huko mbele au kwa watoto waliokulia maisha ya kiulaya ulaya, mbona kawaida tuuu”
Kila mtu mitaani alikuwa akiongea lake, uamuzi ambao alikuwa ameufanya Martin ulionekana kuwashangaza kupita kawaida. Hakukuwa na kitu walichokisubiria zaidi ya kuisubiria siku ile ambayo ilipangwa, baada ya wiki mbili ifike ili kuishuhudia harusi hiyo ambayo ilitarajika kufanyika katika kanisa la Praise And Worship huku watu wengi wakijiahidi kuihudhuria kanisani hapo.
“Siku tano zimebaki kabla ya harusi”
***********
Siku ambayo ilikuwa ikisubiriwa na watu wengi ikafika. Watu wakaanza kujisogeza katika kanisa la Praise And Worship lililokuwa Mwenge kwa ajili ya kushuhudia harusi ya msanii wa muziki ambaye alikuwa ameachana na muziki kwa kipindi kirefu, Martin ambaye alikuwa akijulikana kwa jina la kisanii la Mapac ambaye alikuwa akifunga ndoa siku hiyo na msichana Patricia, msichana ambaye alikuwa hajiwezi kitandani kwa muda wa miaka mitatu mpaka kipindi hicho.
Wasanii wengi wa muziki, viongozi mbalimbali wa siasa pamoja na viongozi wengine wa dini walikuwa wamekusanyika kanisani hapo kwa ajili ya kuiona harusi hiyo ambayo ilionekana kushika hisia za watu nchini Tanzania.
Kanisa lilikuwa limejaza watu wengi kiasi ambacho mpaka wengine wakatakiwa kubaki nje kutokana na watu zaidi ya elfu mbili kuwa ndani ya kanisa hilo kubwa. Kwaya mbalimbali zikaanza kuimba kama kuvutia muda ili maharusi hao waweze kuingia kanisani hapo ifikapo saa tano kamili asubuhi siku hiyo ya Jumamosi.
 
SEHEMU YA MWISHO
COUNT-DOWN - 10


Kila wakati watu walikuwa wakiangalia saa zao, waliuona muda ukienda sana lakini wala maharudi hawakuweza kufika kanisani hapo. Dakika zilikatika zaidi na zaidi, magari ya maharusi yakaanza kuingia ndani ya eneo la kanisa lile.
Waandishi wa habari wakaanza kupiga picha. Picha zilipigwa kwa mfululizo na kwa haraka sana. Kila mwandishi wa habari kwa wakati huo alikuwa akifikiria kuhusiana na magazeti ambayo wangeyatoa siku inayofuata na siku nyingine pia.
Kikundi cha matarumbeta bado kilikuwa kikiendelea kupiga matarumbeta mahali hapo mpaka pale bwana harusi, Martin alipoteremka kutoka garini. Suti nzuri nyenye rangi nyeusi, shati jeupe na tai nyekundu vilionekana kumpendezesha kupita kawaida. Akaanza kupiga hatua kadhaa, alipofika mlangoni akasimama kumsubiria bibi harusi.
Kitanda alichokuwa amelazwa Patricia kikaanza kusukumwa na wapambe wa bibi harusi mpaka pale ambapo alisimama Martin. Uso wa Martin ukajawa na tabasamu pana kila alipokuwa akimwangalia patricia aliyekuwa pale kitandani.
Shela kubwa ambalo lilionekana kuwa la thamani lilikuwa limempendezesha Patricia. Uzuri wake siku hiyo ulionekana kuvutia zaidi huku vijipambo vingi vikiwa vinaung’arisha uso wake.
Bibi Beatrice pamoja na mpenzi wake, Bwana Thomson walikuwa miongoni mwa watu ambao walitembea karibu na kitanda alicholazwa Patricia. Kitanda kikaanza kusukumwa kuelekea mbele ya kanisa, watu walikuwa wakipiga vigelegele huku kwaya nazo zikiendelea kuimba.
Machozi yakaanza kumtoka Martin. Ni kweli alitamani sana kumuoa Patricia, katika maisha yake hiyo ndio ilikuwa ndoto yake ya kila siku. Siku hiyo ndio ilikuwa siku ile ambayo alikuwa akiisubiria katika kipindi chake chota. Alikuwa akimuoa Patricia lakini tatizo lilikuwa ni kwa jinsi Patricia alivyokuwa.
Kwa wakati huo wala hakuonekana kujali, kitu ambacho alikuwa akikijali kwa wakati huo ni kumuoa patrici a tu na kisha kumuita mke wake. Huku wakiwa wanasogea mbele ya kanisa kwa mwendo wa taratibu, mawazo ya Martin yakaanza kujirudisha nyuma kama mkanda wa filamu.
Akaanza kukumbuka kipindi kile ambacho walikuwa shuleni. Katika kipindi ambacho alikuwa akifanya kila jitihada za kuongea na patricia, msichana
 
SEHEMU YA MWISHO
COUNT-DOWN - 9


ambaye alikuwa mrembo kuliko wasichana wote shuleni pale. Alikumbuka mpaka katika siku ya kwanza ambayo aliongea na Patricia huku akionekana kusahau maneno mengi ambayo alipanga kumwambia mara tu atakapoongea nae.
Mawazo yake hayakuishia hapo, alikumbuka vilivyo alivyokuwa akisaidiwa mambo mbalimbali na Patricia, alipokuwa akisaidiwa nguo, fedha na vitu vingine vingi. Kwa wakati huo alikumbuka kila kitu, alikumbuka mpaka pale alipomtamkia neno ‘Nakupenda’ kwa mara ya kwanza, mpaka pale ambapo Patricia alipokataa kuwa mpenzi wake.
Akaendelea kukumbuka zaidi, akakumbuka mpaka siku ambayo alifanya nae mapenzi hotelini na kuutoa usichana wake. Alikumbuka mpaka siku ambayo Patricia alikuwa akisafiri kuelekea nchini Marekani huku akiwa amemuachia barua ambayo ilimuumiza kupita kiasi. Alikikumbuka kiasi cha fedha cha shilingi milioni kumi na tano ambacho aliachiwa na msichana huyo kwa ajili ya kuanza maisha yake.
Kwa wakati huo bado alikuwa akiendelea kukumbuka mambo mengi. Alikumbuka mpaka miezi ambayo msichana yule, patricia alipokuwa akimtumia kiasi kikubwa cha fedha katika akaunti yake. Katika kila kitu ambacho alikuwa akikikumbuka kwa wakati huo, alijiona kuwa na kila sababu ya kumuoa Patricia.
Walipofika mbele ya kanisa, mchungaji akaanza kuhubiri maneno machache kuhusiana na ndoa na kisha pete kuletwa mikononi mwake. Mchungaji Mshana akazichukua pete zile na kisha kumtaka Martin achukue kipaza sauti.
“Martin Mruma. Umekubali kumuoa Patricia Thomson awe mke wako katika shida naraha, hzuni na fura, maumivu na faraja, ugonjwa na afya?” Mchungaji Mshana alimuulliza Martin.
“Ndio nimekubali” Martin alijibu huku akiachia tabasamu pana.
Mchungaji Msahana akarudia swali lile mara tatu, bado jibu la Martin lilikuwa lile lile, ‘Mdio nimekubali’. Mchungaji akataka kipaza sauti kiwekwe karibu na mdomo wa patricia na kisha kumuuliza maswali yale yale.
“Ndio nimekubali” Patricia alijibu kila alipoulizwa.
Kanisa zima likaanza kupiga makofi ya shangwe. Martin akakabidhiwa pete na kisha kumvarisha patricia na kumbusu. Kwa niaba ya Patricia, mama yake, Bi Beatrice akapewa pete na kumvarisha martin, kanisa zima likaanza kupiga makofi.
 
SEHEMU YA MWISHO
COUNT-DOWN - 8

Kutokana na furaha kubwa ambayo alikuwa nayo, Martin akashindwa kujizuia, machozi yakaanza kumtoka, akamsogelea Patricia na kumbusu shavuni. Siku hiyo ikaonekana kuwa siku ya furaha kuliko siku zote katika maisha yake, kitendo cha kufunga ndoa na Patricia kilimpa furaha moyoni.
“Nakupenda mke wangu” Martin alimwambia patrica.
“Nakupenda pia” Patricia alijibu na kisha kumbusu tena.
Harusi hiyo haikuwa na sherehe yoyote ile, harusi ilipookwisha, maharusi wakaelekea nyumbani kupumzika. Martin hakutaka kutoka karibu na Patricia, muda wote alikuwa karibu yake akimfariji.
Miezi iliendelea kukatika, hali ya Patricia wala haikubadilika, bado alikuwa vile vile. Martin hakutaka kumuacha Patricia, kila siku alikuwa pamoja nae akimfariji katika ile hali ambayo alikuwa akipitia kwa wakati huo. Yeye ndiye ambaye alikuwa akimfariji kama mumewe.
Martin wala hakufikiria kuhusu utajiri mkubwa ambao alikuwa akiumiliki Patricia, kitu ambacho alikuwa akikifikiria kwa kiipindi hicho ni mapenzi mazito ambayo alikuwa nayo kwa Patricia tu.
“Nitakufa mume wangu” Patricia alimwambia Martin.
“Hautokufa mpenzi mpenzi. Usiongee maneno hayo, unaniumiza” Martin alimwambia Patricia.
“Nitakufa tu Martin. Ila sijui kwa nini nimekuwa na safari hii ndefu kuelekea kaburini. Imekuwa ni safari ngumu na nzito kuipitia, imekuwa ni safari iliyokuwa na maumivu makali sana” Patricia alimwambia Martin ambaye akaanza kulia kwa sauti hali ambayo iliwafanya Bi Beatrice na Bwana Thomson kuja chumbani mule.
“Kuna nini tena?”
“Patricia mama”
“Amefanya nini?”
“Anaonekana kukata tamaa, yaani anaonekana kutotaka kuamini kwamba amepona. Ananiambia maneno yanayoonekana kunitisha, maneno yanayoonekana kunikatisha tamaa moyoni” Martin alimwambia Bi Beatrice ambaye akaanza kumsogelea Patricia pale kitandani.
“Utapona binti yangu. Naomba usimtishe mume wako” Bi beatrice alimwambia Patricia.
“Sikumtisha mama. Nilikuwa nikimwambia ukweli”
“Sasa huo ukweli wako ndio uliokuwa ukimtisha na kumkatisha tamaa.

Je nini kitaendelea?
Je Patricia atapona na mwili kutengemaa?
 
SEHEMU YA MWISHO
COUNT-DOWN - 7



Watanzania bado walikuwa wakimtaka Martin arudi katika muziki kama alivyokuwa zamani kutokana na wasanii ambao walikuwa wakiendelea kufanya muziki kuonekana kuupoteza muziki huo. Kwa martin lilionekana kuwa jambo gumu sana, asingeweza kufanya muziki na wakati mke wake alikuwa mgonjwa kitandani.
Watanzania hawakuonekana kukubali, bado walikuwa wakimtaka Martin aendelee kuimba muzi. Martin akaanza kufuatwa na waandishi mbalimbali wa habari ambao walikuwa wakimwambia jinsi watu walivyokuwa wakimtaka arudi katika muziki.
“Mke wangu ni mgonjwa. Sitoweza kusafiri mikoani kwa ajili ya kufanya muziki. Ninahitaji kuwa nae karibu” Martin alimwambia mwandishi wa habari.
“Kwa hiyo unataka tuwaambie vipi wapenzi wako?”
“Nipande jukwaani kwa mara ya mwisho. Hii itakuwa kwa mara ya mwisho, baada ya hapo nitastaafu kabisa muziki na kuendelea maisha na mke wangu” Martin alimwambia mwandishi wa habari.
“Kwa hiyo niwaambie kwamba utapanda jukwaani?”
“Ndio. Ila usisahau kuwaambia kwamba hii ndio itakuwa mara yangu ya mwisho kupanda jukwaani. Siku hiyo nitatambulisha nyimbo zangu tatu ambazo nilizitunga kwa ajili ya mke wangu katika kipindi nilichokuwa nchini Marekani. Baada ya hapo, muziki sitoendelea nao tena” Martin alimwambia mwandishi wa habari.
Kama alivyoambiwa na ndivyo ambavyo alivyotangaza. Kila mtanzaia hakuonekana kuamini kama Martin au Mapac Jnr alikuwa ameamua kurudi jukwaani kwa mara ya mwisho kabla ya kuachana rasmi na muziki huo. Kila mtu akawa na shauku ya kutaka kuhudhuria tamasaha lake ambalo likapngwa siku ya kufanyika.
Tiketi zikatolewa. Ni tiketi elfu mbili ndizo ambazo zilitakiwa kuuzwa kutokana na ukumbi wa Diamond Jubelee kuwa mdogo. Tiketi zile zikaisha na watu wengi kuonekana kutaka kuzihitaji. Zikatolewa tiketi nyingine elfu mbili, zikaisha huku watu wengi wakihitaji tiketi za kuhudhuria tamasha lile.
Wahusika wakaanza kufanya mipango, wakaomba vibali kwamba tamasha lile lifanyike uwanja wa taifa. Walipopewa vibali, wakatangaza kwamba tamasha lile llingefanyika katika uwanja wa mpira wa taifa.
Tiketi zikaendelea kuuzwa zaidi na zaidi. Kitu ambacho kilionekana kigumu kuaminika, tiketi zaidi ya laki moja zilikuwa zimeuzwa. Hali hiyo ilimaanisha
 
SEHEMU YA MWISHO
COUNT-DOWN - 6


kwamba watu elfu sabini wangekaa kaika viti vyote uwanja wa taifa na kuufanya uwanja huo kujaa wote huku elfu thelathini wengine kusimama ndani ya uwanja ule.
Idadi ile ilionekana kuwa kubwa kuliko uwanja ule, waandaaji wa tamasha lile wakatamani uwanja ule ungekuwa mkubwa zaidi kwa ajili ya kuchukua mapato zaidi. Watu wakawa wamekwishajaa, tiketi zimekwishaisha lakini bado watu wengine walikuwa wakihitaji tiketi.
“Zimekwisha” Muandaaji wa tamasha lile alisema.
“Kweli?”
“Ndio”
“Kwa hiyo sisi hatuwezi kupata tiketi? Si mtutengenezee tiketi nyingine. Yaani tumetoka mikoani kwa ajili ya kuangali tamasha hili halafu mnatuambia tiketi zimekwisha”
“Ndio. Nyie ndio mliochelewa. Kuna wengine wametoka nje ya nchi na wamekuja mapema sana na tiketi wamepata. Ukiachana na hao, kuna wengine wametoka mikoani pia lakini tiketi wamepata. Nyie ndioo mliochelewa” Muandaaji aliwaambia watu hao waliokuwa wakilalamikia uchache wa tiketi.
“kwa hiyo tufanye nini sasa?”
“Inabidi mfuatilie kwenye televisheni kwani tumetangaza kwamba tamasha hili litakuwa likirudhwa moja kwa moja kwenye vituo mbalimbali vya televisheni”
“Hata kama. Hatutofaidi kabisa kaka. Tutengenezeeni tiketi bwana. Unajua watu kama elfu ishirini wamekosa tiketi. Hebu chukua hizo elfu ishiririni halafu zidisha na elfu kumi, unafikiri utapata kiasi gani?” Jamaa aliuliza.
“Tutapata kiasi kikubwa cha fedha. Ila hatuangalii fedha tu, tunaangalia na uhai wa watu. Watu wakiwa wengi sana wanaweza kufa humo uwanjani” Mwandaaji alisema.
Bado watu walikuwa wakiendelea kuhitaji tiketi. Hakukuwa na mtu ambaye alitaka kuiona shoo hiyo katika televisheni zao, kila mtu alikuwa akitaka kuangalia moja kwa moja uwanjani pale.
*******

“Gari linanisubiri nje mke wangu. Naondoka kufanya shoo hii ya mwisho maishani mwangu. Baada ya hapo, nitatulia pamoja nawe kuendelea na maisha na wala sitojishughulisha na muziki tena” Martin alimwambia Patricia.
“Nenda salama mume wangu. Usijali, Mungu akutie nguvu na umalize salama” Patricia alimwambia Martin huku akitabasamu.
“Nitarudi mapema sana. Nitataka mpaka saa kumi na mbili niwe nimekwishafika hapa nyumbani. Sitotaka kukaa sana. Kwa sababu shoo
 
SEHEMU YA MWISHO
COUNT-DOWN - 5


itakuwa inaonyeshwa kwenye televisheni, naomba nawe uiangalie pia” Martin alimwambia mke wake huku akimuwekea televisheni pembeni yake.
Wasanii wengine wakawa wamekwishaanza kutumbuiza katika tamasha lile huku tayari ikiwa imekwishatimia saa nane na nusu mchana. Alipokamilisha kila kitu, akambusu patricia na kuondoka chumbani humo na kulifuata gari ambalo lilikuwa limekiuja kumchukua.
Ndani ya gari, Martin alikuwa na mawazo mengi juu ya mke wake, alitamani Patricia nae angekuwepo uwanjani pale akimuona akitumbuiza tamasha lake la mwisho katika maisha yake.
Wasanii wengine bado walikuwa wakiendelea kutuiza kwa zamu, ilipofika saa kumi kamili, mtangazji akaanza kumuita Martin kwa jina la Mapac Jnr kama alivyokuwa akijulikana na wengi.
Uwanja mzima ukaripuka kwa shangwe, kelele zikaanza kusikika uwanjani hapo. Televisheni kubwa ambayo ilikuwa uwanjani hapo ikaonganishwa na kiuanza kuonyesha kila kilichouwa kinaendelea jukwaani.
Martin akaanza kuja jukwaani pale. Wakinadada wakashindwa kuvumilia, wengine wakaanza kupanda jukwaani kwa ajili ya kumkubatia tu na kujiwekea kumbukumbu maishani mwao.
Mabaunsa walikuwa makini sana. Wakawawahi madada wale na kisha kuwateremsha jukwaani. Wale ambao walikuwa na mioyo dhaifu wakaanza kulia, kila walipokuwa wakimwangalia Martin, kumbukumbu zao zikaanza kumkumbuka Patricia ambaye alikuwa kitandani.

“Yeah! Kama kawa nitakwenda kutambulisha nyimbo tatu ambazo nilizitunga nchini Marekani kwa ajili ya mke wangu kipenzi, Patricia. Ninampenda sana mke wangu, yeye ndiye ambaye ananifanya kuachana na muziki. Ninahitaji kuwa karibu nae zaidi, sitaki kuwa mbali nae. Ninampenda sana mke wangu, Patricia” Martin aliwaambia watu waliokusanyika uwanjani pale na kisha kuanza kuimba.
Siku hiyo ilikuwa ni burudani juu ya burudani, watu walikuwa wakiruka ruka kwa furaha. Muda mwingi martin alikuwa akiziangalia kamera kwa kuona kwamba hata mke wake alikuwa akimwangalia.
Martin alikuwa amefunika kupita kawaida. Mpaka muda huo, tayari alikuwa ameimba nyimbo zaidi ya kumi na mbili. Watu wakaridhika, wakaridhika na shoo ile, kiingilio cha shilingi elfu kumi walichokitoa kikaonekana kwenda kihalali kabisa.
“Najiandaa na kuja kupiga nyimbo mbili za zamani. Nipeni dakika mbili”
 
SEHEMU YA MWISHO
COUNT-DOWN - 4


Martin aliwaambia watu waliohudhuria uwanjani mule. Huku jasho likimtoka, akaenda sehemu ambayo alikuwa akibadilishia nguo zake tayari kwa kubadilisha na kuvaa mavazi mengine.
Akatoa simu mfukoni mwake. Simu kadhaa zilikuwa zimepigwa. Martin alipoziangalia, akagundua kwamba alikuwa Bi Beatrice. Ukiachana na missed calls hizo, pia kulikuwa na meseji kutoka kwa Bi Beatrice, akaifungua na kuanza kuisoma.
“IT’S OVER MARTIN... PATRICIA AMEFARIKI” Meseji ile ilisomeka, Martin akapigwa na mshtuko mkubwa.

“Vipi?” Bwana Hasimu, muandaaji alimuuliza baada ya kuuona mshtuko wake wa waziwazi.
Bwana Jonathan akawa mzima kabisa. Muda wote alikuwa akiilia tu kanisani pale. Hata mkewe, Bi Leticia alipokuwa akimsogelea na kumfariji lakini bado mzee huyo alikuwa akiendelea kulia tu. Kumbukumbu za tukio la nyuma ambalo alikuwa amelifanya zikaonekana kumuumiza moyoni mwake.
Bado hakujisikia amani kabisa moyoni mwake, alitakiwa kufanya jambo fulani kwa wakati huo hata kabla maisha yake hayajaendelea mbele zaidi, kutubu kwa kiile kitu kibaya ambacho alikuwa amekifanya.
Akaomba kipaza sauti na kisha kuanza kulielezea kanisa kila kitu ambacho alikuwa amekifanya cha kusababisha ajali ile mbaya. Kanisa zima likashtuka, hawakuamini kusikika kile ambacho Bwana Jonathan alikuwa amekifanya. Si kanisa pekee lililokuwa limeshtuka, bali hata mke wake alikuwa ameshtuka kupita kawaida.
Bwana Jonathan alikuwa akilia kupita kwaida, alionekana kutubia kila kitu ambacho alikuwa amekifanya katika kipindi kilchopita. Akapiga magoti chini, akatupa kipaza sauti, machozi ambayo yalikuwa yakimtoka yakaanza kuloanisha shati alilokuwa amelivaa.
“Natana kuokoka mchungaji” Bwana Jonathan alimwambia mchungaji.
Hakukuwa na kitu kilichoendelea kwa wakati huo zaidi ya bwana jonathan na mkewe, Bi Leticia kumkabidhi Yesu maisha yao. Kutokana na kipindi hicho mapolisi kuendelea kuchunguza chanzo cha ajli ile ambayo ilitokea miaka mitatu iliyopita, wakamchukua Bwana Jonathan na kumfikisha katika mkono wa sheria.
 
SEHEMU YA MWISHO
COUNT-DOWN - 3


“Hata nikihukumiwa kifo, kwa kuwa nina Yesu moyoni, natumaini atanipokea huko niendako” Bwana Jonathan alimwambia mkewe.
Dunia nzima ikashtuka mara baada ya toba yake kutangazwa katika vyombo mbalimbali vya habari. Hawakuamini kama mzee yule angeweza kufanya jambo zito kama lile kwa sababu tu alikuwa amekataliwa kimapenzi na Patricia..

Taarifa zile zilipofika nchini tanzania, watu wakalalamika kupita kawaida huku wakitaka Bwana Jonathan ahukumiwe kifo kwa kile alichokifanya. Watu wakaanza kuandamana na mabango mikono mpaka katika ubalozi wa marekani kumtaka mzee huyo ahukumiwe kifo tu.
Kutokana na kile alichokifanya, mawakili wake walivyokuwa wamemtetea kwa nguvu zote, Bwana Jonathan akahukumiwa kifungo cha miaka kumi na tano jela. Kwa hukumu hiyo, kidogo Watanzania wakaonekana kufurahi.
“Namshukuru Mungu kwa kuwa najua nitaendelea kumtumikia katika maisha yangu yote jela. Ninamshukuru Mungu kwa kunipa nafasi hii” Bwana Jonathan aliiambia mahakama huku akiishika vizuri Biblia aliyokuwa nayo.
*********
Martin akashindwa kuendelea kusimama, akajikuta miguu ikilegea na kukaa chini. Akaanza kulia kama mtoto, kila alipokuwa akiulizwa hakutoa jibu lolote lile, alikuwa akiendelea kulia. Bwana Hashimu akaichukua simu ile na kuanza kuisoma meseji ile, nae akaonekana kushtuka pia.
“Naondoka. Naomba uwaambie watu kilichotokea kwamba mke wangu amefariki hivyo sitoweza kuendelea na shoo” Martin alimwambia Bwana Hashimu.
Hakukuwa na sababu ya kupoteza muda, Martin akachomoka ndani ya chumba kile na kuanza kukimbia kuelekea nje. Watu ambao walikuwa nje ya uwanja ule walipomuona, wakaonekana kumshangaa, hawakujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea.
Martin akaingia garini, dereva wake ambaye alikuwa nje ya gari lile nae akaingia. Safari ya kuelekea nyumbani ikaanza. Njia nzima Martin alikuwa akilia kama mtoto, hakuonekana kuamini kile ambacho kilikuwa kimetokea.
“Its over Martin...Patricia amefariki” Meseji ile ilimrudia mara kwa mara kichwani mwake.
Gari lilipokaribia karibu na maeneo ya nyumbani kwake, wala hakutaka kulisubiria lisimame, akufungua mlango na kutoka nje. Kutokana na kukosa balansi akajikuta akianguka na kuchubuka mikononi, hakuonekana kujali, akainuka na kuanza kuelekea ndani.
 
SEHEMU YA MWISHO
COUNT-DOWN - 2


Kitu cha kwanza mara baada ya kuingia ndani ni kwenda moja kwa moja chumbani kwake. Patricia hakuwepo kitandani, mipira ilikuwa imebaki pale pale huku televisheni ikiendelea kuonyesha kila kilichoendelea uwanjani, watu walikuwa wakiondoka huku wengine wakilia.
Martin akatoka chumbani mule na kuanza kumuita mfanyakazi wake wa ndani na kuanza kumuuliza mahali walipokuwa mke wake, Patricia pamoja na mama yake Patricia, Bi Beatrice.

“Wamekwenda hospitalini”
“Wapi?” Muhim...” Hata kabal ahajamaliza jibu lake, Martin akachomoka kwa kasi.
Martin alionekana kuchanganyikiwa kupita kawaida. Akaingia garini na kumwambia dereva kuendesha gari kwa kasi ya ajabu. Foleni ambazo zilikuwa barabarani zikaonekana kumkera.
“Vunja sheria” Martin alimwambia derava.
“Unasemaje?”
“Hebu sogea nikuonyeshe” Martin alimwambia dereva ambaye alipisha katika kiti kile.
Martin akaanza kuendesha gari kwa kupitia katika njia za waendao kwa miguu. Kwa wakati huo alikuwa tayari kwa kitu chochote kile, hakujua kama kuvunja sheria lilikuwa kosa au la, alichokuwa akikitaka yeye ni kufika hospitalini haraka iwezekanavyo.
Mapolisi wa barabarani walipoliona gari lile likivunja sheria, wakaanza kulifuata kwa kutumia pikipiki zao kwani walishaona kulikuwa na kitu kinaendelea. Japokuwa walikuwa wakilitaka gari lile lisimame lakini Martin hakutaka kusimama.
Alipofika katika eneo la hospitali ya Muhimbili, akalisimamisha na kuanza kuteremka. Akaanza kukimbia kwa mwendo wa kasi, alionekana kuchanganyikiwa kupita kawaida. Muda wote alikuwa akitokwa na machozi, hakuamini kwamba mwanamke ambaye alikuwa akimpenda, Patricia tayari alikuwa amefariki kitandani, tena katika siku ambayo alikuwa amevunja historia na kuweka rekodi kwa kuujaza uwanja wa taifa kuliko hata mechi za Simba na Yanga.
Watu wengi ambao walikuwa wakimuona hospitalini pale walikuwa wakitamani kupiga picha na Martin kwani nafasi ile ilionekana kuwa adimu machoni mwao. Kutokana na jinsi Martin alivyoonekana kuwa na haraka, hawakupata nafasi ile kabisa.
“Mke wangu yupo wapi?” Martin alimuuliza dada wa mapokezi ambaye hata kabla ya kujibu, dokta Williams ambaye alisoma nae akatokea.
“Karibu Martin” Dokta Williams alimkaribisha.
“Nimekuja kumuona mke wangu”
“Nifuate”
 
SEHEMU YA MWISHO

Martin na dokta Williams wakaanza kupiga hatua kuelekea ndani zaidi, safari yao ikaishia nje ya chumba cha kuhifadhia maiti, Bi Beatrice alikuwa benchini akilia.
Martin akaanza kumsogelea Bi Beatrice, alipomfikia akamkumbatia. Wote wakaanza kulia, Martin alionekana kuumia zaidi. Kufariki kwa mke wake, Patricia kulionekana kumuumiza kupita kawaida.
“Patrica wangu! Kwa nini umeniacha Patricia?” Martin aliuliza kwa sauti kubwa iliyowafanya watu waliokuwa wakipita kuanza kusogea na kugundua kwamba mwanaume yule alikuwa Martin.
“Usilie Martin. Yote ni mipango ya Mungu” Bi Beatrice alimwambia Martin huku nae akilia.
“Amemchukua Patricia wangu. Amemchukua mke wangu. Kwa nini Mungu? Kwa nini umeamua kufanya hivi?” Martin aliuliza.
“Usimlaumu Mungu bali yakupasa kumshukuru kwa kila jambo” Bi beatrice alimwambia martin.
“Inaniuma mama. Inaniuma sana. Bado ninampenda Patricia” Martin alimwambia Bi Beatrice.
Kulia kwao hakukuweza kubadilisha kitu chochote, ukweli ukabaki vile vile kwamba Patricia alikuwa amefariki dunia. Tukio lile la kumpoteza mke wake kipenzi, Patricia likabaki kuwa kumbukumbu katika maisha yake.
Picha za Patricia zikabaki kuwa kumbukumbu katika maisha yake yote. Martin hakutaka kuendelea kujishughulisha na muziki, alibaki kimya huku utajiri wote aliokuwa nao Patricia ukimfikia mikoni mwake.
Martin akafungua miladi mingi ambayo ilikuwa ikimuingizia fedha kila siku. Martin hakutaka kuoa tena, alichokifanya ni kuandika kitabu cha maisha yake, kitabu ambacho kilielezea mambo mengi tangu alipozaliwa, alipokutana na Patricia na hadi alipoanza muziki.
Kitabu kile kilinunuliwa na watu wengi, kilimuingizia zaidi ya milioni mia moja kwa kuwa kiliandikwa katika lugha mbili, Kingereza na kiswahili. Utajiri wake ukazidi kuongezeka mpaka kufikia kipindi cha kuingiza milioni mia mbili kwa mwezi kupitia biashara mbalimbali alizokuwa amefungua pamoja na vituo kadhaa vya mafuta.
Baada ya kutakiwa sana na wananchi kuoa, hapo ndipo alipoamua kumuoa msichana Rosemary, rafiki wa Patricia ambaye alisoma nae toka shuleni. Pamoja na kuoa na kufanikiwa kupata watoto lakini bado kumbukumbu za marehemu mke wake hazikuweza kumtoka kichwani mwake, bado alikuwa akiendelea kumkumbuka huku mara kwa mara akienda makaburini kuliona kaburi la Patricia na kuweka maua.
“Nitaendelea kumpenda milele” Martin alijisemea huku akilibusu jina la Patricia lililoandikwa katika msalaba pale kaburini.

SEMA LOLOTE KUHUSU SIMULIZI HII

MWISHO


BURE SERIES
 
TUPIA COMMENT YAKO, TUANZE NA SIMULIZI IPI... SIMULIZI IKICHAGULIWA MARA 5 TUNAANZA NAYO.

KIGUU NA NJIA ✅

SALAMU KUTOKA KUZIMU✅

MIKONONI MWA NUNDA✅

MALAIKA WA SHETANI

MTAMBO WA MAUTI

ZAWADI YA USHINDI

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

NAJISIKIA KUUA TENA

ROHO YA PAKA

NOTI BANDIA
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom