Sehemu ya 16
Huo ulikuwa mtihani mkubwa kwake, hakuamini mtu kama yeye kupendwa na mwanaume mwenye fedha kama Razak, hakutaka kuamini, moyoni, alihisi kama alikuwa akitaniwa, na Razak hakumaanisha alichomwambia.
“Unanipenda mimi?” aliuliza Aisha huku akionekana kushtuka.
“Ndiyo!”
“Umenipendea nini?”
“Aisha...kila kitu ulichokuwa nacho, nimekipenda, nimependa jinsi ulivyo, kila kitu kwa pamoja, nimekupenda,” alisema Razak.
Razak akamsogelea Aisha pale alipokuwa na kisha kuubusu mdomo wake. Mwili mzima wa Aisha ulikuwa ukitetemeka kama mtu aliyesikia baridi kali.
Wakati yote hayo yakitokea, Ahmed na Mohammed walikuwa pembezoni mwa sebule huku wakichungulia kisiri, kila kitu kilichokuwa kikendelea, walikuwa wakikiona tu.
Hapo ndipo walipojua sababu ya Razak kumtafuta Aisha kwa udi na uvumba, mpaka kufikia hatua hiyo, tayari wakajua kwamba hata wao maisha yao yangekuwa mazuri kwani kwa Aisha, wao walisimama kama ndugu zao.
“Kumbe anampenda!” alisema Ahmad kwa mshangao.
“Nilijua tu, nililigundua hilo mapema kabisa,” alisema Mohammed.
Maisha yake yalikuwa ya kimasikini, hakuwahi kupata maisha mazuri tangu alipozaliwa. Mama yake alikufa miaka mingi iliyopita, alizaliwa huku mama yake akiwa mitaani kwa hiyo hata kipindi hicho bado aliendelea kuishi hukohuko mitaani.
Hakuwa na ndugu, kama alikuwa nao hakuwa akiwafahamu kabisa. Watu wa karibu aliokuwa amezoeana nao ambao kwake walikuwa kama ndugu ni watoto wa mitaani na wale mapacha wawili ambao kwake walikuwa kila kitu.
Alimkubali Razak, hata kama mwanaume huyo alikuwa na fedha lakini naye mwenyewe moyo wake ulianza kumuingiza mwanaume huyo ila hakutaka kumwambia kwani alijua fika kwamba kuna siku tu mwanaume huyo angetamka maneno hayo.
Alipokubaliwa, Razak hakuamini, alichokifanya ni kumnyanyua Sabrina kisha kumkumbatia kwa mahaba mazito, joto la miili yao, likakutana na kujisikia tofauti, kilichotokea baada ya hapo ni kuufungua ukurasa mpya wa mapenzi.
*****
Kelele zilikuwa zikisikika kutoka ndani ya jumba moja la kifahari, watu watatu walikuwa wakibishana, mmoja alikuwa mwanaume mzee, mwingine mwanamke mzee lakini huyo wa tatu alikuwa msichana mwenye umri usiozidi miaka ishirini, huyu alikuwa Sabrina.
Mara baada ya kuanza uhusiano mpya na Sharifu, Sabrina aliamua kuwaita wazazi wake na kuwaeleza kweli kwamba alikuwa amepata mwanaume mpya na si Razak ambaye alikuwa naye tangu alipokuwa mtoto mdogo.
Wazazi wake hawakuamini kile walichokisikia, walimkubali Razak, kwao, mwanaume huyo alionekana kuwa sahihi kuwa mkwe wao, hawakutaka kuona binti yao akiwa na mwanaume mwingine tofauti na Razak.
Walitoa baraka zote kama wazazi kwa kumwambia Sabrina kwamba waliridhia kuona mwanaume huyo akimuoa binti yao, hivyo wao kama wazazi kitu pekee walichokuwa wakikisubiria kilikuwa ndoa tu.
Baada ya kupita muda fulani, leo binti yao aliwaletea habari nyingine, mpya ambayo iliwasisimua sana baada ya kuwaambia kwamba alikuwa amemuacha Razak kwa sababu alipata mwanaume mwingine mwenye mchanganyiko wa rangi aitwaye Sharifu.
Wazazi wakachanganyikiwa, hawakuamini kile alichokisikia, walimwangalia binti yao, walihisi kama alichanganyikiwa, hawakuamini kabisa kile walichoambiwa.
Walimfahamu Razak, hakuwa mwanaume machepele, alikuwa mwanaume mpole aliyejitoa kwa kila kitu, wao kama wazazi walimpenda sana, sasa kitendo cha binti yao kuwaambia kwamba aliachana na Razak kwa ajili ya mwanaume mwingine, iliwachanganya.
“Haiwezekani Sabrina....” alisema baba yake kwa sauti kubwa.
“Nimeamua baba, mtake, msitake ni lazima Sharifu anioe...” alisema Sabrina.
“Mimi si ndiye mzazi?”
“Na mimi si ndiye mtoto?”
“Utaona, hakuna ndoa hapa, huwezi kuolewa na mwanaume mchafu hata kama ana fedha kiasi gani,” alisema baba yake kwa sauti kubwa, alionekana kukasirika mpaka mishipa ya shingo kumtoka.
Je nini kitaendelea...