[h=1]Nilipanga Nyumba moja na Majini-12-[/h]
ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
MUDA mwingi niliwaza maisha ya kwenye ile nyumba, hasa usiku wa siku hiyo ambapo najua wale watu wakija ndiyo balaa litakuwa kubwa zaidi.
"Halafu usiku wa leo lazima watakuja kunifanyia maajabu yao, lakini dawa yao nisilale. Oke, kumbe bangi itapulizwa leo, kidogo itakuwa nafuu," nilisema moyoni, nikashtuliwa na sauti ya kike nyuma yangu iliyoita jina langu.
SASA ENDELEA…
NILIPOGEUKA nyuma, nikamwona dada mmoja aitwaye Mwantumu Seleman nilikuwa naishi naye Mwananyamala. Akaniuliza habari za siku. Niliamua kumsimulia janga langu, lakini ghafla likaja gari, akaingia huku akiniambia atanitafuta siku nyingine.
Baadaye nilirudi kazini huku nikiwa na hali ya wasiwasi, hata kazi zangu zikuzifanya sawasawa kama ilivyo kawaida yangu. Iliniuma sana!
Muda wa kazi ulipokwisha, niliondoka moja kwa moja hadi nyumbani. Sikutaka kupitia mahali siku hiyo, lakini nilishakubaliana na yule mfanyakazi mwenzangu aliyesema atakuja na bangi yake.
Wakati nafungua mlango mkubwa nilibaini wenzangu walisharudi maana mlango haukufungwa na funguo, nikaingia ndani. Nilipofika kwenye mlango wangu wa kuingilia sebuleni, wakati naufungua nikasikia mlango wa chooni unafunguliwa, yaani kumaanisha kwamba kuna mtu anatoka.
Ukisimama mlangoni pangu, mtu akitoka chooni unamuona bila kificho, hususan kama anakuja vyumbani. Lakini pia hata akiwa anatoka kwenda uani, utamuona kwa mgongoni. Nilisita kuingia nikiamini nitamwona mtu huyo. Nilianza kuona miguu ikitoka, moyo wangu ukashtuka, mara nikamwona mtu mwenyewe.
Nilijikuta nikisisimka mwili, niliamini naona kivuli chake na si yeye. Ni mtu mweusi, wakati nilitarajia angekuwa mweupe.
Alivyozidi kunisogelea, nikabaini kuwa, ni yule kijana muuza maji kwenye mkokoteni.
"Ha! Wewe vipi, unatafutwa sana unajua?" nilimwambia.
Badala ya kunijibu, alikata kona kuufuata mlango mkubwa. Na mimi nikamfuata kwa nyuma, nilimkuta akiwa anamalizikia kutoka nje. Niliitupa simu kwenye kochi kisha nikatoka kumfuata, na mimi nilifungua mlango ambao ulishaanza kurudi baada ya yule kijana kutoka.
Nilishangaa kutomuona popote kule nje. Wazee wawili walikuwa wanapita, nikawauliza kama wamemuona mtu ametokea mlangoni pale, wakasema hapana, ila kuna mbwa alitokea ndani kazunguka nyumba.
"Mh! Mbwa tena?" niliwauliza wale wazee, nao wakasisitiza kuwa ni mbwa, tena mweusi.
Mapigo ya moyo yalianza kwenda mbio, wasiwasi uliongezeka kiasi cha kunifanya niishiwe nguvu. Wakati huo wale wazee walikuwa wakimalizikia kwa mbali. Niliogopa kurudi ndani, nikawa nimesimama mlangoni.
Wazo lilinijia kwamba, nimpigie simu yule mfanyakazi mwenzangu kumuomba aje mapema maana hali ni mbaya sana. Lakini simu nayo ilikuwa sebuleni kwenye kochi, nitaipataje, yaani nitaifuataje kule ndani wakati niliamini tayari kumeshakuwa ukanda wa kifo?
Niliteremka na kusimama nje kabisa, ghafla kwenye dirisha la chumbani kwangu nikaona kama mtu anachungulia nje, nilikaza macho ili kumwangalia vizuri, akapotea.
"Mh! ni kweli?" nilijiuliza mwenyewe. Ukweli ni kwamba alikuwepo mtu, tena mweusi au niseme Mwafrika kama mimi.
Nilikwenda pale dirishani, nikapanda ili kuchungulia, nikaona mlango unafunguka kuashiria kuna mtu alitoka maana mlango ule ulikuwa hauwezi kukaa wazi, ni lazima ujifunge wenyewe na mbaya zaidi mimi nilikuwa sijaufungua zaidi ya ule wa sebuleni.
Kuna jamaa mmoja alikuwa anakuja kutokea upande ninaoondokea kwenda kazini, simfahamu lakini nilimsimamisha.
"Bro kuna ishu hapa inatisha kidogo, naomba msaada wako."
"Kuna nini?" aliniuliza.
Nilimsimulia kila kitu cha siku ile tu lakini, sikugusia mambo ya nyuma.
"Du! Kwa hiyo mimi nikusaidieje?"
"Naomba tuingie wote ndani, nataka nikachukue simu yangu tu nimpigie huyo jamaa."
"Da! Itakuwa ngumu kidogo, unajua mimi nina haraka sana leo," alijitetea yule mtu ambaye kwa umbo ni bonge la mtu. Nilijua ni uoga tu, hakuwa na kuwahi wala kuchelewa.
Alipopita, akatokea mwingine, mzee mmoja, kichwa chote kilichafuka kwa mvi. Nilimsalimia huku nikimwonesha ishara kwamba nataka kuzungumza naye.
"Mzee samahani sana."
"Bila samahani kijana."
Naye nikamsimulia tukio la siku ile, lakini wakati ananisikiliza, mara nilimwona anatupia macho dirishani na mimi nikageuka kuangalia, sikuona mtu.
"Umeona nini mzee wangu?"
"Nimeona msichana ananizomea."
"Kweli?"
"Ee. Ndiyo hayo mambo unayosema?"
"Ndiyo hayo mzee."
"Twende," alisema, nikaanza kutangulia mbele, mzee akanifuatia kwa nyuma. Hatukuwa tukiongea chochote, najua sababu. Kila mmoja alikuwa anaiwaza hatari ya mbele.
Tuliingia ndani, tukafika sebuleni, lakini sikuiona simu kwenye kochi.
"Ona sasa mzee, simu niliitupia hapa, lakini haipo."
"Au unayo mfukoni kijana?"
"Hapana, nina uhakika," nilisema huku nikijipapasa mifukoni, hakukuwa na simu.
"Nitajie namba nijaribu kuibipu," yule mzee aliniambia huku akitoa simu yake mfukoni. Nilimtajia namba zote, akawa anaziandika, kisha akapiga huku simu akiwa ameiweka kwenye sikio lake la kulia. Nilishtuka sana kusikia simu yangu inaita kutokea kwenye chumba cha wale wapangaji wenzangu.
"Si hiyo?" yule mzee aliniambia akiniangalia kwa mshangao.
Mzee alikata kisha akapiga tena, ikaita tena kutokea kulekule, nilizidi kuogopa, nikamwambia tutoke lakini uzee kweli dawa, aliniambia hakuna haja ya kutoka dawa ni kupambana tu.
Alinisogelea na kuniambia kwa sauti ya chini:
"Niwagongee mlango?"
"Si watakasirika?"
"Sasa kama unaogopa watakasirika, unadhani simu yako utaipataje?"
"Haya wagongee. Lakini subiri, kwa nini tusiende kwanza chumbani tukajua nani alikuwa anachungulia nje?"
Je, nini kiliendelea? fuatilia baadae...