SEHEMU YA 62
Deborah alilia sana, alihuzunika, maisha yake yalikuwa ya majonzi kupita kawaida, alikonda mno, aliteseka lakini wazazi wake hawakutaka kujali kabisa.
Alitia huruma, kila mtu aliyekuwa akimwangalia alimsikitikia kwani hakuonekana kuwa kama yule Deborah wa kipindi cha nyuma, huyu alikuwa mwingine kabisa.
Mawazo yakawa makubwa, akaanza kupata vidonda vya tumbo vilivyoanza kumtesa na kumpa maumivu makali, akaanza kuchagua aina ya vyakula ambavyo alitakiwa kula, vingine aliambiwa asile, hasa vile vilivyokuwa na asidi.
Wazazi wake walimuonea huruma lakini kamwe hawakutaka kujutia kile walichokifanya, waliamini kilikuwa kitu kizuri kwa sababu walifanya kila lililokuwa bora, hawakutaka binti yao aangukie kwenye mikono ya mwanaume ambaye angeshindwa kumfanyia kitu chochote hasa kumpa maisha ambayo aliyahitaji.
Walizungumza naye kila siku, kila walipoongea naye, alionekana kuwa na majonzi mazito, hasira kali dhidi ya wazazi wake.
Alitamani kuufumbua mdomo wake na kuwaambia ni kwa namna gani alikuwa akiwachukia lakini alishindwa kufanya hivyo kwa kuwa tu aliwaheshimu, ila moyoni mwake aliwachukia kupita kawaida.
Hakuonana na John, mwanaume huyo alifukuzwa kazi, hakupata hata muda wa kwenda nyumbani kwake, kila alipokuwa, mama yake alikuwepo, alikuwa kama mlinzi kwake, alitakiwa kurudi nyumbani mara tu anapomaliza kazi.
Kwa kuwa waliamini kitendo cha kumuona John kingemfanya kurudi tena nyuma, wakaamua kuhama kanisa, yote hayo ni kwa sababu hawakutaka kuona binti yao akiungana na mwanaume huyo tena.
Maisha yalikuwa ni ya mateso mno, hakuyapenda lakini alitakiwa kuyaishi kila siku katika maisha yake. Siku ziliendelea kukatika na baada ya miezi saba ya kuwa na maisha yenye maumivu makali ndipo akapata mwanaume aliyemwambia alikuwa akimpenda mno.
Mwanaume huyo aliitwa Jericho Michael, mmoja wa kijana aliyetoka kwenye familia iliyokuwa na uwezo mkubwa kama wao.
Jericho hakumpata hivihivi, aliwatumia wazazi wake ambao walikwenda kuzungumza na wazazi wa Deborah na wao wakazungumza na binti yao na hatimae wawili hao kuwa wapenzi.